[wanabidii] ZITTO KABWE,MBONA U MSAHAULIFU?

Friday, December 13, 2013
Na Happiness Katabazi

SISI Wanyambo ambao ni wenyeji wa wilaya ya Karagwe mkoa wa Kagera tunamsemo mmoja maarufu usemao; "Omusheija ainduka aha Kitanda,tainduka aha lulimi'.

Kwa tasfiri ya lugha ya Kiswahili maana yake ni kwamba "Mwanaume ana geuka kitandani,habadilishi kauli aliyokwisha itoa mdomoni mwake.Yaani akisema amesema."

Nimelazimika kutumia msemo huo kwasababu makala yangu ya leo itajadili kauli zinazokinzana zilizotolewa na mtu mmoja kwa nyakati tofauti na mtu huyo si mwingine ni Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia(CHADEMA), Zitto Kabwe, kuhusu mawaziri wa wanaotaka kuwania urais mwaka 2015 wafukuzwe kazi na kauli zake mwenyewe kuhusu kauli zake za kinafki na sitaki nataka wadhifa wa urais mwaka wa Tanzania.

Gazeti la Tanzania Daima Jumapili toleo la Novemba 28 mwaka 2011, ilikuwa na kichwa cha habari kisemacho ; " Zitto awalipua mawaziri, asema hawafanyi kazi,wanauwaza urais".

Habari hiyo ilisomeka hivi,Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Zitto Kabwe, amemtaka Rais Jakaya Kikwete kuwafukuza kazi mawaziri wake tisa wanaotaka kuwania urais kupitika chama hicho mwaka 2015.

Bila kuwataja majina mawaziri hao, Zitto alisema hivi sasa hawafanyi kazi ya kujenga uchumi wa nchi na badala yake wamejiingiza katika 'vita' ya kuwania uongozi huo.

Kauli hiyo aliitoa Novemba 27 mwaka jana jijini Dar es Salaam mara baada ya kufungua mkutano wa Muungano wa vyama vya Kidemokrasia Afrika (DUA) uliojumuisha vijana kutoka katika nchi 22 ambapo Baraza la Vijana la CHADEMA (BAVICHA) ndio wenyeji.

Zitto alisema uchumi wa Tanzania umeporomoka na kufikia asilimia 17, hali ambayo imesababishwa na mawaziri wa serikali ya Rais Jakaya Kikwete kushindwa kufanya kazi kikamilifu.

Alisema kwa sasa hali ya nchi ni mbaya ukilinganisha na wakati wa utawala wa Rais Benjamin Mkapa, ambapo uchumi ulishuka kwa asilimia 4.5 na mfumuko wa bei ulidhibitiwa kwa kiwango kikubwa.

Aidha Machi 1 mwaka 2012:Gazeti hili la Tanzania Daima lilikuwa na kichwa cha habari kisemacho; "Nikiombwa nitagombea urais-Zitto"

Zitto katika habari hiyo alinukuliwa akisema kuwa ikiwa chama chake kitaona kuwa anafaa kuwania nafasi ya urais ama nyingine yoyote, hatasita kupokea wajibu huo.
Lakini Gazeti la Mwananchi Jumapili la Machi 25 mwaka huu, lilichapisha habari iliyokuwa na kichwa habari kisemacho "Zitto: Nitagombea urais 2015".

Katika taarifa yake aliyoituma katika gazeti hilo Zitto alisema; " Kwanza atakayekabili changamoto hizi. Ninaamini ninaweza kuwaongoza Watanzania wenzangu kukabili changamoto hizi."

Alitamba anao uwezo kwa kuwa ni mzalendo, mwenye utashi wa kuleta mabadiliko stahiki kulingana na nchi inavyoongozwa. Katika taarifa hiyo ameeleza kuwa kwa sasa nchi imesahau maendeleo ya watu badala yake imejikita katika maendeleo ya vitu.

Kwa mtiririko huo hapo juu wa kauli za Zitto alizozitoa katika tarehe tofauti na magazeti tofauti na kwamba hadi leo hii naandika makala hii sijaona wala kumsikia Zitto akikanusha kauli zake hizo, ni wazi zimenipa msukumo wa kuweza kujadili kauli hizo ambazo kwa mtizamo wangu nadiriki kuziita ni kauli zinazo kinzana ambazo zinatoka kinywa cha mtu mmoja.

Kwanza Ikumbukwe kuwa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzaia ya mwaka 1977 , inatoa haki kwa wananchi wake ya kuchagua au kuchaguliwa.Lakini kwenye kiti cha urais, Ibara ya 39(1) (b) ya Katiba hiyo inasema 'Mtu hatastahili kuchaguliwa kushika kiti cha urais wa Jamhuri ya Muungano , isipokuwa tu kama; ametimiza umri wa miaka arobaini.

Kama Novemba 27 mwaka jana, Zitto alinukuliwa akiwatuhumu mawaziri wa serikali ya awamu ya nne inayoongozwa na Rais Jakaya Kikwete ambao mawaziri wote hao ni wanachama wa CCM, watimuliwe kazi bila kuwataja majina yao kwasababu hawafanyi kazi wanauwaza urais wa mwaka 2015 , halafu Machi 25 mwaka huu, Zitto huyu huyo anaibuka na kusema anautamani rais na kwamba anasifa za kuwa rais.

Kwa kweli baada ya kumsikia akitoa tamko hilo , binafsi nilimshukuru mwenyezi Mungu kwa ameweza kufanyakazi yake ya kuanza kufanyakazi yake ya kutuonyesha sisi waje wake ili tufumbuke macho na tuone kuwa Zitto kumbe na yeye ni jamiii ile ya baadhi ya wanasiasa wale wale wenye hulka za kinyang'au ambao wanakasumba ya kuzungumza uongo mbele ya umma, ili umma uwapende na uamini kuwa kiongozi huyo ni mtu safi na mtetezi wa wanyonge, kumbe siyo kweli.

Kwa watu tunaofuatilia matendo na kauli za viongozi wetu wa kitaifa, uwa tunatunza akilini na maktaba zetu baadhi ya matamshi wanayoyatoa kwa lengo ya kuzisoma na kujifunza kama nitaona zina mantiki ndani yake.

Ieleweke wazi hapo nyuma Zitto alitokea kujizolea umarufu mkubwa ndani ya jamii kwa kile kilichoelezwa ni mwanasiasa kijana ambaye ana misimamo thabiti na asiyeyumba katika kile anachikiami.

Lakini hivi sasa kadri siku zinavyozidi kwenda ule mvuto aliokuwa nao awali umeanza kutoweka kwa sababu mbalimbali ambazo binafsi bado sijazithibitisha ila baadhi ya wanananchi mitaani na wengine ni wanachama wenzake wamekuwa wakieleza kuwa Zitto hana usafi wowote,anakisariti chama chake na kwamba yupo pale kwaajili ya kutaka kukivuruga chama.Na kwamba viongozi wa chama chake wameishamfahamu wanachokifanya ni kumpuuza.

Sisi waumini wa sheria tunasema tuhuma zitabaki kuwa tuhuma hadi pale zitakapothibitika na mahakama au vikao husika vya chama chake.Lakini kwa kuwa mungu ni mwema kadri siku zinavyozidi kwenda mbele atazidi kutuonyesha kama kweli Zitto ni mwanasiasa msafi ,mhadilifu kuliko wanasiasa wenzake wanaotoka katika vyama mbalimbali vya siasa.

Na kwa kuanzia naona mungu ameanza kutufunulia kuwa naye Zitto ana tabia ile ile ya wanasiasa wenzake ambao leo wanapinga jambo hili lisifanywe na wanasiasa wenzao lakini kesho yeye anaibuka na kufanya jambo hilo hilo na wakati akifanya jambo hilo analialalisha yeye kulifanya ni halali ila wenzie wakifanya siyo halali. Kama siyo ubinafsi,unafiki na uchonganishi nini?

Zitto alitaka mawaziri watimuliwe kazi kwa kitendo chao cha kuwaza urais wa mwaka 2015 licha hadi sasa hakuna waziri yoyote alijitokeza adharani akatangaza nia ya kugombea au kukiri kuwa ana uwaza au anautamani urais kama alivyofanya yeye.

Tumuulize Zitto tukimuita yeye ni mbinafsi na mnaki na muongo tutakuwa tumekosea?

Maana yeye Zitto aliuambia umma kuwa kuna mawaziri tisa bila kuyataja majina yao wanautaka urais na eti watimuliwe kazi, lakini yeye baadaye akaibuka na kusema akiombwa na chama chake agombe atagombea na baadaye katika kipindi kifupi hata chama chake hicho akijamuomba wala kumpa ridhaa akiibukia kwenye gazeti la Mwananchi na kusema anautamani urais na kwamba ana sifa.

Kama hivyo ndivyo hatuoni Zitto ana kasumba ya ubinafsi ambayo anataka apate yeye wenzie wasipate?Mawaziri wakiuwaza urais yeye kwake ni haramu ila yeye akiutamani urais tena adharani siyo haramu?

Zitto ulipendekeza mawaziri hao tisa watimuliwe kazi licha mawaziri hao hawajajitokeza adharani kama wewe kutangaza nia, Sasa Je na wewe wafuasi wa Chadema wamuombe Mwenyekiti wako Freeman Mbowe na vikao husika wakuvue madaraka unayoyashikilia kwenye chama Chama chako kwasababu na wewe ndiyo kabisa umetangaza adharani kuwa unautamani urais na kwa hatua hiyo hufanyikazi za kujenga chama chako?

Nimebaki kujiuliza Zitto ana ubongo wa Ndezi?.Kwani wataalamu wa viumbe hai wanatueleza kuwa ndege huyo aina ya Ndezi moja ya sifa yake kuu ni kusahau mambo.

Kuutaka urais kwa kufuata utaratibu husika ulioanishwa kwenye Katiba ya Nchi siyo kosa la jinai na ndiyo maana sisi waumini wa sheria tulivyomsikia Zitto kwa mara ya kwanza akimtaka rais Kikwete awatimue kazi mawaziri tisa ambao hakuwa taja majina eti kwasababu wanawaza urais, tulimpuuza na kumuona ni mbumbumbu wa sheria.

Kwasababu Zitto akutaja majina ya mawaziri wale ,ni wazi hakutoa ushahidi unaoonyesha moja kwa moja mawaziri hao hawafanyikazi kabisa wanauwaza huo urais.Na kwakuwa rais Rais Kikwete ni msikivu aliupuuzia ombi hilo kwasababu halina mashiko.

Wananchi kwa kauli hizo za Zitto zimenifanya nianze kujiuliza hivi kama hali ndiyo Je ahadi alizokuwa akizitoa jimboni kwake nyakati za kampeni atazitekeleza kweli?
Na ndiyo maana hivi sasa ameanza kupoteza mvuto na wananchi hawampapatikii kama walivyokuwa wakimpapatikia zamani kwani wananchi walijijengea akili mwao kuwa eti huyo ndiyo ni mkombozi wao na viongozi wengine ni mafisadi na wachumia tumbo.

Na kama hivi ndivyo,Zitto ana tofauti gani na wale baadhi ya mawaziri ambao amekuwa akizikosoa bajeti zao bungeni kuwa mawaziri hao wameingiza takwimu za uongo katika bajeti zao?

Maana kiongozi au mwananchi wa kada yoyote akishaanza kuwa na tabia ya leo anaibuka na kutaka wenzake waadhibiwe kwa kufanya jambo fulani halafu kesho kiongozi huyo anaibuka na kufanya jambo lile lile linalofanywa na wenzake halafu yeye anataka umma umuone yupo sahihi ila wenzie wamekosea, kiongozi wa aina hii ni hatari kwa mustakabali wa taifa na hafai kupewa madaraka makubwa ya kuiongoza nchi yetu kwani mwisho wa siku sisi wananchi tutakachojifunza kutoka kwa kiongozi wa aina hiyo ni ubinfasi na uchonganishi.

Aidha napenda kumshauri Zitto na vijana wenzake ambao wameonyesha tamaa ya kupata madaraka makubwa kwa kutumia hoja ya umri wa kuwa rais ubadilishwe kwenye Katiba ili vijana wenye umri wa chini ya miaka 40 waweze kugombea nafasi hizo, wapunguze papara kwani wahenga walisema Mbio za Sakafuni uishia ukingoni.

Kwani Watanzania wa leo siyo wale wa mwaka 1947, wanakufahamu vizuri wewe Zitto na hao vijana wenzako na hiyo kilicho nyuma ya ajenda hiyo ,msione wamewanyamazia kimya mkawaona ni majuha.

Wanafahamu fika hoja yenu hiyo ni kwa maslahi ya kikundi cha vijana wachache wenye madaraka ya kisiasa ambao hivi sasa wameanza kutuhumiwa huku mitaani kichini chini kuwa wana mali ambazo haziendani vipato vinavyotambulika na mamlaka husika na wenye tamaa ya kupata madaraka makubwa kuliko umri kwa haraka.

Kwa mtazamo wangu bado Tanzania hatujafikia hatua ya kuwa na rais kijana mwenye umri wa chini ya miaka 40 kwa kisingizio tu etu tunaenda na wakati. Sababu ya mimi kuwa na mtazamo huo licha mimi bado ni kijana mwenye umri wa miaka 33 ni kwamba hulka za sisi vijana wengi zinafahamika.

Lakini pia narudia kusisitiza kuwa kiti cha urais wa Tanzania, siyo kitu rahisi, rahisi kama watu wanavyodhani, ni kiti chenye heshima na hadhi ya kipekee ambacho kimebeba dhamana ya kuwaongoza watanzania wote wakubwa kwa wadogo, hivyo tusifanye majaribio katika kiti cha urais.

Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika

0716 774494
www.katabazihappy.blogspot.com

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumapili, Aprili Mosi mwaka 2012

--
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/groups/opt_out.

Share this :

Previous
Next Post »
0 Comments