Hoja za Dk. Slaa zipimwe
JUZI, aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Mendeleo (Chadema), Dk. Wilbrod Slaa, alijitokeza hadharani kwa mara ya kwanza baada ya takriban mwezi mmoja hivi wa ukimya, na kuibuka na zile alizodai kuwa ni vielelezo (ushahidi) juu ya tuhuma mbalimbali zinazomkabili Edward Lowassa.
Katika mtindo ule ule uliozoeleka wakati akiwa Mbunge wa Karatu, Dk. Slaa alizungumza kwa ufasaha na kwa kujiamini huku akisapotiwa na nyaraka zake mwenyewe za kuthibitisha tuhuma hizo dhidi ya mgombea urais wa Ukawa.
Aliyoyazungumza si mageni sana masikioni mwa Watanzania wengi, ila ni msisitizo tu wa kile kilichokuwa kikidaiwa cha kutokuwapo ushahidi wa tuhuma kadhaa zilizokuwa zikielekezwa kwa Lowassa zinazoweza kusababisha kushitakiwa kwake au kumpotezea sifa za kuwa Rais bora wa Tanzania.
Kwa mwanasiasa aliyedumu kwa zaidi ya miaka 10 kwenye nafasi ya Katibu Mkuu wa chama kikubwa kama Chadema, anayeheshimika ndani na nje ya nchi, kusimama hadharani na kuzungumza mambo mazito kama hayo, haistahili kumpuuza hata kidogo.
Iwe ametumika, ametumiwa au amejituma bado hoja zake zinapaswa kuchukuliwa kwa tahadhari nzito na kuzijadili kwa kina ili kupata majawabu sahihi kwa kuwa yeye si Mtanzania wa kawaida sana kwani amekuwa kwenye uongozi wa juu ndani ya siasa kwa miaka mingi sana na kwa vyovyote vile kuna anayoyafahamu.
Hatutaki kuamini hata kidogo kwamba chuki binafsi kati ya watu hawa wawili, Dk. Slaa na Lowassa, ni miongoni mwa mambo yaliyomsukuma kuzungumza kama alivyozungumza juzi au uchu wa madaraka na ukubwa ndio uliosababisha hayo yote kuwekwa hadharani.
Hoja ni je, yana ukweli kiasi gani? Kama ni ya uongo, ni kwa nini aliyatoa hadharani? Kwa nini asishitakiwe kwa kuhatarisha amani? Na kama yana ukweli, utaathiri vipi mustakabali wa kisiasa na kijamii wa taifa letu?
Haja za Dk. Slaa na maswali haya ndivyo vinavyotufanya kuwataka wahusika (Lowassa na wenzake) watoe majawabu, wajisafishe ili kuondoa shaka mioyoni mwa Watanzania na kudhihirisha uadilifu wao kwa taifa.
0 Comments