WATAALAMU wa mifumo ya utawala wanaainisha hatua tano muhimu ambazo taasisi yoyote hupitia, vikiwemo vyama vya siasa. Hatua hizi ni kuzaliwa, kubalehe, kuimarika, kung'ara, kuchakaa na hatimaye kufa. Naziainisha hatua hizi katika mazingira ya kukua na kusinyaa kwa vyama vya siasa Tanzania na kuangalia maana yake katika ushindani wa vyama hivi tunapoelekea katika Uchaguzi Mkuu mwakani.
Hatua ya kwanza ni kuzaliwa. Katika hatua hii, wazo au ndoto hujitokeza miongoni mwa kikundi cha watu wachache waliokutana na kuamua kuanzisha taasisi kwa ajili ya kutekeleza wazo au ndoto yao hiyo. Katika hatua hii taasisi huendeshwa kama mali ya familia kwa njia ya maelewano, pasipo na taratibu, kanuni au sheria rasmi. Hiki ni kipindi ambacho taasisi yoyote ina amani na utulivu na uwepo wake hauonekani au haugusi jamii pana.
Hatua ya pili ni kubalehe. Katika hatua hii taasisi hupitia maumivu ya kukua. Watu wapya hujiunga na taasisi na kuingia kwao kunaanza kutisha waanzilishi. Ni kipindi ambacho taasisi inaanza kuwa na raslimali na watu wenye maslahi binafsi kuvutiwa nayo, ikiwemo fedha, mamlaka na heshima katika jamii. Kwa sababu hii waanzilishi wa taasisi watajaribu kushika usukani na kuonyesha kwamba wao ndio wenye uchungu na wanaoelewa malengo mapana ya taasisi, na kwamba bila wao taasisi itakufa. Wanachama wapya watajaribu kusukuma uwepo wa mifumo rasmi ya kuendesha taasisi kwa njia ya taratibu, kanuni na sheria, lakini waanzilishi hujitahidi kuonyesha kwamba wanajua dira na mwelekeo wa taasisi husika na hawa wanachama wapya wana nia mbaya ya kutaka kuvuruga taasisi. Kufanikiwa kupita salama katika hatua hii kutategemea na waanzilishi kukubali kukua kwa taasisi na kuwaamini wanachama wapya kwamba wao pia ni sehemu ya taasisi na kwamba taasisi inaweza ikatembea na kutekeleza malengo yake wao wakiwemo au bila hata wao kuwepo. Kama taasisi itafanikiwa kuvuka salama katika hatua hii itaingia katika hatua ya tatu. Lakini ikishindwa itabaki katika hatua hii hii na hatimaye kudumaa na kuna uwezekano mkubwa kwamba itaishia katika hatua hii na hatimaye kuanza kurejea katika hatua ya kwanza ya kubaki kataasisi kadogo kakifamilia.
Hatua ya tatu ni kuimarika. Kama taasisi itapita salama katika hatua ya pili ya kubalehe itaingia katika hatua ya kuimarika. Katika hatua hii taasisi inakuwa na mifumo imara ya kuendesha taasisi. Kwa upande wa vyama vya siasa, ni kipindi ambacho chama kinakuwa na itikadi, falsafa, misingi na sera imara, pamoja na kwamba mifumo hii bado haijatambulika sana katika jamii pana nje ya taasisi yenyewe. Uwepo na uimara wa taasisi katika hatua hii unategemea zaidi busara za viongozi kuliko mifumo ya uendeshaji kitaasisi. Ndio kusema, kuvuka katika hatua hii kunategemea zaidi uwezo, utashi na maadili ya viongozi waliopo katika kipindi husika.
Hatua ya nne ni pale ambapo taasisi inaanza kung'ara. Kwa upande wa chama cha siasa, ni kipindi ambapo itikadi, falsafa, misingi na sera zake zinaanza kuenea na kujadiliwa katika jamii. Ni kipindi ambacho chama kinakuwa na mifumo iliyowazi ya kulea na kubadilishana uongozi. Katika hatua hii chama ni kikubwa kuliko wanachama, na kwamba hakuna tena mtu anayesema chama hakiwezi kuwepo bila yeye kuwepo. Ni hatua ambayo wanachama wanajiamini na kwamba taasisi imeshavuka mipaka na kuwa mali ya umma. Ni katika hatua hii ambapo chama kina uwezo, kutegemeana na mikakati yake, wa kuaminiwa na umma na hatimaye kuchaguliwa kuongoza serikali.
Hatua ya tano ni pale ambapo taasisi inaanza kuchakaa na kuchokwa katika jamii. Ni hatua ambayo dira ya taasisi inaanza kupotea au angalu kufubaa na jamii haiguswi tena na taasisi hii. Kwa upande wa chama cha siasa, ni hatua ambayo huvikumba vyama vya siasa ambavyo vimekaa madarakani kwa muda mrefu. Bila kuchukua hatua madhubuti, chama tawala huweza kupoteza madaraka. Ili kisikumbane na adha ya kupoteza madaraka, chama kinapofika katika hatua hii lazima kijihuishe katika mifumo ya utawala na aina ya uongozi ili kirudi katika hatua ya nne ya kung'ara.
Kwa muktadha wa vyama vya siasa hapa Tanzania, kati ya vyama 22 vilivyosajiliwa, kwa maoni yangu, vyama vilivyokwishavuka hatua ya kwanza havifiki vitano, ambavyo ni CCM, CHADEMA, CUF na NCCR-Mageuzi. Ni hatua hii pia ambayo chama kipya kilichosajiliwa hivi karibuni cha ACT-Tanzania kinapita. Vyama vya CHADEMA, CUF na NCCR-Mageuzi vinapambana kuvuka hatua ya kubalehe ili viingie hatua ya kuimarika na hatimaye kung'ara. Katika kipindi cha miaka minne iliyopita, CHADEMA imepambana bayana katika kuvuka hatua mbili za kubalehe na kuimarika, na ilikuwa na kila dalili kuingia hatua ya kung'ara.
Ni wazi kuwa Chama cha Mapinduzi kipo katika hatua ya tano. Ni chama ambacho kimechakaa na kinaanza kuchokwa kwa kasi ya kutishia uhai wake madarakani. Ni hatua ambayo Chama cha Mapinduzi kilifika mwaka 2005 lakini kikajihuisha kwa kumchagua Jakaya Kikwete kuwa mgombea wake. Kwa yanayoendelea ndani ya Serikali ya Kikwete ni wazi kwamba chama hiki kimezidiwa na kuna uwezekano mkubwa kwamba kitaangushwa na uzito wake wenyewe. Kwa upande wa CHADEMA, ni maoni yangu kwamba chama hiki kilikuwa na nafasi nzuri sana ya kuvuka hatua ya kubalee na kwenda hatua ya nne na ya tano. Hata hivyo, jitihada zake hizi zimekwamishwa na kiburi cha kupendwa.
Je, CCM ina nafasi gani ya kujihuisha kabla ya uchaguzi mkuu ujao? Na, je, ni kwa kiasi gani muungano wa UKAWA utakisaidia CHADEMA kukivusha kutoka hatua ya kubalehe? Nitajaribu kujibu maswali haya katika sehemu ya pili ya makala hii.
- See more at: http://www.raiamwema.co.tz/ccm-inaangushwa-kwa-uzito-wake-upinzani-kwa-kiburi-cha-kupendwa#sthash.qqQa1lSH.dpufSend Emails to wanabidii@googlegroups.com
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/d/optout.
0 Comments