[wanabidii] KIAMA CHA MAJANGILI CHAJA, BATHAWK YAZINDUA NDEGE MAALUM KUPAMBANA NAO

Thursday, September 17, 2015
KIAMA CHA MAJANGILI CHAJA, BATHAWK YAZINDUA NDEGE MAALUM KUPAMBANA NAO

Na Daniel Mbega, Mkomazi
NI majira ya saa tatu asubuhi Jumatano, Septemba 16, 2015 wakati tunawasili kwenye uwanja mdogo wa ndege (air strip) katika eneo la Kisima ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi inayotenganisha mikoa ya Kilimanjaro na Tanga.
Uwanja unaonekana mweupe, hakuna ndege! Nikashangaa kwa sababu wenyeji wetu kampuni ya Bathawk Recon wametuambia tunakuja kushuhudia uzinduzi wa ndege maalum zinazopambana na ujangili.
Kilichoonekana mbele yetu ni hema kubwa ambalo mbele yake kulionekana minara midogo iliyosimikwa kama fimbo. Kwenye banda kubwa ikaonekana ndege ndogo aina ya Twin otter. Nikadhani ndiyo inayozinduliwa, lakini Idrisa Jaffary, mwenyei wetu tuliyekuwa naye kwenye gari akasema, hapana siyo hiyo.
Mshangao ukanipata baada ya gari kusimama wakati nilipokiona kifaa mfano wa ndege kikiwa kimeegeshwa kwenye bomba maalum kana kwamba ndege inataka kupaa.
Kama nisingekuwa nazifahamu ndege hizi maarufu kama drones, ningeweza kusema kwamba huo ni mdoli ambao mwanangu angefurahia kama ningempelekea akauchezea.
Kwa siku za karibuni zimekuwa maarufu kwani zinatumika kupeleka misaada mbalimbali hata katika maeneo hatari ya vita ambako hakufikiki kirahisi.
"Hii ndiyo ndege yenyewe," Idrisa akatueleza. "Hee! Ndiyo hii?" tukajiuliza kwa mshangao. Kwamba Tanzania tumeanza kuitumia teknoloia hii yanaweza kuwa maendeleo mengine mapya.
Mshangao wetu ulimalizika wakati Phil Jones, ofisa mwendeshaji wa mitambo hiyo kutoka kampuni ya MartinUAV ya Marekani iliyotengeneza ndege hiyo aina ya Super Bat DA-50 UAV, alipoanza kutuelezea namna 'ndege'hiyo (drone) inavyofanya kazi huku akituonyesha kila sehemu na kazi yake.
"Hii ni ndege ambayo haihitaji kuwa na rubani, inaongozwa kwa kompyuta maalum, ina antenna mbili, ina kamera maalum ambazo zinaweza kupiga picha usiku na hata mchana," akatueleza.
Akasema ndege hiyo ina uwezo wa kuruka urefu wa futi 20,000 kutoka usawa wa bahari na kwenda katika nusu kipenyo cha kilometa 35 kutoka ilipo mitambo ya kuiongoza.
Jones, ambaye baadaye alinieleza kwamba yeye rubani wa zamani wa ndege za kijeshi katika Jeshi la Uingereza aliyestaafu mwaka 2014 ambaye kwa sasa anaishi nchini Marekani, akasema ndege hiyo inayorushwa kwa mtindo wa manati (catapult launch system), inaweza kuruka mfululizo kwa muda wa saa 10 ikiwa angani kabla ya kutua na kujazwa mafuta tena.
"Ina mfumo maalum wa kamera ambazo zina uwezo wa kupiga picha hata usiku wa manane na kutambua mienendo ya viumbe wenye damu ya moto kama hayawani na binadamu, hivyo ni rahisi kubaini kama kuna majangili," akafafanua.
Baada ya maelezo ya takriban nusu saa, hatimaye yeye na wasaidizi wake wakaamua kuirusha ndege hiyo baada ya kuiwasha. Ilichomoka kwa kasi ya ajabu na kuelekea angani ikaanza kuzunguka.
Hapo ndipo tukasogezwa kwenye hema kubwa ambako tuliwakuta wasaidizi wake – Austin Howard na Kory Ferguson – wakiendesha kompyuta hizo na tukashuhudia mazingira halisi ya hifadhi katika eneo husika pamoja na kuona wanyama mbalimbali.
"Sasa hapa unaweza kuona kama kuna wavamizi (majangili) na inakuwa rahisi kuwasiliana na askari wa wanyama pori na kwenda kwenye eneo husika kuwakamata," anasema Jones.
Hata ilipotua, ilikuja kama ndege za kawaida zinavyokuja, tofauti yake tu yenyewe haina magurudumu. Naam, unaweza kuwa ufumbuzi mwingine wa kupambana na ujangili nchini, tatizo ambalo haliko Tanzania tu, bali katika nchi nyingi barani Afrika.
Taasisi mbalimbali za ndani na nje zikiwemo serikali za mataifa makubwa zimekuwa zikijitahidi kusaidia mapambano hayo kama alivyofanya Rais Barack Obama wa Marekani alipoahidi kutoa Dola milioni 10 (sawa za Shs. 20 bilioni) ili kuimarisha mapambano hayo nchini.
Takwimu zinaonyesha kuwa Bara la Afrika mwaka 1930 lilikuwa na tembo 50 milioni na kwamba hadi kufikia mwaka 2013 tembo waliobakia katika bara zima ni  500,000...
http://www.brotherdanny.com/2015/09/kiama-cha-majangili-chaja-bathawk.html

--
DANIEL MBEGA
INVESTIGATIVE JOURNALIST, BLOGGER, RESEARCHER & PUBLISHER
CELL: +255 767 939 319/ +255 715 070 109
WHAT'S APP: +255 656 331 974
BLOGS: www.kilimohai.wordpress.com
               www.brotherdanny5.blogspot.com

"Kama hawatuwekei mgombea mzuri, kwanini watutawale?" Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Dar es Salaam, 1995

--
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/d/optout.

Share this :

Related Posts

0 Comments