[wanabidii] MAONI NA MTAZAMO WA WANAZUONI VIJANA KUHUSIANA NA MAADHIMIO YA BUNGE KUHUSU RIPOTI YA CAG YA NOV 26-28.2014

Sunday, December 14, 2014
JUMUIYA YA WANAZUONI VIJANA TANZANIA.
MAONI NA MTAZAMO WA JUMUIYA YA WANAZUONI VIJANA TANZANIA KUHUSIANA NA MAADHIMIO YA BUNGE KUHUSU RIPOTI YA CAG YA NOV 26-28.2014

UTANGULIZI.
SISI ni mkusanyiko wa vijana, ambao ni wahitimu na wanazuoni vijana tuliopata kusoma shahada ya kwanza katika vyuo vikuu nchini na wengine wapo vyuoni wakisoma huku pia wengine tukiwa ni miongoni mwa watanzania wachache walisomeshwa shahada ya pili nje ya nchi kwenye fani zinazohusiana na masuala mbali mbali ya madini, nishati ikiwemo mafuta na gesi. 
Tunafurahi sana kupata nafasi hiyo ambayo tulidhaminiwa na serikali kupitia wizara ya nishati na madini, hivyo tunajivunia kuwa ni miongoni mwa watanzania wachache tuliowezeshwa na kufika mbali zaidi kielimu na serikali.
Tunawajibu mkubwa wa kuitetea nchi na kuisemea pale tunapoona kuna jambo baya limefanyika, kwa kuwa uelevu wetu umetokana na kupata elimu bora iliyotokana na kodi za watanzania wenzetu na hatupo tayari kuona mambo yakienda mrama.
Kama Taifa, hivi karibuni tumeshuhudia upepo mkali wa kisiasa ukivuma, wapo tuliouelewa, wapo tuliouamini, wapo tuliousadiki, wapo tulioutilia mashaka na zaidi ya yote wapo tuliobakia juu juu na kufuata mkumbo wa mambo.
Tukiwa kama wasomi vijana, tuna wajibu kwa taifa letu kulipigania ili kuhakikisha kuna usawa kwa kuwa Tanzania ni taifa huru na linahitaji kuwepo kwa wanasiasa huru na wenye maono ya kuifikisha nchi pahala salama kwa kuwa uwezo na maadili yao ni muhimu.
Tuna wajibu chanya kabisa, kuhakikisha nchi yetu inaendeshwa kwa kufuata misingi imara ya ukweli, uwazi, uwajibikaji huku ikizingatia msingi mkuu wa haki kwa kila mtu na watanzania waelewe kuwa kujiudhuru sio ushujaa au uzalendo. Jiulize wote waliojiudhuru hadi sasa ni wazalendo wa kweli wa nchi yetu?. 
Panapotokea masuala yote ya kitaifa, masuala yanayohusu kuwajibishana, kutuhumiana, kushughulikiana kama wengine wanavyosema, basi lazima misingi yote iende sambamba na haki kwa kila mtuhumiwa.

KUHUSU RIPOTI YA CAG
Sote tunakumbuka kwamba hivi karibuni Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) amekabidhi ripoti ya uchunguzi kuhusiana na sakata la TEGETA ESCROW, sakata ambalo msingi wake unahusiana na kampuni ya kufua umeme ya IPTL.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya CAG tumeshuhudia namna Taifa lilivyokuwa na hamu kutaka kujua kilichomo ndani yake.
Ripoti iliarifu juu ya Hadidu za rejea zaidi ya 11 iliyopewa na Waziri Mkuu, Bunge na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini.
Kwa nyakati tofauti, na kwa namna tofauti, sisi wenyewe, tumeshuhudia ripoti hiyo, na tumestahajabishwa na kugeuzwa geuzwa kwa mapendekezo ya ripoti hiyo kulikofanywa na kamati ya bunge ya PAC.
Katika ripoti ya CAG pamoja na viambatanisho vyake vyote, tumesoma na kuvirudia na kusoma na kuvirudia, hakika hakuna sehemu CAG ameshauri, ama kupendekeza, ama kutafsiri kwamba pesa iliyokuwepo katika ESCROW AKAUNTI ni mali ya UMMA.
Katika ripoti ya CAG, hakuna sehemu hata moja, wala kurasa hata moja, wala aya hata moja, iliyosema kwamba Waziri mkuu amelisababishia hasara Taifa.
Katika Ripoti ya CAG, hakuna sehemu yoyote inayosema kwamba Waziri wa Nishati na Madini amehusika kwa namna yoyote ile kulihujumu Taifa
Katika Ripoti ya CAG, hakuna sehemu yoyote inayosema kwamba Katibu Mkuu wa wizara ya Nishati Na madini amefanya uzembe, zaidi ya yote, ripoti imemtaja katibu mkuu huyu kuwa amefanya jitahada kadhaa kuhakikisha serikali inachukua tahadhari na kama ni kweli muhusika anastahili kulipwa fedha alizoomba kulipwa ama la.
Katika ripoti ya CAG hakuna sehemu yoyote inayosema kwamba pesa iliyotolewa kwenye akaunti ya ESCROW ni ama Bil321 au bil 306 kama wanavyouaminisha umma.
Ndugu zangu, najua mtachelewa kutuelewa, na mtashangaa kwa nini tumeamua kusema haya, lakini ni lazima tubadili sasa mfumo wetu wa siasa za Tanzania na siasa za kutatua matatizo na changamoto kama ilivyo sasa.
Kwa sasa hivi wanasiasa hasa wabunge, wamekuwa wakifanya maamuzi kishabiki, kichuki, ki maslahio binafsi na bila kuzingatia ukweli na misingi ya Utawala bora.
Ndugu zangu, kwenye Ripoti ya CAG kumesema wazi kwamba, serikali imefanya jitihada stahili kuhakikisha taratibu zinafuatwa ili kujiondoa kwenye madhara yanayoweza kutoke baada ya pesa kufuatwa.
Ripoti ya CAG haijamtia hatiani mtu yeyote. Tunashindwa kuelewa misingi ya kamati ya PAC ya kutaka kuwajibishwa kwa watu bila ya kuwa na hatia.
Vyovyote itakavyokuwa, na vyovyote itakavyotafsiriwa, sisi tunaamini na tunataka watanzania waamini kwamba, kuwapoteza watu kama Pro.MUHONGO, kwenye utumishi wa umma, kwa sababu tu hana mahusiano mazuri na MADALALI wa rasilimali za nchi hii, ambao historia imeonyesha maeneo kadhaa walipoiaminiwa na kuharibu.
Kumpoteza Muhongo kwa sababau tu tangu kuingia kwake ofisini ameziba mianya ya uchotwaji mkubwa wa pesa za watanzania kupitia sekta ya madini, na sasa mabepari wameungana na wabunge wenye husda kupambana dhidi ya kweli na haki anayosimamia Muhongo.
Kumpoteza Muhongo kwa sababu tu yeye na Katibu mkuu wake Eliakim Maswi, hawana mawasiliano mazuri na Mwenyekiti wa PAC Zitto Kabwe (Hii inatokana na kitendo chao kudhibiti udalali wa Rasilimali)
Kumpoteza Muhongo kwa sababu tu yeye na katibu mkuu wake hawana mahusiano mazuri na Mbunge Christopher Ole Sendeka kwa sababu hizo hizo za utetezi wa Rasilimali
Kumpoteza Muhongo kwa sababu tu yeye na Katibu Mkuu wake wamesitisha mkataba wa kutetewa kisheria na Mbunge Nilmrod Mkono wa Mkono & Co Advocate ambao mpaka unavunjwa alishalipwa zaidi ya Bilioni 65.
Kumpoteza Muhoingo kwa sababu tu amejitahidi kupambana kukomesha Mgao na sasa wauza Dizeli na Majenereta wamekosa sehemu ya kuuzia na kuamua kuunganisha nguvu kupambana nae. 
Sisi tunasema, wanaweza kuunganisha nguvu kupambana na Muhongo na Kumshinda, lakini sio kwenye Hili la ESCROW. 
Tunawashuri wakatafute SKENDO nyingine ambayo angalau iwe na chembe za ukweli ndani yake.
Kwenye Hili la ESCROW tunaamini, wabunge wamekurupuka, wabunge wametumiwa, wabunge wamehongwa na wao wamekubali kutumika.
KAMATI YA PAC IMETOA WAPI MAPENDEKEZO YAO?.
Msingi mkuu wa mapendekezo ya ripoti ya kamati ya PAC ulipaswa kuwa ni Ripoti ya CAG, 
Tumejaribu kuchambua Ripoti ya CAG na hatujaona wapi PAC wamepata mapendekezo waliyokuja nayo, hatujaona nab ado tunaamini kamati hii kama zilivyowahi kutumika kamati nyingine nayo hii pia imetumika kisiasa kufanikisha matakwa ya kifisadi.
MASWALI KWA PAC
1. Tunaitaka kamati hii itueleze, ni katika ukurasa wa ngapi, aya ya ngapi, nukta ya ngapi iliyopo kwenye ripoti ya CAG inayosema kwamba ESCROW ni MALI YA UMMA?.

2. Tunaitaka PAC itueleze, ni katika ukurusa wa ngaopi, aya ya ngapi, nukta ya ngapi iliyopo kwenye ripoti ya CAG inayosema kwamba MUHONGO na wenzake wamefanya makosa hivyo wawajibishwe.

3. Tunaitaka PAC ituonyeshe, ni wapi katika ripoti ya CAG imesema fedha ambazo IPTL imezichukua kutoka kwenye ESCROW ni BIL ama 321 au 306 kama wanavyodai.

4. Tunaitaka PAC itueleze, kama kulikuwa na mchezo mchafu, na wakauthibitisha, iweje wizara ya fedha isihusike?, kwanini Gavana wa BOT na timu yake na Waziri wa fedha na Timu yake nao wasihusike kwenye hilo kwa kuwa fedha ilikuwa kwao?.

5. Kama kweli kulikuwa na mchezo mchafu, iweje BRELLA, na wizara inayoisimamia ambayo ni Viwanda na Biashara na waziri wake na timu nzima wasiwajibishwe nao kusajili kampuni ambayo wanadai siyo halali?.

6. Kama ni kweli kuna tatizo, iweje TRA wakubali kupokea kodi ya zaidi ya Bil 30 kutoka kwa mbia wa IPTL ambao ni VIP iliyotokana na mauzo ya hisa 30% kwa PAP?. Kwanini TRA isiwajibishwe kwa kupokea fedha haramu na kuziingiza kwenye mapato ya serikali ilihali ikijua ni fedha haramu?.

7. Kama PAC walikuwa wanachambua Ripoti ya CAG, kwanini walimwita tena CAG na kutumia mawazo yake binafsi na ambayo hajayaweka wazi moja kwa moja, na kwanini hawakuwaita watuhumiwa waliowabaini?. Uko wapi utawala wa sharia hapa?.

8. PAC itueleze, tangu lini Bunge limekuwa walalamikaji, waendesha mashtaka, wasikilizaji kesi, majaji, na waandika hukumu?.

MAPENDEKEZO NA MSIMAMO WETU.
Kwa kuwa Bunge wao wamepeleka maombi yao haramu kwa Rais, nasisi tunapeleka mapendekezo yetu kwa Rais na kumsihi afanye yafuatayo.

1. Kwa kuwa Swala zima la ESCROW limegubikwa na siasa, maslahi binafsi, chuki, wivu na kukomeshana, hivyo tunamuomba Rais asitekeleze azimio hata moja mpaka kwanza umma utakapoelewa ukweli halisi wa mbivu na mbichi na kila lililo nyuma ya pazia kuhusiana na sakata hili

2. Tunamuomba Rais Aunde chombo huru, ili swala hili lichunguzwe na kufanyiwa maamuzi huru ikiwemo na Tuhuma za baadhi ya Wabunge kuhongwa, kununuliwa na kuwa mawakala wa Benki ya Standard Charterd.

3. Tunamuomba Rais, aviagize vyombo vyake vya ulinzi na usalama viwachunguze wabunge hawa kwa kukubali kutumiwa, kuhongwa na kununuliwa ili kutuondolea watetezi wetu wa Rasilimali.

MWISHO
Ni mwendawazimu pekee ambaye, ama mtu mwenye wivu, chuki au maslahi binafsi kama ilivyo kwa baadhi ya wabunge na wajumbe wa PAC ndiye atakayeweza kudharau kazi nzuri nay a kizalendo inayofanywa na serikali hasa kupitia wizara ya nishati na madini na waziri wake.

Sisi ni Watanzania, na hawa ni wabunge wetu, panapotokea wao kufanya madudu kama walivyofanya hivi sasa tuna wajibu wa kuwaonyesha, kuwaeleza na kuwakumbusha kwamba haya ni madudu. Na hivyo tunawakemea, kuwakanyqa, na kuwaambia wasirudie tena kufanya uzembe mwengine kama ule, kutumia kodi zetu watanzania kwenda kutumiwa na wazungu, madalali wa rasilimali na mabepari wachache ambao wanaona mfumo hauwafurahishi. Tuna ushahidi kwamba wapo wabunge wamehongwa kusema na kufanya waliyoyafanya.
Tunawaahidi watanzania wote na watetezi wa Rasilimali, kwamba tutazunguka nchi nzima kuhamasisha watanzania kusimamia ukweli, kutetea haki, wajibu na kuhakikisha hakuna mtanzania mtetezi wa Rasilimali ataonewa na wanasiasa wasaka tonge kama ilivyotaka kutokea hivi karibuni.

Tunaanzisha sasa hati ya maombi maalum kwa Raais (Petition Form) itakayosainiwa na mamilioni ya watanzania wanaoitakia mema nchi yetu kumuomba Rias apuuze maazimio haya ya mabepari, wahujumu uchumi na wasaka tonge walioungana na wasaka Urais.

Mungu ibariki Tanzania
Mungu wabariki wazalendo na watetezi wa kweli wa Rasilimali.

Imesomwa na
Shaibu Sufiani
Kaimu Mratibu Umoja wa wanazuoni vijana Tanzania

--
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/d/optout.

Share this :

Related Posts

0 Comments