KUNRADHI KWA PICHA HIZI. MATUKIO HAYA YANAZUILIKA, KWANINI WATAWALA WANAPENDA KUMWAGA DAMU?
Tazama unyama wa Polisi!
Na Daniel Mbega
KICHWA cha habari kilichonivutia ni 'Kova aongeza idadi ya 'tume' D'Salaam' ambacho kipo kwenye gazeti la Mwananchi toleo la Jumatano, Septemba 3, 2014.
Habari hii imefuatia hatua iliyofanywa na Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, baada ya kutangaza jopo la wapelelezi kuchunguza kifo cha mtuhumiwa Liberatus Matemu (55) aliyefia katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili akidaiwa kupigwa na polisi katika Kituo cha Stakishari na maiti yake kukataliwa na nduguze. Kabla ya kufariki Jumapili iliyopita, Matemu alikuwa chini ya ulinzi katika kituo hicho kilichopo wilayani Ilala ambako alikaa kwa siku nane. Jopo hilo la wapelelezi litaongozwa na Mkuu wa Upelelezi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Costantine Masawe.
Tumeshazowea kusikia 'tume' zikiundwa kila yanapotokea matukio mbalimbali, mengi yakiwa yamefanywa ama kuwahusisha hao hao wanaounda tume hizo. Mifano iko mingi, na inadhihirishwa na vichwa vya habari kama vile… "Jeshi la Polisi launda Tume kuchunguza mauaji ya Mwangosi!", "Tume ya kuchunguza majuaji Morogoro yaundwa!", "Walioua raia Songea wachunguzwa!", "Polisi wachunguza mauaji Nyamongo!", "Msako waanza utekwaji wa Kibanda!" "Aliyemteka Dk. Ulimboka hajulikani!" "Mabomu ya Arusha yaacha maswali".
Naam, vichwa vya habari vya aina hii vimekuwa vikijitokeza kila wakati kwenye vyombo vya habari nchini kila mara yanapotokea mauaji katika vurugu mbalimbali, na mauaji haya mara nyingi yamekuwa yakisababishwa ama kufanywa na askari wa jeshi hilo hilo la polisi.
Lakini ukitazama jopo lililoundwa na Kamanda Kova, binafsi nasema ni usanii mwingine unaoendelea kwa sababu mpaka sasa hakuna taarifa zozote za uchunguzi zilizotolewa na kamanda huyo kuhusu matukio kadhaa yaliyotangulia, ambayo alidai yanachunguzwa baada ya kuyaundia 'tume'.
Itakumbukwa kwamba, Julai 23, 2014, Kova huyo huyo aliunda timu ya wataalamu saba kuchunguza kashfa ya viungo vya binadamu vilivyookotwa Mbweni Mpiji, wilayani Kinondoni ambavyo vilidaiwa vilikuwa vikitumiwa katika Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Tiba na Afya (Imtu) lakini hadi sasa wananchi hawajajulishwa kuhusu majibu ya uchunguzi huo.
Aidha, Mei 21, 2014, Kova aliunda tena jopo la wapelelezi liliongozwa na Mkuu wa Upelelezi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jaffari Mohamed kuchunguza kifo cha aliyekuwa Meneja Biashara ya Petroli wa Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura), Julius Gashaza aliyedaiwa kujinyonga na hadi leo taarifa za uchunguzi huo hazijatangazwa.
Mnamo Januari 7, 2014, Kamanda Kova aliunda jopo la wapelelezi nane walioongozwa tena na RCO Jaffari Mohamed kuchunguza tukio la kutekwa Mwenyekiti wa Chadema, Wilaya ya Temeke, Joseph Yona na matokeo yake hayajawekwa wazi.
Wanahabari nchini Tanzania jana walikuwa wanakumbuka miaka miwili ya mauaji ya kinyama yaliyofanywa na askari wa jeshi la polisi dhidi ya mwandishi wa kituo cha Chennel Ten, marehemu Daudi Mwangosi, wakati polisi hao 'wakipambana' na wafuasi wa Chadema waliokuwa katika ufunguzi wa tawi la chama hicho katika Kijiji cha Nyololo mkoani Iringa.
Lakini kutekwa na kuteswa kwa Mhariri Mtendaji wa New Habari, Absalom Kibanda pamoja na kutekwa na kuteswa kwa Mwenyekiti wa Chama cha Madaktari, Dk. Steven Ulimboka, bado kumeacha makovu mengi yasiyofutika.
Wakati katika matukio yote ya mauaji polisi ndio wanaohusika, bado jeshi hilo hilo linaibuka na kuunda tume ya kuwachunguza polisi wenzao walioua, hatua ambayo kwa ujumla inaleta mkanganyiko na ndiyo maana ninasema ni 'Tume za Manyani kuchunguza nani kala mahindi'!
Hivi inakuwaje nyani amchunguze nyani aliyekula mahindi wakati huyo huyo anayemchunguza mwenzake kesho naye atakwenda shambani kula mahindi ambayo hakuyalima? Uchunguzi huo unaweza kuwa na haki kweli?
Tumeshuhudia matukio mengi ya mauaji yanayofanywa na jeshi hilo kwa kisingizio cha kutuliza vurugu na maandamano, hasa kwenye mikusanyiko ya kisiasa.
Agosti 27, 2012 polisi wanadaiwa kuua mtu mmoja mjini Morogoro na kujeruhi wengine watatu. Haraka haraka wakaunda tume, siku mbili baadaye tukasikia ripoti yao kwamba 'eti' marehemu Ally Nzona (38) aliuawa baada ya kupigwa na kitu chenye ncha kali.
Siku sita baada ya mauaji hayo, polisi tena wakamuua Daudi Mwangosi, Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari mkoani Iringa (IPC), safari hii siyo kwa 'kitu chenye ncha kali' wala risasi ya moto, bali bomu! Wenyewe wakasema ameuawa kwa 'KITU KIZITO'.
Wakati ulimwengu ukipiga kelele huku tayari jeshi hilo likikimbilia 'kuunda tume', zikaanza tetesi kwamba eti bomu lililomuua marehemu lilirushwa na wafuasi wa Chadema, tetesi nyingine ambazo katu haziingii akilini, zikasema eti marehemu alikuwa na bomu kwenye jaketi lake! Amelitoa wapi? Na awe na bomu ili alifanyie nini? Au kamera yake ndiyo iliyogeuka bomu? Kesi hii iko mahakamani, lakini watuhumiwa wakuu - IGP mstaafu Said Mwema, aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Michael Kamuhanda, Jasusi wa Mkoa wa Iringa (RCO) na Mkurugenzi wa Operesheni Maalum, Paul Chagonja pamoja na Waziri wa Mambo ya Ndani wa wakati huo Dk. Emmanuel Nchimbi, waliokuwa wanastahili kujiuzulu na kushtakiwa kwa mauaji hayo, wako uraiani.
Tunaendelea kushuhudia mauaji mengi ya Watanzania wasio na hatia huku jeshi la polisi likifanya uzembe kwa kutumia silaha za moto kwa wananchi walio mikono mitupu, ambao wangeweza kutulizwa kwa kutumia tu mabomu ya machozi.
Lakini kutokana na askari wa jeshi hilo kuwa na uchu mkubwa wa kumwaga damu, wanaona mabomu ya machozi hayafai, na sasa wamebadili mbinu za matumizi yake, kwamba watayatumia lakini kwa kuwafyatulia wananchi moja kwa moja ili yawaue! Ni unyama wa aina gani huu? Yaani usalama wa raia umegeuka kuwa uhasama wa raia?
Mwangosi aliuawa akiwa mikononi mwa polisi waliokuwa wamemdhibiti kwa kumpa kipigo, lakini pamoja na kelele zake, pamoja na kuonekana na zana zake za kazi, bado polisi waliona kama kiumbe asiyestahili kuishi duniani na njia pekee ni kumfumua kwa bomu! Jamani, hata mbuzi tunamla nyama, lakini kamwe hatujawahi kufikiria kumcharanga mapanga ndipo tumbanike!
Huu ni mfululizo tu wa matukio mengi yanayokwenda kinyume na haki za binadamu na utawala bora, ambao Jeshi la Polisi limekuwa likiyafanya, tena kwa mfululizo, huku viongozi waandamizi wa jeshi hilo, na wahusika wenyewe wakishindwa kuwajibika.
1. Mauaji ya Mwangosi
Kama nilivyotangulia kusema hapo awali, Mwangosi aliuawa akiwa mikononi mwa polisi Septemba 2, 2012, tena akiwa hana silaha zaidi ya kamera yake, ambayo ndiyo zana yake ya kazi, huku RPC Kamuhanda akiangalia! Sijui kama alikuwa amethiriwa na damu, kwani Februari 21, 2012 akiwa RPC wa Ruvuma tulishuhudia vijana wake wakiwamiminia risasi wananchi wanne wasio na silaha, waliokuwa wakiandamana kwa amani mjini Songea. Ni Kamuhanda huyo huyo ambaye katika tukio la Songea alitamka bayana kwamba vijana wake walikuwa na haki ya kuwafyatulia risasi za moto waandamanaji hao kabla ya bosi wake IGP Said Mwema (sasa amestaafu) kuibuka na kuomba radhi kwa tukio hilo.
2. Mauaji ya raia Morogoro
Polisi wakamkamata kiongozi wa Chadema, Benson Kigaila.
Agosti 27, 2012 Polisi mkoani Morogoro wanadaiwa kumuua Ally Nzona, mtu anayedaiwa kuwa mpiga debe katika setendi ya mabasi ya Msamvu, kwa madai kwamba walikuwa wanatawanya maandamano ya Chadema.
Ripoti ya haraka ya polisi ikasema eti aliuawa kwa kitu chenye ncha kali, siyo risasi. Hawakusema nani aliyemchoma. Hili bado lina utata.
3. Mauaji ya Raia Songea
Februari 21, 2012 Mauaji ya wananchi wanne yaliyofanyika mjini Songea pamoja na wengine 41 kujeruhiwa ni sehemu tu ya uozo mkubwa na utumiaji wa mabavu unaofanywa na Jeshi la Polisi nchini. Pamoja na Said Mwema kuomba radhi na kuunda Tume, lakini hawezi kuiosha mikono yake na damu isiyo na hatia ya Watanzania waliokuwa wanapeleka kilio chao kuhusu wapendwa wao waliouawa na 'watu wasiojulikana' tangu Novemba 2011. Tunasikia kwamba watuhumiwa wanne walikamatwa kuhusiana na mauaji hayo ya kishirikiana ambao ni Johari Kassim (16), Onesmo Hinju (14), Samason Haule (22) na Mussa Fuala (20) wote wakazi wa Mtaa wa Lizaboni mjini Songea.
Polisi, kwa makusudi kabisa, waliamua kufyatua risasi za moto kwenye umati wa waandamanaji ambao siyo tu hawakuwa na silaha zozote, lakini pia walikuwa wameibeba na maiti iliyouawa kikatili na 'watu wasiojulikana' katika matukio ya imani za kishirikina.
Jambo baya zaidi, na kwa mujibu wa taarifa za wananchi wa Songea, ni kwamba, mara kadhaa walikuwa wameripoti matukio ya watu kuuawa kinyama na kunyofolewa sehemu zao za siri, lakini polisi hao wakapuuza.
4. Wapiga Nondo Mbeya
ISOME ZAIDI HAPA: http://brotherdanny5.blogspot.com/2014/09/kamanda-kova-aunda-tume-ya-manyani.html--
"Kama hawatuwekei mgombea mzuri, kwanini watutawale?" ~ Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Dar es Salaam, 1995
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/d/optout.
0 Comments