[wanabidii] SITTA AMEPUNGUKIWA SIFA SITA ZA UONGOZI

Sunday, August 10, 2014
NA ANANILEA NKYA

SITTA AMEPUNGUKIWA SIFA SITA ZA UONGOZI

Watanzania tuna bahati kubwa maana  kwa kupitia Bunge Maalum la Katiba angalao tumeweza kufahamu vema  tabia   ya Mwenyekiti wa Bunge Maalum  la Katiba  Samweli Sitta. Katika kutekeleza majukumu yake kwenye Bunge hilo Sitta amejibainisha wazi kuwa anapungukiwa sifa SITA  alizotakiwa kuwa nazo kiongozi  yeyote  katika nchi yetu ikiwa ni pamoja na   Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba. Sitta amepungukiwa sifa sita  zifuatazo.

   (1)  Uwezeshaji wa  maridhiano

Samweli Sitta ametudhihirishia kwamba hana ujuzi wala dhamira ya  kujenga maridhiano pale watu wanapotofautiana. Tumeona wazi kuwa  ameshindwa kujenga maridhiano miongoni  wa wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba kama alivyofanya Jaji Joseph Sinde Warioba kwenye Tume ya Mabadiliko ya Katiba.  Hii ni  ishara kwamba Sitta akipewa uongozi wa nchi ataipasua nchi vipande vipande hata kama angeweza  kuepuka kwa kujifunza kutoka kwa  kiongozi aliyemtangulia. Kwa mfano  angeweza kujifunza  kutoka  kwa kiongozi wetu mahiri na mzalendo wa ukweli,  Jaji Joseph Sinde Warioba ambaye aliweza kujenga maridhiano miongozi wa wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba. Hakuna ubishi kwamba wajumbe wa Tume  ya Warioba waliingia kwenye tume hiyo wakiwa vipande vipande maana walikuwa na itikadi tofauti za kisiasa, imani tofauti za dini na hata viwango tofauti vya uelewa wa masuala yanayohusu nchi yetu.  Lakini  wote waliweza kufanya kazi kubwa  tena kwa wakati na iliyopokelewa kwa kishindo cha furaha na umma wa Watanzania.  Tume iliweza kufanya kazi hiyo kwa sababu bila shaka Mwenyekiti wake hakuwa mbabe.  Akijinyenyekeza  akamsikiliza kila mjumbe na kujifunza kutoka kwao  na hivyo  akafanikiwa kujenga muafaka na ndipo tume ikaweza  kujinyenyekeza kwa wananchi  ili kusikiliza wananchi wanataka  nchi yao iendeshwe vipi.  Baada ya kukusanya maoni tume iliweza kuyachakata na kuandika Rasimu  kwa maridhiano tena bila kupiga kura. Hivyo, tume iliweza kutoa mfano wa kuigwa kwa  umma kwamba MARIDHIANO yanawezekana na yanaweza kujengwa katika kila hatua ya  mchakato wa kuandika Katiba Mpya. 

Lakini  baada ya Rasimu kufikishwa katika Bunge Maalum la Katiba na Samweli Sitta kukabidhiwa kazi  ya kuongoza Bunge hilo kuijadili na kuipitisha Rasimu hiyo, badala ya kuhakikisha kuna MARIDHIANO baina ya wajumbe yanakuwepo, tumeshuhudia akikumbatia ushabiki wa kivyama,  ubabe na unafiki  na mwishowe baadhi ya wajumbe wamesusia mchakato na  wamekataa kurejea  Bungeni. Tena  anajinasibu kwamba  Katiba itaandikwa  hata kama baadhi ya  wajumbe hawapo Bungeni.  Lo! laiti angelijua kwamba  kiongozi wa ukweli angeugua moyoni hata kama ni mjumbe mmoja tu ameudhika na kukataa  kushiriki kazi hiyo muhimu maana Katiba ni MARIDHIANO  au MUAFAKA  wa Kitaifa.  Laiti  pengine hajui  kuwa  mbabe na mnafiki hawezi kuongoza timu ikafikia maridhiano. Anapaswa kujua kwamba hata mchunga kondoo wa ukweli ikitokea  kondoo wake mmoja amebaki porini kitamuuma sana na atarudi porini kumtafuta hata kama kundi la kondoo wengine elfu moja litakuwa limerejea kwenye zizi.

(2) Ujasiri wa kutetea nchi na wananchi

Kupitia kazi muhimu  aliyopewa ya kuongoza Bunge Maalum la Katiba tumeshuhudia jinsi anavyoweka mbele maslahi yake binafsi na ya chama chake  badala ya maslahi ya  wananchi na nchi yetu, TANZANIA. Mfano alivunja kanuni za Bunge Maalum la Katiba na kumpotosha   Rais  wetu kutoa maoni  yake Bungeni badala ya kufanya kazi yake kama mkuu wa nchi ya  kufungua Bunge hilo. Hapa Sitta alipaswa kuonyesha ujasiri  kwa kumshauri  Rais kufanya alichotakiwa kwa wakati husika. Kwa kutokuwa na ujasiri wa kumshauri Rais kwa upendo  na ukweli ameweka wazi kwamba hana chembe ya ujasiri wa kutetea wananchi na nchi yetu. Amedhihirisha kwamba yeye anaweka mbele zaidi  maslahi yake binafsi na dirisha lake analopitia kutafuta uongozi (chama chake cha siasa) naanasahau kwamba Tanzania ni kiubwa kuliko sisi sote.

 (3)  Kulinda maadili na utamaduni wa Mtanzania

Kwa kipindi chote alichoongoza Bunge Maalum la Katiba tumeshuhudia jinsi alivyokaa kimya huku baadhi ya wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba  wakirushiana  matusi  ya nguoni. Aidha alikaa kimya pia hata pale baadhi ya wajumbe wa Bunge hilo walipomtukana, kumbeza na kumdhihaki Mwenyekiti wa Tume ya mabadiliko ya Katiba Jaji Joseph Sinde Warioba. Watu makini wanaamini  kwamba  waliomtukana na kumbeza Jaji Warioba  waliwabeza na kuwatukana pia Watanzania wote,   Tanzania na Rais wetu aliyeiteua tume hiyo kufanya kazi. Bunge Maalum la Katiba limeacha sifa mbaya sana kwa jamii kuwa viongozi wanawake na wanaume  wanaweza kusimama hadharani na kuporomosha matusi ya nguoni. Lakini ni wazi kuwa kama Sitta angekuwa ni mtu anayejali na kuthamini maadili ya taifa letu, angalao angekemea  wajumbe waliokuwa wanaporomosha matusi na hata ikibidi kuwachukulia hatua za kisheria.

 

 

4) Kuheshimu uhuru wa  kujieleza

Tumeshuhudia  Samweli Sitta  akivinyooshea kidole vyombo vya habari hasa  televisheni na redio  za kitaifa kwa  kutangaza midahalo kuhusu Rasimu ya Pili ya Katiba Mpya. Alijidhihirisha zaidi  hasa pale Tume ya Mabadiliko ya Katiba ilipotokeza hadharani kusahihisha upotoshaji  mkubwa uliokuwa unafanywa  kimkakati  na wahafidhina wa mabadiliko kuhusu Rasimu ya Pili ya  Katiba Mpya.  Mtu  huyu akipewa uongozi wa nchi siyo tu kwa kukosa uvumilivu katika kukuza demokrasia, ataweza kuvifungia  vyombo vya habari ambavyo vitakuwa vinakosoa uwajibikaji wa serikali,  bali pia hata kufuta  usajili  wa mashirika ya kijamii yatakayokosoa utendaji wa viongozi wa nchi na pengine  hata vyama vya siasa vya upinzani. Kiongozi wa namna hii ni mtu hatari kwa amani na maendeleo ya nchi yetu. 

(5) Kukubali mabadiliko.

Mtu yeyote ambaye anaogopa mabadiliko chanya ni mtu hatari maana bila mabadiliko ya kimfumo na kifikra  nchi yetu haiwezi kupata maendeleo ya kweli kwa zama hizi mpya.   Rasimu ya Pili ya Madadiliko ya Katiba kwa mujibu wa Jaji Warioba ikipitishwa italeta mabadiliko makubwa ya kimfumo na kiuongozi   na hivyo maendeleo makubwa nchini. Lakini kwa jinsi  Sitta alivyokimbilia kubadilisha kanuni za Bunge  Maalum la Katiba  katika awamu hii ya pili inadhihirisha wazi kuwa amedhamiria kabisa kukwamisha kwa makusudi  mabadiliko chanya katika nchi yetu ambayo yangeletwa na Katiba Mpya iliyotokana na maoni ya wananchi. Hii inadhihirisha kwamba  Sitta anakumbatia uafidhina na waafidhina  wanaodhani kuwa wao ni wakubwa kuliko nchi yetu.

 (6) Hana huruma  kwa wananchi

Sitta anajuwa wazi kwamba Katiba Mpya itakayokubalika na kuheshimiwa na umma mpana wa wananchi  haiwezi kupatikana bila maridhiano  ya kitaifa. Lakini tumemuona aking'ang'ania  Bunge Maalum la Katiba liendelee hata pale  wajumbe kadhaa wa Bunge hilo akiwepo Naibu Waziri wa Fedha  Mwingulu Mchemba alipoinuka kwa ujasiri akamshauri  kwamba tathmini ifanyike kwanza kuona kama  theluthi mbili inayotakiwa kupitisha vifungu vya Katiba hiyo inafikiwa.  Endapo haifikiwi Bunge lisitishwe maana ni likiendelea  ni sawa na kubariki kupoteza mabilioni ya fedha za kodi za  wananchi  ambao wanakabiliwa  na hali  duni ya maisha.  Yeye Sitta kwa ubabe alishupaa na kusema theluthi inayotakiwa ipo na  walioko nje watakuja tu.! Je  kama ikibainika theluthi hiyo haipo na wasiokuwepo wasipokuja atalipa fedha za umma ambazo kila mjumbe  wa Bunge hilo Maalum la Katiba anayehudhuria  kikao cha sasa atakuwa ameweka mfukoni mwake zaidi ya shilingi milioni 25 ili hali wananchi wengi wakiwa hawana hata uwezo wa kula milo miwili kwa siku?

Hivyo, sisi wananchi  tunapotafakari  tunaona kwamba  endapo nchi yetu itakuwa imekwama kupata Katiba Mpya iliyotokana na maoni ya wananchi,  Mwenyekiti wa Bunge Maalum la katiba Samweli Sitta ndiye wa kubebeshwa lawama zote .

--
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/d/optout.

Share this :

Related Posts

0 Comments