chachari
NIANZE makala hii kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuiwezesha Tanzania yetu kufika salama siku ya kupiga kura katika Uchaguzi Mkuu na hatimaye uchaguzi huo kufanyika kwa amani na usalama kwa kiasi kikubwa. Ni rahisi kudhani kilichotokea ni jambo dogo pengine kwa vile tumeshazoea kuona chaguzi takriban zote zikifanyika kwa amani na utulivu.
Lakini tukifumbua macho na kuangalia japo kwa baadhi ya majirani zetu tu, tutatambua kuwa tumefanikiwa katika mtihani mkubwa sana.
Pili niwapongeze Watanzania wenzangu ambao licha ya tofauti za kiitikadi, kwa kiasi kikubwa mmetanguliza maslahi ya taifa letu, kwa kutumia haki zenu za kidemokrasia bila kuwakwaza wale mnaotofautiana nao kiitikadi.
Japo katika wakati wa kampeni, baadhi yetu tuliandamwa na matusi kwa vile tu tulionekana kutofautiana kimtimzamo na wenzetu, lakini kwa ujumla ninaamini uchaguzi huu umeikumbusha dunia kuhusu asili na silika ya Watanzania katika kujali na kuenzi amani na utulivu.
Hadi wakati huu ninapoandika makala hii, Chama cha Mapinduzi (CCM) na mgombea wake Dk. John Magufuli wanaoongoza kwa kura nyingi. Binafsi sijayapokea matokeo hayo kwa mshangao kwa sababu siku chache kabla ya uchaguzi huo, nilibandika 'ubashiri' wangu huko mtandaoni. Nilibashiri mambo sita: Kwanza, Magufuli na CCM watashinda kwa wastani wa asilimia 60.
Pili, kwa matokeo hayo maana yake Ukawa na mgombea wake, Edward Lowassa watashindwa, kwa maana ya idadi ya kura za jumla za urais, ubunge na udiwani.
Tatu, nilibashiri Chadema kupoteza viti vingi zaidi (japo dalili zaashiria nimekosea katika hili). Nne, nilibashiri kuwa kufuatia kushindwa kwa Lowassa na Ukawa kwa ujumla, viongozi wakuu wa Chadema – Mbowe - na NCCR- Mageuzi –James Mbatia, aidha watajiuzulu nyadhifa zao au watafukuzwa.
Tano, nilibashiri migogoro katika vyama hivyo viwili ambayo hatimaye itavidhoofisha. Na sita, nilibashiri, ACT- Wazalendo kuja kuwa chama kikuu cha upinzani.
Hadi hapo matokeo yote ya jumla yatakapotangazwa, huo unabaki kuwa ubashiri tu. Pasi haja ya kurejea niliyokwishayaandika kwa muda mrefu, ushindi wa CCM, pamoja na mambo mengine, unachangiwa na ukweli kwamba tukiweka kando suala la vyama vinne kushirikiana na kusimamisha mgombea mmoja kwa mwamvuli wa Ukawa, jambo ambalo ni la kihistoria katika siasa zetu, na tukiweka kando ukweli kuwa mgombea wa kambi kuu ya upinzani, Waziri Mkuu wa zamani, Lowassa, alihama kutoka CCM, pamoja na Waziri Mkuu mwingine wa zamani, Frederick Sumaye, takriban mazingira mengine yote ya uchaguzi huo yalibaki kuwa yale yale kama ya miaka iliyopita.
Na ndio maana baadhi yetu tulikuwa tukiwakumbusha 'wana-mabadiliko' kwamba kuwa na matarajio makubwa katika uchaguzi unaofanyika katika mazingira yale yale ambayo kila mara wanashindwa ni sawa na kusoma kitabu cha hadithi hadi mwisho na kurudia kukisoma tena kwa matarajio kuwa kitakuwa na hitimisho tofauti na la awali.
Kwa vile hadi wakati ninaandika makala hii, Tume ya Uchaguzi haijatangaza rasmi matokeo yote, ni vema kutoendelea kuandika kwa hisia, na kuangalia masuala mengine yanayohusiana na uchaguzi huu. Moja ya masuala yaliyoonekana kuwagusa Watanzania wengi, hususan waliopo mtandaoni, ni jinsi baadhi ya vyombo vya habari vya kimataifa vilivyoonekana kuwa na kiu ya kushuhudia vurugu katika uchaguzi huo.
Hadi muda huu, baadhi ya vyombo hivyo vya habari vimeendelea kuripotiwa katika hali inayojenga picha kuwa hali si shwari huko nyumbani.
Lakini kana kwamba hiyo haitoshi, Ukawa kupitia kwa mshauri wao wa kimataifa, Joe Trippi, wanapaswa kushutumiwa vikali kwa jitihada zao za makusudi kujenga picha nje ya Tanzania kuwa hali si shwari katika uchaguzi huo. Japo ninatambua haki yao ya kikatiba kulalamikia kasoro zilizojitokeza, lakini si katika namna inayoweza kuchochea vurugu.
Majuzi, Trippi, mshauri wa masuala ya siasa nchini Marekani,aliweka picha ya uongo kwenye mtandao wa kijamii ya twitter akidai kuwa inathibitisha vurugu zinazoendelea huko Zanzibar. Hata hivyo, picha hiyo ilipigwa wakati wa vurugu za uchaguzi huko Visiwani mwaka 2005. Hata kama lengo la Mmarekani huyo lilikuwa kuifahamisha dunia kuwa kuna vurugu za hapa na pale, kutumia picha isiyo sahihi lilikuwa jambo lisilo na busara hata kidogo.
Kwa umoja wao, Watanzania huko twitter waliungana kumbana mshauri huyo na kuanzisha hashtag #StopJoeTrippi ambayo ilivuma kwa muda mwingi jioni ya Jumatatu iliyopita. Hatimaye, Trippi aliiondoa picha hiyo lakini hadi ninaandika makala hii ameonekana kutokuwa tayari kuomba radhi kwa kosa hilo.
Lakini pengine japo ni sahihi kumlaumu Mmarekani huyo, kwa kiasi kikubwa alichokuwa akiandika alikuwa akipatiwa na Ukawa. Kwa hiyo, laiti lolote lingejitokeza kutokana na 'tweets' za Trippi, basi Ukawa wasingeweza kuepuka lawama.
Nimalizie makala hii kwa ahadi ya kuandika makala nyingine ndefu katika toleo lijalo ambapo ninatumaini tutakuwa tumeshapata matokeo kamili ya uchaguzi huu. Kwa wakati huu, ninaendelea kuwakumbusha Watanzania wenzangu kuwa 'kuna msiaha baada ya uchaguzi.' Tusifarakane kwa vile tu 'mgombea wangu kushindwa.'
Tanzania yetu ni muhimu zaidi ya uchaguzi au wanasiasa wetu. Kadhalika, wakati tutakuwa na chaguzi kadhaa huko mbeleni, na hivyo kuwa na fursa nyingine ya kurekebisha makosa, tukiipoteza Tanzania yetu, kamwe hatutopata fursa nyingine ya kuwa na nchi tuliyonayo leo.
Mungu Ibariki Tanzania –
Chanzo Raia Mwema 28/11/2015
0 Comments