[wanabidii] Nilichokisema jana kutokana na kauli ya Mhe. LOWASSA.

Wednesday, May 27, 2015
(Ndugiu hii nimecopy tu kama ilivyoandikwa na mwenyewe)

Nilichokisema jana kutokana na kauli ya Mhe. LOWASSA.

Mimi nilianza kushiriki siasa toka nikiwa mdogo sana. Kuanzia Chipukizi, Greenguard wa UVCCM na baadaye UVCCM. Miaka ya mwanzo ya 90 nilivutiwa sana na mijadala ya mfumo wa vyama vingi ama kimoja. Nakumbuka, binafsi nilivutiwa zaidi na mfumo wa kutanua demokrasia, nakumbuka nilichangia hoja zangu kwenye mkutano wa tume pale Nzega mjini, viwanja vya parking pembeni ya jukwaa.

Wengi kwa hakika hawakuunga mkono mfumo wa vyama vingi. Waliamini katika chama kimoja. Nilijiunga rasmi CCM mwaka 1994. Mwaka 2005, niligombea Ubunge wa Jimbo la Nzega, kura hazikutosha kwenye mchakato wa maoni ndani ya CCM na vikao vilisema kuwa wakati wangu bado.

Niliendelea kufuatilia kwa ukaribu sana kilichokuwa kinaendelea kwenye duru za siasa. Mijadala ya Bungeni ilikuwa ya moto sana, mara nyingine ikitutia simanzi sisi vijana wa CCM haswa namna tulivyokuwa tukishuhudia wabunge wachache sana wa upinzani wakiishambulia serikali yetu ya CCM kuhusiana na wimbo mpya kwenye duru za siasa za miaka hiyo, 'ufisadi'. Ufisadi ikiwa ni order of the day.

Ufisadi ikiwa ni mtaji na ajenda kuu ya wapinzani Bungeni, of-course pia ajenda ya kikundi kidogo cha wabunge wa CCM waliojitambulisha kama vinara wa kupinga ufisadi. Miaka hiyo kila mtu akiuchukia ufisadi na mafisadi.

Mwaka 2008, mimi nikiwa kijana mwana mabadiliko na ninayechukia ufisadi na mafisadi, kama walivyokuwa vijana wenzangu wengi, kwenye duru za siasa na nje ya duru za siasa, nilivutiwa na mijadala iliyokuwa Bungeni kutokana na hoja iliyowasilishwa bungeni na Dr. Harrison George Mwakyembe kuhusiana na mchakato wa kununua umeme wa dharura, na zabuni hiyo kupewa kampuni ya Richmond Development Company LLC ikidaiwa kuwa mchakato huo ulikuwa na ubatilifu na mazingira ya rushwa ndani yake.

Nikiwa kama mwananchi mwenye strong affinity na siasa, uongozi na namna nchi yetu inavyoendeshwa, nilivutiwa sana na namna wabunge wengi wa CCM walivyoamka na kuonesha kwa dhati ya mioyo yao namna walivyokerwa na ufisadi wa Richmond. Nakumbuka Mbunge wangu Lucas Selelii alikuwa kinara mmojawapo.

Mwanzoni sikutarajia kama Waziri Mkuu niliyempenda sana na kumuamini, niliyemtazama kama kiongozi wa mfano kwangu, aliyenivutia sana kwa namna alivyokuwa akichapa kazi na akitoa kauli za straight forward kwenye mambo mengi ya msingi, akikemea uzembe, akiadhibu wabadhirifu bila soni wala huruma, akifika kila kona ya nchi ambapo akitokea tu, basi wazembe na wabadhirifu wanaangusha angusha karatasi hovyo, Mhe. Edward Ngoyai Lowassa eti naye angehusishwa kwa namna yoyote ile! Sikuamini. Lakini sikuamini zaidi niliposikia anajiuzulu...tena eti kwa sababu ya Richmond.

Nakumbuka sana kwenye duru za siasa yeye na Mjomba wangu Mhe.Jakaya Kikwete walipochukua fomu za kuwania Urais mwaka 1995, wakiwa na ujana ujana mwingi na sisi tukiwashangilia na kuwapenda kama inspirational figures wetu. Na ilipotokea mwaka 2005 alipoingia Mjomba, nilijua wazi kabisa kuwa Waziri Mkuu angekuwa Mhe. Lowassa, na tulitabiri kipindi kile kuwa Mhe. Lowassa angekuwa Rais baada ya kumaliza kipindi cha Uwaziri Mkuu, yaani 2015.

Nilisimamisha kagari kangu maeneo ya Biafra na kukimbia kwenye Pub moja pale jirani kutazama televisheni iliyokuwa inarusha kutoka Bungeni, nakumbuka watu walijaa kwa wingi sana na wengi wakishangilia kuonesha kufurahishwa kwao namna serikali ilivyokuwa ikiwajibika Bungeni. Sikuamini. Serikali imeanguka! Lowassa out. Sikuamini kabisa.

Jana nikapata habari kuwa Mhe. Edward Lowassa amezungumza na wahariri wa vyombo vya habari nchini - amekana kuhusika kwake na Richmond. Nikashtushwa sana na hili.
Nikajiuliza hivi ni nini kinataka kutokea kwenye siasa za nchi yangu? Mjadala wa Richmond ulifungwa Bungeni miaka 7 iliyopita, je inabidi ufunguliwe upya, na watu wapya tutafakari upya? Maana kuna minong'ono kuwa Mhe. Lowassa anataka kuwania Urais mwaka 2015, na ana mpango wa kutangaza nia muda si mrefu. Nikajiuliza, ni kwa nini imemchukua Mhe. Lowassa zaidi ya miaka saba kujibu hadharani kuwa hakuhusika na Richmond?

Kwa nini anatamka maneno haya leo na kwa nini hakujitetea Bungeni siku ile alipojiuzulu? Nakumbuka siku ile alisema tatizo ni uWaziri Mkuu, kwa nini hakufafanua na alikuwa na fursa hiyo kama 'primus inter pares (first among equals)?' Kipindi fulani alisemekana kuwa ni 'gamba' na lingepaswa kuvuliwa...likaishia kiunoni! Ni kwa nini halikuvuka? Maswali haya sijawahi kuyapatia majibu.

Hivi ilikuwaje Rais wa Nchi, ambaye ni Mwenyekiti wa CCM, Kamati ya Wabunge Wote wa CCM Bungeni, na mamlaka zote za kiserikali kushindwa kumlinda Waziri Mkuu wake dhidi ya tuhuma za kuhusika kwake kwenye Richmond mwaka 2008?

Maana kwenye siasa za mabunge yanayofuata mfumo wa Westminster, Waziri Mkuu ni 'primus inter pares', kwamba ana fursa ya kwanza ya kuzungumza kwenye mijadala Bungeni na ana-enjoy nguvu ya kuwa na majority bungeni kuendesha mambo ya serikali na kutawala mijadala na maamuzi.

Ilikuwaje Chama kilimuacha Waziri Mkuu wake akaanguka? Ilikuwaje? Maswali: je kulikuwa na ukweli dhidi yake kuhusiana na tuhuma za Kamati? Ama Kamati ilitumika vibaya na mahasimu wake? Yeye amekana, sasa wanakamati inabidi wamjibu watuweke wazi, na wamjibu kwa uwazi bila kuficha, maana kama alionewa ijulikane na sisi tuliohuzunishwa ama kufurahishwa na Bunge wakati ule tuujue ukweli. Yeye anasema hakuhusika na ndiyo maana Kamati ya Mwakyembe haikuona haja ya kumwita kumhoji. Ukweli tunauhitaji sana leo kuliko jana. Ukweli huu ni haki yetu.

Kama Kamati ilimuonea, basi imuombe radhi na ituombe radhi watanzania wote. Kama kweli Mhe. Lowassa atagombea Urais Twentyfifteen, itakuwaje kwenye mijadala ya uchaguzi na CCM itasimamaje (kama itampitisha kuwa mgombea) kumuombea kura wakati ilimuangusha Bungeni kutoka kwenye nafasi nyeti ya Uwaziri Mkuu? CCM itatoa majibu gani kuhusu kwa nini ilimuita 'gamba' na ikatangaza hadharani kuanza mchakato wa kuvua magamba (ambao haukukamilika).

Nilisema jana, Mhe. Lowassa amefungua pandora box, na kama atatangaza kweli kuwania Urais, inabidi haya mambo yawekwe wazi, yamalizwe, maana hauwezi jua ya kesho - ikitokea akawa mgombea wetu, tutaanzia wapi kumnadi na kusema ni mtu safi, muadilifu, anayechukia rushwa na ubadhirifu na kwamba anafaa kuwa Rais, wakati juzi tulisema hafai kuwa Waziri Mkuu na tukamtoa?

Nilisema jana kuwa , CCM haipaswi ku-risk kuteua wagombea wenye mambo mengi ya kutolea maelezo kwa wananchi, ikifanya hivyo itaangushwa asubuhi ya saa nne. Watanzania wa leo siyo wa juzi

Imeandikwa na HKigwangalla

--
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com

Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma

Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/d/optout.

Share this :

Previous
Next Post »
0 Comments