Na Ananilea Nkya
Uchaguzi wa kumpata Rais wa Tanzania mwaka huu umeanza kwa kuvunja kanuni na Katiba ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na huenda ukamalizikia kwa kuvunja Katiba ya nchi na sheria ya uchaguzi hapo tarehe 25 jumapili ijayo Oktoba 2015 kama kauli ya Rais Jakaya Kikwete kuwashughulikia wananchi watakaoamua kukaa karibu na vituo vya kupigia kura itatekelezwa.
Hii itakuwa ni aibu kwa nchi yetu inayojinasibu kuwa inazingatia demokrasia katika kupata viongozi wake.
Kadhalika kama taifa tutakuwa tumeudhihirishia ulimwengu kwamba kwenye suala muhimu ya kupata rasilimali uongozi ya kuchochea maendeleo ya nchi yetu, tuko tayari kuvunja Katiba, Sheria na Kanuni kulinda maslahi ya kikundi kidogo cha watawala waliojitajirisha kufuru huku mamilioni wakibaki mafukara.
Mmoja wa wanaCCM wakongwe Mzee Kingunge Ngombale Mwiru, kitendo cha kuvunjwa kwa Kanuni na Katiba ya CCM wakati wa uteuzi wa mgombea Urais kimemuudhi kiasi cha kuamua kuondoka CCM, chama ambacho amekitumikia kwa miaka 61 tangu kikiwa vyama viwili TANU na ASP.
Siku Kingunge alipoondoka CCM tarehe 4 Oktoba 2015 aliliambia taifa kwamba, tofauti na chaguzi nyingine katika historia ya nchi yetu, Kanuni na Katiba ya CCM vilivunjwa wakati wa mchakato wa kumpata mgombea Urais wa chama hicho—mchakato ambao ulimuibua Dr John Magufuli kuwa mgombea Urais kwa tiketi ya CCM.
WanaCCM wengine mashuhuri waliowahi kuitumikia nchi katika nyadhifa mbali mbali ambao wameondoka CCM kwa kuchukizwa na kuvunjwa Kanuni na Katiba ni Mawaziri wakuu wastaafu Fredrick Sumaye na Edward Lowassa, Waziri wa Mambo ya Ndani Mstaafu Lawrence Macha na Balozi Juma Mwapachu.
Aidha Mwapachu amesema hata Baba wa Taifa Julius Nyerere angekuwa hai asingevumilia kilichofanyika ndani ya CCM mwaka huu—viongozi kwa makusudi kuvunja Katiba na Kanuni, hivyo naye angejiondoa kwenye chama hicho.
Aidha walioshuhudia mazingira halisi yalivyokuwa pale Dodoma waliona vyombo vya dola vilikuwa vimewekwa katika hali ya tahadhari kama vile nchi ilikuwa iko vitani!
Ilikuwa tofauti kabisa na chaguzi za miaka ya nyuma ambazo kumpata mgombea Urais kwa tiketi ya CCM lililikuwa ni tukio la amani na lenye shamrasha na vyombo vya dola kamwe havikutumika kuwatisha wananchi kana kwamba nchi imevamiwa kivita.
Kadhalika tuliona Watanzania walivyotahadharishwa kuwa kwa wale ambao hawakuwa wanahusika na vikao vya CCM kumpata mgombea, hata kama mtu alikuwa shughuli muhimu huko Dodoma alizuiliwa asiende asithubutu kufika Dodoma eti kuepusha kuhatarisha maisha yake.
Tujiulize: Ni kwa nini CCM na serikali yake waliamua mchakato wa kumpata mgombea Urais kwa tiketi ya CCM mwaka huu kufanyika katika hali ya tahadhari kama vile nchi ilikuwa vitani na hivyo wananchi hawakupaswa kufika karibu na uwanja wa vita?
Moja kati ya majibu ya swali hili ni kwamba ni kwa vile watawala na wahafidhina ndani ya CCM walikuwa wanajuwa kuwa mchakato huo ungehusisha ubakaji wa demokrasia kwa kuvunja Kanuni na Katiba ya CCM.
Hivyo kuwazuia watu wengi (wapambe wa watia nia 38) wasiende Dodoma kushuhudia mchakato wa kumteua mgombea ilikuwa ni mkakati wa kufanikisha lengo la watawala na wahafidhina wa CCM bila kulazimika kuingia kwenye mapambano na wafukarishwa.
Mapambano hayo yangekuwa kati watawala wenye vyombo vya dola na wananchi wanaCCM ambao wangejaribu kufurukuta kupinga ubakaji wa demokrasia kwa kutumia uvunjaji wa Kanuni na Katiba yao.
Uvunjaji wa Kanuni na Katiba ya CCM ilikuwa ni jinai ambayo ingeanzisha mapambano kati ya watawala na watawaliwa (katika ngazi ya chama---CCM).
Watawala katika nchi yetu wamejitajirisha kufuru kwa fedha na mali za nchini ikiwa ni pamoja na kujigawia nyumba za umma zenye thamani ya mabilioni ya fedha wakati mamilioni ya wananchi wakiwepo wanaCCM wengi wakiwa wamebaki maskini wa kutupa na sasa wanataka mabadiliko ya uongozi wa nchi yao.
Hata hivyo, ingawa serikali ilitumia vibaya vyombo vya dola kuogofya wanaCCM (nguvu ya umma) kufurukuta kuzuia uvunjaji huo wa Kanuni na Katiba ya CCM katika kumpata mgombea Urais, sauti ya umma wa wanaCCM ilichomoza kiaina katika moja ya vikao.
Sauti hiyo ya umma ilichomoza wakati viongozi wakuu wa chama hicho walipokuwa wanaingia kwenye ukumbi wa mkutano walipokutana na sauti kumbwa iliyowakilisha wafukarishwaji ikiimba: ''Tuna imani na Lowassa…oya, oya, oya. Lowassa kweli, kweli, kweli kweli Lowassa''.
Edward Lowassa alikuwa ni mmoja wa kati ya watia nia 38 na alionekana kukubalika zaidi siyo tu na wanaCCM bali pia nje ya chama hicho.
Kingunge anasema Baba wa Taifa aliwaasa wanaCCM kwamba wakati wa kumtafuta mgombea Urais kwa tiketi ya chama hicho ni lazima wazingatie kuteua mtu anayekubalika ndani na nje ya CCM.
Kukubalika kwa Lowassa ndani na nje ya CCM kumedhibidhishwa pia na Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Freeman Mbowe.
Mbowe amesema siku za nyuma kabla CCM kuingia kwenye mchakato wa kumpata mgombea wake wa Urais, CHADEMA ilikuwa imefanya utafiti na kubaini Lowassa alikuwa anakubalika zaidi kwa wananchi kuliko mwanasiasa mwingine na kungeisumbua CHADEMA katika kushinda uchaguzi mwaka huu iwapo CCM ingemteua Lowassa kuwa mgombea wao.
Aidha kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi yetu, vyama rafiki wa CCM kutoka nje ya nchi hawakualikwa kushuhudia mkutano mkuu wa CCM ulivyokuwa unamchagua mtu wa kugombea nafasi muhimu ya uongozi katika nchi ---Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Tunapaswa kujiuliza ni kwa nini Mwenyekiti wa CCM ambaye pia ni Rais wa Jamhuri, katika uchaguzi wa mwaka huu iliamua kutoalika vyama marafiki kutoka nje ya nchi kushuhudia mchakato huo kama ilivyokuwa kawaida katika chaguzi zilizotangulia tangu utawala wa chama kimoja hadi vyama vingi?
Kimsingi kwa mtu anayefikiri sawa sawa atabaini kuwa sababu mojawapo ilikuwa ni kuogopa chama hicho kujifedheesha mbele ya mataifa kwa sababu viongozi walikuwa wamepanga kutumia nguvu kuvunja Kanuni na Katiba ya chama kutimiza matakwa yao kinyume na hitaji la demokrasia.
Muhimu, kuvunjwa kwa Kanuni na Katiba ya CCM katika kumpata mgombea Urais ikikuwa ni mbinu chafu ya watawala na wahafidhina wa CCM wanaotaka kuzuia mabadiliko ya uongozi wa nchi katika uchaguzi wa mwaka huu—mabadiliko ambayo yanaongozwa na mamilioni ya wananchi waliochoka na umaskini huku wakiwaona viongozi wao wakiwa matajiri kufuru.
Kuvunjwa kwa Kanuni na Katiba ya CCM ilikuwa ni sehemu ya siasa za maji taka zilizolenga kuhadaa Watanzania kwamba eti CCM na serikali yake siyo fisadi ila fisadi ni Edward Lowassa.
Hivyo kauli ya Rais Kikwete ambayo Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Jaji Damiani Lubuva na Msajili wa Vyama vya Siasa Jaji Fransis Mutungi wanaishabikia ni muendelezo wa siasa za maji taka zenye lengo ovu.
Lengo hilo ovu ni kutengeneza kuvugu—mapambano kati ya vyombo vya dola na wananchi siku ya uchaguzi tarehe 25 jumapili ijayo Oktoba 2015.
Siku hii, kwa tafsiri ya kauli aliyoitoa Rais Kikwete huko Dodoma – vyombo vya dola kupambana na wananchi watakaokuwa karibu na vituo vya kupigia kura.
Huu utakuwa ni ni mwendelezo wa azma ya serikali ya Kikwete na waafidhina wa CCM kuvuja Katiba na Kanuni ya CCM na sasa kuvunja Katiba ya Jamhuri ya Muungano na sheria ya uchaguzi—ili wafanikiwe kubaka demokrasia kupora Watanzania haki ya kuchagua viongozi wao.
Watafanyaje kufanikisha hili? Hii ni kazi rahisi. Vyombo vya dola vitaanzisha vurugu—kuwapiga mabomu wananchi watakaokuwa wamekusanyika mita 200 nje ya vituo vya kupigia kura.
Vyombo vya dola vitadai kuwa vinatekeleza amri haramu ya Rais kuwataka wananchi wasidhubutu kutumia haki yao kissheria kufuatilia upigani kura, uhesabuji kura na utangazaji wa matokeao---hatua muhimu ambayo vyama vya upinzani vimeuita ni 'ulinzi wa kura'.
Katikati ya vurugu hizo, kutakuwa ni mwanya wa wawakala wa watawala na wahafidhina wa CCM kutimiza azma yao kumpatia ushindi mgombea wao kwa kutumia 'goli la mkono' (wizi) kwa kuchezea sanduku la kura.
Lakini je serikali itafanikiwa kutumia polisi na/au jeshi kudhibiti umma ulioamua kubaki karibu na vituo vya kupigia kura kufuatilia upigani kura, uhesabuji kura na utangazaji wa matokeo (kulinda kura)?
Pengine serikali ya Rais Kikwete na waafidhina wa CCM wanapaswa kujua kwamba ingawa walivunja Kanuni na Katiba ya CCM katika kumteua mgombea Urais kwa tiketi ya CCM na kufanikiwa kudhibiti nguvu ya umma (wanaCCM ) kuanzisha mapambano kule Dodoma, ni hatari kutumia mkakati huo siku ya kura tarehe 25.
Hii ni kwa sababu kudhibiti nguvu ya umma wa wapiga kura mafukara nchi nzima unaofahamu kuwa sheria ya uchaguzi inawapa haki ya kukaa kwa amani mita 200 kutoka kituo cha kupiga kura, serikali itakuwa imeamua kuwa chanzo cha kuvunja amani na umwagaji damu mkubwa katika uchaguzi wa mwaka huu.
Zaidi kama vyombo vya dola vitakuwa vimekubali kutumika kutimiza azma hii ovu ya watawala wachache waafidhina wa mabadiliko itakuwa ni balaa kwa nchi yetu kwani watu wengi wataumia na pengine kufa.
Huu utakuwa siyo uchaguzi wa kidemokrasia, bali mapambano ya kivita katika nchi ambayo hata uhuru wake kutoka kwa wakoloni haukuhusisha umwagani wa damu hata tome moja.
Kadhalika amani ya nchi iliyotokana na haki kutendeka kwenye uchaguzi itakuwa imechezewa kwa kumpata mkuu wa nchi kwa kipindi cha miaka mitano kwa kuvunjwa Kanuni na Katiba ya CCM na kuvunjwa kwa Katiba ya Jamhuri yetu na sheria ya uchaguzi.
Je hali hii itaiacha Tanzania salama katika umoja na amani au nchi itapasuka vipande kama CCM ilivyopasuka baada ya kumalizika kwa mchakato wa kumpata mgombea wa Urais kwa kuvunjwa Kanuni na Katiba ya chama hicho? Tafakari na chukua hatua kuepusha balaa hilo. Mungu ibariki Tanzania.
Note: Naridhia mwenye kutaka kusambaza au kuchapisha andiko hili afanye hivyo.
@@@@@@@@@@@@@@@@@
Ananilea Nkya
E-mail:ananilea_nkya@yahoo.com
--
Unapokea Email hizi kwa sababu umejiunga na Jukwaa la 'Mabadiliko'.
Kuchangia mada tuma kwenye Email hii: mabadilikotanzania@googlegroups.com
For more options, visit this group at:
http://groups.google.com/group/mabadilikotanzania?hl=en?hl=en
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Mabadiliko Forum" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to mabadilikotanzania+unsubscribe@googlegroups.com.
To post to this group, send email to mabadilikotanzania@googlegroups.com.
Visit this group at http://groups.google.com/group/mabadilikotanzania.
To view this discussion on the web visit https://groups.google.com/d/msgid/mabadilikotanzania/1445185443.78869.YahooMailBasic%40web163904.mail.gq1.yahoo.com.
For more options, visit https://groups.google.com/d/optout.
0 Comments