Waislamu nchini kwa muda mrefu wamekuwa wakidai kuwepo na Mahakama ya Kadhi katika Tanzania itakayoangalia na kushughulikia mambo maalum ambayo yanajumuishwa zaidi na Sharia za Kiislamu kuliko Sheria za Mahakama za kawaida.
Ukweli kwamba tayari ipo Mahakama ya Biashara (Uchumi), ni uthibitisho tosha kwamba mambo maalum (ya aina moja) yanahitaji kushughulikiwa na Mahakama maalum ambayo vitabu vya Sheria vya kawaida huyafafanua kwa nadra (uchache).
Hata hivyo, tayari inakubalika kimsingi kwamba hakuna utata katika suala hili, kwani Rais Benjamin Mkapa ameshasema atayashughulikia matatizo yote yanayowakera Waislamu na kuhakikisha kuwa Waislamu wote nchini hawajisikii kunyanyaswa kwa vile sera ya Chama tawala (Serikali) ni Usawa miongoni mwa Wananchi wake, bila kujali jinsia, rangi (Utaifa), au Dini.
Kwa mantiki hii, mapendekezo kadhaa yanatolewa kuisaidia Mahakama ya Kadhi iweze kufanya kazi zake kwa ufanisi na kupatikana madaraka kamili ya kisheria ya Mahakama ya Kadhi.
Ili Mahakama iweze kupata hadhi yake, haya ni mapendekezo ambayo yangeweza kusaidia kufikia lengo hilo.
Mswada unalenga kuanzishwa kwa Mahakama ya Kadhi katika kila Wilaya ya Tanzania, ili kuangalia mambo yote yahusianayo na Sharia ya Kiislamu katika masuala ya Ndoa, talaka, haki ya kulea watoto, mgawanyo wa mali, Urithi n.k. pale ambapo wahusika wa utata huo ni Waislamu, waliooana kwa mujibu wa sharia na desturi ya ndoa za Kiislamu.
Ukweli ni kwamba makusudio ya mswada huu ni mazuri, lakini upo uwezekano mkubwa kwamba kutokana na ukosefu wa Kitabu makhususi cha Sheria za Kiislamu, Makadhi katika wilaya mbali mbali wakifikia kwenye uamuzi wa kesi zinazofanana, wanaweza wakatoa hukumu zinazopingana.
Hivyo, upo umuhimu wa kukiandaa kitabu makhsusi kitakachotumika kama Mwongozo wa Makadhi ili kuiepuka migongano.
Hapo zamani mwaka 1964, Bunge la Tanganyika kwa wakati huo lilipitisha "Sharia ya Kiislamu (Sheria ndogo)" iliyompa madaraka Waziri aliyehusika na mambo ya Sheria kuandaa na kuchapisha kipengele cha Sharia ya Kiislamu baada ya kushauriana na wanachuoni wa Sharia za Madh-hebu za Kiislamu.
Katibu Mkuu wa Bunge wakati huo, alikamilisha kuandika Mswada wa ndoa wenye sehemu 4 (kama ulivyokubaliwa na wanachuoni wa Sharia za Kiislamu kutoka Madh-hebu matatu Kiislamu Shafi'i, Hanafi na Shia).
Mswada huu uliotolewa kama Sharia ndogo chini ya kifungu kidogo cha Sharia ya Kiislamu (Na: 56 ya mwaka 1964) ikiwa ni sehemu ndogo ya Gazeti la Serikali na Na: 34 la tarehe 27, Juni, 1967.
Ilifahamika kuwa sehemu zilizosalia, kuhusiana na kuwalea watoto na talaka n.k. zingechapishwa mapema. Lakini zoezi hili lilisitishwa na badala yake serikali ilitunga sheria ya 'Ndoa' kupitia Mswada wa Ndoa wa mwaka 1971.
Hata hivyo, kanuni ya Sheria ya Ki-Islamu 1964 bado haijafutwa na bado ni sehemu ya Kitabu cha Bunge. Na kwa sababu sasa serikali inakusudia kuanzisha Mahakama za Makadhi katika kila Wilaya, ni wakati muafaka wa kufufua tena mswada wa sheria ya Kiislamu ya mwaka 1964 ili ufanyiwe kazi na kazi hii ianzie pale ilipoachiwa.
Jambo muhimu hapa ni kuepusha uwezekano wa Makadhi kutoa hukumu zitakazoleta utata. Vinginevyo, mzigo wa kazi za Mahakama Kuu utaongezeka kwa kuwa rufani kutoka Mahakama za Makadhi zitajazana kwenye Mahakama ya Rufaa.
Madhehebu za Makadhi wa Wilaya:
Kwa vile Waislamu wengi wa Tanzania ni wafuasi wa Madhehebu ya Shafii ni vizuri makadhi wa Wilaya watokane na Madhehebu ya Shafii.
Lakini iwapo wahusika au mhusika wa mgogoro ni wa Madhehebu isiyo ya Shafii, inapendekezwa kuwa Kadhi wa Wilaya asaidiwe na wanachuoni wa madh-hab inayohusika.
Hii itafuta uwezekano wa kutolewa hukumu isiyo sawa na itawapa imani ya kutendewa haki wahusika au mhusika. Wasaidizi wa Kadhi wa Wilaya waliotajwa hapo juu itabidi watayarishwe katika kila Wilaya na wanaweza kuangaliwa upya (kuteuliwa) muda baada ya muda.
Iwapo mapendekezo mawili muhimu yaliyotajwa hapo juu katika makala haya yatakubalika na kufanyiwa kazi, itakwenda hatua kubwa kuwatendea haki na usawa Waislamu wote nchini.
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/d/optout.
0 Comments