[Mabadiliko] Zanzibar - Koloni la Tanganyika

Monday, July 07, 2014
Kwa mujibu wa utafiti yakinifu nilioufanya, nimegundua kwamba kuna mambo ya msingi ya kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni ambayo Tanganyika imekuwa ikiinyonya Zanzibar na hatimaye kuigeuza kama koloni lake kwa muda wa zaidi ya miaka 50 ya Muungano! Nitafafanua baadhi ya mambo hayo katika uzi huu ili kuuweka ukweli huo bayana.
 
ANGALIZO
Naomba tujadiliane hoja hii kwa nidhamu na kwa ufasaha, bila ya jazba wala mihemuko yoyote ili hatimaye tufikie muafaka utakaokomesha unyonyaki huu ili wazanzibar wasiendelee kunyonywa na watanganyika tena.
…………………………………………………………………
Katika Muungano huu, Zanzibar ilikabidhi sehemu muhimu ya mamlaka yake (mahusiano ya nchi za nje, ulinzi na usalama, uraia, kodi na ushuru, sarafu, nguvu kuu za kuendeshea uchumi na mengineyo) kwa Tanganyika; na kisha Tanganyika ikajigeuza jina na kujiita Jamhuri ya Muungano.
 
 
Muungano huu ni kielelezo cha unyonyaji na ukandamizaji mkubwa ambao nchi ndogo ya Zanzibar imefanyiwa na nchi kubwa ya Tanganyika. Ni mfano wa jinsi ambavyo nchi moja kubwa ya Kiafrika inaweza kuigeuza nchi nyingine ndogo ya Kiafrika kuwa koloni lake.
 
Kwa miaka mingi Zanzibar imelalamika kwamba inapunjwa katika mgawanyo wa mapato yanayotokana na fedha zinazotolewa na nchi wafadhili na taasisi za kimataifa kwa Jamhuri ya Muungano. Sio tu kwamba Zanzibar haipati stahili yake ya mapato yanayopatikana kwa jina la Jamhuri ya Muungano kutoka vyanzo vya nje, bali pia fedha zinazopatikana kutokana na mambo ya Muungano zinatumika kwa mambo yasiyo ya Muungano ya Tanganyika.
 
Jambo chengine ni kuhusu hisa za Zanzibar zilizokuwa katika Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki kabla ya Bodi hiyo kuvunjwa mwaka 1965 na Benki Kuu ya Tanzania kuanzishwa. Fedha za Zanzibar katika Bodi ya Sarafu zilichukuliwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano baada ya masuala ya fedha, sarafu na Benki Kuu kufanywa kuwa mambo ya Muungano mwaka 1965, sisi tuliozaliwa ndani ya Muungano. Kwa muda mrefu Zanzibar imekuwa ikiiomba Tanganyika kuwapa hisa zao lakini wametia nta masikioni na hawawasikilizi wazanzibar kuhusu hisa hizo ambazo serikali ya Tanganyika imeamua kuziatamia moja kwa moja. Na sio tu kwamba Wazanzibari hawajui ni kiasi gani cha fedha zao zilichukuliwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano kufuatia kuvunjwa kwa Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki, bali pia hawana uhakika watazirudishiwa lini!"

Kwanini Serikali hii ya CCM imeshindwa kurudisha fedha hizo kwa Wazanzibari kwa takriban miaka hamsini tangu fedha hizo zinyakuliwe na Serikali ya Jamhuri ya Muungano (Serikali ya Tanganyika)? Tunahitaji kuelezwa Serikali hii inahitaji muda wa miaka mingapi mingine ili iweze kurudisha fedha za watu na
kuwaepusha Watanganyika na laana ya wizi wa fedha za Wazanzibari?

Suala chengine ni kuhusu gawio la misaada isiyokuwa ya bajeti. Serikali ya Tanganyika (iliyovaa joho la Muungano) imekuwa ikiipunja Zanzibar katika mgawo wa fedha zitokazo na misaada isiyokuwa ya kibajeti kwa muda mrefu sana. Iliamuliwa kwamba wazanzibar, kwa sababu ya udogo wake kijiografia na kidemografia,  Zanzibar iwe inagawiwa 4.5% ya mapato yote. Lakini kwa muda wa takribani miaka 50, serikali ya Tanganyika (Muungano), hutoa chini ya 2% ya fedha hizo na wakati mwingine kutozitoa kabisa.
 
Nini kifanyike ili kudai fedha zao walizodhulumiwa mpaka sasa?
 
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar au Wazanzibari wenyewe katika umoja wao, wana haki ya kutumia njia yoyote ile watakayoona inafaa, ikiwamo kufungua kesi za madai katika mahakama za ndani au mahakama za kimataifa, kudai fedha zake zote halali ambazo zimeibiwa na Tanganyika kwa kutumia kivuli cha Muungano katika kipindi chote cha miaka hamsini ya Muungano huu.

Kwa sababu ya Muungano huu, uhusiano kati ya Tanganyika na Zanzibar ni uhusiano wa kinyonyaji. Kwa sababu hiyo, huu ni uhusiano wa kikoloni. Ni uhusiano kati ya 'himaya' ya Tanganyika na 'koloni' lake la Zanzibar. Himaya za kikoloni huwa zinadhibiti masuala yote ya ulinzi na usalama, mambo ya nje na uhusiano wa kimataifa, uraia, kodi, fedha, sarafu na benki kuu ya makoloni yao. Na himaya za kikoloni huwa zinatumia nguvu na udhibiti wao wa masuala haya kuyanyonya makoloni yao kiuchumi, kuyadidimiza kijamii na kuyatawala kisiasa. Hivi ndivyo ambavyo imekuwa kwa mahuasiano kati ya Tanganyika na Zanzibar tangu kuzaliwa kwa Muungano huu tarehe 26 Aprili, 1964.

Muundo wa Muungano
 
Mfumo wa Muungano uliopo sasa hauinufaishi Zanzibar na hivyo haukubaliki kwa Wazanzibari. Koti la Muungano kama lilivyo sasa linabana sana. Wakati umefika tushone koti jipya kwa mujibu wa mahitaji ya zama hizi."

"rasilmali za Muungano ziwe ni milki ya pande mbili za Muungano; na rasilmali hizo ndio zitumike katika uendeshaji wa Mamlaka za Muungano. Ugawaji wa rasilmali ufanywe kwa uwiyano maalum utakaokubaliwa kwa pamoja na pande mbili za Muungano."

Tangu mwanzo Muungano wa Tanganyika na Zanzibar haukuwa Muungano wa usawa. Huu ni Muungano ulioipa Tanganyika – ikiwa imevalia koti la Jamhuri ya Muungano - mamlaka ya kuingilia uhuru na mamlaka ya Zanzibar.
 
Hata kwa kuangalia watu ambao wamewahi kupata fursa ya kuongoza Jamhuri ya Muungano, ni wazi kwamba Watanganyika ndio wamekuwa mabwana na Wazanzibari wamefanywa watwana katika masuala ya haki za kiutawala. Hivyo, kwa mfano, katika kipindi cha miaka hamsini ya Muungano huu, ni Mzanzibari mmoja tu ndiye aliyepata fursa ya kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano, kwa miaka kumi kati ya miaka hamsini hiyo.
Kwa utaratibu huo huo, tokea mwaka 1964, Zanzibar haijawahi kutoa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Mkuu wa Jeshi la Polisi au Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania. Zote hizi ni taasisi za Muungano. Aidha, Zanzibar imewahi kutoa Waziri Mkuu mmoja tu, tena kwa kipindi cha mwaka mmoja na nusu, na Jaji Mkuu mmoja tu katika kipindi hicho cha nusu karne ya Muungano huu. Vile vile, katika Diplomatic Corps, kwa sasa kuna Wazanzibari wawili tu ambao ni mabalozi wa Tanzania nchi za nje kati ya mabalozi 32 wanaoiwakilisha Tanzania nchi za nje.

Katika miaka yote ya Muungano, hakuna Mzanzibari ambaye amewahi kushikilia nafasi ya Spika au Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano. Baada ya nusu karne ya Muungano wa aina hii, wananchi wa Tanganyika na, hasa wa, Zanzibar hawako tayari kuendelea na utaratibu huu wa kinyonyaji na kikandamizaji. Wananchi wanataka mabadiliko ya msingi ya muundo wa Muungano na uendeshaji wake.
 
 
Nini kifanyike kuleta usawa?
 
Wananchi wanataka kufanya maamuzi kuhusu kama wanataka kuendelea na Muungano na, kama jibu ni ndiyo, muundo wa Muungano huo.
Kinachotakiwa kufanywa ni kuwauliza wananchi wa Tanganyika na Zanzibar – kwa kutumia kura ya maoni - kama bado wanataka kuendelea na Muungano huu. Na kama jibu lao litakuwa ni ndiyo, basi wananchi waamue, katika kura hiyo, ni muundo gani wa Muungano wanautaka. Miaka hamsini ya watawala kuamua masuala haya muhimu peke yao inatosha. Huu ni wakati muafaka kwa wananchi kufanya maamuzi haya makubwa kwa maisha yao na kwa nchi zao mbili.

Nawasilisha.
 

Share this :

Previous
Next Post »
0 Comments