[wanabidii] Hotuba ya Msemaji Mkuu wa Kambi ya Upinzani; Wizara ya Ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa MWAKA WA FEDHA 2014/2015

Tuesday, May 13, 2014
HOTUBA YA MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI, MHE MASOUD ABDALLA SALIM (MB) WIZARA YA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA KUHUSU MAKADIRIO YA MATUMIZI YA WIZARA YA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA KWA MWAKA WA FEDHA 2014/2015


(Inatolewa chini ya Kanuni ya 99 (9), ya Kanuni za Kudumu za Bunge Toleo la Mwaka 2013)

1. SERA NA SHERIA YA ULINZI WA TAIFA 

Mheshimiwa Spika
, Sera na Sheria ya Ulinzi wa Taifa ilitungwa tangu mwaka 1966 kwa madhumuni ya kuunda, kuendesha, kusimamia na kuhudumia majeshi ya Ulinzi kulingana na majukumu yake. Kwa miaka kadhaa sasa serikali imekuwa ikitoa ahadi nyingi Bungeni tangu mwaka 2008 kuwa ipo katika michakato ya kuweza kurekebisha Sera na Sheria ulinzi wa taifa ili kuendana na maendeleo ya sayansi teknolojia. 

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inahoji ni sababu zipi za Msingi zilizopelekea serikali kutoleta Bungeni kwa muda wa miaka saba sasa tangu serikali ilipoahidi kuleta sera na mapitio ya sheria hiyo kama ilivyokusudiwa. 

Mheshimiwa Spika, Ikumbukwe kuwa suala la Ulinzi na Usalama ni suala la Muungano. Kambi Rasmi ya Upinzani inahoji na kutaka majibu ya serikali juu ya namna Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kama nchi mshirika wa Muungano ilivyoshirikishwa juu ya jambo hili katika kutoa maoni na mapendekezo kama ilivyohitajika. 

2. 
MAENEO YA JESHI NA FIDIA KWA WANANCHI 

Mheshimiwa Spika
, kumbukumbu ya taarifa za utekelezaji wa ahadi za serikali Bungeni ukurasa 377 hadi 379 ya Januari 2007 serikali ilieleza jinsi gani imeweka mkakati wa upimaji wa maeneo ya jeshi na JKT na kuyapatia hati miliki yake na taratibu za kutoa fidia kwa wananchi waliochukuliwa maeneo yao kwa ajili ya Jeshi la Ulinzi na JKT. 

Mheshimiwa Spika
, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inataka kujua kigugumizi cha serikali kwa muda wa miaka sasa kulidanganya Bunge na kuwadanganya wananchi kwa kutowapatia haki zao tangu mwaka 2007 yakibakia maandishi yasiyo na utekelezaji. 

Mheshimiwa Spika
, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inahoji mkakati wa serikali wa kutoa fidia maeneo ya raia yaliyochukuliwa na jeshi kama ifuatavyo; · Mkoa wa Arusha- Oldonyo Sambu (Tanganyika Packers 977KJ). Serikali hamjawailipa wananchi na walalamika na Je ni lini wananchi hao watalipwa? · Mkoa wa Dar es Salaam- Kunduchi Transit Camp (Kunduchi Rifle Range), Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa pamoja na Makao Makuu ya Jeshi, Ubungo Kibangu (691 Det), Mwenge TPDF flats, Keko TPDF flats na Magogoni (691 KJ Det). Katika maeneo haya serikali hadi leo hamjatoa fidia na ahadi zimekuwa ni nyingi na hivyo kupelekea malalamiko makubwa ya wananchi. Je ni lini fidia hizi zitatolewa?

· Mkoa wa Dodoma ni Makutupora JKT, Kombania ya Radar Dodoma (02/692 KJ). Katika maeneo haya wananchi wamechoka kupewa ahadi hewa zisizo na majibu kwa miaka mingi sasa. Je ni lini fedha zao mtawapatia? 
· Mkoa wa Kagera- Biharamuro (23 KJ), Mkoa wa Kigoma- Bulombora JKT nako manung'uniko yamekuwa ni makubwa na serikali imeahidi utekelezaji bila majibu hadi sasa. Je kuna mpango wowote wa kuwalipa? 
· Mkoa wa Lindi (Singino Radar).
· Mkoa Mara- Rwamkoma JKT, Kiabakari 253 KJ, Buhemba JKT ambapo napo masikitiko yamezidi kiwango na wanahoji kuwa je haya ndiyo malipo ya serikali yao waliyoichagua kuthubutu kuwadhulumu?
· Mkoa Morogoro- Chita JKT, Ngerengere, wananchi wanauliza na kuhoji kuwa ni lini haki zao watazipata? Au mpaka watoto wa marehemu nao wafariki wote?
· Mkoa Mtwara- Umoja Camp, katika eneo hili pia ni kilio kisichoisha kwa wananchi kudai haki zao, wamekata tama, je serikali inaeleza? · Mkoa wa Ruvuma- Mlale JKT, Tunduru TPDF. 
· Mkoa wa Rukwa – Kasanga TPDF Det. · Mkoa wa Tanga- Maramba JKT, Mgambo JKT, Songa 37 KJ. Kwa maumivu waliyonayo wananchi imepelekea kuuliza serikali ina mkakati gani wa kuwapatia fedha zao.

Mheshimiwa Spika, Zaidi ya hayo Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inapenda kujua hatma ya maeneo yaliyofanyiwa tathmini kwa kusubiri fedha za fidia kama ifuatavyo; · Duluthi Estate Tengeru. · Singino Kilwa. · Mapinga Bagamoyo.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inasikitishwa na inahuzunishwa na serikali kulidanganya Bunge na kuwadanganya wananchi kutowapatia haki zao hizo kwa miaka saba sasa. Kambi Rasmi inaitaka serikali kutoa mkakati wa haraka wa kuwafidia wananchi wa maeneo haya na hasa ikizingatiwa na kudhihirika kuwa baadhi ya maeneo yaliyochukuwa wananchi waliokuwa wanayamiliki wameshafariki.

3. JESHI LA KUJENGA TAIFA

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa JKT inachukua vijana waliomaliza kidato cha sita kwa mujibu wa sheria. Na kwa kuwa vijana wanaotarajia kumaliza kidato cha sita kwa mwaka huu ni arobaini na tano elfu (45,000).

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inahoji na kutaka kujua ni sababu zipi za msingi zilizopelekea fedha za maendeleo za JKT mwaka 2013/2014 ambazo zilikuwa kiasi cha Shilingi Billioni 6 lakini hadi sasa zimetolewa ni Shilingi Milioni 525 huku ikiwa imebakia miezi miwili kumalizika kwa bajeti. Je hii si aibu kwa serikali?

Mheshimiwa Spika, fedha hizo za maendeleo za JKT ambazo zimekwishatolewa ni asilimia 8.8, huku serikali ikijisifu kuwa inahitaji kuendeleza JKT. Je huo sio uongo wa serikali kulidanganya Bunge na wananchi kwa ujumla wake? Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inahoji aibu na fedheha hii ya kutoipatia fedha za maendeleo JKT ni lini itakoma na je fedha hizi za maendeleo serikali ina mkakati gani wa ziada wa kuzitoa kabla ya tarehe 30 Juni mwaka huu ili kukamilisha miradi ya maendeleo ya JKT.

Mheshimiwa Spika, kambi ya JKT Kanembwa Kigoma imetelekezwa kwa muda mrefu na hasa askari wa JKT Kanembwa ambao hawajalipwa fedha zao za mizigo na hawajalipwa fedha za likizo kwa muda mrefu sasa tangu mwaka 2007.

Mheshimiwa Spika, baya zaidi ya hilo, pamoja na mkakati wa serikali a kudhibiti UKIMWI Jeshi bado serikali imewatenganisha askari hao na familia zao kwa muda mrefu sasa, jambo ambalo hupelekea migogoro kati ya familia za vijiji jirani na Kambi hiyo ya Jeshi. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inataka maelezo sahihi juu ya malipo ya madeni ya fedha za likizo na mizigo katika Kambi ya JKT Kanembwa na maeneo yote ya Jeshi la Wananchi na JKT. 

Mheshimiwa Spika, Shirika la Uzalishaji mali la JKT (SUMA JKT) liliagiza matrekta kutoka nchini India kwa mkopo wa bei nafuu katika mpango wa Kilimo Kwanza, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inataka kujua ni kwa kiasi gani hadi sasa tumeanza kurejesha fedha hizo za madeni ya matrekta hayo na serikali ina mkakati gani wa kuweza kuagiza tena matrekta mengine ili kuweza kuboresha mpango wa Kilimo Kwanza.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inataka kuelewa kiwanda cha kushona nguo cha kijeshi CAMISUMA kimepata faida kiasi gani kwa mwaka wa fedha 2013/14. Sambasamba na hilo Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inataka kuelewa juu ya ubia wa kiwanda cha kutengeneza madawa baina ya Tanzania na China (TANZANSINO) kwa kushirikiana na ubia wa Kampuni ya Halley Group.


4. JESHI LA WANANCHI NA ULINZI WA AMANI KATIKA UMOJA WA MATAIFA 

Mheshimiwa Spika, Jeshi letu bado linaendelea kushiriki katika operesheni za Ulinzi wa amani katika Umoja wa Mataifa. Pamoja na jeshi letu kushiriki katika ulinzi huo Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inapenda kuhoji na kuitaka serikali kueleza na kutoa taarifa kwa Bunge lako tukufu kuhusu hali za wanajeshi wetu huko nchini Sudan, DRC, Sudan Kusini, Lebanon na Ivory Coast.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inahoji na inataka kujua idadi ya wanajeshi mpaka sasa waliouwawa katika kulinda amani katika mataifa hayo. 

Mheshimiwa Spika
, ieleweke kuwa wanajeshi ambao wanauwawa katika operesheni wameacha familia na wajane huku nyumbani. Katika muktadha huo Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inahoji na kuitaka serikali kueleza Bunge lako tukufu juu ya namna ambavyo inasaidia familia za waliofiwa ikiwemo wajane na watoto ambao ni tegemezi kwa wanajeshi hao waliouwawa. 

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka serikali kueleza mkakati wa ziada kwa familia za wafiwa wa marehemu waliouwawa kwenye kulinda amani na elimu kwa familia za wanajeshi wote. 

5. 
KUONDOLEWA KWA ALAMA ZA MIPAKA (BEACONS) YA NCHI

Mheshimiwa Spika,pamoja na jitihada za serikali za kuanza kurejesha alama za mipaka (beacons), Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inahoji na kutaka kujua alama za mipaka zilizong'olewa baina ya Tarime Tanzania na Migori Kenya katika Vijiji vya Kirongwe, Ikoma, Panyakoo, Ruche, Kagoja na Nyamhunda. Ni lini alama hizo zitarejeshwa kwa kuwa suala hili ni mtambuka kwa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujanga Taifa, Ardhi, Mambo ya Nje pamoja na TAMISEMI. Hivyo Kambi Rasmi ya Upinzani inataka ufafanuzi wa ziada ni nchi gani jirani tulizopakana nazo wanaokwamisha zoezi hili. 

Mheshimiwa Spika
, Aidha katika Mkoa wa Kagera alama za mipaka zilizong'olewa ni katika Vijiji vya Kakunyo, Bugango, Rubale, Mtukula, Minziro na Kashanze. 

Mheshimiwa Spika, alama hizo zilizong'olewa zinahatarisha ulinzi na usalama mipakani lakini pia zinaweza kuleta mgogoro unaoweza kulikumbuka taifa na nchi jirani. Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni inahoji kwa nini tatizo hilo limeshindwa kutatuliwa kwa muda mrefu na lini litapatiwa ufumbuzi ili kuepusha migogoro inayoweza kutokea.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imegundua kuwa fedha zinazohitajika katika kutatua tatizo hili la alama za mipaka zimekuwa hazitolewi na serikali. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka serikali kutoa fedha hizi haraka iwezekanavyo ili kuliepusha na migogoro na nchi jirani. 

6. 
WASTAAFU WA JESHI LA WANANCHI

Mheshimiwa Spika, maisha ya wanajeshi wetu wastaahafu yanasikitisha licha ya kulitumikia taifa hili kwa muda mrefu, kwa uadilifu na uzalendo mkubwa. Hata hivyo hali zao za maisha zimekuwa duni, mbaya na kubakia ombaomba ambayo hailingani na utumishi wao walioufanya kwa uadilifu na uzalendo wa hali ya juu. 

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa serikali imewatelekeza wanajeshi wastaahafu na kuwaacha mitaani bila kujua ni kitu gani cha kufanya, tayari wameanzisha umoja wao unaojulikana kama Muungano wa Wanajeshi Wastaahafu Tanzania (MUWAWATA). Mheshimiwa Spika, wanajeshi hawa wastaahafu ni jeshi la akiba (Reserved Army). Kambi Rasmi ya Upinzani inahoji na kuitaka serikali kutoa mkakati wa serikali wa kuweza kuboresha maisha ya wanajeshi wastaahafu na hasa kwenye viwango vya pensheni kwa maofisa na askari wa kawaida toka private hadi Brigedia General. 

Mheshimiwa Spika
, Wizara ya Ulinzi ya India imeweka mazingira mazuri ya kuwasaidia wanajeshi wastaahafu kuajiriwa uraiani au kuwezesha kujiajiri wenyewe ni jambo jema na lenye mfano wa kuigwa. Je Tanzania ina mpango gani juu ya kurekebisha kasoro hizi. 

Mheshimiwa Spika, ikumbukwe kuwa kila askari wa leo ni mstaahafu mtarajiwa. Hata hivyo askari wastaafu wanaendelea kudharauliwa, kupuuzwa na kutotendewa haki kwa madai ya msingi juu ya hatma ya maisha yao.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inahoji sababu zilizoepekelea kuwafanya wanajeshi wetu wastaafu kuwa ombaomba kwani hata haki zao wanazostahili kupewa yaani pensheni za kila baada ya miezi mitatu hazitolewi kwa wakati. Huu ni mtindo wa kuwadhulumu na kuwanyonya askari wetu wastaafu.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka serikali kuacha mara moja tabia ya kuwadhulumu na kuwanyonya askari wastaafu. 

Mheshimiwa Spika, inakuaje leo mstaahafu wa staff sergent aliyeitumikia nchi hii kwa muda wa miaka 32 kwenye mazingira magumu leo mnawalipa pensheni ya Shilingi 350,000 kwa muda wa miezi mitatu ambayo ni sawa na Shiling 117,000 kwa mwezi, ambayo ni pia ni wastani wa Shilingi 4,000 kwa siku fedha ambazo hata chai ya asubuhi kwa familia hazitoshi. Je haya ndiyo malipo waliyostahili kulipwa?

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inashindwa kuelewa juu ya mkakati wa serikali wa kuweza kuboresha pensheni za askari wastaafu huku gharama za maisha zikipanda kila kukicha. Je kwa mwaka huu wa fedha askari wastaafu wa Jeshi wataongezewa kiasi gani cha fedha? 

7. 
SIKU YA MASHUJAA

Mheshimiwa Spika, serikali imekuwa ikiadhimisha siku ya mshujaa kwa kila mwaka kwa ajili ya kuwakumbuka mashujaa wetu walioshiriki katika vita vya Msumbiji pamoja na vita ya Kagera. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inataka kujua namna familia za marehemu za mashujaa hao zinapata matunzo.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imebaini kuwa wajane wa marehemu wa mashujaa hao hali zao za kimaisha ni mbaya na wanatesekea na njaa huku watoto wa mashujaa hao wakiwa wamekosa hata kupata elimu. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inahoji na kutaka kujua mkakati wa ziada wa serikali wa kuweza kuboresha maisha ya wajane wa mashujaa hao pamoja na familia zao kwa ujumla.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inashangazwa sana na kutumika kwa mamilioni ya fedha kuchimba mifupa ya mashujaa hao nchini Msumbiji kwa gharama za mamilioni ya fedha na kuizika Naliendele Mtwara huku serikali ikizitelekeza familia za marehemu na kuwaacha ombaomba na kuendelea kulalamika. Je serikali ina mkakati gani wa ziada wa jambo hili kulipati ufumbuzi wa kudumu?

Mheshimiwa Spika, Mashujaa waliopata ulemavu kwenye vita vya Kagera na Msumbiji nao wametelekezwa na serikali na wamekuwa wakijiuliza maswali mengi bila majibu.

8. UJENZI WA MAGHALA

Mheshimiwa Spika, ujenzi wa maghala ya kuhifadhia silaha ni njia moja muhimu sana katika kulinda maisha ya wanajeshi na raia. Katika bajeti ya mwaka 2013/14 ambayo inakaribia kukamilika fedha zilizokuwa zimetengwa ni kiasi cha Shilingi Bilioni 5.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imegundua kuwa fedha kwa ajili ya ujenzi wa maghala 2013/14 hadi leo fedha hizo hazijatolewa mpaka sasa. Kambi rasmi ya Upinzani inataka kujua ni sababu zipi za msingi zilizopelekea fedha za ujenzi wa maghala kutotolewa mpaka sasa.

Mheshimiwa Spika, ikumbukwe kuwa maghala ya silaha yameshaleta madhara mara kadhaa katika Mkoa wa Dar es Salaam maeneo ya Mbagala na Gongolamboto. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inasikitishwa na serikali kutojifunza kwa madhara ambayo yameshatokea kuhusu masuala hayo.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inataka kujua ni kwa kiasi gani serikali imelipa fidia ya waathirika wa milipuko katika Kambi ya Gongolamboto. Na kama wapo wananchi ambao hawajalipwa ni sababu zipi zilizopelekea hadi kutopatiwa fedha zao?

9. MADENI

Mheshimiwa Spika, kumekuwepo na madeni ya muda mrefu ya wanajeshi na wazabuni waliolihudumia jeshi letu. Hata hivyo Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imegundua kuwa baadhi ya wazabuni wametishia kusitisha huduma zao hadi hapo watakapolipwa. 

Mheshimiwa Spika, ili kutatua tatizo hili kubwa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inahoji na inataka kujua ni nini mkakati wa serikali kulipa madeni hayo ili kuondokana na aibu inayoweza kulikumba jeshi letu. Kwa kuwa fedha za maendeleo kwa fungu 38 ngome kwa mwaka wa fedha 2013/14 ziliidhinishiwa Shilingi Bilioni 10 na hadi Machi 2014 fedha zilizotolewa zilikuwa Shilingi Bilioni 1.6 sawa asilimia 16, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inahoji kuwanyima na kuwadhulumu kwa kutowapatia wanajeshi fedha zilizoidhinishwa na Bunge tukufu, ni kwa nini fedha hizi hazitolewi na ni lini mtindo huu mchafu utakoma?

Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inahoji kuwa serikali iliyopelekea kutotoa fedha za maendeleo kwa JKT na Jeshi la Wananchi ni mfumo wa serikali mbili tulionao na wala sio mfumo wa serikali tatu.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaweka msimamo wake hadharani baada ya kugundua kuwa kuna mchezo mchafu wa serikali kupitia hazina kwa pamoja kunyima fedha za maendeleo fungu 38 JKT na fungu 38 Ngome na kuazimia ifikapo tarehe 29/06/2014 fedha Bilioni 5.4 za JKT hazijatolewa na Bilioni 8.4 za Ngome hazijatolewa tutafanya maandamano makubwa nchi zima kuilazimisha serikali kutoa fedha hizo za maendeleo na tunaomba watanzania watuunge mkono kwani suala la Ulinzi halina mjadala.

10. HOSPITALI ZA JESHI

Mheshimiwa Spika, Jeshi la wananchi wa Tanzania lina hospitali moja tu ya rufaa iliyopo Lugalo Jijini Dar es Salaam na nyingine za Kanda kama vile Nyumbu Kibaha, Mbeya, Arusha, Mwanza na Zanzibar na kimsingi asilimia themanini (80%) ya huduma ya hospitali hizi hutolewa kwa raia. 

Mheshimiwa Spika
, pamoja na umuhimu wa hospitali hizi serikali kwa mwaka uliyopita ilitoa fedha kidogo sana ambazo hazifiki asilimia kumi za mahitaji. Ni maoni ya Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni kuwa serikali inaleta mchezo na afya za wanajeshi wetu. Hivyo basi Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inahoji ni kwa nini serikali isiongeze fedha kutoka Shilingi Bilioni 2.4 hadi Bilioni 10 kwa kuwa hospitali hizi huhudumia pia raia kama tulivyokwishasema. 

11. 
VITUO TEULE VYA JESHI

Mheshimiwa Spika, vituo teule sambsamba na barabara za mipakani ni jambo muhimu sana katika ulinzi wan chi yetu. Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni inataka kujua mkakati wa ziada wa serikali wa kuzikarabati barabara zote zinazokwenda kwenye vituo teule kuweza kutumika wakati wowote. 

Mheshimiwa Spika, ikumbukwe kuwa katika nchi zingine duniani suala la kuzikarabati barabara za mipakani ni jukumu la Wizara ya Ulinzi na sio jukumu la Halmashauri kama ilivyo serikali ya Tanzania. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inahoji na kutaka kujua ni lini serikali itazihamisha barabara zote teule kuwa chini ya Wizara ya Ulinzi na Kujenga Taifa.

12. AJIRA JESHINI

Mheshimiwa Spika, kuwekuwepo na malalamiko ya muda mrefu juu ya vijana wanaoajiriwa kutoka ngazi za Mikoa na Wilaya wanaojiunga na Jeshi la Wananchi wa Tanzania kuwa mfumo huo haupo wazi mbali na mkakati wa vijana hao kuchukuliwa JKT na JKU. 

Mheshimiwa Spika, malalamiko haya ya kuwepo kwa uwazi katika uajiri hata wabunge wenyewe na hasa kutoka Zanzibar hawaelewi ni lini na wakati gani ajira zinapatikana. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungani inahoja na kutaka kujua mkakati wa Wizara ya Ulinzi kuwapatia taarifa Waheshimiwa Wabunge wa Jamhuri ya Muungano ya muda, siku na mazingira ya ajira hizi jeshini. 

13. HALI YA UHARAMIA KATIKA PWANI YA AFRIKA MASHARIKI

Mheshimiwa Spika, kwa muda mrefu sasa hali ya uharamia katika Bahari ya Hindi na hasa katika Pwani ya Afrika Mashariki imedhibitiwa kwa kiasi Fulani. Na tangu kufanyika kwa marekebisho ya Sheria yetu ya Makosa ya Jinai ili kuruhusu mashataka dhidi ya maharamia wanaokamatwa Bahari Kuu kushtakiwa nchini. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inahoji na kutaka kujua ni maharamia wangapi wamekamatwa kutoka Januari 2013 hadi Machi 2014.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Dar es Salaam ni kituo cha upashanaji habari za majini kwa ukanda wa nchi wanachama wa Mkataba wa Djibout kufuatia ushirikiano wa Jeshi la wananchi wa Tanzania (TPDF) na nchi za Umoja wa Ulaya ambapo Jeshi letu lilifanikiwa kuwanasa watuhumiwa watano wa uharamia kwenye kisiwa cha Ukuza Wilaya ya Kilwa tangu tarehe 18/04/2012. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inataka kujua watuhumiwa hao wako wapi na hukumu yao ilitolewa lini?

14. MAPITIO YA UTEKELEZAJI WA BAJETI KWA MWAKA WA FEDHA

Mheshimiwa Spika
, kwa kuwa Wizara ya Ulinzi imeidhinishiwa kiasi cha Shilingi Trilioni 1.269 kwa mgawo ufuatao ; Fungu 57 Wizara ya Ulinzi Bilioni 19.7 kwa matumizi ya kawaida na Bilioni 230 kwa matumizi ya maendeleo kwa ujumla fungu hilo ni Bilioni 249.7.

Mheshimiwa Spika, Fungu 38 Ngome fedha kiasa cha Bilioni 803.5 zimetengwa kwa matumizi ya kawaida na Bilioni 12 kwa miradi ya maendeleo, jumla ni Bilioni 815.5. 

Mheshimiwa Spika, Fungu 39 JKT kiasi cha fedha Shilingi Bilioni 196.8 zimetengwa kwa matumizi ya kawaida na Bilioni 7 kwa miradi ya maendeleo. Jumla ya fedha zote katika fungu hili ni Bilioni 203.8. 

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inasisitiza kuwa fedha za maendeleo za JKT zimetolewa asilimia 8 tu hadi sasa na fedha za maendeleo za ngome zimetolewa asilimia 16 tu hadi sasa. Fedha hizo ambazo hazijatolewa, zitolewe haraka sana kabla ya mwisho wa fedha na hizo zilizotengwa zitolewe mapema iwezekanavyo ili kuepuka hali ya mwaka wa fedha uliopita. Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni naomba Kuwasilisha;
……………………………………….

Mhe. Masoud Abdalla Salim

Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni

Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa

--
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/d/optout.

Share this :

Related Posts

0 Comments