[wanabidii] Ufafanuzi wa IPTL kwa Bunge

Tuesday, May 13, 2014
KAULI YA SERIKALI KUHUSU FEDHA KATIKA AKAUNTI YA ESCROW KUHUSIANA NA MKATABA WA IPTL
HISTORIA YA MRADI WA IPTL

Mheshimiwa Spika, katika mjadala wa Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, baadhi ya Waheshimiwa wabunge wamehoji utoaji wa fedha kwenye Escrow Account baada ya Hukumu ya Mahakama Kuu ya Tanzania.

Mheshimiwa Spika, Makubaliano kati ya Serikali na Kampuni ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL) kuanzisha mradi wa kufua umeme wenye uwezo wa kuzalisha MW 100, yalifikiwa ili kukabiliana na tatizo la uhaba wa umeme katika miaka ya 90. Serikali ilialika sekta binafsi kuwekeza katika uzalishaji umeme kwa vile haikuwa na fedha za kugharimia miradi ya umeme. Kampuni ya VIP Engineering and Marketing Ltd ya Tanzania (VIP) iliweza kuishawishi Serikali kualika Kampuni ya Mechmar Corporation ya Malasyia (MECHMAR), na baada ya MECHMAR kuonyesha kuwa inaweza kuzalisha MW 100 katika mji wa Dar es Salaam ilisaini MoU na Serikali. Mwaka 1994 Kampuni ya MECHMAR na Kampuni ya VIP kwa pamoja zilianzisha Kampuni ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL) kama kampuni binafsi iliyokuwa inamilikiwa na MECHMAR kwa asilimia 70 na VIP kwa asilimia 30. Kampuni ya IPTL ilipewa leseni ya kujenga, kumiliki na kuendesha (Build-Own-Operate) mtambo wa kuzalisha MW 100 za umeme wa mafuta mazito katika eneo la Tegeta-Salasala. 

Mheshimiwa Spika, Mkataba wa Kununua Umeme kati ya TANESCO na IPTL, (Power Purchase Agreement-PPA) ulisainiwa tarehe 26 Mei, 1995 kwa kipindi cha miaka 20, ingawa utekelezaji wake ulianza 2002. Katika Mkataba wa PPA, TANESCO ndiye mnunuzi pekee wa umeme toka mtambo wa IPTL. Kulingana na IPTL inatakiwa kuiuzia TANESCO umeme usiopungua asilimia 85% ya umeme unaozalishwa kila siku. Pamoja na mkataba huo, Serikali ilisaini mikataba miwili ambayo ni Mkataba wa Utekelezaji (Implementation Agreement) na Mkataba wa Dhamana (Guarantee Agreement) ambapo ilikusudiwa kuwa, endapo TANESCO itashindwa kulipa gharama za kununua umeme, Serikali ichukue dhamana ya kulipa gharama hizo kwa niaba ya TANESCO.

Mheshimiwa Spika, Gharama za uwekezaji wa mradi huo zilikadiriwa kuwa Dola za Marekani milioni 150. IPTL walitakiwa kutoa asilimia 30 kama mtaji na asilimia 70 kama mkopo. Makubaliano kati ya wanahisa hao ni kwamba MECHMAR watoe fedha za mtaji na mchango wa VIP uwe huduma muhimu za kuwezesha kuanzishwa kwa IPTL na eneo la kiwanja kitakachojengwa mtambo wa kuzalisha umeme huko Tegeta Salasala. Kwa maelezo yote hayo, utaona kuwa Serikali na TANESCO siyo wabia bali wateja wa Kampuni ya IPTL. Hata hivyo, Wanahisa wa IPTL (MECHMAR na VIP) hawakutoa asilimia 30 ya mtaji kama walivyotakiwa ila waligeuza fedha za mkopo kuwa mtaji.Kwa lugha nyingine wanahisa hao walidanganyana wenyewe.

Mheshimiwa Spika, Baada ya mkataba huo kutiwa saini, tarehe 4 Februari, 1997 IPTL iliingia mkataba wa ujenzi (EPC Contract) na Kampuni ya Wartsila ya Uholanzi. Tarehe 28 Juni, 1997, IPTL iliingia mkataba wa mkopo (Syndication Loan Agreement) na umoja wa mabenki ya Malaysia kwa ajili ya mkopo wa Dola za Marekani milioni 105 ikiwa ni asilimia 70 ya mtaji wa IPTL. 

Mheshimiwa Spika, Hata hivyo, IPTL walitakiwa kuchukua Dola za Marekani 85,862,022.08 kutoka Dola za Marekani milioni 105 zilizotolewa kama mkopo. Serikali wala TANESCO hawakuwa sehemu ya Mkataba huo. Mkopo huo ulitakiwa kurudishwa katika kipindi cha miaka nane (8) na riba ilikuwa asilimia 2.5 kwa mwaka. Grace period ya mkopo huo ilikuwa miezi 18. Dhamana ya mkopo huo ilikuwa kiwanja cha Tegeta ambapo mtambo wa kuzalisha umeme utawekwa pamoja na mtambo wa kuzalisha umeme. Mradi wa IPTL ulianza uzalishaji umeme mwezi Januari, 2002 na ndiyo utekelezaji wa mkataba ulpoanza.

Mheshimiwa Spika, Kulingana na PPA, malipo ya gharama za umeme ambazo TANESCO inatakiwa kulipa ni ya aina mbili energy na capacity charges. Capacity charge ni gharama za uendeshaji na matengenezo (O&M) pamoja na vilainishi, ambazo zinalipwa hata kama TANESCO haitumii umeme unaozalishwa na IPTL. Energy charges ni gharama za kuzalisha umeme ambazo TANESCO inalipa ikitumia umeme wa IPTL.

Mheshimiwa Spika, Ujenzi wa mtambo ulianza mwaka 1997 na kukamilika mwaka1998, lakini uzalishaji ulianza tarehe 15 Februari, 2002 (Commercial Operational Date). Mtambo ulichelewa kuanza uzalishaji kutokana na mgogoro kati ya TANESCO na IPTL katika Mahakama ya Usuluhishi ya Kimataifa (ICSID).

AKAUNTI YA ESCROW

Mheshimiwa Spika, Akaunti ya Escrow ilifunguliwa katika Benki Kuu ya Tanzania baada ya Mkataba wa Escrow kusainiwa na Serikali (kwa niaba ya TANESCO), Independent Power Tanzania Limited (IPTL) na Benki Kuu ya Tanzania, tarehe 5 Julai, 2006. (Kiambatisho Na. 1)

Mheshimiwa Spika, Kufunguliwa kwa akaunti ya Escrow kulitokana na ushauri wa Mkono and & Co. Advocates in association with Denton Wilde Sapte wa tarehe 30 Juni, 2004. Ushauri huo upo kwenye kifungu cha 10.1 na 10.2. (Kiambatisho Na. 2)

Mheshimiwa Spika, Mkataba wa Escrow ulitokana na Mkataba wa Ununuzi wa Umeme kati ya TANESCO na IPTL uliosainiwa tarehe 26 Mei, 1995. Kulingana na kifungu Na. 6.8 cha PPA, kinachoeleza kuwa, iwapo pande mbili za mkataba hazikubaliani na gharama za umeme, fedha za gharama za umeme zilipwe kwenye akaunti ya Escrow hadi hapo mgogoro wa malipo utakapotatuliwa. (Kiambatisho Na. 3)

Mheshimiwa Spika, Fedha zilizokuwa kwenye akaunti ya Escrow zilikuwa zinalipwa na TANESCO kutokana na mgogoro wa gharama za malipo kati ya TANESCO na IPTL. TANESCO ilidai kuwa inalipa gharama za juu kutokana na IPTL kutumia fedha za mkopo kama mtaji, kukokotoa gharama za umeme wakati fedha halisi za mtaji wa IPTL si zaidi ya Dola za Marekani 1,000. IPTL walikuwa wakidai kuwa fedha za mkopo zihesabiwe kama mtaji kukokotoa gharama za umeme. Aidha, TANESCO walikuwa wakilipa fedha kwenye akaunti ya Escrow kuanzia tarehe 22 Septemba, 2006 hadi Agosti 2009 walipoacha kuweka fedha kwenye akaunti hiyo. (Kiambatisho Na. 4) kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo IPTL kuwa kwenye ufilisi na kuendelea kutoa dispute notice kwa ushauri wa Wakili wao.

Mheshimiwa Spika, kulingana na kifungu cha XXII cha "Implementation Agreement" ya tarehe 8 Julai, 1995 kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na IPTL, Serikali ilitoa dhamana (Guarantee) kulipa fedha yoyote ambayo TANESCO itashindwa kulipa kama itatokea hivyo na siyo kama IPTL itakopa au mtu yeyote atakopa kwa niaba ya IPTL. Dhamana ya Serikali ilihusu "Capacity Charge" na si vinginevyo. Mkopeshaji yeyote ambaye siyo sehemu ya PPA hawezi kujigeuza na kudai ni sehemu ya mkataba huu. Mawakili (Mkono & Company Advocates) wetu wanaelewa hivyo lakini hawataki kusema kwa kuwa watapoteza au kuacha kulipwa na Serikali pamoja na TANESCO.

Mheshimiwa Spika, Kwa maelezo hayo, na kwa mtazamo wangu, kampuni pekee inayonufaika na dhamana ya Serikali ni IPTL au yeyote atakayekuwa anamiliki IPTL na Serikali pia ilikubali kulingana na sheria za nchi.

Mheshimiwa Spika, Ni vizuri ikaeleweka kuwa, akaunti ya Escrow ilifunguliwa kutokana na "Dispute" iliyotolewa na TANESCO na sasa, "Dispute" haipo, na hivyo Serikali yeyote makini haina sababu ya kuzuia fedha ambazo zipo kwenye akaunti ya Escrow kwa sababu yoyote ile.

Mheshimiwa Spika, IPTL ni Kampuni binafsi na siyo kampuni ya Serikali, na TANESCO kama Mnunuzi wa umeme, wajibu wake ni kununua umeme na siyo kuingilia masuala ya ndani ya Kampuni. Kama "dispute" imeisha sasa fedha hizo zinazuiwa ili ziende wapi na zifanye nini?

Mheshimiwa Spika, Katika hukumu yake, ya tarehe 5 Septemba, 2013 na pia "consent order" iliyotolewa na Judge Utamwa J, tarehe 17 Januari, 2014, katika kesi yake Misc. Civil Case No.49/2002 and Misc. Civil Case No.254/2003 states "among other prayers that, by this settlement order, parties have discharged all of their respective outstanding performance obligations required in completion of execution of the contract". (Kiambatisho Na. 5 )

Mheshimiwa Spika, Siamini kama Bunge letu tukufu lingependa kuhoji maamuzi ya Mahakama. Ninaamini Mahakama zetu zina-uhuru wa kutoa uamuzi wowote na kulinda haki za Wananchi. Vyama vya upinzani wakifukuzana kwenye Ubunge (kama ilivyo kwa Mhe. Zitto Kabwe na Mhe. David Kafulila) hukimbilia mahakamani na wanapopewa haki hawalalamiki na huona ni sawa, lakini katika kesi hii kati ya VIP na IPTL imeisha na mahakama imeamua hatutaki kukubali. Tumefikia mahali hatuiamini Mahakama kama chombo cha kutoa haki? Kwa nini hakuna aliyekata rufaa kupinga maamzi ya Mahakama? 

Mheshimiwa Spika, Kwa mujibu wa Hati ya Makabidhiano (Handing Over Note) ya tarehe 5 Septemba, 2013 (Kiambatisho Na. 6), IPTL inaonyesha inaidai TANESCO jumla ya Tshs.370,738,773,651.09 sawa na Dola za Marekani milioni 227.45 kufikia tarehe 5 Septemba, 2013.

Mheshimiwa Spika, Kutokana na hukumu ya Mhe. Jaji Utamwa ya tarehe 05 Septemba, 2013 kuondoa IPTL kwenye ufilisi na kutambua PAP kama mmiliki kwa asilimia 100 wa IPTL, TANESCO ilifanya mazungumzo na IPTL kwa ajili usuluhisho wa hesabu ya fedha ambazo TANESCO ilikuwa haijaweka kwenye Akaunti ya Escrow na kukubaliana jinsi ya kulipa fedha hizo. 

Mheshimiwa Spika, Aidha, kwa mujibu wa barua ya IPTL ya tarehe 20 Septemba 2013, IPTL wanadai TANESCO jumla ya Dola za Marekani milioni 239.6 na Tshs. 33,370,147,675.88/- kama Capacity Charges. Hata hivyo, baada ya TANESCO kukaa na kufanya hesabu upya na IPTL; walikubaliana kuwa madai halali ya IPTL ni Dola za Kimarekani 79.05 milioni. (Kiambatisho Na. 7)

Mheshimiwa Spika, Wakati wa kufunga akaunti ya Escrow Desemba, 2013 kulikuwa na jumla ya Dola za Marekani 22,198,544.60 na Shilingi za Tanzania 161,359,686,585.34 (sawa na Dola za Marekani milioni 122). Baada ya makubaliano kati ya TANESCO na IPTL, Serikali ilisaini makubaliano na IPTL ya kuruhusu fedha za Escrow zilipwe kwa IPTL na kuagiza Benki Kuu ya Tanzania kulipa fedha hizo kwa IPTL na kufunga akaunti hiyo. (Kiambatisho Na. 8).

Mheshimiwa Spika, Pamoja na maelezo ya hapo juu, napenda kusistiza kuwa IPTL ni Kampuni binafsi ya kuzalisha umeme kama ilivyo Kampuni ya Symbion na Songas, Serikali haijihusihi na masuala binafsi ya Makampuni hayo. Mgogoro iliyopo ni kati ya Benki ya Standard Charterd Hong Kong na IPTL, Serikali si sehemu ya mgogoro huo.

Mheshimiwa Spika, ni vizuri sisi kama viongozi wa wananchi tukaheshimu Mahakama zetu na tusipende kuwa wasemaji tu bila uhakika baada ya kupata habari za mitaani.

Mheshimiwa Spika, Naomba kutoa hoja

--
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/d/optout.

Share this :

Related Posts

0 Comments