ALLIANCE FOR CHANGE AND TRANSPARENCY
(ACT – TANZANIA)
"MABADILIKO NA UWAZI"
HOTUBA YA KATIBU WA ACT-TANZANIA NDUGU SAMSON MWIGAMBA KWA WAJUMBE WA KIKAO CHA NDANI CHA WANACHAMA MKOA WA ARUSHA
Utangulizi:
Ndugu wana ACT-TANZANZIA, napenda kuwasalimia kwa salaam ya chama!
Naomba nichukue nafasi hii kwanza kabisa kuwapongeza kwa kuwa miongoni mwa wanachama waanzilishi wa chama kipya cha ACT-Tanzania. Watu wote waliokwishajiunga na watakaojiunga kabla ya usajili wa kudumu wa chama watapewa hadhi ya kuwa wanachama waanzilishi wa ACT-Tanzania.
Ndugu wanachama, natambua kwamba baadhi yenu hamjapata nafasi ya kukaa karibu na viongozi wa juu kama Katibu mkuu wa chama bali mmekuwa mkitegemea zaidi taarifa za kwenye vyombo vya habari na kuna maneno mengi yameandikwa kwenye mitandao ya kijamii. Napenda kutamka mapema kabisa kwamba taarifa rasmi kuhusu ACT – Tanzania ni hizi ninazozitoa leo na zile ambazo zitakuwa zinatolewa na viongozi mbalimbali waliochaguliwa ambao wa kitaifa tumeshawatambulisha na wa mkoa wenu tutawachagua hapa leo wakati wa wilaya uchaguzi wao utasimamiwa na wa mkoa tunaowachagua leo.
ACT Tanzania ni chama kipya cha siasa kinachoamini katika demokrasia jamii na chenye shabaha kuu ya kupigania na kusimamia mabadiliko na uwazi nchini Tanzania. ACT-Tanzania inaamini kuwa mabadiliko yoyote katika jamii lazima yainufaishe jamii husika, na kwamba wananchi wenyewe ni lazima washiriki katika kuleta mabadiliko hayo kwa uwazi na uzalendo.
Mwongozo wa sera za ACT-Tanzania ni maendeleo shirikishi na kuhakikisha uwepo wa uongozi adili na weledi katika ngazi zote. ACT – Tanzania inatokana na maneno "Alliance for Change and Transparency". Kwa mujibu wa Katiba ya ACT-Tanzania, kirefu cha jina la chama kitakuwa ni, "Alliance for Change and Transparency" na kifupi ni, "ACT-Tanzania". Ni Umoja (alliance) wa Mabadiliko na Uwazi. Ni umoja kwa kuwa chama kinawaunganisha na kuwaleta pamoja watanzania wote wanaotaka kufanya mabadiliko ya kweli katika nchi hii.
Kwa sababu hiyo tunatamka rasmi na ieleweke kwa kila mtu kwamba ndani ya ACT – Tanzania tangu kuanzishwa kwake na kuendelea, hakuna mtu mmoja atakayejulikana kama muasisi wa chama wala kikundi cha watu wachache kitakachojulikana kama waasisi wa chama. Ndiyo maana hatujawahi kuwatambulisha hata wale watu wawili waliokwenda kujaza fomu ya maombi kwa Msajili, hatuoni haja ya kuwatambulisha maana kwetu sisi wanachama waanzilishi ni watanzania wote waliokwishajaza fomu na kuchukua kadi na wanaoendelea kufanya hivyo ili chama hiki kiweze kusimama na kuimarika nchi nzima na kujiandaa kuwaletea watanzania mabadiliko ya kweli waliyoyangoja kwa miaka mingi sana!
Ndugu zangu, hiki chama hakina wala hakitakuwa na mwenye chama, ni chama cha watanzania wote waliokubali na watakaoendelea kukubali kwamba mabadiliko ya kweli yanahitajika na kwamba uwazi ni tunu ambayo taifa hili linaihitaji sana kwa sasa. Wenye chama ni Watanzania waliokwisha kubali na watakaoendelea kuikubali itikadi ya chama hiki, misingi ya chama, ahadi za mwanachama na sera za chama. Baadaye kwenye mada ya "Ijue ACT-TANZANIA" nitafafanua kwa kina Itikadi ya chama, misingi mikuu mitano ya chama na ahadi tano za mwanachama. Nitawaelezea pia maendeleo ya chama, mipango yetu ya baadaye na ratiba ya mambo mbalimbali yaliyo mbele yetu.
Tunataka kutengeneza chama cha pekee, chama mbadala wa vyama vyote:
Ndugu wanachama, ACT-Tanzania inakuja wakati ambapo kuna ombwe la uongozi wa kisiasa katika nchi hii. Mfumo wa vyama vingi nchini ulianzishwa kwa malengo makubwa mawili:
• Kupanua wigo wa demokrasia na uhuru kwa wananchi na taifa kwa ujumla ili kuweza kulinda ushindani wa kisiasa nchini
• Kupanua wigo wa kifikra ili kuweza kupata mawazo mbadala juu ya namna ya kukabiliana na changamoto za kimaendeleao, na kuweza kuibua falsafa na sera mbadala katika kuzijibu changamoto hizo ili hatiamye wananchi waweze kuamua kuchagua chama chenye sera bora zaidi kuliko vingine.
Ilitarajiwa kwamba vyama vya siasa vinavyoanzishwa vimilikiwe na wananchi wenyewe badala ya vikundi vya watu wachache waliovianzisha kujiita waasisi.
Tangu mfumo wa vyama vingi urejeshwe hapa nchini mwaka 1992 kuna Mafanikio na Changamoto zilizojitokeza:
• Katika miaka 20 ya vyama vingi hapa nchini, wananchi wameupokea na kuukubali mfumo wa vyama vingi. Wananchi sasa wanavithamini vyama vyote bila kujali ni chama tawala au cha upinzani.
• Vyama vya upinzani vimefanikiwa kutoa changamoto na ushindani wa kutosha kwa chama tawala
Hata hivyo:
• Vyama vingi vya upinzani vimeendelea kuwa vya upinzani lakini vimeshindwa kujipambanua kama vyama mbadala kwa chama tawala kwa kuwa havijaweza kuibua falsafa na sera mbadala
• Demokrasia ndani ya vyama katika nchi yetu imeendelea kuwa finyu. Matokeo yake vyama hivi vimeendelea kujipambanua zaidi na waasisi na waanzilishi wa vyama badala ya wananchi. Kwa kifupi ni kwamba vyama hivi vimeshindwa kujiachia kutoka mikononi mwa vikundi vichache walioanzisha na kujiachia vimilikiwe na wananchi wenyewe
Chama ambacho tumekianzisha kinalenga kuwa chama mbadala katika:
• Kupanua na kuimarisha demokrasia pana ndani ya chama kama msingi wa kujenga demokrasia ya kweli katika jamii ya watanzania
• Kuibua falsafa na sera mbadala zinazolenga kutokomeza ubwanyenye katika kila ngazi na kuzingatia falsafa ya maendeleao shirikishi kwa kuwalenga wakulima, wafanyakazi, na wajasiriamali wanaopambana kuinua kipato chao na kuchangia kujenga taifa kwa nguvu zao. Tunalenga pia kuwapa uhuru kamili wafanyabiashara wakubwa kufanya biashara halali na kutekeleza wajibu wao wa kulipa kodi halali kwa nchi ili kodi hiyo itumike kutoa na kuboresha huduma kwa wananchi wote
• Wajibu mkuu wa mwanachama na kiongozi wa ACT Tanzania utakuwa BIDII na WELEDI KATIKA KAZI kwa kuwa tunaamini kwamba kufanya kazi kwa bidii ndio msingi wa maendeleo ya mtu mmoja mmoja na jamii kwa ujumla.
• Uwazi katika uendeshaji wa chama ili kuwashirikisha watanzania wote wajue nini kinafanywa na viongozi kwa maslahi yao. Uwazi kama tunu ya taifa, utakuwa ndio msingi wa uendeshaji wa serikali ya ACT-Tanzania baada ya kukabidhiwa dola na watanzania kwa njia ya kura.
Nini kinaendelea:
Ndugu wanachama, mara baada ya kupata usajili wa muda, sheria ya vyama vya siasa inakitaka chama husika kusajili wanachama wapya wasiopungua 200 katika mikoa angalau 10 kati ya hiyo miwili lazima iwe ya Zanzibar. Ili kutimiza sharti hilo ilitubidi tuandae kadi na vifaa vingine vinavyohitajika tayari kwa zoezi hilo. Nafurahi kuwatangazia nyote kwamba zoezi hilo limekamilika na uchambuzi pia umekamilika na Jumatatu ya tarehe 24 Machi, tutawasilisha orodha ya wanachama ikiambatana na fomu walizojaza ambazo zilitolewa na ofisi ya msajili wa vyama vya siasa. Kimsingi tumepita lengo kwa kuwa hatukwenda kwenye mikoa 10 tu bali tulienda kwenye mikoa yote ya Tanzania bara na visiwani. Kila mkoa tulipeleka kadi 1000 na hakuna mkoa ambao kadi zilibaki bali katika kila mkoa kuna watu wamebaki wakidai kadi. Nichukue fursa hii kuwashukuru sana watanzania wote katika mikoa yote waliojitokeza kuwasikiliza wawakilishi wetu na kuwaelewa na hatimaye kukubali kujiunga na chama hiki. Ni chama pekee hapa Tanzania ambacho kilianzishwa na umati wa watu nchi nzima.
Tumechagua mikoa 11 kwa upande wa Tanzania bara na mikoa 4 kwa upande wa Tanzania visiwani ambayo ndiyo tunaipeleka kwa msajili wa vyama kwa ajili ya uhakiki. Katika mikoa hiyo mkoa wenu wa Arusha pia umo ukiwa ni wa pili kwa idadi ya watu waliojitokeza kujiandikisha. Naomba mjipongeze kwa hilo!
Kuhusu matukio yaliyo mbele yetu pamoja na ratiba ya kazi za chama kwa wakati ujao, nitaeleza kwa kina kwenye mada yangu ya "Ijue ACT-Tanzania".
Maelekezo mahsusi kwa wanachama na wafuasi wa ACT-TANZANIA:
Napenda kuwasihi wanachama, wafuasi na wapenzi wa ACT-Tanzania katika mkoa wa Arusha na popote mlipo nchini kukumbuka kwamba chama hiki malengo yake ni kusimamia mabadiliko ya kweli. Ni imani yangu kwamba sote tunatambua kwamba tunahitaji mabadiliko haraka kwenye utawala wa nchi hii lakini hatuhitaji mabadiliko ambayo yatawatoa watawala wabovu na kuwaingiza watawala wabovu zaidi, ama kuwatoa watawala wakatili na kuingiza madarakani watawala wakatili zaidi, ama kuwatoa watawala mafisadi na kuwaingiza mafisadi wasiosaza, ama kuwatoa watawala wasio waadilifu na kuwaingiza madarakani ambao uchafu wao umepindukia. Tunahitaji watawala hawa wakiondoka, waingie wazalendo, walio tayari kusimama na wananchi wanyonge, wanaoipenda nchi yao, wanaojali maslahi ya taifa kuliko ya vikundi vyao, ambao wakati wote wanalifikiria taifa kwanza kabla ya vyama vyao. Kwetu sisi, Taifa letu Tanzania kwanza!
Ndugu zangu, Ikiwa hivyo ndivyo, ni muhimu kwa kila mwanachama na mfuasi ama mpenzi kutambua kwamba sisi ni nyota ing'aayo kwa ajili ya kuonyesha dira. Kila mwanachama ahakikishe mahali alipo anawakilisha misingi mitano ya chama. Kila mwanachama aonyeshe kwa vitendo kwamba sisi tupo kwa ajili ya watanzania na tumejiandaa kuwakomboa watanzania. Hatujaanzisha chama hiki kwa ajili ya kuonyeshana umwamba na chama chochote cha siasa kati ya vyama vyote vilivyo na usajili wa kudumu ama wa muda. Hatuna muda huo. Muda tulionao ni wa kuwatumikia watanzania. Na tunaanza kuwatumikia hata kabla ya kuingia madarakani. Lolote lenye maslahi kwa jamii ya watanzania lililo ndani ya uwezo wako kama mwanachama mmoja ama kundi la wanachama ama ngazi fulani ya uongozi wa chama, lifanyeni kwa faida ya watanzania wenzenu. Hatuna muda wa kusubiri mpaka tuanze kukusanya kodi. Yapo mengi yasiyohitaji kukusanya kodi ndipo ulitumikie taifa lako kwa faida ya wengi.
Ndugu wanachama, kuna baadhi ya vyama vimekwishaagiza wanachama wao na kila chombo cha vyama vyao kuishughulikia ACT – Tanzania. Hao tayari wameanza matusi, kejeli, kashfa na kila aina ya propaganda dhidi ya chama chetu. Msihangaike nao, kama kuna jibu zuri mnaloweza kuwarudishia kwa kejeli zao, kwa kashfa zao, kwa propaganda zao, kwa matusi yao, basi ni kuwapuuza! Kuna vyama vinatengeneza matawi ya vyama vyao kwenye mitandao ya kijamii. Waacheni waendelee na kazi hiyo njema kwao, tutakutana Oktoba 2014 na 2015. Iwe ni mwiko kwa mwana ACT-Tanzania kutumia mtandao wowote wa kijamii kurusha matusi na kutukanana na wanaharakati ambao wako busy kufungua ID mpya za mitandao ya kijamii kiasi cha mtu mmoja kuwa na ID saba mpaka kumi halafu kisha anaanza kupost upuuzi huko kwa ID moja na kujipongeza kwa ID tisa zilizobaki na viongozi wake wakiona hivyo wanajilisha upepo kwamba wanachama wameongezeka sana.
Kila mwana ACT-Tanzania akumbuke kwamba wanachama wanapatikana mitaani na vijijini na kila uongozi utakaochaguliwa iwe wa muda ama wa kudumu katika ngazi yoyote, kazi iwe ni kushuka haraka na kutengeneza matawi na mashina ya chama kwenye ngazi ya chini kabisa kukifanya chama kuwa imara na kujiandaa kushinda uchaguzi ujao.
Shukrani:
Napenda ninapomaliza niwashukuru kwa namna ya pekee nyinyi wote kwa kuwa wanachama waanzilishi wa chama hiki. Nawashukuru nyote kwa chochote ulichokifanya katika kuwezesha chama hiki kuwepo na kusonga mbele. Hata kuwepo kwako hapa ni mchango ambao sisi viongozi wa chama tunauthamini sana. Lakini basi mniruhusu niwatambue watu wachache maalum. Kwanza kabisa niwashukuru wale waratibu wa zoezi zima la uandikishaji wanachama waliojitolea kuhakikisha zoezi hili linafanikiwa kwa mkoa wetu wa Arusha. Wale wote waliochukua fomu na kadi na kuwapelekea wengine tafadhali msimame kwa pamoja tuwapigie makofi.
Nawashukuru pia wajumbe wa kamati ya maandalizi ya mkutano wa leo waliohakikisha kwamba tunapata ukumbi wa kukutania, chakula cha mchana na nauli za wenzetu waliotoka mbali kama Ngorongoro, Longido na Karatu. Mwenyekiti wao Ndugu Kivuyo, Katibu Simba, Mhazini Gerald Emmanuel, mkuu wa mawasiliano Mchungaji, na wajumbe Jonas, Basil, Gerald Majengo, na wengine ambao sikupata majina yao mapema ni:……..
Najua mliochangia chama mpaka sasa mko wengi na sitaweza kuwataja kwa majina wote kwa leo lakini siku ya uzinduzi rasmi wa chama, tutawatambua kwa majina na michango yenu wote mlio na mtakao – endelea kuchangia chama hiki kusimama bila kujali aina ya mchango. Narudia kusema sisi viongozi wenu wa kitaifa tumekubaliana kwamba katika chama hiki utakuwa ni utaratibu wetu kila baada ya kipindi fulani tunapotoa taarifa ya maendeleo ya chama, kuwatambua wote waliochangia pesa, muda, raslimali nyinginezo na hata vipawa na taaluma zao katika kuendeleza chama. Nawashukuru pia wataalam wetu ambao wamekuwa wakijitolea kutumia utaalam wao kutushauri katika maeneo kama utafiti, uongozi, sera, raslimali, usimamizi wa fedha, mawasiliano, sheria, sayansi ya siasa, na kadhalika. Tunawashukuru wote popote mlipo na siku ya uzinduzi nanyi tutawatambua mmoja mmoja. Ombi letu ni kwamba muendelee kutusaidia.
Hivi sasa tunakwenda katika hatua ambayo tunawataji zaidi. Tunakwenda kuiboresha rasmu ya katiba yetu na kanuni zake na kutengeneza sera za chama. Tunaomba muendelee kutuunga mkono. Tunatoa wito kwa wataalam wengine tutakaowafikia kuwaomba mtusaidie, tafadhali msisite. Tunahitaji kuwa na katiba ya wananchi, tunahitaji kuwa na sera mbadala na zinazotekelezeka na zitakazotatua matatizo ya nchi hii ya kiuchumi, utawala, miundombinu, huduma za jamii, nk. Na katika hili naomba niwaambie kwamba tutashirikiana na wataalam bila kujali itikadi zenu. Tunahitaji utaalam wako usaidie katika kutengeneza kitu kwa manufaa ya watanzania wote na hivyo hatuna shida na itikadi yako ya kisiasa. Hatuna pesa za kulipia ujuzi mnaotupatia lakini siku taifa hili likipata mabadiliko yanayotakiwa, historia itawaenzi.
Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki ACT-Tanzania, ahsanteni kwa kunisikiliza!
Samson Maingu Mwigamba,
Katibu mkuu Taifa.
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/d/optout.
0 Comments