Ndugu zangu,
Kuna habari kubwa leo; mkutano wa Zitto na Dr. Kitila Mkumbo na Watangazaji wa habari.
Wengine sisi ni wadadisi na wachambuzi wa habari. Kuna wanaotuita wachunguzi wa mambo. Na ndio kazi ninayoifanya sasa.
Naam, nimesoma ya magazetini na michango ya mitandaoni kuhusiana na sakata la Zitto na chama chake, Chadema.
Nionavyo, Chadema kwa sasa iko kwenye ' Civil War'- Ni vita yake ya ndani, lakini, kuna walio nje ya Chadema wanayoifuatilia kwa karibu sana vita hii, ikiwemo ' Watani' wao wa jadi, CCM.
Na CCM hawana hata kimoja cha kuiombea heri Chadema kwenye vita hii ya ndani ya chama hicho. Anayefikiri vingine hazijui siasa za nchi hii.
Kuna mawili yanayoweza kutokea kwenye ' Civil War' hii ya Chadema; Mosi, kuwa yaweza kuwa mwanzo wa mwisho wa Chadema au mwanzo wa mwisho wa Zitto Kabwe. Kwa Chadema ni mwanzo wa mwisho wa kuwa chama kikuu cha upinzani. Na kwa Zitto ni mwanzo wa mwisho wa kuwa mwanasiasa anayeheshimika na kuonekana makini kwenye siasa za upinzani na harakati za mageuzi nchini. Hii ni vita isiyo na matokeo ya kutoka sare, lazima mshindi apatikane.
Ni vita isiyo na suluhu. Na media inaweza kutumiwa kama ' Uwanja wa Mapambano'. Yawezekana pia kukawa na ' media war' katika vita hii, kwamba media nayo itapambana yenyewe kwa wenyewe kwa vile kuna watakaochagua upande. Naam, sambamba na media, uwanja mwingine wa vita utakaotumika ni mikutano ya hadhara.
Na vita hivi vikiendelea kwa muda mrefu vitakuwa na madhara makubwa si tu kwa wahusika wakuu, bali, vitarudisha nyuma juhudi za nchi yetu kujenga misingi imara ya demokrasia ya vyama vingi ambayo inahitajika sana katika dunia tunayoishi sasa.
Na Zitto Kabwe anakwenda kuwaambia nini Watangazaji wa Habari?
Kuna mawili ninayoyaona;
1. Haitarajiwi kuwa Zitto atakwenda kuwaambia watangazaji wa habari kuwa ' Anatua mbanji' na kwamba yalopita si ndwele.
Zitto anakwenda kujibu mapigo. Hivyo, atapigana kupangua shutuma alizoshushiwa na chama chake. Kisha ataahidi kubaki Mwanachadema na atawaachia wanachadema watoe hukumu yao na hivyo, waamue hatma ya mgogoro uliopo na hatma yake.
2. Zitto na mwenzake Kitila Mkumbo wanaweza, baada ya hotuba ya utetezi, kutangaza rasmi kujitoa Chadema. Hivyo basi, kufanya kitakachoitwa ' Maamuzi Magumu'. Wanaweza pia, ama kutangaza anwani ya chama wanachokwenda kuhamia, au kuliacha hilo kuwa ni jambo ambalo hawajalifanyia maamuzi. Kwamba wanatafakari.
Na ni nini sababu hasa ya vita hivi?
Yawezekana sababu ziko nyingi. Lakini, moja kubwa ninayoiona ni ukweli, kuwa ni vita ya kugombea uongozi na mamlaka. Ni kuanzia ndani ya chama hadi kwenye dola, kuelekea 2015. Na hili ni tatizo la vyama vyetu vya siasa, ikiwamo CCM. Kinachowasaidia CCM ni ukweli kuwa wao ni Chama Dola. Kiukweli hatuna misingi imara ya demokrasia za ndani ya vyama- Intra party democracy.
Wengi wa wanasiasa wetu huwa hawajui chama wanachokitumikia kinataka nini, ila wanajua, wao kama wao wanataka nini. Mara nyingi Vyama vyetu hivi huwa havina misimamo na maono ya pamoja ila ya kiongozi mmoja mmoja. Kila mtu na lwake, au la kijikundi chake. Na misimamo ya pamoja itokane na uwepo wa uwazi na uhuru wa kutoa fikra , hata zenye kukera. Kutokakuwepo kwa mazingira hayo ni moja ya udhaifu mkubwa ndani ya vyama vyetu hivi.
Na mara nyingi imesemwa, kuwa chama ni vikao, lakini, chama ni zaidi ya hapo. Chama ni chaguzi. Maana wajumbe wa vikao wanatokana na kuchaguliwa na wanachama. Hivyo basi, chaguzi za wazi na haki, na kwa mujibu wa kalenda za vyama ni moja ya njia za kupunguza hatari ya kuwepo kwa migogoro ndani ya vyama.
Maana, katika yote tuyafanyayo, tuhakikishe, kuwa maslahi ya nchi yetu yanawekwa mbele, kwamba tunaimarisha demokrasia ya vyama vingi na hivyo kuifanya nchi yetu kuwa ya kisasa zaidi.
Kamwe tusishiriki harakati zitakazochangia kuirudisha tena nchi yetu sio tu kwenye mfumo wa chama kimoja, bali hata jirani na mfumo huo. Ni mfumo uliochangia kudumaza fikra za Watanzania kwa kuwajengea raia hofu. Ni mfumo uliotengeneza viongozi ' Miungu Watu'. Ni mfumo kandamizi.
Jumapili Njema.
Maggid Mjengwa.
0754 678 252
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/groups/opt_out.
0 Comments