[wanabidii] Mapinduzi ya Zanzibar: Ukombozi wa wanyonge au uvamizi na ukandamizwaji wa haki?

Monday, August 05, 2013
Tangu kufanyika kwake siku ya tarehe 12 Januari 1964, Mapinduzi ya Zanzibar yameacha mjadala miongoni mwa wanasiasa na wataalamu wa masuala ya historia, siasa na sheria. Wakati baadhi yao wakiyaona mapinduzi hayo kuwa tukio muhimu la kihistoria lililong'oa mizizi ya ubaguzi, wapo pia wanaoyaona mapinduzi hayo kuwa uvamizi wa serikali halali uliofuatiwa na uvunjwaji mkubwa wa haki za binadamu.

Katika kipengele chetu cha leo cha mnyukano wa hoja, tunawaletea makundi mawili ya wanasiasa na wasomi wa kizanzibari yanayopingana kuhusu mapinduzi ya Zanzibar. Kama ilivyo desturi yetu, wasomaji wetu ndiyo majaji kwa kupitia "comments'' hoja, na mitazamo yenu. Karibuni Sana!

Sasa tuanze na kundi la kwanza. Kundi hili linawahusisha wale wanaoyaona mapinduzi ya Zanzibar kuwa
tukio la kidhalimu la kuipoka madaraka serikali halali. Kwa bahati mbaya, maandiko ya kundi hilo hayasemwi sana na baadhi yamepigwa marufuku. Baadhi ya watu wa kundi hili huyapiga kijembe mapinduzi ya Zanzibar kwamba yalipangwa na kuratibiwa na watu kutoka nje na si Wazanzibar wenyewe. Hebu tuwapitie  baadhi yao:

  1. Amani Thani Fairoz: Huyu amewahi kushika nafasi ya ukatibu wa Chama kilichopinduuliwa cha Hizbul Wattan (Zanzibar Nationalist Party). Kwenye kitabu chake ''UKWELI NI HUU: KUUSUTA UWONGO'' anajenga hoja kwamba mapinduzi ya Zanzibar yaliongozwa na wageni na kwamba yaliipindua serikali halali iliyochaguliwa na wananchi. Kwa maneno yake mwenyewe anasema (Uk 65-66) ''Mafisadi wachache kwa ajili ya maslahi ya nafsi zao hawakutahayari kuchanganyika na wageni waliokuwepo ndani ya nchi na walioletwa kutoka nchi za jirani kwa makusudio khasa ya kuivamia Zanzibar na kuiondoa Serikali ya Wananchi. Wananchi mafisadi hao walikubali kuongozwa na wageni, John Okello aliyetoka kwao Uganda, Injin alyetoka kwao Kenya na Mfaranyaki aliyetoka kwao Tanganyika, kuivamia nchi yao katika usiku wa manane wa kuamkia tarehe 12 Januari 1964. Wananchi mafisadi kwa sababu ya maslahi ya nafsi zao hawakuhisi uchungu kuipoteza nchi yao, wala kuzipoteza roho za wazee wao, za ndugu zao na marafiki zao. Kwa mujibu wa kitabu cha huyo aliyejipa ujemedari wa hayo ''mavamizi''…John Okello amesema kuwa watu waliokufa…ni 13,000. Hii ni idadi ndogo kabisa aliyopenda kuitaja.''

  2. Madai haya ya Amani Thani yanaungwa mkono na Issa Nasser Issa Al-Ismaily mwandishi wa kitabu cha ''ZANZIBAR: Kinyang'anyiro na Utumwa'' (Uk 95-96) ''Ni wazi kuwa serikali hiyo haiwezi kulaumiwa kwamba ilipinduliwa kwa makosa haya au yale ya utawala mbaya kwa sababu haikuwa haikuwa katika madaraka kwa muda wowote wa kutosha….Serikali halali ilipinduliwa kwa dhulma tu bila ya makosa yeyote. Huu ni ukweli ulio wazi na usioweza kupingwa kwa njia yeyote. Wengi kati ya hao waliopindua hawakuwa raia wa Zanzibar. Walikuwa wageni.'' 

  3. Prof Ibrahim Noor Sharif kwenye utangulizi (Zinduo) wa kitabu cha ''ZANZIBAR: Kinyanganyiro na Utumwa'' anayakosoa mapinduzi ya Zanzibar n kuwa jambo lililoleta balaa badala ya neema (Uk xxv-xxvi) ''Iwapo sababu kubwa ya kufanya mapinduzi ni kuondosha dhulma zilizokuwapo wakati wa ukoloni, mbona katika mapinduzi yenyewe na kwa miaka mingi iliyofuata raiya wengi walidhulumiwa bure-walifungwa bila ya sababu, waliadhibiwa vikali na hadi kutolewa roho zao kama mijusi, na haya yalifanywa kuwa mambo ya kawaida tu!—Ukhabithi uliopita Zanzibar hatujapata kuuona wala kuusikia ila katika utawala wa Kiportugizi. Natija kubwa ya matendo maovu na mengineyo kama hayo yameifanya Zanzibar kufikia katika hali ya chini na ya kusikitisha sana takribani katika kila kitu. La iwapo sababu kubwa ya kufanya mapinduzi ni kuifanya nchi na viongozi wake wawe wan chi huru, wanahishimiwa duniani, na kuwafanya wao na raiya kuishi maisha mazuri kiuchumi, haya yote yanakosekana…Zanzibar leo imetawaliwa na moja kati ya nchi za kifakiri kabisa duniani, bila ya wazanzibari wenyewe kufurukuta. Zanzibar imekuwa kama pweza juu ya makaa ya moto! Kutaka kujinusuru na moto wa makaa hayo, pweza huyo huzidi kujisogezea makaa ya moto!''

  4. Dk Harith Ghasani. Katika kitabu chake cha ''Kwaheri Ukoloni, Kwaheri Uhuru'' ambacho ni mkusanyiko wa simulizi za watu mbalimbali kuhusu mapinduzi, Dk Ghasani amekusanya mitazamo mbalimbali inayokinzana kuhusu mapinduzi ya Zanzibar na Muungano. Mtazamo unaopewa nafasi kubwa ndani ya kitabu ni kwamba mrengo mkuu wa mapinduzi ni ule uliopangwa na kuratibiwa Tanganyika chini ya Oscar Kambona. Simulizi zinajenga dhana kwamba Kambona alikuwa akitekeleza maagizo ya Mwalimu Nyerere. Wasimuliaji wanaibua madai kwamba baadhi ya wanamapinduzi walikuwa wafanyakazi wa Mkonge waliofunzwa kwenye mapori ya Tanga.

  5. Maalim Seif Sharif Amadi kwenye utangulizi wa kitabu kuhusu kumbukumbu za maisha yake na Ali Sultan (Race, Revolution and Struggle for Human Rights in Zanzibar ambacho tutakiita kwa kifupi RRS) mwandishi anamuelezea Maalim Seif kuwa miongoni mwa wayapingao mapinduzi kwa kigezo cha uvunjifu wa haki za binadamu(Uk 3) ''Seif Sharif Ahmad, however, regards the revolution a disaster in terms of human rights, an event to be regretted deeply''. Pia Maalim Seif ni miongoni mwa wanaoamini kwamba nguvu kutoka nje ndizo zilifanikisha mapinduzi (Uk 22 wa kitabu cha ''Kwaheri Ukoloni, Kwaheri Uhuru'') ''Julius Nyerere, Rais wa Tanganyika ana sehemu ya lawama kwa mapinduzi ya Zanzibar. Aliamini kuwa Zanzibar ni sehemu ya Tanganyika na alianza kuyaingilia mambo ya Zanzibar mapema kuanzia miaka ya 1950… Mpaka sasa hivi hadithi iliyopo ni kwamba Wazanzibari ndiyo walioyapanga mapinduzi, lakini kuna ushahidi kuwa Tanganyika ilihusika ten asana…kwa kutumia ujanja, Watanganyika waliyagubika mavamizi yaonekane kuwa mapinduzi na ndio mwanzo wa matatizo ya Zanzibar kama dola.

Hisia yangu ni kuwa Nyerere ndiye alikuwa kichwa nyuma ya mapinduzi. Ni vigumu kuziamini hadithi zenye kusema kuwa mwanzoni wanamapinduzi waliipindua serikali kwa mapanga tu; silaha walizozitumia zilitoka bara. Nyerere anabeba lawama pamoja na wanasiasa wa Kizazibar kutoka pande zote mbili…Wanasiasa wetu wenyewe walimpa Nyerere fursa kuyaingilia mambo ya Zanzibar.''

Sasa tuwageukie wale wanaoyaona Mapinduzi kuwa tukio la lazima na la ukombozi wa wanyonge.

  1. Ali Sultan Issa anayaona mapinduzi kuwa tukio liliondosha unyonyaji wa kimatabaka. (Uk 3 wa RRS) ''Ali Sultan Issa supports the revolution on socialist principle as an event that liberated islanders from a colonial system of class exploitation''
  2. Dk Salmin Amour kwenye tasnifu yake ya Shahada ya uzamivu kwenye chuo kikuu cha ''Karl Marx Party College''( RRS uk 4) anayatetea mapinduzi kwa kigezo cha kuifanya Zanzibar kuwa chini ya udhibiti wa Waafrika. ''Amour's image of pre-colonial past makes possible his claim that the revolution restored island society to its former moral equilibrium and the establishment of the society of tolerance and mutual respect''
  3. Omari Ramadhan Mapuri (RRS uk 4) anayaona mapinduzi kuwa tukio la lazima kwa sababu Mwingereza hakuwa refa wa haki. ''Africans confronted an imagined alliance between the British colonial government, the Sultan and Arab politicians. The British were not neutral referees; they wanted to leave behind an Arab state in Zanzibar and employed all kinds of political maneuvers, intimidations and humiliations intended to divide Africans''
  4. Abood Jumbe kwenye kitabu chake kilichotarjumiwa na Ally Saleh (Partnership: Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Miaka 30 ya Dhoruba) anaeleza mambo kadhaa kuhusu mapinduzi. Kwanza (uk 15) anaelezea matabaka ''kwa kitambo cha vizazi vitatu, Zanzibar ilikuwa imegawanyika katika misingi ya kikabila, kiuchumi na kijamii na kuongozwa na bakora na taratibu za utawala wa Kiingereza. Wazanzibari wakawa watu walio chini ya himaya ya Waingereza na utawala wa usultani wa kiarabu kwa karne tatu. Wakapigana kwa uchungu kushinda chaguzi nne zilizokuwa na upendeleo…'' Kisha anajenga hoja (uk 12) kwamba uhuru wa mwaka 1963 haukuwa wa umma bali ulikabidhiwa kwa Sultan. ''Wakati wa kukabidhiwa uhuru pale ilipotokea kuwa nyaraka za uhuru zilizotolewa na Duke wa Edinburgh zilipotolewa kukabidhiwa kwa Mfalme Jamshid bin Abdullah Khalifa Haroub na sio Waziri mkuu Mohamedi Shamte, ujumbe wa ASP ulikwenda Pemba…Mikutano kadhaa ya hadhara ilifanyika ili kuwapoza wapenzi na wanachama wa ASP na kuwahakikishia kuwa tama ya kuleta uhuru haijapotea. Biramu letu kuu likawa INSHALLAH, Mungu yuko, Waafrika tutajitawala''.  Mzee Jumbe anaelezea pia kuwapo kwa mrengo wa kijeshi wa chama ambao hata yeye licha ya kuwa katibu wa mipango wa chama, aliufahamu asubuhi ya mapinduzi. Kwa maoni yake, huu ndiyo uliotekeleza mapinduzi chini ya Karume.
…………………………
Kwa maoni yako, unadhani ni upande gani uko sahihi kati ya makundi haya mawili?
………......

Ili kufahamu taarifa/simulizi/uchambuzi wa vitabu, endelea kutembelea ukurasa wetu wa "Kitabu Nilichosoma'' kwenye Facebook.com. Usisahau pia ku-like ukurasa wetu ili kukuza mtandao wa watu tutaowafikia. Kaulimbiu yetu ni KITABU NI SILAHA.


Source: http://www.wavuti.com/4/post/2013/08/mapinduzi-ya-zanzibar-ukombozi-wa-wanyonge-au-uvamizi-na-ukandamizwaji-wa-haki.html#ixzz2b5ew2X2u

--
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/groups/opt_out.
 
 

Share this :

Previous
Next Post »
0 Comments