[wanabidii] Lowassa na TB Joshua?

Sunday, July 03, 2016
NIANZE makala haya kwa kukiri kuwa hakuna wakati nimeona fahari kuwa raia wa Tanzania kama sasa. Inaelekea kuwa Rais, Dk John Magufuli, hataki mizaha. Ni dhahiri kuwa hakuna cha msalia mtume. Bila shaka mafisadi wanaandaliwa tukio la kihistoria.

Nilifikia hatua ya kufikiri kuomba uraia wa China. China inanivutia kwa jinsi inavyokabiliana na maovu. Ukikamatwa na dawa za kulevya China umekwisha. China unanyongwa ukipatika na hatia ya kuuza, kuingiza ama kutengeneza japo gramu 50 tu ya dawa za kulevya.

Dunia inakumbuka vyema jinsi Janice Linden, raia wa Afrika Kusini, alivyonyongwa
hadi kufa China kwa kupatikana na kilo tatu tu za dawa za kulevya. Pamoja na jitihada za Rais Jacob Zuma kunusuru maisha ya mwanamama huyo mrembo China bado ilimnyonga hadi kufa 2011.

Kama ilivyo kwa dawa za kulevya China haitaki mzaha kwenye ufisadi. Wakikukamata wanakushitaki na ole wako upatikane na hatia. Kifo kinakuhusu. Wanakunyonga hadi kufa.

Philemon Ndesamburo, aliyewahi kuwa Mbunge wa Jimbo la Moshi Mjini, anakubaliana nami. Ndesemburo ni miongoni mwa wabunge makini walioijadili taarifa ya Kamati Teule ya Bunge iliyochunguza mchakato wa zabuni ya kuzalisha umeme wa dharura ulioipa ushindi Richmond LLC ya Houston, Marekani 2006, iliyosababisha, Waziri Mkuu, Lowassa, kujiuzulu.

Ndesamburo, akiwa na ghadhabu isiyo na kifani aliliambia Bunge, "…nchi za wenzetu kama za China, wahujumu wa namna hii siyo kwamba wanajadiliwa, wananyongwa hadharani."

China, kwa mfano, ilimhukumu kunyongwa tajiri Liu Han Februari 2015. Hii ni pamoja na kwamba Han alikuwa na shilingi trilioni 10. Fedha hizo za kifisadi hazikuweza kuinusuru nafsi yake na kuzimu. Gazeti la Telegraph la Uingereza la Februari 9, 2015 liliripoti kuwa Han alikamatwa 2013 na kunyongwa hadi kufa mara moja baada ya kupatikana na hatia ya ufisadi.

China ina operesheni maarufu kwa jina la operesheni Kamata Mbweha. Operesheni hiyo imefanikisha kukamatwa watuhumiwa wa ufisadi 680 waliokimbilia Marekani, Canada, Australia na kwingineko. Walirudishwa China kujibu mashitaka ya ufisadi. Waliopatikana na hatia tayari wamekwishanyongwa. China haitaki porojo kuhusu ufisadi hata kidogo.

Takriban miezi saba ya urais wa Magufuli, kw akweli nilikwishamsahau Edward Lowassa, ambaye Juni 19, mwaka huu gazeti la moja la kila siku nchini lilichapisha habari kubwa yenye kicha cha habari "Lowassa atoboa siri ya TB Joshua Dar." Habari hiyo ilinikumbusha kashfa ya Richmond; kashfa pekee iliyowahi kusababisha Waziri Mkuu kujiuzulu. Ni kashfa ya mfano. Kuicha hivi hivi bila hatua za kisheria ni kosa kubwa.

Habari ile ya Lowassa na TB Joshua ilinikumbusha zaidi kuhusu Kamati ya Dk. Mwakyembe iliyompa Lowassa masharti mawili. Kwanza, ajipime kutokana na ushahidi uliopatikana dhidi yake. Pili, au Bunge lithibitishe ushiriki wake kama angegoma. Nikakumbuka kuwa Februari 7 mwaka 2008 Spika wa Bunge, Samuel Sitta, alimpa Lowassa nafasi ya kujitetea. Lowassa alikuwa na muda wa kutosha kujipanga kujibu lakin badala ya kujitetea alijiuzulu, pengine alifahamu kuwa asingeweza kuwababaisha wabunge makini kama Dk.Wilbroad Slaa.

Pamoja na kukumbuka hayo kuhusu Richmond, nilijiuliza maswali kadhaa; kwamba inakuwaje Lowassa huyu aliyeshindwa urais aanze kuzungumzia masuala hayo ya TB Joshua na uchaguzi mkuu ambao alishindwa kwa njia ya kidemokrasia? Baada ya kujiuliza kwa nini aendelee kujihami licha ya uchaguzi mkuu kupita, nikabaini, pamoja na kwamba bahati mbaya umri wake umesogea na ameukosa urais, pengine bado anakabiliwa na deni kubwa la ahadi binafsi kwa kundi kubwa la washirika wake lililokuwa limemuunga mkono

Sidhani kama ni sahihi kuueleza umma taarifa zenye shaka eti kwamba TB Joshua hakuhudhuria sherehe za kuapishwa Dk. Magufuli kwa sababu yeye, Lowassa. Hatua hiyo nadhani ni sawa na mantiki iliyomo kweye usemi maarufu wa lugha ya Maa kwamba; "Mee esikiria itu eshik." Tafsiri isiyo rasmi ya usemi huo ni "punda hafi bila kurusha ngokoye."

Chanzo Raia Mwema

Share this :

Previous
Next Post »
0 Comments