ALIYEKUWA Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Wilbrod Slaa, amesema mbinu za kukwepa vikao vya Bunge haitavisaidia vyama vya upinzani kama haviwezi kuibua hoja nzito.
Katika mazungumzo yake na gazeti hili aliyoyafanya kutoka Ottawa, Canada, Jumatatu wiki hii, Slaa alisema mbinu hiyo ya kukacha mikutano ingekuwa na nguvu endapo upinzani ungekuwa na viti vingine bungeni na si kama ilivyo sasa ambavyo chama tawala cha CCM ndicho chenye wingi wa wabunge.
Wabunge wa upinzani wamekuwa wakitoka nje ya Bunge la Tanzania katika mkutano huu wa bajeti kwa madai ya kutoridhishwa na uongozi wa Naibu Spika, Dk. Tulia Ackson; wanaodai kuwa ni wa uonevu.
"Nimekuwa Mbunge katika Bunge la Nane, Bunge la Tisa na Bunge Kumi. Ni kweli pia kuwa hapakutokea migongano mikubwa kama ilivyo katika Bunge la sasa. Aidha katika Bunge la Tisa na 10 nimekuwa sehemu ya Uongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni.
"Katika mabunge yote hayo niliyoshiriki, tuliwahi kupinga hatua mbalimbali kwa kutoka nje ya Bunge. Hizi ni haki za kibunge duniani kote, kwa wachache kuonyesha kutoridhika kwao na jambo fulani. Aidha, Ni utamaduni (parliamentary practice) katika demokrasia kuwa 'walio wengi hufanya uamuzi na wachache hupewa haki ya kusikilizwa'.
"Kambi Rasmi ya Upinzani daima tulitambua uchache wetu, na hivyo kwa kutambua hili, hatukuwahi kufanya uamuzi, kwa mfano wa kumsusia Spika, kwa kutambua kuwa hata kama hatumtaki, hatuna wingi wa kutosha kumkataa".
"Tuliendelea kupigilia hoja ili jamii pana ituelewe. Huu ndio mkakati tuliotumia, tofauti na mkakati unaotumika sasa kumkataa Naibu Spika, ambao sina hakika kama utazaa matunda kutokana na wapinzani kuwa wachache bungeni.
"Hii ni halisi na siyo ya kufikirika. Aidha sina hakika wasipofanikiwa watatoa maelezo gani, kuwa wanaonewa! Majibu yako wazi kwa mwenye kufunua macho na masikio yake.
"Kwa kutambua uchache wetu, ukombozi wetu daima ulikuwa katika kukazania matumizi sahihi ya Kanuni za Bunge. Ninavyoona, pamoja na dalili za 'uonezi' zinazoonekana, lakini pia hali hiyo inatokana na matumizi yasiyo sahihi ya Kanuni kwa upande wa upinzani.
"Ni jambo la kawaida, hata mahakamani watu kukosa haki inayoonekana ya msingi kwa kosa dogo la kisheria au kanuni (technicality). Kama huna akidi, basi unatakiwa kufidia uchache wenu kwa ubora na umakini wa hali ya juu ili kufikia malengo yenu.
Hili naliona ni dosari kubwa," alisema Slaa aliyewahi pia mgombea urais kwa tiketi ta Chadema kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010.
Katibu Mkuu huyo wa zamani aliyeachia wadhifa wake huo kupinga chama hicho kumteua Edward Lowassa kuwa mgombea wake wa urais kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana alishauri upinzani kufanya mambo ambayo yatawagusa wananchi na si kutoka bungeni pekee.
"Upinzani ufanye uchambuzi wa kisayansi, utafiti wa kitaalamu ili kuibua hoja mpya. Upinzani ukitaka kufanikiwa, lazima kwanza uaminiwe siyo tu na umma bali hata na watumishi wa serikali.
"Kila kitu pia kina wakati wake. Ukichanganya kila kitu kwenye chungu kimoja inawezekana chakula hicho kikakosa ladha au kisilike kabisa. Hiki ndicho kinachotokea. Kwa sasa, hakuna hoja za msingi zinazolenga serikali ya Magufuli bali ni malalamiko kuhusu Serikali ya CCM. Malalamiko hayo hayana tija sana, kwa kuwa wananchi wamemchagua JPM kwa nguvu ya hoja zake wakati wa kampeni," alisema.
Wakati huo huo, Slaa ameeleza kwamba mojawapo ya matatizo yanayovikuta vyama vya upinzani hapa nchini ni aina ya matamshi wanayoyatoa kwa serikali wakati wa kueleza hoja zake.
Akitoa mfano, alisema tamko lililotolewa Kahama, Shinyanga hivi karibuni halikuwa la kisiasa bali la kutangaza mapambano na kwamba pengine hiyo ndiyo sababu ya hatua zilizofuata kuchukuliwa na dola baada ya kauli za namna hiyo.
"Katika hali ya kawaida, tamko lile ni kauli ya mapambano. Ukitangaza mapambano (jambo ambalo ni tofauti kabisa na mikutano au kazi za kawaida za kisiasa kwa mujibu wa Sheria na 5/ 1992) ni lazima basi, uwe tayari kupokea kitakachoteka (consequence).
"Kazi ya Polisi kisheria ni kulinda amani na usalama wa raia. Tamko lolote la kibabe au la kimapambano ni dhahiri litapokelewa kwa mfumo ambao sasa unalalamikiwa. Siasa ni hoja tena kwa utaratibu wa kisheria na siyo mapambano kama ilivyotangazwa ( naomba msome tena lile tangazo ili kuelewa ninachosema).
"Hivyo nadhani vyama vinahitaji kujitafakari ( self reflection) kabla ya kulalamika, na waone walikosea wapi. Haki ya Kikatiba ya Mikutano ya kisiasa haiko hewani, ipo ndani ya mfumo uliowekwa iliyowekwa na sheria na mfumo huo nadhani ni muhimu ikaheshimiwa," alisema.
Chanzo Raia Mwema
0 Comments