[wanabidii] Wapinzani kutoka bungeni ni mkakati wa kimakosa

Sunday, July 03, 2016

KWENYE Jamhuri mengine hayawezekani kubadilishwa kwa wabunge kutoka tu kwenye vikao vya Bunge. Kuna wakati mbunge Tundu Lissu hakuonyesha kumtambua Rais. Ni hivi, kwenye Jamhuri Rais akishaapishwa ndio ameshakuwa Amiri Jeshi Mkuu.

Hii ndio tafsiri halisi ya jambo hilo. Yawezekana, mwingine akaona, kuwa aliyeapishwa si Rais wake, nalo haliwezekani, kama Rais atakula kiapo kulitumikia Bunge la Jamhuri, basi, huyo ndiye rais pia kwa wabunge waliomo bungeni, ni kwa miaka mitano ijayo.

Maana, unaposema Jamhuri haina Rais una maana Jamhuri haina pia Amiri Jeshi Mkuu. Na kwenye Jamhuri ambapo unaweza kusimama na kusema hayo na kurudi nyumbani kwa amani na utulivu, basi, ujue Jamhuri hiyo ina Rais, na hivyo, mfumo wa kidola unaoheshimu haki za raia kujieleza kwa uhuru na hata kulindwa dhidi ya watakaochukizwa na kauli zao.

Tukaona wakati ule, kuwa Rais alihutubia Bunge, kuna wabunge wa upinzani wakaleta rabsha za hapa na pale, na kuna waliotulia kumsikiliza Rais wa Awamu ya Tano alipotoa mwelekeo kwa taifa.

Kilichopo sasa, wabunge wa upinzani wanatoka wakimsusia Bunge Naibu Spika, Dk. Ackson Tulia. Swali la kujiuliza; Unafanyaje na Naibu Spika aliyechaguliwa na wabunge wenyewe na kuapishwa?

Hakika swali hili lilipaswa wajiulize wabunge wa upinzani wenye kutoka bungeni kila baada ya dua ya asubuhi. Kwa kufuatilia kwangu siasa za nchi hii na dunia, na kwa kuyaangaalia mahitaji ya wananchi kwa sasa, naona mkakati huu wa wabunge wa upinzani ni wa kimakosa.

Ni mkakati utakaokuwa na gharama zaidi kwa wapinzani huko tunakokwenda kuliko Chama cha Mapinduzi chenye wabunge wengi bungeni. Unapopanga kulifanya jambo ni vema ukatafakari pia matokeo ya jambo husika. Kwa sababu za kibinadamu, ikiwamo kupandwa na jazba na mengineyo, wapinzani kutoka Bungeni siku ile ya kwanza baada ya mtafaruku kuanza ingeeleweka kwa wapiga kura.

Lakini, kwa kuendelea kwao kutoka kila asubuhi ya siku ya kazi za Bunge walizotumwa na wapiga kura kwenda kuzifanya inaanza kujenga hisia miongoni mwa Watanzania, mimi mmojawapo, kuwa huko ni kukosekana kwa umakini.

Niliangalia Bunge lilipoanza jana asubuhi na hakika nilisikitika moyoni. Naamini, siko peke yangu, maana, hayo si matarajio ya Watanzania kuwa na wabunge watakaokuwa wakichaguliwa na kufanya mambo kama yale.
Kama nchi, hakuna namna yeyote ya kuikimbia mifumo na kanuni tulizojiwekea. Haina mashiko, hoja ya kumkataa mtu katika nafasi yake na ambaye hajafanya lolote linalomtaka ang'atuke kwa mujibu wa kanuni, sheria na taratibu zetu kimfumo.

Kama mbunge hamtaki au hampendi Naibu Spika, hakuna anayemlazimisha, nje ya Bunge, kumwalika Naibu Spika kwenye kipaimara cha mwanawe au sherehe ya Maulid.

Na kimsingi, yanapotokea mapungufu ya kimfumo ndani ya kanuni, sheria na taratibu zetu mahali pekee kwa kuanzisha jitihada za kuyabadili hayo ni ndani ya Bunge au mahakamani. Si kwenye viwanja vya Bunge. Na kwa ilivyo sasa hakuna namna, Wabunge wanaotoka itafika siku itawalazimu wabaki tu ndani ya Bunge na Naibu Spika huyo huyo. Tatizo hapa watakuwa wamepoteza muda mwingi nje ya Bunge badala ya kuwa ndani na kufanya kazi ya kuwatumikia wananchi kupitia Bunge.

Hii ni Nchi Yetu sote. Iko siku wapinzani ndio watakaounda serikali na Spika au Naibu Spika atatoka miongoni mwa wapinzani wa sasa. Kama wabunge wa CCM watafanya haya ya kutoka bungeni kwa vile tu hawatampenda au kumtaka Spika, basi, kwa namna hii hii, tutawashutumu wabunge hao wa CCM kwa wakati huo.


Chanzo Raia Mwema

Share this :

Previous
Next Post »
0 Comments