[wanabidii] Lipumba, Mbatia na Mbowe mnanidai Mijeledi

Tuesday, August 04, 2015

Lipumba, Mbatia na Mbowe mnanidai Mijeledi

Luqman Maloto

Juzi, nikiwa nimeketi sebuleni natazama taarifa ya habari, upande wa pili mtoto wangu Nyambo alikuwa anafanya 'homuweki' yake. Kila mmoja alikuwa 'bize' na majukumu yake ya kumalizia siku.

Ila yeye alikuwa ananisumbua, "baba hii ni nini?" Shule afundishwe yeye, majibu nitoe mimi. Nyambo anadhani baba yake ni 'jiniaz', ananiporomoshea 'viingereza' vyake "what is this?" Habari kwamba umande ulinitesa nikatoka nduki hana!

Nilikuwa natazama Televisheni ya Al Jazeera idhaa ya Kiingereza, labda kwa kuona hivyo ndiyo akadhani 'kiinglishi' kinapanda. Nikimwambia sijui mtoto anakuwa mkali, "teacher said you should help me" hapo ikabidi niwe mkali nikamwambia "tusitukanane mtoto, ohoo!"

Nikabadilisha 'chaneli', nikarudi kikwetukwetu! Si ndiyo nikakutana na habari moto ya Ukawa kumsafisha Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward Ngoyai Lowassa! Mchana wake nilisikia minong'ono kuwa ameshajiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema). Hapo nikaamini safari imekwiva!

Baba mtu nikaanza kupayuka: "Yeees CCM kwisha, 2015 CCM out!" Mtoto akanihoji: "Unashangilia Lowassa kwenda upinzani au Ukawa kumsafisha Lowassa?" Nikamjibu: "Hapa ngoma inogile mwanangu, Matumaini ameondoka, CCM vipandevipande, CCM siwapendi walimkata Matumaini."

"Bora wewe huipendi CCM, mimi nawachukia Ukawa ni waongo sana," Nyambo alisema kwa sauti yenye ghadhabu, ikabidi nimrudi: "Wewe fanya homuweki yako achana na haya mambo ya wakubwa, unapiga kura wewe?"

"Mengine yatapita, hili halipiti baba, Ukawa waongo sana na ukiendelea kuwatetea, siku nikisema uongo nisikuone unanishikia fimbo, patachimbika," alisema akiwa anawaka, akafunga daftari kwa hasira na kuondoka.

Nikaona dogo anataka kunipanda kichwani, nikamwita sauti ya kwanza kimya, ya pili hakujibu akawa anaenda tu, mara ya tatu nikakaza sauti kiume, akaitika, nikamwambia arudi haraka.

Akaja 'kinundanunda', nikamuuliza kinachomtatiza, maana 'testi' yote ya Matumaini kutoka CCM ilikuwa imetoweka kwa ajili yake. Akanijibu: "Wewe kila siku nikikuongopea unanichapa halafu wengine wakisema uongo unawashangilia." Ile sauti ya Nyambo ilikaa kulialia na macho yalilengwa machozi, kama baba ninayempenda mtoto wangu, nilijisikia vibaya, ikabidi niwe mpole.

"Kwani hao Ukawa wamekudanganya nini mwanangu?" Swali langu liliamsha mizuka ya Nyambo, alikuwa mkali kama pilipili kichaa. "Huyu Profesa Ibrahim Lipumba wa Cuf si ni yeye aliyesema CCM imewakosea Watanzania kwa kumpa Lowassa fomu ya kuomba kuteuliwa kuwa mgombea Urais?

"Tena alisema mtu aliyepaswa kuwa jela kwa kosa la ufisadi anajitokeza kugombea Urais na anakwenda kuchukua fomu anapewa. Hawa akina James Mbatia wa NCCR-Mageuzi na Dk. Emmanuel Makaidi, si walikuwa wanatangaza huku na huko Lowassa fisadi? Leo hii wanamsafisha bila aibu!"

Nilikosa cha kuzungumza kwa muda nikawa namtazama Nyambo, nikawaza sijui katumwa kunishawishi nibaki CCM! Alipoona nimekaa kimya akazidi kumiminika: "Siku ile Juni 18, mwaka huu kwenye mdahalo wa wakuu wa vyama vya siasa, ulioandaliwa na Taasisi ya CEO Roundtable, si ilikuwa Mwezi Mtukufu wa Ramadhan?"

Nikapiga hesabu, nikamjibu ndiyo. Akasema: "Basi Lipumba hakufunga siku hiyo, maana nilimuona kwenye runinga akiwa amekaza misuli akielezea jinsi Lowassa anavyostahili kuwa jela, leo hapa anamsafisha, anasema kama ni mchafu mbona hajapelekwa mahakamani, huyu babu vipi?"

"Homuweki yako umemaliza?" Nilimhoji ili asiendelee kukoroma, mtoto mdogo anakoroma mbele ya mkubwa, nilimuona ananikata 'stimu'. Jibu nililokutana nalo lilinikata maini. Nyambo wa siku hiyo si sawa na wa siku zote: "Nitafanya homuweki ukiniahidi na hao Ukawa utawachapa kwa kusema uongo kama vile ambavyo huwa unanichapa nikiongopa."

Nikamtolea macho, jamani mimi nina ubavu gani wa kuwacharaza viboko Ukawa! Tatizo la watoto wanadhani sisi wazazi wao tuna nguvu za kupiga dunia nzima. Alipoona nipo kimya akanisisitiza: "Tena yule Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe na katibu wake Dk. Willibroad Slaa ndiyo uwachape mijeledi mingi."

Aliposema hivyo alikimbilia chumbani kwangu, aliporejea alikuwa ameshikilia nakala tatu za gazeti linalomilikiwa na Mbowe. "Baba unaona jinsi hawa watu wasivyofaa kuaminika? Hapa Mbowe anasema Lowassa dhaifu hatakiwi Ukawa kwa sababu ni bubu. Hili lingine linasema Lowassa anakaribishwa Ukawa.

"Hili la tatu linasema Slaa amekataa watakaokatwa na CCM kwa sababu ni makapi, Ukawa hawatasimamisha mgombea aliyekatwa na CCM. Leo naona chereko za Ukawa kumpokea Lowassa na kumsafisha. Kuna uongo mkubwa kuliko huu? Kuudanganya umma wa Watanzania."

Nyambo ndiye alikuwa nyota wa mazungumzo yetu siku hiyo, aliteleza kama amekanyaga ganda la ndizi: "Septemba 15, 2007 nilikuwa sijazaliwa ila baada ya kuzaliwa na kukuta Dk. Slaa anaitwa shujaa, niliamua 'kugugo' niuone ushujaa wake ulianzia wapi.

"Nikakuta aling'ara kwa kuanika majina 11 ya watu wanaofilisi nchi. Orodha ya Mafisadi, List of Shame! Katika majina hayo aliyoyataja, Lowassa ni namba tisa na washirika wake Rostam Aziz na Adrew Chenge pia wamo!

"Katika Uchaguzi Mdogo wa ubunge Arumeru Mashariki mwaka 2012, Slaa alisisitiza Lowassa ni fisadi na ndiyo maana baada ya kutajwa kwenye orodha ya mafisadi mwaka 2007 hakwenda mahakamani. Akasema Lowassa amejijengea ofisi binafsi ya mbunge yenye thamani ya shilingi milioni 800 wakati wanafunzi wa Monduli wanakaa chini, vilevile alipora mradi wa maji Arumeru na kuupeleka Monduli.

"Sasa baba huyu aliyetupiwa kashfa zote hizo anasafishwaje leo na watu haohao? Fisadi papa wa jana, leo amekuwa kamanda, kivipi? Juni mwaka huu, Slaa aliandika kwenye akaunti yake ya Twitter jinsi ambavyo Lowassa hafai kwa sababu ana madoa ya uadilifu."

Mtoto akachukua kompyuta mpakato, akatafuta vya kutafuta kisha akanionesha 'twiti' za Slaa, zilisomeka: "Lowassa tumemtaja katika Orodha ya Mafisadi walioifikisha nchi hii katika hali mbaya kabisa. Kilele kikiwa sakata la Richmond."
Nyingine ikasomeka: "Suala kwamba watu wenye madoa ya uadilifu wanaota Urais wa nchi ni wazi kwamba kupita katika chama chao si uadilifu."

Akaniuliza: "Umeona?" Kwa sauti ya iliyokosa unyoofu nilimjibu: "Ndiyo mwanangu." Kwa hakika Nyambo alinithibitishia kuwa yeye ni mzaliwa hasa wa kizazi cha kuhoji. Kwa siku hiyo alinitoa 'nokauti' kwa hoja zake nzito. "Sijui shuleni kwao mwalimu huwa anawapigisha stori za siasa," niliwaza, maana kwenye madaftari yake hakuna somo la siasa.

Nyambo katika ubora wake: "Nilisoma pia Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Mashariki, Mabere Marando alimhusisha moja kwa moja Lowassa na ufisadi wa fedha Benki Kuu kwenye Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA), vilevile Mwanasheria wa Chadema, Tundu Lissu amekuwa mshereheshaji sana wa ufisadi wa Lowassa. Sasa leo tunaona nini?

"Sasa chama kipi ambacho hakizingatii maadili katika kupitisha majina ya wagombea? CCM au Ukawa? Mtu ambaye kwa zaidi ya miaka nane ameimbwa nchi nzima kuwa ni fisadi, leo hii anasafishwa kienyeji tu! Eti mbona hakupelekwa mahakamani, walitaka apelekwe na nani kama waimbaji ni wao wenyewe?

"Yaani wewe mwenyewe utoe tuhuma halafu baadaye umsafishe uliyemtuhumu kwa sababu hakupelekwa mahakamani na unaongezea hakuna mwenye ushahidi aliwahi kujitokeza. Kwa hiyo ulikuwa unatoa tuhuma za uongo kufurahisha genge? Unajijenga kisiasa kwa uongo! Yaani baba usipowachapa hawa Ukawa na mimi hunichapi tena."

Kwa sauti ya unyenyekevu, nilimwambia: "Basi mwanangu malizia homuweki tukalale." Akaja juu: "Nimekwambia simalizii mpaka uniahidi utawachapa mijeledi Ukawa, waongo sana! Yule Godbless Lema aliwahutubia wananchi Arusha kuwa kumkataa na kumzomea Lowassa ni jambo lenye heshima kubwa kwa nchi kwa sababu ni fisadi, leo anatamba kuwa Safari ya Matumaini inaendelea Chadema, huyu naye ni muongomuongo lazima umchape.

"Wanajitetea eti Lowassa hakuwa tatizo bali mfumo uliopo CCM, wakati kila siku walimtaja moja kwa moja kwamba ni tatizo. Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika alisema CCM inamlinda Lowassa kwa sababu upo ushahidi wa ufisadi wake, leo hii CCM wamemkataa kuwa mgombea Urais, Chadema na Ukawa wamemkubali, nani anamlinda?"

Nilimwangalia, akanisistiza nijibu swali. Nikamwambia sijui, akaendelea: "Hujui eeh! Hivi Ukawa wanaposema tatizo ni mfumo, mfano mtu akiwa anaishi nyumba jirani, kila siku mnalamika hamlali anawaibia, siku akihamia nyumbani kwenu ndiyo mnasema tatizo la wizi wake lilisababishwa na nyumba aliyokuwa anaishi? Baba nijibu utawachapa huwachapi?"

Kwa upole ikabidi nimwambie: "Nitawacharaza mijeledi waongo sana hao." Nilijibu hivyo ili kumaliza ubishi. Akasema: "Hapo sawa, nami namalizia homuweki yangu nikalale. Usipowachapa hatutaelewana, siyo unaniitikia tu. Na ukiwachapa uwaambie mimi ndiye niliyekutuma

 JamboLeo

Share this :

Related Posts

0 Comments