[wanabidii] CHADEMA na demokrasia staili ya Sepp Blatter!

Thursday, September 18, 2014

KUNA watu duniani Mungu amewapa kipaji cha kushawishi. Mmoja wa watu hao wanaonisisimua ni Rais wa FIFA, Joseph Sepp Blatter.

Blatter ana kipaji cha kuwafanya watu anaozungumza nao waamini katika kile anachokisema - hata kama kitu chenyewe ni uongo. Waingereza wana neno linalozungumzia sifa hii – cunning. Haishangazi kuwa kabla hajajitosa kwenye soka aliwahi pia kuwa mshereheshaji wa harusi aliyekuwa akikodiwa kwa malipo ya pauni 75 tu. Sifa yake kubwa ilikuwa kuimba na kutoa mizaha iliyovunja mbavu waalikwa kwenye sherehe za harusi.

Rais huyo wa FIFA ametumia mchanganyiko wa vipaji hivyo kukaa madarakani kwa vipindi vinne, na sasa anataka kugombea tena uongozi wa chombo hicho kwa kipindi cha tano katika uchaguzi utakaofanyika mwakani.

Ingawa inaaminika kuwa Blatter hutumia pia mapesa yake kuwahonga wenye nia ya kuchuana naye waachane mapema na wazo hilo, lakini ni u-cunning wake ndiyo mara nyingi humsaidia kuwafanya wapinzani wajitoe, na hivyo kuchaguliwa kirahisi kuwa Rais wa FIFA.

Katika uchaguzi wa 2011, Blatter alimshawishi Michel Platin asijitokeze kuchuana naye, na akamuahidi ya kuwa uchaguzi wa mwaka 2015 atamwachia yeye agombee. Platini akamuamini, akaacha kugombea.

Lakini kilichotokea hivi karibuni ni kwamba Blatter amemgeuka Platini. Ametangaza kwamba atagombea tena 2015 kwa awamu ya tano. Hoja yake ni kuwa eti "bado ana kazi hajaimaliza FIFA". Na kwa u-cunning wake, amefanikiwa kumshawishi tena Platini asubiri hadi uchaguzi mwingine!

Kinachokera wengi ni kwamba karibu marais wa mashirikisho yote ya soka duniani ambayo yako 208 yanamuunga mkono hata pale anapotoa matamshi tata yanayoweza kutafsiriwa kuwa ni kejeli dhidi ya uwezo wa kufikiri wa wapenzi wa soka duniani.

Mfano wa matamshi hayo ni yale kwamba: "A mission is never finished, and my mission is not finished. They begged me to contest. It is a matter of respect to the 'FIFA Family' to say I will be ready, I will be a candidate (malengo hayaishi, na malengo yangu katika FIFA hayajaisha. Wamenibembeleza nigombee; nami naona ni jambo la heshima kwa 'Familia ya FIFA' kuwakubalia na kusema ndiyo nitakuwa tayari kugombea, nitagombea."

Kwa kauli yake hiyo kwamba 'malengo hayaishi', ni dhahiri Sepp Blatter atagombea urais si tu awamu ya tano bali pia ya sita, saba nk kulingana na hali ya afya yake itakavyokuwa. Hivi sasa ana umri wa miaka 78.

Sasa, huyo ndiye Sepp Blatter wa FIFA. Ni mtu ambaye ameleta mapinduzi makubwa chanya katika mchezo wa soka duniani, lakini dosari yake moja kubwa ni hiyo ya kung'ang'ania uongozi na kutaka kuchaguliwa bila kuwa na mpinzani!

Kama nilivyosema mwanzo, ukiacha mapesa anayoyamwaga kwa baadhi ya marais wa mashirikisho ya soka duniani kumuunga mkono, ni mtu mwenye mvuto na kipaji cha kuzungumza kinachoshawishi umuamini hata pale anaposema uongo!

Kama vile baba anayezungumza na wanawe waliomzunguka mezani wakila chakula, Sepp Blatter huwachukulia marais hao wa mashirikisho ya soka duniani kuwa ni "Familia ya FIFA", na hujiona yeye kama ndiye baba pekee wa hiyo familia!

Na hao marais hujisikia kama vile wao kweli ni 'watoto wa Blatter', na hivyo ni lazima waheshimu anachotaka baba – hata kama ni kuiongoza FIFA kwa vipindi 10! Maneno haya au lugha hii ya "The Family" hutumiwa pia na ma-Godfather wa vikundi vya uhalifu vya Mafia duniani.

Kwa sababu ya kuchotwa akili zao na ghiliba hiyo ya FIFA Family, marais hao wa mashirikisho ya soka duniani hawahoji kitu hata pale Blatter anapotamba mbele yao kuwa katika miaka yake takriban 20 ya kukaa FIFA (ikiwemo 11 kama rais) ameimarisha mno demokrasi ndani ya FIFA!

Hawathubutu kuhoji au kuulizana: Inakuaje mtu anayetamba kuwa ameimarisha demokrasi katika FIFA awe madarakani kwa takriban miaka 20, na sasa agombee tena urais kwa kipindi cha tano? Je, demokrasi si pamoja na kupisha wengine wenye uwezo kuongoza? Na inakuaje agombee bila kuwa na mpinzani? Huko ndiyo kuimarisha demokrasia katika FIFA?

Si lengo langu leo kuijadili FIFA na Sepp Blatter wake, lakini naweza kudiriki kufananisha kinachoendelea FIFA na kinachoendelea ndani ya vyama vyetu vya siasa Tanzania; hususan vya Upinzani – CHADEMA, CUF, UDP, NCCR, TLP nk.

Chukulia mfano wa CUF. Kwa kipindi cha zaidi ya miaka 20, viongozi wa juu wa chama hicho wamekuwa ni wale wale – Seif Shariff Hamad na Profesa Lipumba. Hivi kweli huo ndiyo ujenzi wa demokrasia? Kwamba katika miaka 20 ni wao tu ndiyo wenye uwezo wa kukiongoza chama hicho? Na wanaweza kujisifu kwa hilo?

Angalia chama kama UDP cha John Cheyo. Chama hiki kimekuwa kama NGO au mali binafsi ya John Cheyo. Tangu kianzishwe kiongozi ni huyo huyo tu, na akiwa jukwaani au bungeni hujenga taswira kwamba ni mpiganiaji wa demokrasia nchini. Lakini ni demokrasia gani hiyo anayoipigania ambayo yeye mwenyewe haifuati katika chama chake? Vivyo hivyo kwa TLP ya Mrema – ni kama NGO yake binafsi tu!

Chukua mfano mwingine wa chama kikuu cha upinzani nchini – CHADEMA. Hiki nacho kwa miaka zaidi ya 10 viongozi wa juu ni wale wale – Freeman Mbowe, Dk. Slaa nk. Na sasa Freeman Mbowe amegombea tena kukiongoza kwa kipindi cha tatu!

Kwa mujibu wa taarifa ambazo sina sababu ya kutoziamini, Kamati Kuu ya chama hicho ilibidi ikutane mwaka 2006  kurekebisha Katiba ili kuondoa kifungu kinachoweka ukomo wa uongozi. Hilo lilifanyika ili kina Mbowe na wenzake wapate kugombea tena uongozi!

Sishangai kwamba hata Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi hafurahishwa na hilo ingawa hana cha kufanya. Kwa hakika, mpenda demokrasi yeyote wa kweli nchini hawezi kufurahishwa na hatua hiyo.

Ukomo wa uongozi ni kitu muhimu katika demokrasi zetu hizi changa, kwa sababu kiongozi anaweza kuendesha chaguzi za uongo na kweli zikamweka madarakani kihila hata kwa zaidi ya miaka 20!

Ndiyo maana chama kinachojinadi kwa umma kuwa kinapigania demokrasi hakiwezi kuwa cha kwanza kuondoa kwenye Katiba yake kifungu kinachoweka ukomo wa uongozi ili tu "mwana familia" (rejea Blatter na 'familia' yake FIFA)  aweze kugombea tena kwa mara ya tatu!

Kwa nini watu wasiamini kuwa chama cha namna hiyo kikikamata dola na kuingia Ikulu kinaweza kupigania pia kuondolewa kwa ukomo wa urais kwenye Katiba ili "Baba wa Familia" aendelee kutawala?

 Lakini zaidi ya yote, chama kinachojinadi kuwa kinapigania demokrasia nchini, hakiwezi kukubali kuweka mgombea boya agombee dhidi ya 'mwana familia' ili tu 'mwana familia' apite kirahisi.

Nina hakika hata Mbowe mwenyewe angeliridhika moyoni kama angekuwa amemshinda mtu kama Zitto Kabwe katika nafasi ya mwenyekiti, na si huyo aliyembwaga kwa tofauti ya kura nyingi!

Ninachojaribu kueleza ni kwamba hulka hii ikiachwa iendelee katika CUF, NCCR, UDP, TLP, CHADEMA nk, itavigeuza vyama hivyo vya Upinzani kuwa ni vya watu binafsi au ni vya genge la watu fulani (The Family) kama ilivyo kwa Sepp Blatter na FIFA  yake.

Isitoshe, vyama vya namna hiyo popote pale duniani huwa na kawaida ya kuitelekeza agenda yake kuu ya asili ambayo ni kukamata dola. Viongozi wake huuchukulia baadaye uongozi kama 'kadi' yao ya kualikwa na mabalozi majumbani mwao au kualikwa Ikulu kunywa chai na Rais na mialiko mingine!

Ndugu zangu, ni kweli kwamba Blatter amefanya mambo makubwa mazuri akiwa FIFA. Ni kweli pia kuwa kina Lipumba, Seif, Mbowe nk wamefanya mambo makubwa mazuri katika CUF na CHADEMA. Hata hivyo, ifike mahali wakubali nao kuwa uongozi una kikomo – na demokrasia ni pamoja na kubadilishana vijiti vya uongozi!

Kauli kama ile ya Blatter kwamba "a mission is never finished, and my mission is not finished" - hata baada ya kuwa ameongoza kwa miaka 11, haziwezi kukubalika kwa vyama vya siasa vinavyojinadi kuwa vinapigania ujenzi wa demokrasia nchini.

Kina Lipumba, Seif na kina Mbowe wetu - kama wana 'misheni' ambazo hawajazikamilisha, wafike mahali wakubali kuwa zinaweza pia kuendelezwa na viongozi wengine! Wasipokubali hivyo, basi watakuwa si wajenzi wa demokrasia nchini bali wajenzi wa udikteta.

Na mwisho, nimtakie kila la heri Mbowe kwa kupata fursa nyingine ya kuiongoza CHADEMA kwa kipindi cha tatu mfululizo. Ni matarajio yangu, hata hivyo, kwamba hatagombea tena kwa mara ya nne uchaguzi mwingine utakapowadia.

Kama Mbowe atafanya hivyo, basi atakuwa ameigeuza CHADEMA kuwa The Family, na yeye kuwa 'Baba wa CHADEMA' kama ambavyo Blatter ameigeuza FIFA. Huo utakuwa mwanzo wa udikteta mkubwa katika chama hicho utakaokikwaza kushinda uchaguzi hata kama kitafanya kampeni kikiwa na chopa 20!

Tafakari.

- See more at: http://www.raiamwema.co.tz/chadema-na-demokrasia%C2%A0staili-ya-sepp-blatter#sthash.P0vqrcyr.dpuf

--
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/d/optout.

Share this :

Related Posts

0 Comments