[wanabidii] KUJADILI MUUNGANO ISIWE DHAMBI,USALITI

Wednesday, June 04, 2014
KUJADILI MUUNGANO ISIWE DHAMBI,USALITI
Na Happiness Katabazi
KWA muda mrefu Watanzania walikuwa wameaminishwa kuwa kuhoji, kukosoa au kujadili masuala yanayohusu muungano wa Tanganyika na Zanzibar uliofanyika Aprili 26, mwaka 1964 ni dhambi au usaliti.

Dhana hiyo kwa kiasi kikubwa ndiyo iliyosababisha baadhi ya watu kuendelea kutoa manung'uniko ya chini chini yaliyozaa kitu kinachoitwa kero za muungano zilizoanza kutishia uwepo wake, hasa baada ya kusikia mapendekezo ya rasimu ya katiba mpya inayopendekeza uwepo wa serikali tatu.

Kadiri siku zinavyozidi kusonga mbele, kasumba hiyo ya kuutukuza muungano bila kuhoji sababu za kuungana, matatizo na faida zake, sasa imeanza kupotea, watu wanaoanza kuhoji mambo hayo nao wameanza kuonekana si wasaliti au wenye nia ya kuuvunja.

Watanzania wengi hasa wale wa Tanzania bara walikuwa wakihofia kujitokeza hadharani kutoa hoja zinazokosoa baadhi ya upungufu uliomo kwenye muungano na kinachofanywa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), lakini sasa hofu yao inaanza kuyeyuka kama iyeyukavyo theluthi inapokutana na joto.

Baadhi ya Wazanzibar kwa muda mrefu wamekuwa wakilalamikia muundo wa muungano uliopo hivi sasa kwamba umekuwa ukiwanyonya na kukosa fursa ya kujikwamua kiuchumi ikiwemo kujiunga kwenye mashirika mbalimbali ya kimataifa yenye lengo la kuzikwamua kiuchumi nchi wanachama.

Malalamiko ya kuonewa, kunyonywa kutoka kwa viongozi au wananchi wa Zanzibar ndivyo vilivyochangia baadhi ya wanasiasa Tanzania bara kuogopa kuwakosoa wenzao kwa hofu ya kupokea lugha chafu au kushambuliwa kwa kuitwa wabaguzi.

Miaka ya nyuma ilidaiwa kuna baadhi ya wanasiasa, waliwahi kushughulikiwa kimya kimya, tena kikamilifu na dola au vyama vyao kwa kisingizio tu walikuwa wanapinga Muungano.

Kimsingi waliokuwa wakikosoa, kuhoji na kujadili muungano baadhi yao nilizungumza nao, hawakuwahi kufikiria kuvunja Muungano, isipokuwa walikuwa na mtazamo tofauti kuhusu baadhi ya mambo ndani ya Muungano na walikuwa wanataka yarekebishwe kwa njia ya amani.

Mitazamo hiyo pengine ingeachiwa fursa ya kusikika, kero nyingi za muungano zingetatuliwa, na Watanzania hivi sasa wangekuwa wanazungumzia mambo mengine ya maendeleo.

Tunaona baadhi ya wanasiasa waliosulubiwa kule Zanzibar, kimya kimya kwa fitna eti ni wapinga Muungano, Mungu amewajalia kupata madaraka makubwa ndani ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK), ule uovu waliokuwa wakihusishwa nao wa kuvunja muungano, umezikwa ingawa sijui ni katika makaburi gani.

Mei 27, mwaka huu, Mbunge wa Nkasi Kaskazini, Ally Keissy (CCM), aliwashambulia Wazanzibar, kwamba hawana sababu ya kulalamikia kutaka haki sawa kwenye kila jambo la muungano wakati hawachangii kitu kwenye Serikali ya Muungano.

Keissy alitoa kauli hiyo ndani ya Bunge, wakati akichangia hoja ya Hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kwa mwaka wa fedha 2014/2015, inayoongozwa na Waziri Bernard Membe.

Alichangia hoja hiyo akijibu hoja ya Kambi Rasmi ya Upinzani iliyosema kuna upendeleo mkubwa na uwiano usio sawa kati ya Tanzania Bara na Visiwani katika uteuzi wa mabalozi wa Tanzania nje ya nchi.

Anasema kwa zaidi ya miaka 20 Zanzibar haichangii kitu katika Serikali ya Muungano, lakini ndiyo vinara wa Kulalamika na kutaka usawa kwenye kila jambo, hivyo kama wanahitaji haki sawa basi waanze kuchangia fedha.

Wakati akiendelea kuchangia hoja hiyo, Mbunge wa Chakechake, Mussa Haji Kombo (CUF), aliomba mwongozo wa Naibu Spika dhidi ya kauli hiyo huku akitumia maneno yafuatayo:

"Mheshimiwa Spika, kuna mwendawazimu mwingine ni mtu anayepiga piga mawe hovyo, mwingine anakuwa mtu wa kuchekacheka, akipita anaweza kuwa anacheka tu 'kwekwekwe', na mwendwazimu mwingine ni yule anayeongea ovyo mbele ya watu wenye heshima zao kama tulivyo humu ndani."

Baada ya kauli hizo kulitokea malumbano ndani ya Bunge huku baadhi ya wabunge wa Zanzibar kudai Keissy anafanya ubaguzi, amewadhalilisha Wazanzibar kwa kuwaona ni masikini na pia wakampiga marufuku asifike visiwani humo.

Malumbano hayo yalikatizwa na Naibu Spika Job Ndugai, alipoamua kuahirisha Bunge, lakini mambo yaliendelea nje ya Ukumbi wa Bunge ambapo wabunge kutoka Zanzibar waliwahi kutoka nje kumkabili Keissy.

Kama si uwepo wa baadhi ya wabunge wa CCM walioamua kumuweka kati Keissy, mbunge huyo angepigwa na wabunge kutoka Zanzibar ambao walionyesha dhahiri kukerwa na kauli zake.

Ibara ya 17 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, inasomeka hivi: "Kila raia wa Jamhuri ya Muungano anayo haki ya kwenda kokote katika Jamhuri ya Muungano na kuishi katika sehemu yoyote, kutoka nje ya nchi na kuingia, na pia haki ya kutoshurutishwa kuhama au kufukuzwa kutoka katika Jamhuri ya Muungano.

Sasa kwa mujibu wa Ibara hiyo, tumuulize huyu Mbunge wa Magogoni, Kombo Khamis Kombo, amepata wapi madaraka ya kutaka Keissy azuiwe kwenda Zanzibar?

Hivi tukisema Kombo ndie kinara wa ubaguzi na amevunja Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 ya kutaka Keissy asiruhusiwe kwenda Zanzibar, tutakuwa tumekosea?

Wale wabunge wa Zanzibar, walipaswa watuambie tena kwa njia ya amani ni lini walichangia muungano. Mimi namuunga mkono Keissy, kwamba baadhi ya Wazanzibar, kwa sababu wanazozijua wao wamekuwa vinara wa kulalamika kila kukicha, kwamba wanaonewa, mara Muungano uvunjwe, wananyonywa sana na Tanzania Bara na hawaoni faida ya Muungano na kwamba Wabara tuwaachie Zanzibar yao.

Sasa kosa la Keissy hapa liko wapi hadi wabunge hao Wazanzibari watake kumshikisha adabu? Keissy amesema ukweli kuwa baadhi ya Wazanzibar wamekuwa ni vinara wa kulalamika na kutaka uwiano sawa katika kila jambo la Muungano wakati Zanzibar inachangia kidogo.

Kwani si kweli Tanzania Bara inachangia pato kubwa katika Muungano kuliko Zanzibar? Shida inatoka wapi? Mbona nafasi nyingi za uongozi huko Zanzibar zimeshikwa na Wazanzibar na Watanzania Bara hawalalamiki katika hilo?

Napata wasiwasi kuwa huenda wale wabunge waliozua tafrani walikuwa na ajenda yao nyingine wakasingizia Keissy amewakera. Maana haiingii akilini kabisa kilichosemwa na Keissy, ndio kiwapandishe jazba na kutaka kumpiga wakati aliyoyasema siyo mambo mapya na wabunge hao walishindwa kutoa vielelezo vinavyoonyesha aliyosema ni uongo.

Keissy amekuwa jasiri kati ya wanasiasa wachache wa Tanzania Bara ambao wengi wao wamekuwa na mtazamo kama wake, lakini wamekosa ujasiri wa kuuzungumza wazi kwa kisingizio kuwa wanaogopa kutolewa lugha chafu kutoka kwa baadhi ya Wazanzibar na kuambiwa kuwa wanataka kuvunja muungano.

Wengi wa wabunge walizoea kusikia kauli za kukosoa, kujadili muungano kutoka kwa Tundu Lissu, ambaye kwa muda mrefu alikuwa akionekana mstari wa mbele kugusa maeneo yaliyokuwa yakionekana ni dhambi au usaliti kuyazungumzia.

Kauli ya Keissy haiwezi kuwa chanzo cha kuvunjika kwa Muungano wetu, jambo la msingi linalopaswa kufanywa na viongozi ni kuuzungumzia kwa uwazi ili kuuboresha zaidi badala ya kuficha ficha mambo.

Hivi Zanzibar siku hizi wamegeuka kuwa miungu watu hadi hawataki wasemwe au wakosolewe? Maana kila linapozungumzwa jambo lao hata kama ni la ukweli wamekuwa wakali kama pilipili na kuwashambulia wanaotoa kauli husika.

Waziri Mkuu Mizengo Pinda, aliwahi kusema Zanzibar si nchi, baada ya hapo alishambuliwa kana kwamba alifanya uhaini fulani.

Ibara ya 1 ya katiba ya nchi inasema hivi: "Tanzania ni nchi moja na ni Jamhuri ya Muungano."

Ibara ya 2 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inasomeka hivi: "Eneo la Jamhuri ya Muungano ni eneo lote la Tanzania Bara na eneo lote la Tanzania Zanzibar, na ni pamoja na sehemu yake ya bahari Tanzania inapakana nayo."

Lakini kuna baadhi ya wanasiasa kutoka Zanzibar, kwa sababu wanazozijua wamekuwa wakipotosha ukweli huo kwa kusema Zanzibar ni nchi.

Wasomi wa sheria tunafahamu kuwa Zanzibar sio nchi kwa sababu inakosa sifa ya kuwa na uwezo wa kuingia mikataba na mataifa ya nje, tunapaswa kujadiliana matatizo ya muungano bila jazba ili kuondoa mazonge yote yaliyomo la sivyo tutaendelea kufuga matatizo.

Tuendelee kudumisha Muungano wetu.

Chanzo: Gazeti la Tanzania Daima la Jumapili, Juni 1 Mwaka 2014.



Sent from my iPad

--
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com

Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma

Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/d/optout.

Share this :

Related Posts

0 Comments