NA MHARIRI
4th May 2014
Wiki moja tangu Watanzania waliposherehekea miaka 50 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Makamu wa Rais, Dk. Mohamed Gharib Bilal amewataka Watanzania kudumisha Muungano uliopo kwa maslahi ya nchi na kuwapuuza baadhi ya watu wanaotaka uvunjike.
Makamu wa Rais aliyasema hayo mjini Bukoba mkoani Kagera mwishoni mwa wiki wakati akizindua mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa, kwenye uwanja wa Kaitaba ambapo uzinduzi huo ulihudhuriwa na viongozi mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi.
Dk. Bilal alisema Muungano wa serikali mbili uliasisiwa na waasisi wake ambao ni hayati Julius Nyerere na Abeid Amani Karume, hivyo akasisitiza kuwa wananchi hawana budi kuulinda na kuuheshimu, kwani alisema huu ni urithi kwa Watanzania na vizazi vijavyo.
Alisema waasisi wa nchi hii walijenga misingi ya umoja na mshikamano wa kitaifa huku akihimiza uwajibikaji kwa wananchi na viongozi na kupiga vita rushwa, ugonjwa wa malaria pamoja na Ukimwi.
Wakati wa sherehe hizo, Makamu wa Rais aliwataka Watanzania kupuuza masuala yenye viashiria vya kuvunja Muungano huo na kusisitiza kuwa kuna masuala mengi yanayohitaji mapitio ili yaende na wakati.
Kwa kutumia mbio za Mwenge, Dk. Bilal alisema jamii haina budi kuyapuuza yale yote yanayoashiria kuwapo kwa uvunjifu wa amani na utulivu kwa Watanzania, akawasisitiza wananchi kuwajibika kwa kuzingatia heshima.
Tunaunga mkono kauli ya Makamu wa Rais kwa kukemea vitendo vyenye dalili za kuutikisa Muungano wetu, tunaamini kuwa hali ya utulivu na mshikamano unaoendelea nchini umeimarishwa na Muungano ambao uliasisiwa na wazee wetu na kuridhiwa na Watanzania wengi, na tunaamini kuwa Muungano huu ni tunu yathamani kubwa ambayo inabidi tuilinde kwa gharama zote.
Viashiria vya kuuvuruga Muungano vinaweza kupitia katika mianya ya kisiasa, kidini, kiuchumi nk. na vinaweza kupenyezwa kwa hoja ambazo zimejengeka katika mazingira ya kawaida ya mifumo tuliyoizoea, na ndiyo maana Makamu wa Rais Dk. Bilal alisisitiza kuwa Watanzania wawajibike kwa kutowaonea haya wanaoonyesha dalili za kuvuruga Muungano huu.
Watanzania wanavyo vipaumbele vya mahitaji yao ya lazima katika maisha yao, kimsingi ni yale yote yanayoweza kuwanyanyua katika hali ya maisha yao na kuwa bora zaidi.
Watanzania sasa hawahitaji mbwembwe za kisiasa, na katika hali ya ushiriki wao katika mchakato wa kuipata Katiba Mpya, wanachohitaji ni uwakilishi wa wabunge walio makini na wanyenyekevu katika mijadala yao bila kuingiza misuguano ambayo inaweza kuyumbisha umoja na mshikamano wao.
Moja ya viashirio vya kuvuruga Muungano ni pamoja na mgawanyiko wa wabunge katika kujenga hoja zenye manufaa kwa Watanzania, wananchi wanapoanza kukosa matumaini na wawakilishi wao Bungeni, ni suala hatari kwa usalama wa taifa.
Wabunge wakiwa kama moja ya nguzo na mhimili mkubwa, wanatarajiwa kuwa msingi wa kuondoa tofauti zao za kiitikadi na kujumuisha nguvu za hoja kufikia maamuzi yenye maslahi kwa Watanzania wote.
Hatutarajii kuliona Bunge letu linakuwa chanzo cha kuvunjika kwa Muungano wetu, kwani tumeshuhudia pia baadhi ya nchi nyingine duniani zikiingia katika misukosuko ya kisiasa ambayo hatimaye kukawa na uvunjifu wa amani.
Tuuone Muungano kama nguzo kubwa ya amani na mshikamano miongoni mwa Watanzania wote, tuuheshimu na kuuenzi kwa faida ya taifa letu pamoja na vizazi vijavyo.
Tunaamini Watanzania wote ni wapenda amani, na ndiyo maana Mwenge uliowashwa na Makamu wa Rais Dk. Bilal unabeba ujumbe ambao unaenzi maelekezo ya waasisi wa Tanzania Mwalimu Julius Nyerere na Abeid Aman Karume, maelekezo hayo ni ya kuulinda na kuuthamini Muungano wetu.
Tunawasihi Watanzania wazidi kuimarisha Muungano kwa kufichua njama na viashiria mbalimbali vinavyoweza kuvuruga umoja wetu.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/d/optout.
0 Comments