Kwa kuwa JK ameaumua kuziba nta masikioni na kupuuzilia mbali matatizo wanayoyapata wananchi kutokana na mawaziri mizigo, ninawashauri Nape na Kinana warudi kwa wananchi 'wakamshitaki' kwa kushindwa kusikia kilio chao—kilichofikishwa kwake kufuatia ziara ktk mikoa ya kusini na nyanda za juu kusini. Wakifanya hivyo, watakuwa wamejiondolea lawana pindi wananchi watakapoamua kukitosa chama chao mwaka 2015.
Kuliko ikaonekana kwamba JK, Nape na Kinana lao ni moja, ni heri hawa mabwana wawili wakajitenga na JK na kuegemea upande wa wananchi ili kuepuka kuhukumiwa kwa pamoja. Wananchi ndio wanaotaabika na ugumu wa maisha kwa kubebeshwa mizigo ya mawaziri wasiobebeka na ambao JK ameamua waendelee kuwaelemea wananchi.
Litakuwa ni jambo la busara na hekima endapo Kinana na Nape watarejea kwa wananchi na kuwaambia kinagaubaga juu ya namna JK anavyofanya maisha kuwa magumu kwa kupuuzia kilio cha wananchi. Endapo hawa wawili hawatasoma alama za nyakati na kurejea kwa wananchi haraka kuwapa mrejesho wa kilio cha kwa JK, hali ya chama itakuwa mbaya sana mwaka 2015 kwani wananchi (waliokwisha kata tamaa) watakiweka katika wakati mgumu chama na hatimaye kuking'oa madarakani.
Yawezekana JK hajali kwa kuwa mwaka 2015 atamaliza ngwe yake ya uongozi lakini anapaswa kufahamu kwamba anawaharibia makada wenzake na kuwaweka katika wakati mgumu wakati watakporejea kwa wananchi kuomba ridhaa yao ya kuendelea kuongoza. Kwa jinsi hali ilivyo ni kwamba hata bwana mkubwa ameishakata tamaa na ameamua kwamba na 'liwalo liwe'. Ukaidi wake wa kutozingatia kilio na matatizo ya walalahoi utakipeleka chama chake kuzimu punde si punde. Tatizo ni kwamba huyu bwana mkubwa akili za kuambiwa, huwa hachanganyi na za kwake. Madhara ya kutochanganya akili yatasababisha lawama ambazo zitakuja kumrudia yeye na atakosa mahali pa kuuficha uso wake.
0 Comments