[wanabidii] HATUWEZI KUWA NA SERIKALI TATU NA BADO TANZANIA IKABAKI SALAMA

Saturday, January 11, 2014
Mchakato wa katiba mpya ni fursa adhimu na tunu kwa watanzania kuamua aina ya taifa tunalotaka kulijenga kwa kipindi cha miaka zaidi ya 50 ijayo. Ni kufanya maamuzi juu mfumo wa serikali yetu, mfumo wa usimamizi wa rasilimali zetu na ni kufanya maamuzi juu ya aina ya jamii tunayotaka kuijenga. Hivyo, kufanya makosa katika mjadala huu ni kuhatarisha uhai wa taifa kwa ustawi wa kizazi kilichopo na kijacho. Itatuchukua miezi 18 kuandika katiba lakini itatuchukua miaka zaidi ya 100 au haitawezekana kabisa kurekebisha makosa tuliyofanya ndani miezi 18. Hapo tutakua tumekwisha na taifa litakuwa limepoteza dira. Kwa kiasi kikubwa mjadala huu umemezwa na hatma ya muungano wetu. Bila shaka ni kwa sababu ya umuhimu wake na nafasi yake katika kujenga umoja na mshikamo ambao ndio mhimiri wa ujenzi wa taifa imara na endelevu. Nina hakika kila mmoja, atakubaliana nami kwamba amani, umoja na mshikamano wa Tanzania vitaendelea kuimarika endapo tu, tutafanya maamuzi sahihi zaidi kuhusu muungano wetu na masuala mbalimbali yanayogusa maslahi ya watanzania.

Kwa maana hiyo, tunapojadili kuhusu muungano wetu jambo la kwanza na la msingi kwa kila mtanzania ni kuwa na dhamira ya kweli na msimamo usioyumba juu ya kuutetea na kuulinda muungano kwa gharama yeyote ile. Dhamira hiyo iambatane na kutanguliza mbele maslahi ya Tanzania kwanza na kuwa wajinga wa msalahi yetu binafsi, vyama vyetu au maslahi ya dini zetu. Tukiwa na dhamira ya dhati ya kuulinda muungano wetu sambamba na kuweka mbele maslahi ya taifa ndipo tufike hatua ya kua na muafaka wa kitaifa juu ya aina gani ya muungano tunauhitaji kwa maendeleo ya watanzania. Muafaka huu kamwe hauwezi kujengwa kwa kuwashinikiza wananchi kuamini kile ambacho vyama vyetu vya siasa au dini zetu wanakiamini, la hasha. Muafaka wa kitaifa utajengwa kwa watanzania kuachwa huru kufanya maamuzi yao kwa maslahi yao na taifa lao. Wapo baadhi ya watu wanaotumia mwavuli wa elimu ya uraia kupotosha umma kwa kuwamezesha yale ambayo wanayaamini wao. Kwa maoni yangu elimu ya uraia ilipaswa kujikita katika kueleza kiunagaubaga nini msingi wa muungano na faida zake, kufanya uchambuzi wa kina wa mifumo yote ya serikali yaani muungano wa serikali moja, mbili na tatu sambamba na kueleza faida na hasara ya kila mfumo kwa mustakabali wa Tanzania ya miaka 100 ijayo. Baaba ya hapo wananchi waachwe waamue, kwa kuzingatia uelewa wao. Hiyo ndiyo elimu ya uraia ambayo kwa maoni yangu ndiyo ni sahihi kutolewa kwa watanzania.

Aidha, viongozi wa kisiasa, wanaharakati na wanazuoni wanapaswa kuwa makini na kauli zao. Wao wana mchango mkubwa katika kufanikisha ama kutofanikisha kuijenga Tanzania tunayoitaka. Baadhi ya wanasiasa wamekuwa na kauli tata za misimamo yao kuhusu muungano, licha ya kuwa ni watu ambao hawajasoma muungano kwenye vitabu bali walikuwapo tangu muungano ulipoasisiwa, wao ni sehemu ya waasisi na wanafahamu nini msingi wa muungano wetu. Viongozi hawa wanapaswa kuwa waalimu kwa watanzania walio wengi hasa vijana. Hata hivyo tunashindwa kutambua upi ni ukweli ambao tunapaswa kuusimamia kuhusu muungano pale wanapodiliki kuwa popo. Ndimi zao mbili zinatuweka njia panda na zinatupa mashaka ya dhamira zao kwa taifa letu.

Nikirejea kauli ambazo Mwenyekiti wa Tume ya Katiba, Jaji Mstaafu Mzee wangu Joseph Warioba, alizozitoa katika mahojiano yake na gazeti la Raia Mwema, toleo la 209 la Agosti 26,2011, Jaji Warioba alinukuliwa akisema ""Suala la Muungano pia liwe katika Katiba. Tusipokuwa makini kwa maneno yanayozungumzwa sasa tutavunja Muungano. Muungano huu una misingi yake na upo kwa manufaa ya wananchi. Tufafanue manufaa hayo ni nini kwa mwananchi wa kawaida.Wakati wote kwa mwananchi wa kawaida, kumekuwa hakuna matatizo ya Muungano. Matatizo yanatoka kwenye midomo ya viongozi. Shughuli za wananchi wa kawaida haziangalii orodha ya mambo ya Muungano, bali haki yao kama raia. Wanajiona ni raia katika shughuli zao za kibiashara au nyingine. Mwananchi wa kawaida anaona anayo haki ya kufanya biashara mahali popote. Wananchi wamezoa hivyo. Msiwafikishe mahali wakajiona kuwa kwenda Zanzibar au kuja Bara inabidi wafuate taratibu za kwenda Kenya au Uganda" .

Jaji Joseph Warioba aliendelea kusema "Tunayo matatizo ya madaraka, kwamba unazo Serikali mbili kwa hiyo yale yaliyomo kwenye orodha ya Muungano ni kuonyesha Serikali hii ina madaraka gani. Wanagombania madaraka. Kama suala ni mafuta au mengine tuzungumze. Inategemea mnavyokubaliana, tusije kuongeza au kupunguza kwenye orodha mambo ambayo yatakuja kuwatenganisha wananchi. Kama kwa mfano, kuna watu wanafikiri kuimarisha Muungano ni kuwa na serikali tatu, unaimarishaje?

Sasa hivi kiini ni ugomvi wa madaraka kati ya Serikali ya Muungano na Serikali ya Zanzibar. Hivi ukileta serikali tatu, ugomvi huu hautakuwapo? Ukileta Serikali ya Tanganyika yenyewe haitadai madaraka? Mwisho wataomba madaraka hadi Serikali ya Muungano isiwe na chochote. Hivi Serikali ya Tanganyika kwa mfano ikawapo, ikataka iwe na wimbo wake wa Taifa, bendera yake, nembo yake, kisha inadai ifanye biashara ya nje, unafikiri tutakuwa tumefika wapi? Ni kwamba tutakuwa tunaondoa Muungano na kurudisha Tanganyika na Zanzibar. Lakini kama wananchi wanataka hivyo, sawa. Lakini tukivunja Muungano madhara yake ni makubwa sana kwa pande zote mbili. Mimi naamini wale wanaotaka serikali tatu wanajua nia yao ni kuvunja Muungano na huu ndio ukweli. Ukianzisha serikali tatu, maana yake unavunja Muungano".

Je, leo hii mzee wangu na mwalimu wangu Jaji warioba amesahau kwamba wanaodai serikali tatu wana nia ya kuvunja muungano? Au tume ya katiba inataka kuwaaminisha watanzania kwamba wana ajenda ya kuuvunja muungano? Wamepata wapi ujasiri wa kuwaambia watanzania kwamba serikali tatu ni kuimarisha muungano hali ya kuwa wanatambua fika kwamba hilo ndio kaburi la mototo wetu kipenzi Tanzania?

Gwiji wa sheria Tanzania Prof. Issa Shivji aliwahi kusema "Ukiangalia kwa jicho la kisheria, unasema hati (hati ya muungano) ndiyo msingi, maana yake unasema hati inaendelea kuwa na nguvu ya kisheria na ndiyo sheria kuu inayotawala katiba….lakini hati iliweka serikali mbili sasa iweje rasimu inayozungumzia serikali tatu iwe na msingi ambao ulijengeka kwenye serikali mbili. Katiba iliyojikita kwenye serikali tatu, kwa vyovyote vile, haiwezi kuwa mwendelezo wa hati ya muungano ulioundwa na serikali mbili"

Kwa maana nyingine hati ya muungano ni mkataba wa kimataifa kati ya nchi mbili zilizokuwa huru, yaani Tanganyika na Zanzibar. Kwa mfano Tanzania, tumeridhia mkataba wa kimataifa wa haki za binaadamu (Universal Declaration of Human Rights), kwa maana hiyo katiba yetu haipaswi kwenda kinyume na mkataba huo wa kimataifa wa haki za binaadamu. Vivyo hivyo, kwa mkataba wa muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Katiba ya Tanzania haipaswi kupingana na mkataba huu wa muungano. Sasa basi, kama mkataba wetu umetamka serikali mbili na tume imekuja na serikali tatu, je, huko siyo kuvunja mkataba (muungano)?. Tume imefanya kazi ambayo hawakupewa. Kazi ni kushughulikia katiba wao wamevuka mipaka wakagusia na mkataba wa muungano, kazi ambayo hawakupewa.

Aidha, baadhi ya watu wanajitahidi kwa nguvu zote kupingana na ukweli kwamba serikali tatu ni kuwapa mzigo mkubwa wananchi wa kuwahudumia viongozi. Kwa mujibu wa rasimu, Tanzania itakuwa na serikali tatu, Serikali ya Muungano, Zanzibar na Tanganyika. Kila serikali itakuwa na mihimiri yake yaani bunge, mahakama na dola. Ukizidi kufanya uchambuzi utabaini mzigo mkubwa wa viongozi na watumishi ambao kwa maoni yangu hawatakua na tija kwa taifa. 

Hata hivyo, kwa mujibu wa uchambuzi wa sayansi ya siasa, Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ni Muungano wa kipekee duniani ambao hutokea kulingana na mazingira ya nchi washiriki kwa kuzingatia, hali halisi ya kijamii, siasa na uchumi. Wataalamu wa sayansi ya siasa wanaeleza kwamba katika muungano wan chi mbili ambazo ziko huru kisiasa kuna mifumo miwili ambayo hutokea. Mfumo wa kwanza ni kwa kila nchi kukubari kuachia madaraka yake na kukabidhi madaraka hayo kwa selikari ya muungano na hivyo nchi inakua na serikali moja. Mfumo wa pili ni ule ambao kila nchi kukubali kukabidhi baadhi ya madaraka kwa serikali ya muungano na nchi washiriki hushughulikia masuala ambayo siyo ya muungano. Katika mazingira haya kuna serikali tatu ambazo huzaliwa, yaani ya muungano na serikali mbili za nchi washiriki. Mfumo huu wa pili ndiyo ambao unapendekezwa na Rasimu ya Katiba kuwapo Tanzania.

Binafsi, ninauita uchambuzi huu kuwa ni uchambuzi wa kimapokeo wa sayansi ya siasa ya mifumo ya muungano, ambao sisi watanzania hatupaswi kufungwa nao. Bila shaka wachambuzi wa masuala ya kisiasa walisahau kwamba kuna mazingira ambayo mifumo hiyo miwili haiwezi kufanya kazi ili kukidhi matarajio ya taifa husika. Hapo ndipo ninapoona haja ya kuwa na uchambuzi wa kileo wa sayansi ya siasa ya mifumo ya muungano, ambao unatilia maanani mazingira ya kisiasa, kiuchumi na kijamii ya uundaji wa Muungano. Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ni mfano bora wa mfumo wa tatu wa muungano ambao hutokea kwa washiriki wa muungano kukubaliana kuwa na serikali mbili ili kukidhi haja ya kisiasa kiuchumi na kijamii ya Taifa na hii ndiyo sababu iliyowafanya waasisi wetu Hayati Shekh Karume na Hayati Mwl. Nyerere, kuufanya muungano huu kuwa na serikali mbili. Huu ndiyo ukweli wa siri ya muungano wetu kudumu kwa zaidi ya miaka 50 pamoja kuwa na changamoto kazaa.

Kuwa na matatizo ndani ya ndoa hakufanyi kuwa kigezo cha kuvunja ndoa, bali inatoa fursa kwa wanandoa kutafakari wapi walijikwaa ili kutafuta njia ya kuimarisha na kudumisha ndoa yao. Kuwa na kasoro ndani ya muungano hakutoi msukumo wa kubadili mfumo wa muungano bali kunatoa changamoto kwa washiriki wa muungano kutafakari na kuangalia wapi wanapaswa kurekebisha ili kuendeleza umoja, amani na mshikamano ambavyo vimedumu kwa zaidi ya miaka 50. Kuanza ndoa mpya ya muungano ni kazi kubwa kuliko kuimarisha mfumo uliopo wa muungano. Endapo tutaingia kwenye mfumo wa serikali tatu, na tukafika hatua tukaona kwamba mfumo huu hautufai, ni rahisi kwa ngamia kupenya kwenye tundu la sindano, kuliko kwa Tanzania kurudi kwenye mfumo wa serikali mbili au moja, kitachofuata ni kusambaratika na kuvunja muungano, Mungu aepushe mbali laana hiyo.

Kwa hakika hiki ni kitendawili kikubwa kilichotega taifa letu na mjadala huu unaufanya Tanzania kupitia katika kipindi kigumu zaidi katika historia ya Taifa letu. Binafsi ninaamini na nitaendelea kuamini na huu ndio msimamo wangu kwamba siku ambayo watanzania watapiga kura kuunga mkono serikali Tatu ndiyo siku ambayo tunauzika rasmi muungano wetu. Ukweli utabakia palepale kwamba, hatuwezi kuwa na serikali tatu na bado Tanzania ikabaki salama.

Mwandishi wa Makala hii ni Mjumbe wa Baraza Kuu la UVCCM Taifa.
Anapatikana kwa namba: +255 717 130 156
Barua pepe: jabirimakame@ymail.com 

--
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/groups/opt_out.

Share this :

Previous
Next Post »
0 Comments