Ndugu zangu,
Kila kukicha sintofahamu ya mahusiano ya Rwanda na Tanzania inaongezeka. Kuna mgogoro unaochipua. Ni mgogoro wenye madhara makubwa kama utaachwa ukue na kukomaa. Maana, ni mgogoro wenye kuambukiza.
Na ulikoanzia ni ' Kosovo' ya Afrika- Goma, hivyo basi DRC Congo. Ni Balkan yetu ya Afrika. Na sababu hasa ni MADINI. Na imekuwa hivyo tangu enzi za Mbelgiji. Si inasemwa, kila shetani na mbuyu wake!
Kwa JK kumwomba Museveni kusuluhisha mgogoro wake na Kagame ni hekima kubwa ya Rais. Maana, JK amempa Museveni mtihani mgumu. Ni kwa vile, Museveni na Kagame wana yao ya pamoja. Ni ya tangu Luwero triangle, mapambano ya kumwondoa Obote.
Wengine wameshasahau, lakini NRA ya Museveni ilijaa vijana wa Kinyarwanda waliopambana bega kwa bega na Museveni. Na 1990 ikawa zamu ya Museveni kuwasaidia kurudi Kigali.
Wengine wameshamsahau Fred Rwigyema. Huyu alikuwa Kamanda wa RPF aliyeuawa mwezi ule wa Oktoba 1992, mwanzoni kabisa mwa harakati za vijana wa Kitutsi kurudi nyumbani Rwanda wakitokea Uganda. Watutsi walikimbia kwa wingi kutoka Rwanda baada ya mapinduzi ya Wahutu ya mwaka 1959. Kuna waliokimbilia Tanzania na wengine Uganda.
Hivyo, ifahamike, kuwa Museveni ana ushawishi mkubwa kwa Serikali ya Kigali. Na kuna wakati wawii hawa waligombana, Kagame na Kaguta. Kagame aliona kaka yake hamwachi akue na kujifanyia mambo yake mwenyewe. Ikaonekana, kuwa Kigali ni kama 'Out post' ya Kampala.
Na kuna ajabu ya kimya cha Museveni tangu kuibuka kwa mgogoro huu. Tena akiwa ni Mwenyekiti wa EAC. Ukimsoma Museveni kwenye maandiko yake, unaweza kuona anachokitafuta.
Naam, yumkini ' Mwami' Museveni anaitafuta nafasi yake kwenye nchi za Maziwa Makuu. Mwami ina maana ya Chifu kwenye koo za WaBahima.
Naamini kabisa, itakapofika siku ya Museveni kuwakutanisha Kagame na Kikwete pale Kampala, na yawekekana shambani kwake, na mbele ya ng'ombe zake wa Kinyankole wenye pembe ndefu zilizochanua, basi, yumkini Yoweri Museveni akafanikiwa kusawazisha ya Kagame na Kikwete.
Maana, Kikwete hana kosa alilofanya kwa kutoa ushauri tu. Isipokuwa , kwa vile kuna mengine, basi, anayeyajua anaweza kuyamaliza. Na Yawezekana mwenye kuyajua hayo ni Yoweri Kaguta Museveni. Nani ajuaye?
Na wahenga walisema; Mchawi mpe mtoto amlee...!
Maggid.
Iringa.
Unapokea Email hizi kwa sababu umejiunga na Jukwaa la 'Mabadiliko'.
Kuchangia mada tuma kwenye Email hii: mabadilikotanzania@googlegroups.com
Kujiondoa Tuma Email kwenda; mabadilikotanzania+unsubscribe@googlegroups.com
Utapokea Email ya kudhibitisha kujiondoa kwako.
TEMBELEA Facebook yetu:
http://www.facebook.com/MabadilikoForums?ref=hl
For more options, visit this group at:
http://groups.google.com/group/mabadilikotanzania?hl=en?hl=en
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Mabadiliko Forums" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to mabadilikotanzania+unsubscribe@googlegroups.com.
To post to this group, send email to mabadilikotanzania@googlegroups.com.
Visit this group at http://groups.google.com/group/mabadilikotanzania.
For more options, visit https://groups.google.com/groups/opt_out.
0 Comments