Dhihaka za Rwanda, Kikwete Mpatanishi na Falsafa ya Ushauri!
Imeandikwa na Dkt. Hamisi Kigwangalla
Katika hali ya kawaida kutoa ushauri si jambo baya, na kwa hakika si la lazima pia. Wajibu wa anayepewa ushauri ni kuupokea na kufanya moja kati ya mambo haya mawili: kuukubali ama kuukataa. Ushauri hauna shuruti lolote lile toka kwa mtoa ushauri bali ni jambo la busara, kwa sisi wanadamu tukizingatia kuwa tuna mapungufu yetu ya kibinadamu, kuusikiliza na kuufanyia kazi ushauri wowote tunaopewa, na hatimaye kuchagua moja kati ya hatua mbili hizi nilizozitaja hapa; kuukubali ama kuukataa. Wakati mwingine mshauriwa anaweza kuamua kutokutoa msimamo wake pale pale ama popote pale, na mara nyingi hii itajitokeza pale mshauriwa anadhamiria kutafakari kwa kina zaidi. Japokuwa mara nyingi hili likitokea, watu watataka kuamini kuwa ushauri wao umekataliwa! Mshauri akionekana ameshauri jambo lisilokubalika kwa mshauriwa atajisikia vibaya lakini kwa mtu makini atajua tu kuwa hilo nalo ni jibu alilolitegemea, kuwa amekataliwa, maana hili ni moja kati ya chaguzi mbili zilizokuwepo kwenye suala.
Nimeamua kujitoa, bismillah kuandika katika gazeti hili, na ninaomba manani anijaalie nisipotoke. Napenda kuandika hili kutoa ushauri wangu kwa Rais Paul Kagame wa Rwanda na kwa Rais Jakaya Kikwete wa Tanzania. Nafahamu watakuwa wanazijua chaguzi zote mbili zilizopo na hata mimi pia si mpofu wa uelewa wa uwezekano wa chaguzi zote mbili kutokea kati ya yeyote kati yetu. Maana mimi pia nataka kutoa ushauri hivyo kutegemea moja kati ya chaguzi zilizopo ni aula.
Kumetokea sintofahamu kati ya mataifa haya mawili yaliyo jirani na rafiki, mataifa ambayo yanatarajia kwenda kutengeneza serikali ya shirikisho la nchi za Afrika ya Mashariki pamoja na mataifa mengine jirani katika ukanda huu wa Afrika. Mchakato wa kuelekea kwenye shirikisho unaendelea lakini wengi wetu kutokana na malumbano yanayoendelea tunapata mashaka ya juu ya uwepo wa afya thabiti baina ya mataifa haya. Ukikaa ukasikia sababu na ukajiuliza na kutafuta sababu hauioni. Kisa ni kauli ya ushauri ya Rais Kikwete kwenye kikao cha kusherehekea miaka 50 ya Umoja wa Nchi za Afrika (OAU) aliyoitoa Mei 26, 2013. Rais Kikwete aliwashauri kwa pamoja marais watatu wa nchi zenye makundi ya waasi wanaotumia silaha za moto kupambana na serikali zao. Na hizi ni nchi za Rwanda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Kongo (DRC) na Uganda. Rais Kikwete alitoa pendekezo la jawabu la suluhisho la kudumu la kuleta amani kwenye ukanda wa maziwa makuu kwa kushauri mazungumzo ya mapatano.
Alichokisema Rais Jakaya Kikwete kimsingi ni ushauri wa 'upatanishi', ambao kwa mtu yeyote mpenda amani na umoja hawezi kuuona mbaya, ima ameukubali au ameukataa, maana kimsingi huu ni ushauri wa 'principle' tu na wala si wa nini kifanywe na hivyo ni hiari kuusikiliza na kuufanyia kazi. Kwa mtu yeyote asiyependa vita ama anayeona bora kupatana kuliko kuzipiga kwanza ndipo mrudi kinyume nyume sasa muanze mazungumzo ya kupatana, ataona faida ya ushauri ule. Ushauri ulitolewa kwa Rais Yoweri Museveni, Rais Joseph Kabila na kwa Rais Paul Kagame. Kampala wao waliona ushauri ule ni wa msingi na wataufuata maana vita si chaguzi nzuri sana. Julai 16, 2013, Waziri wa Ulinzi wa Uganda, Mhe. Dkt. Crispus Kiyonga alithibitisha kuwa wao hawako tayari kwa vita na hivyo wako tayari kwa mazungumzo na waasi wa Allied Democratic Forces/National Army for the Liberation of Uganda (ADF-NALU).
Sambamba na ushauri huo kwa Uganda, ambao ulikubaliwa na umeanza kutekelezwa na Rais Yoweri Kaguta Museveni, Rais Kikwete alitoa ushauri unaofanana na huo kwa Rais Joseph Kabila wa DRC kuwa afanye mazungumzo na waasi wa M23 wanaopigana na serikali yake maeneo ya kaskazini mwa nchi yake, kule kwenye miji ya Goma na Kivu. Pamoja na Rais Joseph Kabila kuukubali na kuufanyia kazi ushauri ule, bado anaendelea na mapigano na waasi wa M23. Naye nitampa kipande cha ushauri kuwa hebu awe kaka mkubwa kwenye mazungumzo hayo, aachane na vita asilimia 100, akae azungumze na ndugu zake walioko msituni kwa faida ya makapuku wenzangu wa kule. Vita haitotatua mgogoro uliopo, mazungumzo yatatatua. Vita haijawahi kuwa jawabu la kero popote pale duniani. Majeshi ya kulinda amani ya umoja wa mataifa hayawezi kamwe kuwa suluhisho la kudumu la kuleta amani kwenye eneo lolote lile lenye mgogoro.
Jambo la msingi kabisa la kufanya kwenye jamii yoyote ile ya wastaarabu ni kuzungumza pale kunapokuwa na sintofahamu ama mgogoro. Msipozungumza mtazipiga mpaka asubuhi. Rais Paul Kagame, baada ya kushauriwa kuzungumza na waasi wa FDLR (Democratic Liberation Forces of Rwanda) alikaa kimya na muda haukupita mwingi mawaziri wa serikali yake, na kuna vyombo vingine vya habari vinaripoti kuwa na yeye mwenyewe alitoa maneno ya kifedhuli dhidi ya Rais Jakaya Kikwete, walianza kutoa kauli zilizoashiria kutoridhika kwao na ushauri waliopewa na Rais Kikwete. Hawakuishia hapo tu bali walimdhihaki na kumtusi, jambo ambalo liliwakera sana watanzania wengi na bado linawaudhi, ukisoma vyombo vya habari vya karatasi na hata mtandaoni. Lakini pia ukisoma michango ya wanyarwanda wengi kwenye mitandao ya kijamii utaona kabisa kitendo cha wao kushauriwa kuzungumza na 'wauaji' kiliwakera sana. Wanasema kwamba hali ya waasi wa Kongo na Uganda hauwezi kuilinganisha na ya waasi wa Rwanda, ambao wao wanawakumbusha mauaji ya kimbari, na hivyo wanaamini kabisa hili ni kundi lisilosameheka kamwe. Wanazuoni wengine wanasema kwamba waliopo leo hii FDLR, takriban miaka 20 toka mauaji ya kimbari yatokee nchini Rwanda, wengineo ni watoto na wala hawajui kiini cha mgogoro huu na hawakushiriki hata hayo mauaji na hivyo kuwahukumu na hawa pia na kuwaunganisha na wale wengine ni jambo la uonevu kwao.
Hali hii ni tete, na kwa vyovyote vile haikubaliki. Nini sasa kifanyike? Hapa unakuja ushauri wangu sasa. Na kama ilivyo ada, waheshimiwa hawa wakubwa watakuwa na kazi ya kufanya: kuusikiliza na kuufikiria, kisha kufanya uchaguzi wa kuukubali ama kuukataa. Ama lile chaguo lingine la kukaa kimya, ambalo silipendi sana. Nataka wachukue hatua kwa faida ya sisi makapuku huku chini. Wafanye uamuzi wa kuukubali. Ushauri wangu ni kwamba Rais wa Tanzania, Dkt. Jakaya Kikwete afungashe ujumbe wa kidiplomasia kwenda Rwanda, wabishe hodi ya ujirani mwema na Rais Paul Kagame afungue milango, wakae chini wazungumze tofauti zao. Uzuri ni kwamba tofauti hizi si za binafsi ni za kikazi. Na uzuri mwingine, Rwanda na Tanzania hatuna historia mbaya ya uadui hata ama ya mgogoro hata kidogo. Sasa kwa nini leo tujenge taswira mbaya? Hebu wakaka hawa wawili wakae chini wapigane wavishinde vyeo na ujabari walio nao, wajishushe warudi chini kwa faida ya akina siye pangu pakavu tia mchuzi, ambao kwa kiasi kikubwa wala hatujui nani alienda wapi na akasema nini na kwa faida ya nani. Sisi tunataka maendeleo tu wala hatutaki kingine.
Jamani amani ni tunu, inapaswa kutunzwa. Afrika ni ya waafrika na itajengwa na waafrika wenyewe. Hakuna mmoja wetu anaweza kujidanganya kwamba yeye hamtegemei mwenzake na kwamba anaweza kuifikia nchi ya ahadi bila mwenzake. Kuna wanaoamini hivyo, na labda wajue wanaweza kufika ndiyo lakini kwa kuchelewa sana. Sisi waafrika tuna ile falsafa yetu kwamba ukitaka kwenda mbali kimbia lakini ukitaka kwenda mbali zaidi kimbia pamoja na mwenzako. Kwenye dunia hii ya huku kwetu, Tanzania anamhitaji Rwanda na Rwanda anamhitaji Tanzania. Hakuna ubishi katika hili. Huu ni mchango wangu wa senti hizi mbili kwenye suala hili. Hebu ufikirieni basi wakuu wangu. Zungumzeni.
Mwandishi wa makala hii ni Mbunge wa Jimbo la Nzega, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya TAMISEMI na pia ni mwanafunzi wa Shahada ya Uzamivu (Ph.D.) kwenye afya ya jamii kule chuo kikuu cha Cape Town, Afrika ya Kusini. Na pia ni muhitimu wa Shahada za Udaktari wa Tiba, Uzamili kwenye Afya ya Jamii na Utawala na Uongozi. Anapatikana kwenye namba 0782636963 ama Email: info@hamisikigwangalla.com
"Vision is the ability to see the invisible!"
Hamisi A. Kigwangalla, MD, MPH, MBA
P.O.Box 22499,
Dar es salaam.
Tanzania.
Phone No: +255 754 636963
+255 782 636963
website: www.peercorpstrust.org or www.hamisikigwangalla.com
Email: hamisi.kigwangalla@peercorpstrust.org or info@hamisikigwangalla.com
Skype ID: hkigwangalla
Blog: blog.hamisikigwangalla.com
Unapokea Email hizi kwa sababu umejiunga na Jukwaa la 'Mabadiliko'.
Kuchangia mada tuma kwenye Email hii: mabadilikotanzania@googlegroups.com
Kujiondoa Tuma Email kwenda; mabadilikotanzania+unsubscribe@googlegroups.com
Utapokea Email ya kudhibitisha kujiondoa kwako.
TEMBELEA Facebook yetu:
http://www.facebook.com/MabadilikoForums?ref=hl
For more options, visit this group at:
http://groups.google.com/group/mabadilikotanzania?hl=en?hl=en
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Mabadiliko Forums" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to mabadilikotanzania+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/groups/opt_out.
0 Comments