RAIS wangu, dunia ina maajabu yake! Miezi michache iliyopita tulifiwa na mpendwa wetu! Katika misa ya kuaga mwili wa marehemu, iliyofanyika katika kanisa lililopo Makongo Juu nilishtuka kumkuta mzee wetu mmoja aliyekuwa kati ya viongozi wetu wa NICOL waliofukuzwa, akiwa amevaa sare walizovaa wazee au wasaidizi wa kanisa hilo.
Nikajisemea moyoni, Mungu wangu, utapeli mpaka kanisani? Ama kweli dunia utu umekwisha umebakia unyama!
Januari 26, 2013 ulifanyika mkutano wa wanahisa wa NICOL katika ukumbi ulioko Ubungo Plaza. Nilihudhuria mkutano huo. Pamoja na kwamba Felix Mosha, Mwenyekiti wa NICOL aliyefukuzwa alijitahidi sana kutumia vyombo vya habari kuwaambia wanahisa kuwa mkutano haupo lakini mahudhurio yalionesha jinsi walivyompuuza!
Mtakumbuka wiki iliyopita niliulizwa maswali matatu. "Mwalimu Mkuu nimekuona kwenye NICOL yenu je, umepata faraja? Maana umelia sana!"
Mwingine akaandika, 'Mzee Mayega NICOL yakanusha tuhuma dhidi ya Dk. Reginald Mengi. Poleni wanahisa.' na huyu akaniuliza, 'Mwalimu Mkuu ni kweli Mengi hakuiba NICOL?'
Nitaeleza yaliyojiri katika mkutano ule ili kila mtu apate jibu lake sahihi. Nilishtuka kumwona Reginald Mengi katika mkutano ule. Sikumwona katika mikutano miwili iliyotangulia.
Hata hivyo katika mkutano huu sikumwona Ibrahim Kaduma, Joseph Warioba na wazee wengine wengi mashuhuri ambao kutokana na heshima kubwa waliyonayo katika jamii yetu, walikuwa ndio kishawishi kikubwa kilichowafanya wananchi wengi wawekeze katika NICOL. Lakini Jaji Mark Bomani nimemwona katika mikutano yote.
Nakumbuka Warioba, alipohutubia wanahisa wa NICOL baada ya kuingia katika uongozi miaka kadhaa iliyopita pale Karimjee alisema, "Wala wanahisa msiwe na wasiwasi! Kuna watu wanapotuona wanasema wameingia wale wazee basi NICOL itakufa. Wamestaafu, wana njaa sana wazee wale!" Mkutano mzima ulicheka!
Hawa wazee walipokuwa wanatoka katika uongozi wa NICOL hawakuwa wanatuambia. Kilichowafanya waachie ngazi hatujakijua hadi leo! Na kwasababu hawakutuaga hatukuweza kujua waliondoka na nini!
Ila kwa sababu tunaambiwa siyo wanahisa tena basi walichukua vyao mapema, wakatuacha katikati ya bahari bila kutuachia hata makasia yakutusaidia kulisogeza jahazi letu walau mpaka ufukweni! Tungali tunaogelea kwa mikono mitupu. Hivyo nilipomwona Reginald Mengi nilishtuka na kujiuliza, kulikoni? Wakaniambia huyu mtu bado ni mwanahisa mwenzetu!
Rais wangu, naikumbuka Februari 26, 2011 kama vile ilikuwa jana. Mwenyekiti Mosha aliitisha mkutano uliofanyika Crystal Hall, Ubungo Plaza saa 4:00 asubuhi.
Nilihudhuria kama mwanahisa. Mlangoni kabla hujaingia ukumbini unajiandikisha na kupewa makabrasha. Kuona muda wa kuanza mkutano bado nikaamua kuyapitia yale makabrasha.
Nikaanza na lililoandikwa ' Maoni mapya ya uwekezaji wa nicol!' Nilishtuka kusoma, 'yaliyoamuliwa na mkutano wa wanahisa uliofanyika ukumbi wa crystal', ukumbi wa Ubungo Plaza Februari 26, 2011 saa 4:00 asubuhi.
Rais wangu naomba unielewe, wakati nasoma maamuzi yaliyoamuliwa na mkutano huo unaosemwa, mkutano wenyewe ulikuwa bado haujaanza. Hata saa 4:00 asubuhi, saa ya kuanza huo mkutano ilikuwa bado haijafika.
Kuna mtu alikuja na 'minitisi' zenye maamuzi yaliyofikiwa na mkutano ambao ulikuwa bado haujafanyika. Katika umri wangu huu nilikuwa sijapata kuona uhuni wa kitoto kama huu! Kwa mtu ambaye si mwizi, hawaibii watu, ulaghai huu wa kihuni ulikuwa na ulazima gani?
Mkutano ukaanza, Mwenyekiti Mosha, akisaidiwa na Kaduma na mama mmoja wa Kizungu. Bila kutoa ripoti ya maamuzi yaliyofikiwa katika mkutano mkuu uliotangulia, uliofanyika Februari 2010, wala kutoa mahesabu ya mapato na matumizi, Mwenyekiti Mosha alianza moja kwa moja kueleza kuwa katika miradi yote ipatayo kumi waliyowekeza yote ilikuwa haifanyi kazi isipokuwa mradi mmoja tu, kiwanda cha nyama kilichopo Dodoma.
Hivyo akawa anaomba wanahisa wawaidhinishe wakachukue hisa zilizoko NMB, mtaji pekee uliobaki ili waziuze wapate fedha walipe mishahara na nyizingine eti wakawekeze sehemu nyingine.
Mwenyezi Mungu awabariki watu wa mamlaka ya kuzisimamia kampuni kama hizi, hasa CMSA, kwa kuwazuia. Bila wanawema hawa wa CMSA wanahisa wa NICOL walikuwa wafanyiwe dhuluma ya kutisha! Mungu atawalipa!
Waliochangia walikuwa wengi. Nilipopata nafasi sikuona sababu ya kutafuna maneno. Nilimwambia Mosha kuwa ameitoa NICOL ikiwa na mtaji mkubwa na kuifikisha hapa alipodai mwenyewe kuwa wanashindwa hata kulipa mishahara.
Bado bila aibu wanaomba wanahisa wawaruhusu wakachote hata kile kidogo kilichowashinda kukichukua ili nacho wakakichakachue.
Nikamshauri yeye na wenzake akiwamo Kaduma akisikiliza pamoja na wazee wengine kama Balozi Nyaki, mzee Kileo, mzee Hashimu Mbita, mzee Rupia na mzee wetu Bomani (Jaji), kuwa waombe msamaha kwa uovu uliofanyika na waondoke kwa amani.
Kuna watu waliwekeza fedha zao walizozipata kwa jasho la damu, leo mtu mwingine kuichezea ni hatari. Wanaweza wakawafanya vibaya!
Mosha alinijibu kwa maneno manne tu! 'Haya na wewe tumekusikia.' Halafu ghafla akasema, 'Ndugu Ibrahimu Kaduma ameniambia kuwa katika mikutano kama hii huwa hakuna mengineyo, kwa hiyo mkutano umefungwa!' Na kweli akafunga mkutano. Uhuni mtupu!
Rais wangu, niliyoyasoma katika makabrasha niliyopewa mlangoni yalitisha. Mwenyekiti wa Bodi ya NICOL, Mosha, alikuwa ndiye Mwenyekiti wa Bodi na msaini hundi wa kiwanda cha samaki walichowekeza sh bilioni 3.77. Kilikuwa kimewisha kufa!
Mosha huyohuyo ndiye alikuwa mwenyekiti wa bodi na msaini hundi wa Kiwanda cha Inter-chem Pharmaceuticals Limited ambacho walikinunua kwa sh bilioni 1.731 kikiwa hakifanyi kazi. Walikinunua kutoka kwa ndugu yake Reginald Mengi.
Mwenyekiti huyohuyo Mosha ndiye alikuwa mwenyekiti na msaini hundi wa bodi katika mradi wa Afrika Biofuel and Emission Reduction ambao ulikuwa haufanyi kazi.
Mosha huyohuyo alikuwa mjumbe katika bodi ya East African Meat, ambayo NICOL ilichangia sh milioni 140.02 lakini kiwanda kilikuwa hakifanyi kazi. Pia alikuwa 'Board member' katika hisa zilizoko NMB. Yaani Kampuni ya NICOL, na kampuni tanzu zake zote zilikuwa kama kampuni binafsi za Mosha.
Rais wangu, katika hujuma zote za NICOL iliyoshikiwa bango na kutangaza kuwa viongozi wa NICOL wamewaibia wanahisa ni ile ya sh bilioni 1.7 zilizonunua kiwanda kilichokufa cha Inter-chem Pharmaceuticals Limited.
Ni kweli ndugu Rais, Kiwanda cha Inter-chem Pharmaceuticals Limited kilinunuliwa na NICOL kikiwa kimekufa! Ni kweli pia kuwa mwenye kiwanda hicho ni ndugu yake Mengi. Tena ni kweli pia kuwa Mengi ndiye alikuwa mwenyekiti wa kamati ya uwekezaji ya NICOL wakati huo!
Kilichofunuliwa katika mkutano wa hivi karibuni ni kwamba Mengi aliguswa sana na bango hilo! Hivyo Agosti 3, 2007 alimwandikia barua Mwenyekiti wa NICOL Mosha kumtaarifu kuwa pamoja na kwamba hakuhusika kwa namna yoyote ile na hujuma hiyo, lakini kwakuwa ni ukweli kuwa yule ni ndugu yake na kwamba ni ukweli pia kuwa ndiye mwenyekiti wa kamati ya uwekezaji, dhamira yake imeshindwa kuivumilia hali hiyo hivyo kwa barua ile alikuwa amejiuzulu wadhifa wake kama mwenyekiti wa Kamati ya Uwekezaji ya Kampuni ya NICOL.
Baadaye Mengi aliamua kuendelea baada ya Mwenyekiti wa NICOL Mosha kumwandikia barua Agosti 11, 2007 kumtaarifu kuwa NICOL iliamua kujitoa katika kiwanda hicho.
Hata hivyo Septemba 3, 2009 Mengi alijiuzulu baada ya kubainika kuwa NICOL ilishindwa kujiondoa katika uwekezaji huo kama ilivyokuwa imemuahidi.
Barua ya Agosti 11, 2007 ya Mwenyekiti wa NICOL Mosha iliyoandikwa na kusainiwa na Mosha mwenyewe kwenda kwa Mengi niliiona.
Kuna sehemu inasomeka hivi, 'Pamoja na kwamba mwenyekiti wa kamati ya uwekezaji haukuwapo wakati uamuzi wa kuwekeza katika Kiwanda cha Inter-chem Pharmaceuticals Limited unafikiwa, ndugu Masasi pia hakuwapo.'
Kamati ya uwekezaji ya NICOL ilikuwa na watu watatu. Mengi, Simba na Masasi. Wakati inaamuliwa hujuma hii ifanyike, wanakamati wawili, yaani Mengi na Masasi hawakuwapo kwa mujibu wa barua ya Mwenyekiti Mosha.
Rais wangu, tuitie wacheza bao maarufu wa nchi hii waje watuoneshe, hapa, mwizi wetu nani? Aliye amuru kiwanda kilichokufa kinunuliwe ni nani?
Akichangia katika mkutano huo Jaji Bomani alisema: "Mimi niliwahi kuwa Makamu Mwenyekiti wa NICOL, naelewa yaliyotokea. Suala la uwekezaji katika Kiwanda cha Inter-chem Pharmaceuticals Limited halikufika kabisa katika kamati ya uwekezaji ambayo Mengi alikuwa mwenyekiti wake."
Ndugu Rais, tukamatie wezi wetu wa NICOL. Nani aliamuru sh bilioni 1.7 zichotwe, zinunue Kiwanda cha Inter-chem Pharmaceuticals ambacho tayari kilikuwa kimekwisha kufa?
Tunajiuliza, iweje hujuma hii iongoze kuliko zile kubwa zaidi? Kama huu ndio ushahidi Mengi hapa anaingia vipi? Hili alilisemea mwenyewe Mengi kwa mdomo wake mkutanoni kuwa, "Mimi nasifika sana kwa kutaja majina, lakini kwa leo sitamtaja. Mhusika mkuu wa kunichafua katika hili ni naibu waziri."
Rais wangu, wanasiasa wasio na hofu ya uwepo wa Mwenyezi Mungu wamewachafua wanawema wengi kwa uongo na unafiki wao! Leo imedhihirika kwa Mengi, kesho itadhihirika kwa mhanga mwingine! Wana wa shetani hawajali mustakabali wa nchi wala watu wake. Wanachojali ni masilahi yao tu!
Heshima ya mtu aliyojijengea katika jamii ni amana kubwa kwake kuliko mali. Mengi ana heshima yake katika jamii yetu. Mtu mwingine yuko radhi umwibie sehemu ya mali yake, lakini usimharibie heshima yake iliyojengwa na jamii juu yake.
Kwa hili Mengi, umeumizwa sana, tena umeumizwa pakubwa! Ni kwa neema zake tu yeye aliye juu, wewe leo ungali umesimama! Mwombe anapozuru wengine wewe asikupite! Akuondolee hili wingu jeusi, ili kama atakuhesabia makosa akuhesabie kwa makosa mengine maana nawe u mwanadamu. Mwanadamu kukosa ndiyo jadi yetu sisi sote!
Mwanangu alipomwona Mengi katika TV akila chakula alichowaandalia watu wenye ulemavu, aliniuliza: "Si ndiye huyu baba anayetaka niwe mlemavu wa akili, kwanini alikuibia ada yangu ya shule?"
Mara nyingi nilikuwa naiambia familia yangu kuwa wasione hivi sasa natangatanga huku na huko kumtafutia mwanangu ada, wakadhani mimi ni baba mzembe ambaye sikujiandaa.
Nilimwambia mwanangu kuwa baada ya kulipwa mafao yangu kazini niliwekeza katika NICOL ili mwanangu uje usome kwa amani na katika shule uitakayo. Lakini wajanja kule NICOL wametuibia! (alipokuwa akiniuliza ni wajanja gani NICOL waliniibia, mimi pia nilimtajia Mengi huyohuyo). Kristu aturehemu! Walisema, kama kweli haikudhihirika leo, itadhihirika kesho!
Rais wangu, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, amemaliza mzozo mkubwa wa gesi ya Mtwara kwa muda mfupi sana, chini ya siku mbili lakini ni baada ya maisha ya watu kupotea! Mali za mabilioni kuteketezwa kwa moto! Mamia ya watu wamejeruhiwa na wengine wamebaki na vilema vya maisha.
Kilichojidhihirisha hapa ndugu Rais ni kwamba busara ilikosekana. Kwa busara kidogo tu sekeseke lile limekwisha. Busara ingetumika tangu mwanzo madhara yote yale yasingetokea!
Rais wangu, kwanini kungojea mpaka wanahisa NICOL waandamane, wakawapige mawe wanaowadhania kuwa ni wezi wao au wakawachomee nyumba zao au magari yao kama ilivyotokea Mtwara?
Kwanini busara isitumike sasa, wakamatwe, wahojiwe kieleweke? Tutakuwa yamleka zipita nga masala yatuzana mpaka lini? Kwanini serikali kutenda mpaka itishwe?
Mwambie Waziri mkuu Pinda aingie NICOL sasa. Asingoje kuja kuwaangukia wakuu wa majeshi mambo yatakapoharibika. Jeshi la Ulinzi ni kwa ulinzi wa mipaka ya nchi yetu. Kwa matumizi ya ndani ni mpaka kibali cha Bunge!
Dodoma wanasema: "Mwalimu Mkuu, tatizo la Chama Cha Mapinduzi-CCM na serikali yake, lugha ya mazungumzo kwa njia ya amani hawaielewi! Wanapoielewa wanakuwa tayari wamechelewa na madhara yametokea!
Sisi wananchi wengine tumejifunza kutoka Masasi-Mtwara kuwa, lugha pekee na laini ambayo CCM na serikali yake wanaielewa vizuri na haraka ni petroli na kiberiti."
Rais wangu, tukamatie wezi wetu wa NICOL! Nao waelewe kuwa NICOL haitapita mpaka kieleweke, kwasababu hakuna mahali popote katika kumbukumbu za ulimwengu huu panapoonesha kuwa dhuluma au udhalimu viliwahi kushinda!
TANZANIA DAIMA JUMATANO
0 Comments