MATOKEO HASI YA MATUMIZI KATIKA SERIKALI
Na: Jonathan N. Mnyela
Leo baada ya kuzungumzia juu ya "Dhana ya Muundo Mdogo wa Serikali unavyochochea Ukuaji wa Uchumi", leo ninajikita katika "Matokeo Hasi ya Matumizi katika Serikali". Ikumbukwe kuwa tangu serikali ya Awamu ya Tano iliposhika hata ikiwa chini ya Rias John Joseph Pombe Magufuli, Makamu wa Rais Samia Suluhu, Waziri Mkuu Majiliwa Kasimu Majaliwa, Katibu Mkuu Kiongozi Ombeni Sefue na Mwanasheria Mkuu Geroge Masaju, pamoja na viongozi waandamizi na watendaji katika serikali tumeona mabadiliko makuu yanayotokea na yanayoonesha Tanzania kufikia kuwa nchi ya kipato cha kati inawzekana. Serikali imekuwa pia ikisisitiza juu ya matumizi ya rasilimali fedha zitokanazo na kodi za Watanzania kuwa yanapaswa kuwa yenye nizamu ya hali ya juu, na kuelekeza matumizi sahihi katika shughuli za maendeleo yanayoongeza tija katika kumletea Mtanzania maisha bora katika awamu hii yenye msemo Hapa Kazi Tu. Pia hivi karibuni tumeona msemo mwingine maarufu ukiibuka unaosema What Would Magufuli Do?, ukimaanisha Je, Magufuli Angefanya nini?.
Magufuli ameipokea nchi ikiwa na historia ifuatayo juu ya deni la taifa, pamoja na Zao la Taifa (GDP). Deni la taifa limeongezeka kwa asilimia 21% na kufikia shilingi trilioni 35.6 mpaka mwezi March 2015 ukilinganisha na kipindi kilichopita. Pia kumbukumbu nyingene zinaonyesha kuelekea mwishoni mwa mwaka 2015 deni la Taifa limeongezeka hadi shilingi trilioni 35.10 ongezeko ambalo limetokana madeni ya zamani, madeni mapya ambayo serikali ilipoka ili kugharamia ujenzi na ukarabati wa miundombinu hususani way usafirisahji wa nishati (Majira, June 12, 2015). Kwa mujibu wa gazeti la The Citizen tarehe 1 Desemba 2015, ambalo liliandika juu ya mkutano kati ya Msajiri wa Hazina ndugu Lawrence Mafuru na watendaji wakuu na wenye viti wa bodi mbalimbali za mashirika na taasisi za umma, alisema, "Deni la Taifa sasa linakadiriwa kufikia sh. trillioni 41.08."
Kwa mujibu wa Banki ya Dunia, Zao la Taifa (GDP) linakadilikwa kuwa na thamani ya USD bilioni 49.18 (sawa na shilingi trilioni 98.36 kwa bei ya kubadirishia fedha za sasa) mwaka 2014, ambayo ni sawa na asilimia 0.08 ya uchumi wa dunia, kiwango cha juu zaidi ukilinganisha na Zao la Taifa (GDP) la kiwango chini cha USD bilioni 4.26 (sawa na shilingi trilioni 8.52 kwa bei ya kubadirishia fedha za sasa) mwaka 1990. Ukichukua kumbukumbu za tangu mwaka 1988 hadi 2014 kwa mujibu wa banki hiyo ya Dunia wastani wa Zao la Taifa (GDP) ni USD bilioni 16.16 (sawa na shilingi trilioni 32.32 kwa bei ya kubadirishia fedha za sasa) katika kipindi hicho chote.
Uwiano wa Deni la Taifa ukilinganisha na Zao la Taifa ni sawa na asilimia 41.76. Kwa kuzingatia vigezo vinavyo weza kuaminika (plausible assumptions), na kuacha mambo mengine kubakia kama yalivyo kama vile Zao la Taifa kuendelea kukua kwa asilimia 8.20 kwa mwaka katika siku za usoni, na deni la taifa kuendelea kuongezeka kwa asilimia 14 (kwa kadirio ya chini kabisa) kila mwaka. Basi ifikapo mwaka 2025 uwiano wa Deni la Taifa kwa Zao la Taifa (GDP) utakua na kufikia asilimia 70.92 ukilinganisha na asilimia 41.76 ya uwiano wa sasa. Hali ikiwa hivi basi itazifanya taasisi zinazoikopesha Tanzania kutoza riba kubwa zaidi kila mara ili tuweze kuhudumia deni hilo kwa mujibu wa makadirio ya siku za usoni (forecasts), kutokana na kikokotoleo changu. Hali hii ikitokea tu basi tutakuwa na nakisi kubwa katika bajeti za siku za usoni kitu kitakachoifanya Tanzania ishindwe kufikia malengo yake ya kuwa nchi ya kipato cha kati, na hata kama ikitokea basi itakuwa ni swala la kwenye karatasi na si jambo halisia katika maisha ya Mtanzania.
Mara nyingi hali kama hii ikitokea serikali hukimbilia kuongeza kodi kwa walipa kodi, jambo hili huwa linaleta taabu kubwa sana kwa wananchi, kiuchumi, na kisiasa. Dhana zote za kiuchumi (macro na micro – economic) huainisha kuwa kuongeza kudi huwa inaendana na kupungua kwa kasi ya kukua kwa uchumi, kwa sababu hupunguza uwigo wa ukusanyaji mapato yatokanayo na kodi. Japokuwa makadirio ya siku za mbele yanaonyesha kuongezeka kwa uwiano wa Deni la Taifa kwa zao la Taifa (dept-ratio), kuongeza kodi huwa ni njia ya kuweza kuimarisha uwiano huo jambo hili huendana na ongezeko la watu kukwepa kulipa kodi (tax avaision and avoidance).
Katika mazingira ya kawaida inaweza kutokea kuwa kuongeza kodi isiwe suluhisho katika kuleta uwiano wa kifiskali (fiscal balance). Basi njia mbadala ya kufanya hivyo ni kupunguza matumizi ya serikali. Hata hivyo dhana hii inakutana na upinzani wa aina mbili kama ifuatavyo:
Moja, wachumi wengi wanakubaliana kuwa kupunguza au kukata matumizi fulani fulani katika kipindi kifupi na cha kati hakuna tija kwa sababu hupunguza ukuaji wa uchumi. Kwa maneno mengine matumizi katika serikali huchochea ukuaji wa uchumi katika kipindi kifupi na cha kati. Dhana hii imejengeka katika ile dhana ya Keynesia. Kwa mujibu wa dhana hii haijarishi ikiwa matumizi ni ya tija ama la, matumizi ya serikali huisaidi sekta binafsi kuweza kutoa huduma za bidhaa na huduma hivyo kusaidia ukuaji wa uchumi. Japo kuwa mtazamo wa dhana ya Keynesia inakubaliana kuwa kukata matumizi huwa na matokeo chanya katika kipindi cha muda mrefu, na hupendekeza kuwa kupunguza huku kwa matumizi kusubiri hadi pale ambapo uchumi wa nchi umekaribia kuondoka kabisa tatizo la ajira.
Pili, wanaopinga kupunguza au kukata kabisa matumizi ya serikali wanasema kuwa ni muhimu kwa serikali kuendelea na hali ya sasa ya matumizi yake ili uchumi wa nchi uendelee kuwa wenye tija na unaofanya kazi vizuri kwa sababu matumizi ya serikali hutegemeza utendaji wake wa kazi katika hudumumia kazi zake kama ulinzi na usalama, kutoa elimu, huduma za afya nk. Wanaopenda dhana hii wanasema kabisa kuwa ili kuweza kuhakikisha hakuna mdororo wa kiuchumi ni vyema kuachana na wazo la kupunguza matumizi ya serikali hata katika kipindi cha muda mrefu.
Hadi sasa ule msemo wa WHAT WOULD MAGUFULI DO?, unaonekana kukinzana na dhana hizi mbili, ambapo serikali ya Magufuli imeamua kukata na kupunguza matumizi yasiyokuwa ya lazima, na fedha zilizotengwa kuelelezwa katika shughuli zenye kuleta tija na maendeleo kwa Watanzania. Kwa sababu ikiwa hali ya sasa hivi ambayo ilitengenezwa na Awamu ya Nne ingeendelea kutamalaki basi Tanzania ilikuwa inaenda kukabiriana na hali chungu zaidi ya kiuchumi, kama nilivyoelezea hapo juu kuhusu deni la taifa na uwiano wake kwa Zao la Taifa (GDP) ambapo kwa mujibu wa kikokotoleo change hadi kufikia mwaka 2025 uwiano wa Deni la Taifa kwa Zao la Taifa inakadiliwa kufikia zaidi ya asilimia 79.92 kiwango kikubwa kabisa katika historia ya Taifa hili tangu kupata Uhuru.
Ninakubaliana na Serikali ya Awamu ya Tano, kwa sababu ilishakuta Bajeti ya 2015/2015 imeshaandaliwa kwa mfumo wa serikali ya Awamu ya Nne ambayo ilikuwa ina matumizi mengi ambayo hayakuwa na manufaa wala tija katika kujenge uchumi unaokua kwa afya na jamii inayoendelea. Hivyo basi kubana matumizi na kukata au kuondoa matumizi yasiyo na tija ni lazima pasipo kujali mwonekano wa kifiskali ulivyo kwa sasa. Kwa sasa serikali inapaswa kulenga katika matumizi yenye tija na yenye lengo la kuipeleka Tanzania katika kuwa nchi ya kipato cha kati, kwa sababu matumizi mengi ya sasa au yaliyozoeleka yalikuwa yanapunguza kabisa uzalishaji katika uchumi wa nchi. Hivyo kupunguza na kukata matumizi kunaweza kusababisha uwiano mzuri wa kifiskali na kuamsha ukuaji wa uchumi ulio imara.
Ili kuweza kuelewa na kufanya upembuzi yakinifu wa matumizi ya serikali katika uchumi, ni vyema kujikumbusha kanuni muhimu kama ifuatavyo:
Kanuni ya kwanza: Matumizi huhitaji utozaji wa kodi. Hii inaweza kuendana sambamba na matumizi ya sasa au ya siku za usoni ikiwa serikali itakopa pesa na kufanya shughuli zake kwa nakisi. Njia nyingine mbadala serikali inaweza kuchapisha noti nyingine ili kulipia matumizi, ila hii husababisha kodi za siku za usoni katika mfumo wa mfumuko wa bei.
Kanuni ya pili: Utozaji wa kodi huwa na madhara makubwa sana zaidi ya kuhamisha nguvu ya ununuaji (purchasing power) kutoka kwa walipakodi hadi kwa serikali; madhara mengine huwa ni kuparanganisha maanuzi ya kiuchumi ya walaji wa huduma na bidhaa pamoja na sekta binafsi kwa ujumla. Utozaji wa kodi kwenye mishahara na ujira hudidimiza morali ya kufanyakazi ukilinganisha na kula raha. Kutoza kodi kwenye riba, magawio na ongezeko la mitaji hudidimiza pia uwekaji wa amana ukilinganisha na utumiaji. Kodi katika faida za makampuni didimiza uwekezaji ambao ndiyo hutengeneza faida hizo.
Hivyo, madhara ya kwenda kinyuma na kanuni hizi mbili kitendo cha kutumia fedha fulani katika matumizi ya serikali huendana na kuparanganisha mfumo wa shughuli za kiuchumi ambao serikali hulazimika kutoza kodi ili iweze kulipia matumizi hayo. Kubwa zaidi ni kuwa matumizi ya serikali yana madhara makubwa zaidi katika mfumo mzima wa uchumi. Mparanganisho huu wa shughuli za kiuchumi hujulikana kama Deadweight Loss (DWL). Mfano ikiwa kodi inayotozwa ina DWL ya asilimia 5, na kukawa kuna tumizi la serikalini la shilingi elfu moja (Tsh. 1000.00) ya kiasi ambacho kimekusanywa kugharamia tumizi hilo, jampo hili huugharimu uchumi kiasi cha kuanzia 1050 kwa kila shilingi 1000 ambayo serikali itatumia. Hivyo basi matumizi ya shilingi 1000 ambayo serikali itatumia yatatakiwa kuzalisha kuanzia 1050 au zaidi ili kuweza kupita kile kipimo cha gharama-na-faida (cost-benefit test).
Kutokana na malelezo katika aya iliyopita. Je nimatumizi mangapi ya serikali tumeyaona yakiwa hayana tija. Posho kiasi gani zimelipwa kwa watu ambao hawakuzalisha kiasi cha zaidi za posho hizo? Je ni bidhaa au huduma gapi zinazogharimu mabilioni mangapi ya fedha za walipakodi zimetumika lakini hazijawahi kuwa na tija na faidi za kuletea Watanzania faida inayoendana au kukalibia kufikia kiasi ambacho kingekuwa na matokeo chanya katika uchumi kwa ujuma?
Katika mazingira kama hayo nini kinapaswa kufanyika ili kuleta tija? Hii inakuwa ni makala ya mwendelezo wa maandiko yangu ya uchambuzi ya uchumi nikiangalia utendaji na kwendeno ya serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais John Joseph Pombe Magufuli
Imeandikwa nami, mchambuzi wa maswala ya kisiasa na uchumi wa mtaani. Pia ninatoa ruksa ya kutoa maoni yatakayo ifanya makala hii iweze kuwa sahihi zaidi.
Jonathan N'handi Mnyela.
0714060608
--
P. O. Box 3385
Dar es Salaam
Tanzania
Alternative email: jmnyela@yahoo.com
Blog: www.mnyela4consultation.wordpress.com
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/d/optout.
0 Comments