Privatus Karugendo
NINGEPATA nafasi ya kumshauri Rais Dk. John Magufuli la kwanza na haraka ningemwambia aunde tume. Ingawa mimi si mshabiki wa tume, maana kwa kiasi kikubwa zinafanya kazi nzuri na kazi hiyo kutelekezwa na watalawa, akiunda tume, itamsaidia kuibua mengi, na hiyo itamsaidia kuondoa dhana ya ?nguvu za soda? inayosambazwa na wasiomtakia mema.
Maeneo ya kuundiwa tume ni pamoja na, mfano, kuthibtisha au kufuta minong?ono kwamba viongozi wengi wa umma wanaogelea katika utajiri mkubwa uliopitikana kwa wizi. Kwamba wamepata utajiri kwa kupora mali ya umma, rushwa na udangayifu wa hali juu. Ikiundwa tume, itasaidia. Maana itachunguza na kubainisha ukweli.
Kuna viongozi na wafanyakazi wa serikali wenye mali nyingi, lakini wamewekeza mali hiyo hapa nchini. Wana viwanda, mashamba na biashara nyinginezo. Kwa njia hii wanatengeneza ajira na kulipa ushuru. Kwa njia moja ama nyingine hawa wanachangia kukua kwa uchumi. Ingawa matendo ya kupora si mazuri, lakini kwa vile wanachangia kukua kwa uchumi wetu, tunaweza kuwavumilia kwa vile hawa ni sawa na kosa lenye heri. Lakini pia ni vizuri kuwafahamu kwa majina.
Kazi hii ifanywe na tume itakayoundwa na rais. Tukiwafahamu, waonywe kuhusu tabia yao ya kupora. Wakemewe, wasiendelee. Ila waboreshe biashara,viwanda na mashamba yao ili waendeelee kuzalisha ajira na kulipa ushuru.
Kuna aina nyingine ya viongozi wetu wanaowekeza nje ya nchi. Wana viwanda, mashamba, mahoteli na biashara nyinginezo nje ya nchi. Hawa hawatozwi ushuru na wala hawatengenezi ajira hapa kwetu. Wanatengeneza ajira nje ya nchi na wanasaidia kukuza uchumi wa mataifa mengine. Hawa ni wananchi wabaya kabisa. Hawa hawana upendo na taifa lao.
Na aina nyingine ni wale wanaoweka pesa zao nje ya nchi. Minog?ono ni kwamba wana pesa nyingi kwenye benki za nje. Wanazisaidia benki hizo kufanya faida kubwa. Wakati mwingine faida ikiwa kubwa zaidi, tunapatiwa tu misaada kutokana na utajiri wetu wenyewe au tunapewa mikopo ambayo italipwa na wajukuu zetu!
Sipendekezi kwamba watu hawa wakibainika wanyaganywe utajiri wao huo waliouficha nje ya nchi. Haina maana kumnyanganya tajiri na kumpatia masikini bila mipango endelevu. Tume ikiwabaini watu hawa, basi washinikizwe kurudisha utajiri wao ndani ya nchi. Mali ibaki yao, lakini waiwekeze hapa hapa ndani ya nchi. Kwa kufanya hivyo watalipa ushuru na kutengeneza ajira. Na kama watakuwa na pesa nyingi na za kupindukia, basi waombwe kuchangia miradi ya maendeleo ya taifa letu.
Tume hii inayopendekezwa, ni ya muhimu na ya haraka sana. Hakuna maana kuendelea kuomba misaada kutoka nje wakati kuna watanzania wana pesa nyingi na zimechimbiwa nje ya nchi. Hakuna maana kuendelea kuomba msaada wa chakula, wakati kuna Watanzania wana pesa nyingi na wamezichimbia nje.
Imani yetu ni kwamba mpango wa kuunda tume, na kuwahakikishia waheshimiwa kwamba pesa zao hazichukuliwi bali wanaombwa kuziwekeza hapa hapa nchini, utapunguza wasi wasi kwa waheshimiwa hawa. Kwa vile tume itawahoji na kufanya majadiliano nao, itapunguza makali ya wasiwasi. Na hata kama ikibainika kwamba baadhi yao ni viongozi katika serikali hii mpya wasisimamishwe kazi. Waendelee kufanya kazi, baada kukubali kuwekeza hapa ni ushupavu na kuonyesha uzalendo wa hali ya juu. Hata hivyo watu hawa ni kama benki, walikuwa wametutunzia na sasa watakuwa wanarejesha!
Kuna kundi jingine la tatu ambalo si viongozi na wala si wafanyakazi wa serikali. Kundi hili ni la Watanzania wanaoishi nje ya nchi. Baadhi yao wanaishi huko kwa kutumwa na serikali na baadaye wanazamia kimoja na wengine kwa mipango yao wenyewe. Hawa nao wana biashara, viwanda na biashara nyinginezo huko ughaibuni.Wana kipato ambacho hakitozwi ushuru hapa kwetu. Wakija likizo wananufaika kwa huduma za jamii na usalama wao unalindwa na serikali yetu. Hawa pia ni bora tume iwabainishe.
Tujue ni wangapi na wana utajiri kiasi gani. Nao washinikizwe kuchangia maendeleo au kuwekeza hapa hapa nchini. Nchi kama Somalia, uchumi wake unachangiwa kwa kiasi kikubwa na wasomali wanaoishi na kufanya kazi nchi za nje. Sisi pia tunaweza kuanzisha mtido kama wa Somalia. Hii yote inahitaji maandalizi na mpangilio. Na kubwa ya yote ni kubaini kwanza Watanzania hawa wako wapi na wanafanya nini.
Baada ya tume hii kufanya kazi. Bunge lifanye kazi yake ya kupitisha sheria ambazo zitawalazimisha Watanzania wanaoishi nje ya nchi kuchangia kiasi katika maendeleo ya Taifa. Pia sheria hiyo hiyo iwabane wale wote wanaowekeza na kuweka pesa nje ya nchi yetu. Wasikatazwe kufanya hivyo, ila wafanye hivyo kwa faida na maendeleo ya taifa letu. Ni lazima tuanze kutunga sheria kwa kuangalia maslahi ya taifa letu. Ni wakati wa kuachana na sheria nyingi zilizotungwa na wakoloni, ambazo nyingi zililenga kulinda maslahi ya wakoloni.
Ni lazima tufike mahali tuanze kutafakari pamoja kama taifa. Ni lazima kuanzisha utamaduni wa ukweli na uwazi, si kwa maneno bali kwa matendo. Ni lazima kila Mtanzania aguswe na umasikini wetu, matatizo yetu, matumaini yetu na lengo la kuiandaa Tanzania bora kwa vizazi vijavyo. Ni lazima kushikamana na kutembea kwa pamoja!
Tume yetu, kama kweli Mheshimiwa Rais Magufuli, atakubali kuiunda. Ikibainisha wale wote wenye mali na pesa nje ya nchi, wasinyanganywe, bali washinikizwe kuwekeza hapa hapa nchini. Wanaweza kutumia pesa hizo kununua mashirika ya umma yanayobinafsishwa. Wanaweza kuwekeza kwenye makampuni kama vile ya Vodacom, na makampuni mengine ya mitandao. Au kuwekeza kwenye makampuni ya kuchimba madini, kilimo, uvuvi, utalii na mengine.
Mtanzania, anapowekeza hapa, ni tofauti kabisa na mgeni akiwekeza. Kwa Mtanzania aliye na akili nzuri, akiwekeza hapa ni lazima atatanguliza maslahi ya taifa. Mtanzania, hawezi kuangalia kutengeneza faida bila kuangalia maendeleo ya taifa lake.
Kama kuna asiyeangalia maendeleo ya taifa lake, basi huyo anakuwa na kasoro kubwa. Mtanzania ni lazima ataangalia maendeleo ya taifa lake. Mwekezaji, wa kutoka nje ni lazima aangalie faida na maendeleo ya nchi yake alikotoka. Anakuja hapa kuvuna na kupeleka kwao. Hakuna mtu wa kutoka nje na kuja kuijenga Tanzania
Wawekezaji wengine, wale wanaotoka nje ya nchi, wakishapata faida kubwa wanatoa vijizawadi.Mfano wanatoa misaada kwenye mashule, mahospitali na wakati mwingine kwa watu binafsi. Mashirika ya simu za mikononi, kama yameanzisha bahati nasibu na yanatoa zawadi nzito, kama nyumba na magari. Ukiangalia kwa ndani, hizi si zawadi, bali ni sawa mtu kumpatia mtoto pipi ili asilie.
Ukilinganisha faida wanayoipata wawekezaji na uharibifu wa mazingira, na vijizawadi wanavyovitoa, utagundua kwamba hakuna uwiano wowote ule. Mfano makampuni ya simu za mkononi, viwango vyao viko juu sana ukilinganisha na nchi nyingine. Muda wa maongezi unafupishwa na gharama inakuwa ya juu. Hakuna shaka wanavuna kiasi kikubwa.
Kwa mujibu wa historia yetukuanzia Uhuru, Ujamaa, Azimio la Zanzibar, Utandawazi, Ubinafsishaji na Soko Huria, ni vigumu kwa Mtanzania kuwa na pesa nyingi kiasi cha kuwekeza nje ya nchi na kuweka pesa kwenye benki za nje, bila mtu huyo kuwa amechota pesa hizo kwenye mfuko wa serikali.
Mishahara imekuwa ya chini kiasi hadi leo hii watumishi wa serikali wanalalamika. Kipato cha ziada hakiwezi kupatikana bila kuchota pesa za Watanzania, ambazo zinakuwa zinalenga kujenga miradi ya maendeleo kwa watanzania wote.
Hivyo basi tume ikimaliza kazi yake, kila atakayegundulika kuwa na mali nje ya nchi, ataombwa kushirikiana na tume ? hata hivyo nafsi itakuwa inamsuta, maana alichota kwa uficho na sasa atakuwa anaombwa kurudisha pasipo uficho.
Na Watanzania wakiamua kwamba pesa hizo badala ya kuwekezwa zitekeleze mradi fulani, basi watu hawa ni lazima wakubali! Binafsi, nisingependa pesa zao zichukuliwe. Wabaki nazo, ila waziwekeze na kuanzisha miradi ya maendeleo kwa Watanzania wote. Haya ni maoni yangu na mapendekezo yangu. Ni mtizamo wangu ambao uko chini ya hoja na maoni mbali mbali ya Watanzania.
Kundi la mwisho katika mtizamo huu ni aina nyingine ya watu ambao walipora na wana pesa nyingi lakini hawakuwekeza popote. Pesa zao ziko kwenye benki zinazalisha faida kwao na kwa wenye mabenki. Hawa nao ni bora kuwashinikiza wawekeze pesa zao katika miradi ya kuzalisha kwa faida ya watanzania wote. Pesa za kuweka benki tu bila kuzizungusha, haziwanufaishi Watanzania wote kwa kiasi cha kutosha. Wakiziwekeza kwenye miradi mbali mbali watasaidia kuzalisha ajira.
Matatizo tunayoyapata sasa hivi ya maji, umeme, usafiri, chakula na matibabu yanaweza kupungua kwa kiasi kikubwa kama pesa zetu zilizo nje ya nchi yetu zinaweza kurudi na kuzunguka hapa hapa kwetu.
Mbali na mali na pesa, kuna vipaji vikubwa vimepotelea nje. Hii pia iwe kazi ya tume yetu kuvitafuta vipaji hivi na kuvirudisha nyumbani. Wako Watanzania wengi Amerika, Ulaya, Japan na kwingineko, ambao ni wataalam katika mambo mbali mbali.
Wanachangia maendeleo katika nchi za nje na nyumbani kwao maendeleo yanalala usingizi. Kwa vile tunabaki kusikia na kuhisi tu juu ya wataalam hawa, tume inaweza kusaidia kubainisha ukweli. Tukiwajua idadi yao na utaalam wao, serikali ifanye kazi ya kuwashawishi na kuwaomba warudi nyumbani na kulijenga taifa lao. Awamu zote zilizopita, zilifumbia macho ukweli huu, matumaini yetu ni kwamba serikali ya ?Hapa kazi tu? inaweza kufanya jambo hili. Na hili likifanyika, Tanzania yenye neema itawezekana bila wasi wasi wowote.
Tukifumbua macho na kutumia akili zetu kwa kiwango kinachokubalika kimataifa, tukiuvua ubinafsi na kuuvaa uzalendo, tukiacha kutanguliza tumbo na kulitanguliza taifa, taifa letu linaweza kupiga hatua ya maendeleo kwa haraka hata bila misaada kutoka nje. Inawezekana, timiza wajibu wako.
Raia Mwema.
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/d/optout.
0 Comments