TANGU kutangaza kujiondoa rasmi kutoka uanachama wa CCM aliyekuwa muitikadi mkuu wa chama hicho, Kingunge Ngombale-Mwiru, amekuwa akijitahidi kuhalalisha uamuzi wake huo kwa njia mbalimbali ikiwa ni pamoja na kudai kwamba kufanya hivyo ni kumuenzi Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere. Kujiunga au kujiondoa kutoka katika chama chochote kile cha aina yoyote ile ni uamuzi halali na ni haki ya kidemokrasia.
Kwa mantiki hiyo basi hakuna sababu yoyote ile ya kutaka kujihangaisha kuhalalisha ama kuharamisha hatua hiyo kwa yeyote yule. Mzee Kingunge katika miaka yake aliyokuwa katika CCM ametoa mchango mkubwa sana na kwa hakika kama kuna sifa zozote zile ambazo chama hicho kinastahili basi ni pamoja na yeye binafsi.
Ni Kingunge aliyekuwa amesimamia itikadi ya CCM na kuhakikisha kwamba suala la uadilifu linakuwa ndiyo msingi wa kupata viongozi wanaofaa kwa chama na serikali. Kama kiongozi msomi na aliyebobea katika masuala ya sayansi ya siasa alikuwa mstari wa mbele na alisimama kidete kuhakikisha kwamba viongozi wa chama na serikali wanakuwa ni watu waadilifu kwa kila namna na ambao wanaifahamu itikadi ya chama.
Ni itikadi hiyo aliyokuwa akiisimamia Kingunge ndiyo iliyokuwa ikitumika kama nguzo ya kutengeneza sera za chama ambazo zilikuwa zinawekwa mbele ya serikali kutekeleza kwa ajili ya kuhakikisha kwamba wenye chama chao, yaani wanachama ambao ni wakulima na wafanyakazi wanafaidika na matunda ya uhuru.
Hata hivyo, inapotokea kwamba kuna makosa au upungufu ndani ya chama ambacho Kingunge ndiye alikuwa muitikadi mkuu haiwezekani kuukwepesha ukweli kwamba naye ni muhusika na ni vigumu kujivua lawama kama hilo ni jambo la kufanya.
Mzee Kingunge alikuwa kiongozi wa juu wa chama tawala wakati chama hicho kilipotumbukia katika janga la kufanya urevishenisti yaani kitendo cha kupitia upya itikadi ya chama ili kukidhi matakwa ama ya mabadiliko ndani ya nchi au nje ya nchi.
Serikali ya Tanzania ilijikuta katika wakati mgumu katikati ya miaka ya 1980 ilipokuwa ikilazimishwa na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) na Benki ya Dunia (WB) kutokana na kutaka kupatiwa misaada ya kifedha wakati siasa yake ilikuwa ni ya ujamaa na kujitegemea.
Ni siasa hiyo ya ujamaa na kujitegemea ndiyo iliyotengeneza sera iliyokuwa inatoa huduma muhimu za jamii kutoka katika hazina ya taifa jambo ambalo linasemwa kuwa ni huduma ya bure.
Pato la taifa lilikuwa likitumika kwa ajili ya kuwafaidisha wote kutokana na ukweli kwamba njia zote kuu za uchumi zilikuwa zinamilikiwa na umma chini ya uangalizi wa serikali. Hiki kinachozungumzwa sasa hivi kwamba ni elimu bure, afya bure na kadhalika kwa hakika ni huduma ambazo zilikuwa zikitolewa kutokana na vyanzo vikuu vya mapato kuwa mikononi mwa serikali ambayo ilikuwa ikimiliki makampuni na mashirika takriban yote ya biashara nchini.
IMF na WB walichotaka ni kuachana na sera hiyo ya kutoa huduma hizo kwa kuitumia hazina ya taifa na badala yake serikali iachane na kusimamia uchumi kwa staili hiyo ya kijamaa na kuachia soko huria kuendesha uchumi.
Ni kitendo cha Serikali ya Tanzania kukubali kuachia usimamizi wa moja kwa moja wa uchumi na ushiriki katika biashara mbalimbali kuanzia kilimo kikubwa hadi viwanda ndicho kilicholazimisha kupitia upya siasa ndani ya nchi yetu. Jambo ambalo halikuweza kufanyika bila ya kugusa siasa ndani ya chama tawala wakati ule yaani CCM.
Kingunge alikuwa mmoja wa watu waliochangia sana katika mchakato huo wa kuondokana na siasa ya ujamaa na kujitegemea na kuingia katika siasa za soko huria yaani ubepari. Hilo halisemi popote.
Anajaribu kuonesha kama vile yeye hakuhusika hata kidogo na kwamba madhila yote haya yaliyotokana na ujio wa ubepari mkongwe katika maisha ya Watanzania ni ubunifu wa watu fulani naye hahusiki hata kidogo.
Ili kuhalalisha ujenzi wa ubepari ilikuwa ni muhimu kuondokana na siasa ya ujamaa na kujitegemea. Moja ya nguzo za ujamaa ni kuwa na uongozi wa kiadilifu.
Uongozi ambao hautatumia dhamana wanayopewa na umma kwa ajili ya kujinufaisha na kuwafukarisha wananchi waliowachagua.
Chama tawala wakati huo kilikuwa na uwezo wa kuelekeza mambo ndani ya serikali kwa sababu kilikuwa chenyewe na kilikuwa kimeshika hatamu za uongozi.
Sera ya chama ilikuwa ni zaidi ya sheria na ilikuwa haiyumkiniki kupata nafasi ya uongozi kama uadilifu wako unatiliwa shaka hata ya kudhaniwa tu. La msingi lilikuwa ni kuwa na viongozi ambao hawatiliwi shaka hata kidogo.
Mzee Kingunge anajua kwamba wajanja wachache ndani ya chama tawala walipoamua kusukuma ajenda ya kuondoa sifa na miiko ya uongozi kutoka katika Azimio la Arusha walilenga katika kuhalalisha kile ambacho leo hii anakilalamikia.
Yaani rushwa, ubinafsi, ufisadi na kukiondoa chama kutoka katika njia kuu yaani njia ya ujenzi wa ujamaa na kujitegemea.
Hilo analijua na hata kama hasemi hadharani nafsi yake inamsuta kwamba analijua hilo.
La kusikitisha ni kwamba wakati ajenda hiyo inasukumwa na hatimaye kupitishwa Mzee Kingunge Ngombale-Mwiru muitikadi mkuu wa CCM alikuwepo. Alishiriki. Alikubali.
Hakusema lolote. Inashangaza sana leo hii Kingunge kudai kwamba chama kinanuka wakati yeye ni mshiriki wa kukifanya kioze na hatimaye kinuke. Kama chama hicho kinanuka rushwa na ufisadi ni kwa sababu yeye alisimamia kuondoa vipengele vyote vinavyolinda sifa za uongozi ili kuhakikisha kwamba chama hakikumbatiwi na watu wenye sifa makengeza.
Alijua kwamba kwa kuondoa miiko ya uongozi chama chake kitanuka kwa sababu ni lazima chama kitapitisha watu wenye utata kuwa viongozi katika serikali. Hilo limetimia. Ameshuhudia watu wakijitajirisha kupitia nyadhifa zao hadi sasa uongozi umekuwa ni dili kubwa la mabilioni ya mitaji.
Ameshuhudia jinsi uongozi ulivyogeuzwa mradi mkubwa na kuwaacha wananchi wa kawaida yaani wakulima na wafanyakazi wenye chama chao wakibaki midomo wazi wasijue pa kukimbilia.
Ikumbukwe kimbilio la wakulima na wafanyakazi lilikuwa ni chama chao na kilio kilikwenda kwa muitikadi mkuu ambaye mara nyingi alikuwa akitoa ufafanuzi kuhusu msimamo wa chama kiitikadi.
Kingunge analijua hilo. Wakulima na wafanyakazi wameporwa chama chao na mabwanyenye uchwara na mangimeza na Kingunge amelisimamia hilo na sasa anadhihirisha wazi wazi kulishabikia.
Hivi Kingunge ana uhalali gani leo hii wa kusema kwamba eti anajitoa ndani ya chama tawala kwa sababu ya uchafu? Uchafu huo kausimamia yeye na hata siku moja hakusikika akiukemea.
Hivi sasa kinachojionesha ni kwamba ameingia katika kundi la wazi la wale waliolenga kunufaika na uongozi ndani ya chama na serikali kwa kutumia nguvu ya fedha. Hakika katika hili Kingunge ameshindwa kujificha!
Alianza kuonyesha hisia kama za mtu aliyenyang'anywa tonge mdomoni tangu wakati ule 'mtu wake' alipoenguliwa kwenye uteuzi wa mgombea urais ndani ya CCM.
Inashangaza na ni vigumu kujua Mzee huyu anachotaka kukipata kwa sababu hawezi kujitenga na mafanikio wala udhaifu wa chama alichokikimbia. Huwezi kuzungumzia mafanikio au udhaifu wa CCM bila ya kumgusa Kingunge.
Kwa mantiki hiyo ni vigumu sana Kingunge kumnyooshea kidole yeyote yule katika sakata hili aliloliasisi na kulisimamia kuanzia mwaka 1992 pale Zanzibar.
Inasikitisha kuona jemadari wa vita ya ukombozi wa wakulima na wafanyakazi anakimbia chombo alichokiasisi kwa ajili ya mapambano hayo na badala yake anakwenda kusimama pembeni na kudai kwamba amelazimika kufanya hivyo kutokana na chombo hicho kwenda mrama.
Mwandishi wa makala haya Dk Gideon Shoo ni msomaji na mchambuzi wa gazeti la Raia Mwema.
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/d/optout.
0 Comments