Na Ananilea Nkya
Uchaguzi mkuu utakaofanyika Jumapili tarehe 25 Oktoba mwaka huu 2015 huenda vyombo vya dola vikatumika kifisadi kupora mamlaka ya wananchi kuchagua kiongozi wanayemtaka katika ngazi ya Urais, ubunge na udiwani.
Hii ni kwa sababu Rais Kikwete siku alipozima mwenge wa Uhuru huko Dodoma alitoa kauli hatari kwamba vyombo vya dola vitawashughulikia wananchi ambao watakuwa wako karibu na vituo vya kura kulinda kura zao na kushuhudia kuwa atakayeshinda atakuwa ameshinda kihalali na siyo kwa 'goli la mkono' (wizi).
Kinachoshangaza Rais Kikwete ambaye pia ni mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ametoa kauli hii huku akijua wazi kuwa sheria ya uchaguzi inawaruhusu wananchi kukaa mita 200 kutoka kituo cha kupigia kura kwa lengo la kushuhudia upigaji kura, kuhesabu kura na kutanga matokeo.
Vyama vya upinzani vikiwepo vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) –CHADEMA, CUF, NCCR- Mageuzi na NLD ambavyo vimeamua kusimamisha mgombea mmoja mmoja kwenye nafasi ya urais, ubunge na udiwani vimekuwa vikiwahimiza wananchi kulinda kura.
Kufuatia kauli hiyo ya Rais Kikwete wananchi wanauliza: Rais ambaye anapaswa kuwa mlinzi namba moja wa sheria za nchi inakuwaje ametoa kauli inayoashiria kuwa anakusudia kuvunja sheria ya uchaguzi?
Wananchi wanauliza swali hili kwa sababu Rais kutumia vyombo vya umma vinavyopaswa kulinda usalama wa wananchi kama vile jeshi la polisi au jeshi la wananchi kunyanyasa wananchi siku ya kupiga kura kinyume na sheria ya uchaguzi ni sawa na kufanya ufisadi katika mchakato wa kupata viongozi wa nchi.
Kufanya ufisadi huo siyo tu ni kuvuruga amani na demokrasia ya uchaguzi unaohusisha vyama vingi vya siasa bali pia ni kukwamisha juhudi za kukomesha umaskini unaowatafuna wananchi wengi kutokana ambao chanzo chake ni ufisadi.
Rais Kikwete kutumia vibaya nguvu ya kimamlaka aliyopewa na umma kwa kuagiza vyombo vya dola kunyima wananchi kulinda kura zao ni kutaka viongozi wan chi yetu wapatikane kwa njia za ufisadi na wizi wa kura na hivyo wakiingia madarakani wataendelea ufisadi huo huo katika chaguzi zijazo.
Hii ni hatari kubwa kwa taifa kwa sababu madhara yake ni makubwa kwa maendeleo ya nchi yetu kudumu kwa amani ya kweli inayotokana na haki kutendeka kwenye uchaguzi.
Ndiyo sababu wananchi wanauliza lengo la Rais Kikwete lilikuwa ni nini kutaka kuvunja sheria ya uchaguzi kama siyo anafanya hivyo kuandaa mazingira ya kutekeleza azma ya chama chake ---Chama cha Mapinduzi (CCM) kutumia 'goli la mkono' kupata ushindi kwa gharama yoyote kama wanavyozungumza kwenye majukwaa ya kampeni?
Maswali haya ya wananchi yanatokana na ukweli kwamba kauli ya Rais Kikwete kuzuia wananchi kuwa karibu na vituo vya kupiga kura kinyume na sheria ya uchaguzi ilianza kutolewa kwa msisitizo na Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Jaji mstaafu Damian Lubuva.
Lubuva alinukuliwa akihoji: "Tume inashangaa kwa nini vyama vinang'ang'ania kubaki katika vituo vya kupigia kura''.
Kadhalika, jambo linaloshangaza wananchi ni kwamba hata Msajili wa vyama vya siasa , Jaji Francis Mutungi naye ameunga mkono uvunjaji huo wa sheria ya uchaguzi kwa sababu badala ya kumshauri Rais kufuta kauli yake hiyo , ameuunga mkono.
Jaji Mutungu amenukuliwa akisema ''ni kweli sheria imeruhusu wananchi kubaki katika kituo cha kupiga kura kwa umbali wa mita 200, lakini sheria hiyo ina upungufu ambao wameuona ndio maana Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imetoa kauli hiyo ya kuwezesha uchaguzi kufanyika katika mazingira ya amani''
Wananchi wanauliza kama sheria ya uchaguzi ilikuwa na mapungufu ni kwa nini serikali haikuipeleka Bungeni iweze kufanyiwa marekebisho kabla ya uchaguzi wakati uchaguzi halikuwa jambo ghafla?
Kadhalika wananchi wanauliza: Rais Kikwete pamoja na Jaji Lubuva na Jaji Mutungi wamepatwa na nini gafla kiasi kwamba wameamua kushabikia uvunjifu wa Katiba ya nchi na sheria ya uchaguzi kunakoweka rehani amani, usalama na heshima kubwa ambayo Tanzania imejijengea mbele ya mataifa?
Pengine kinachowafanya wananchi kuamini kuwa huenda Rais Kikwete na na CCM yake wanakusudia kutumia 'goli la mkono' kupata viongozi wa nchi yetu kwa kutumia ufisadi wa kura ni kwamba Jaji Lubuva na Jaji Mutungi wote ni mwanasheria waliobobea na kwa nyadhifa zao wanapaswa kuitiii Jamhuri ya Muungano kama walivyoapa siku walipoteuliwa kushika nyadhifa hizo na siyo vinginevyo.
Kutii Jamhuri maana yake siyo kusema ndiyo kwa kila analosema, kuagiza au analotaka Rais wa Jamhuri yetu, bali ni kutumia busara na kuheshimu kiapo cha utii kwa Jamhuri kumshauri Rais kuepuka kutoa kauli au kupanga mambo maovu yanayoweza kufanya uchaguzi kultumbukiza nchi yetu kwenye machafuko.
Hebu jiulize ni wanawake wangapi, watoto wangapi, wazee wangapi na vijana wangapi wataathirika ikitokea hii kauli hatari ya Rais Kikwete ikitekelezwa na nchi yetu ikakumbwa na machafuko kwenye uchaguzi mwaka huu?
Rais Kikwete ajue kwamba kwa kauli alioyoitoa kama atatekeleza hiyo azma yake ni lazima katika uchaguzi wa mwaka huu kutokee umwagaji mkubwa wa damu kwa sababu kauli yake imewafanya wananchi kuamini kuwa haki yao ya kulinda kura inapokonywa na Rais kwa kuamua kuivunja sheria ya uchaguzi.
Muhimu, wananchi hasa katika wakati huu nchi inaelekea kwenye siku ya uchaguzi mkuu tarehe 25, wanategemea Jaji Lubuva kuonyesha hekima, busara na ujasiri wa hali ya kuu kuhakikisha NEC inasimamia na kutenda ili wananchi waridhike kwa dhati kabisa kwamba haki imetendeka kwenye uchaguzi maana bila haki kutendeka hakuna amani ya kweli nay a kudumu Tanzania.
Aidha wananchi wanatarajia pia kuwa wadau wakubwa wa amani vikiwepo vyombo vya habari na hususan wahariri , viongozi wa dini zote, wakuu wa vyombo vya usalama hususana jeshi la polisi na jeshi la wananchi, viongozi wa vyama vya siasa, mashirika ya kiraia NGOs mfano TAMWA, TGNP na LHRC wasomi, wahanahakati na kila mtu mwenye nia njema na Tanzania anachukua hatua bila woga kumtahadharisha Rais Kikwete kwamba kuvunja sheria ya uchaguzi kwa kuwazuia wananchi kulinda kura zao ni ufisadi mbaya utakaoigharimu nchi yetu .
Bila kumtaadharisha Rais Kikwete, ikitokea vyombo vya dola vikapambana na wananchi walioamua kutumia haki yao ya kisheria kulinda kura, Jaji Lubuva na Mutungi hawatakwepa mkono wa sheria za kimataifa kwa kushiriki jinai ya kufisadi uchaguzi wa mwaka huu kwa kuamua kuwasaidia watawala wa CCM wanaotaka chama chao kung'ang'ania madaraka kwa gharama yoyote hata kama kitakuwa kimekataliwa na wananchi.
Tukumbuke kuwa kauli ya kwamba CCM itashinda kwa gharama yoyote imekuwa ikitolewa na viongozi mbali mbali waandamizi wa CCM akiwepo Katibu Mkuu wao, Abrahamani Kinana.
Hivi sasa baada ya Jaji Lubuva na Jaji Mutungi kuungana na Rais Kikwete kutaka kuvunja Katiba ya nchi yetu na kukiuka sheria ya uchaguzi ili kuwanyima wananchi haki ya kukaa karibu na vituo vyao vya kura hadi mwisho kujua hatma ya kura yao kumewafanya wananchi kuuliza :
Hivi Tanzania imebinafsishwa lini na lini na kugeuzwa kuwa mali binafsi ya Rais Kikwete na watawala wachache wa CCM kiasi kwamba wanaweza kufanya lolote na Watanzania wengine wote hawana tena mamlaka juu ya nchi yao?
Hivi Tanzania imebinafsishwa kwa hivyo hivi sasa nchi hii ni mali binafsi ya Rais KIkwete na watawala wachache wa CCM kwa hivyo wanaweza kufanya watakavyo na wananchi hawana tena mamlaka juu ya nchi yao?
Wananchi wanauliza kama Tanzania haijabinafsishwa kifisadi Rais Kikwete, Jaji Lubuva na Jaji Mutungi wanapata wapi kile Dakta Harrison Mwakyembe alichokiita 'jeuri ya kifisadi' ya kutaka kuvunja sheria za uchaguzi kuruhusu vyombo vya dola kunyanyasa wananchi siku ya uchaguzi ili sauti ya umma inayotaka mabadiliko ya uongozi isisikike kupitia sanduku huru la kura?
Wananchi wanauliza maswali haya kwa sababu wanaona kauli iliyotolewa na Rais Kikwete kwamba ataamuru vyombo vya dola kushughulikia wananchi watakaokuwa karibu na vituo vya kupigia kura na kisha kauli hiyo kushabikiwa na Jaji Lubuva na Jaji Mutungi kunaashiria wanataka Tanzania iingie kwenye balaa zililozikumba nchi kadhaa za Afrika ikiwepo nchi jirani ya Burundi.
Kwa Rais Kikwete kutaka kuivunja sheria ya uchaguzi juu ya haki ya wananchi, tafsiri yake ni kwamba anataka kuweka historia mbaya ya kuingiza Tanzania kwenye machafuko kwa kulaka kulazimisha CCM kubaki madarakani kwa 'goli la mkono' ambalo ni sawa ni sawa na uhaini.
Je kwa Rais Kikwete kwa kutaka kuvunja sheria ya uchaguzi inayoruhusu wananchi kukaa mita 200 kutoka kituo cha uchaguzi anataka kuwaambia Watanzania kuwa tarehe 25 Oktoba 2015 amejiandaa kutumia vyombo vya dola kuwapora wananchi Watanzania mamlaka ya kuamua nani awe kiongozi wao?
Kama Kikwete ndivyo anataka ni vema ajiandae kushtakiwa kwenye mahakama ya Kimataifa ya makosa ya jinai.
Akiamua kutekeleza jinai hiyo siyo tu atakuwa amejidhalilisha mwenyewe na CCM yake bali pia Wanzania wote na Tanzania ambayo inaheshimika duniani kote kutokana na misingi ya haki na kuheshimu wananchi kulikojengwa na muasisi wa taifa hili Juliua Nyerere.
Lakini zaidi itakuwa ni aibu kwa CCM ambayo imeongoza nchi hii miongo mitano kuonekana kuwa serikali yake haikuanzisha vyama vingi kwa nia ya dhali kuleta ushindani wa kisiasa kukomesha umaskini unaotafuna mamilioni ya Watanzania.
Hii ni kwa sababu Rais wa serikali ya CCM kujaribu kuvunja sheria ya uchaguzi kulazimisha CCM kubaki madarakani ni kukataa mfumo wa vyama vingi usifanye kazi kuondoa umaskini.
Huku ni kukataa mabadiliko wakati mmoja wa waasisi mashuhuri wa CCM, Mzee Kingunge Ngombale Mwiru ambaye ameamua kuondoka CCM kwa tuhuma za kukiukwa kwa Kanuni na Katiba ya chama hicho wakati wa mchakato wa kumpata mgombea urais, amekiri hatadhani kuwa chama hicho sasa kimechoka, kimekosa pumzi, uchumi wa nchi umekwama, kinakodisha mavuvuzela kutukana watu , hivyo madadiliko ni lazima mwaka huu 2015.
Lakini zaidi Rais Kikwete asipoacha kutekeleza kauli yake atakuwa ameuthibitishia ulimwengu kwamba Tanzania ni miongoni mwa nchi ambazo wanazuoni Daron Acemoglu and James Robinson kwenye kitabu chao ''Why Nations Fail '' wanadai kwamba chanzo kundi kubwa la wananchi kubaki maskini na kikundi kidogo cha watawala kujajirika kufuru ni chama kinapokuwa madarakani serikali kukataa mabadiliko ya uongozi hivyo kutumia vibaya vyombo vya dola kung'ang'ania madaraka.
Hii itakuwa ni aibu kwa CCM iliyoongoza Tanzania miongo mitano kuonekana kuwa serikali yake haikuanzisha vyama vingi vya siasa kwa nia ya dhati ya kuleta ushindani wa kisiasa kukomesha umaskini unaotafuna mamilioni ya Watanzania. Mungu ibariki Tanzania.
Note: Nimeridhia yeyote anayetaka kuchapisha au kusambaza andiko hili afanye hivyo. Tuwasiliane: ananilea_nkya@yahoo.com
Ananilea Nkya
E-mail:ananilea_nkya@yahoo.com
--
Unapokea Email hizi kwa sababu umejiunga na Jukwaa la 'Mabadiliko'.
Kuchangia mada tuma kwenye Email hii: mabadilikotanzania@googlegroups.com
For more options, visit this group at:
http://groups.google.com/group/mabadilikotanzania?hl=en?hl=en
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Mabadiliko Forum" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to mabadilikotanzania+unsubscribe@googlegroups.com.
To post to this group, send email to mabadilikotanzania@googlegroups.com.
Visit this group at http://groups.google.com/group/mabadilikotanzania.
To view this discussion on the web visit https://groups.google.com/d/msgid/mabadilikotanzania/1444984977.5034.YahooMailBasic%40web163902.mail.gq1.yahoo.com.
For more options, visit https://groups.google.com/d/optout.
0 Comments