KUNA msemo kuwa; "Penye wazee haliharibiki neno". Msemo huu unatumiwa sana kama tahadhari kwenye masuala ambayo yanaweza kuhusisha vijana au watu wengi ambao labda hawana umri wa kuweza kuwa na hekima ya mambo fulani fulani. Msemo huu unatumiwa zaidi katika kutafuta namna ya kusuluhisha jambo ambalo linaonekana bila ushauri na hekima ya wazee basi linaelekea kubaya.
Ninaamini msemo huu utakuwa kweli katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu hasa baada ya makundi ya vijana kuonekana bila kutaka kutafakari, kufikiri au hata kujiuliza maswali wameamua tu "liwalo na liwe" na sasa wako tayari kulipeleka taifa mikononi mwa kundi la viongozi ambao uongozi wao tayari umeshaonesha madhara makubwa. Utakuwa kweli kwa sababu baada ya Lowassa kuingizwa Chadema na kupewa ugombea wa urais na hatimaye kusababisha mvurugano mwingine kwenye chama hicho kama aliousababisha na kuucha ndani ya CCM makundi ya vijana hasa wanaonekana kumfurahia wakiamini kuwa nafasi ya kuiondoa CCM madarakani imefika.
Ni kweli kuwa taifa letu linahitaji mabadiliko makubwa ya kiutawala na wasomaji wangu wanaweza kukumbuka vizuri tu kuwa nimeliandika hili mara nyingi katika miaka hii ya mwamko wa kisiasa nchini. Mabadiliko haya hata hivyo yanaonekana sasa hivi yanalazimishwa kubebwa na mtu ambaye hajawahi kuyasimamia, kuyazungumzia au hata kuonesha kuwa anayajua. Lakini vijana wetu wanaonekana hawajali haya yote kwani wao sasa "wameamua" kuiondoa CCM madarakani "liwalo na liwe".
Na kinachotisha zaidi ni kuwa vijana – wengine ni watu wenye akili tu (za darasani au vinginevyo) – hawana sababu ya msingi ya kwa nini wanamtaka Lowassa kuwa Rais wao zaidi ya matamanio yao ya kuona CCM inaondolewa madarakani. Imefika mahali hata ukiwauliza kwa nini wanamtaka Lowassa hawaoni hata aibu au kusita kwani wanasema tu "hakuna sababu sisi tunataka CCM iondoke!". Na wapo wasomi kabisa na watu ambao vinginevyo unaweza kuamini ni makini na wao pia wamedandia treni hili la Lowassa na wao pia hawana sababu wakisema tu "watu wamechoka" na hivyo basi kutokana na kuchoka basi wako tayari kufanya uamuzi yenye hatari.
Kuna sababu ya kwa nini kwa mfano, madereva wa malori wanatakiwa wapewe muda wa kupumzika hasa kama wana safari zile za masafa marefu. Hii ni kwa sababu dereva hata awe bora kiasi gani kama hajapumzika vya kutosha basi yuko hatarini kusababisha ajali na ajali nyingi za malori makubwa au mabasi zinatokana na madereva kutokulala vizuri au kupumzika na hivyo wanapokuwa barabarani wanakuwa wachovu.
Mtu aliyechoka hapaswi kufanya uamuzi mgumu wenye matokeo katika maisha yake kwani anaweza kujidhuru mwenyewe au kudhuru watu wengine. Watanzania waliochoka na utawala wa CCM hawapaswi kufanya uamuzi wa kumkumbatia Lowassa kwa sababu "wamechoka" kwani hilo peke yake linapaswa kuwa sababu ya kufikiria mara mbili kama wanastahili hata kufanya uamuzi huo.
Watanzania hawa waliopigika katika miaka hii hamsini leo hii wanaonekana kama wamepata nafasi ya pekee ya kuiondoa CCM kiulaini na hivyo hawataki kuipoteza. Ukiwasikiliza mashabiki hawa wa Lowassa utaona kuwa wengi wao wamefikia mahali pa kusema kuwa "hata kama ni fisadi, au kiongozi mbaya sisi tutamchagua tu!". Wengine wamefikia hata kusema kuwa "bora jiwe kuliko CCM" na wanazungumza hivi wakiamini wanazungumza kwa akili kabisa.
Na hapa ndipo ninapoona kuwa – na wananchi wasije kushangaa Oktoba 25 Lowassa akianguka vibaya – Wazee wa
Tanzania watakapoingilia kati na kuliokoa taifa kutokana uamuzi wa watu wenye maumivu, waliochoka na ambao kutokana na mapenzi fulani hivi kwa mtu wao hawawezi kufikiri vizuri. Wazee wataweza kabisa na ninaamini wanasababu ya kuwaangalia hawa vijana wasije kuliingiza taifa kwenye matatizo kama vijana wa mataifa mengine walivyofanya wakiamini wanaleta mabadiliko.
"Mabadiliko" yanatokana na msukumo wa hisia (emotional pressure) ni mabadiliko ya hatari kwani hisia hizo zinapoisha (na hisia huisha) mtu anaweza kukaa na kuanza kujuta; lakini kujuta kwa uchaguzi kama huu kutadumu miaka mitano au kumi! Sidhani kama taifa letu na wazee wetu wanaweza kucheza kamari hiyo na kuona nchi itakuwaje miaka kumi baadaye.
Wazee na watoto ndio wanadhurika zaidi yanapotokea mabadiliko makubwa au migongano ambayo haitoisha na hivyo ni kwa maslahi yao wao wenyewe (wazee) na watoto au wajukuu wao kuweza kuleta "neno" zuri la kuzuia mabadiliko yanayosukumwa na hisia ambayo inaonekana makundi ya vijana yanashabikia.
Hili ni muhimu kueleweka kwani sasa hivi simulizi (narrative) ambayo ipo mitaani ni imani (msingi wake picha za nyomi) kuwa Lowassa atashinda na endapo hatoshinda basi CCM itakuwa imeibakura. Hii ina maana kuwa – na hapa mtu anisome mara mbili – kuna uwezekano mkubwa sana wa machafuko endapo Lowassa hatoshinda kwani tayari makundi ya vijana yanaamini tayari ni mshindi. Ambacho vijana wengi hawajui ni kuwa ni wazee wa Tanzania ambao mara zote wamekuwa wakiamua matokeo ya uchaguzi – siyo vijana; ni wazee.
Ni wazee kwa sababu hawa hutawaona kwa wingi katika hamasa za mikutano ya kisiasa au maandamano lakini sikuya uchaguzi kwa sababu hakuna purukushani nyingi watajikongoja wenyewe na wengi wanapiga kura mapema na kuamua hatima ya uchaguzi. Nina uhakika wa asilimia mia moja kuwa endapo siku ya uchaguzi wazee wengi wataamua kulinda nchi yao na kutoacha viongozi kama Lowassa na wale waliomuingiza kushika hatima ya nchi basi Lowassa siyo tu atashindwa, bali atashindwa na hatoamini; na nina uhakika atajiondoa Chadema mapema asubuhi kwani ndoto yake haitotimia.
Endapo wazee wataamua kukaa pembeni na kuacha vijana wajifunze somo kwa matatizo basi siyo tu watakuwa wanashindwa kutimiza wajibu wao wa kuilinda jamii yao na kuhakikisha wanakirithisha kizazi kijacho nchi ambayo inaweza kuendelezwa. Wazee na watu wengine wenye hekima hawatoacha Tanzania igeuzwe panya wa maabara ambapo viongozi walioshindwa waje kufanyia majaribio. Mbele ya wazee halitoharibika neno. Hili sina hofu nalo
Chanzo Raia Mwema
Related Posts
- [wanabidii] 6 steps to protect your password from hackers
- [wanabidii] New content updates
- [wanabidii] Israel’s Netanyahu on charm offensive in four African states (M&G Africa)
- [wanabidii] Insurance Cover for Motor vehicles and General insurance
- [wanabidii] New content updates
- [wanabidii] New content updates
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Comments