Upatu, Deci, Babu Loliondo na sasa Edward Lowassa!
Johnson Mbwambo
Kwa nini nisiamini tuwavivu wa kufikiri?
NIANZE kwa kuomba radhi wasomaji wangu kwamba katika sehemu ya mwisho ya makala yangu ya toleo lililopita nilifanya kosa la kiufundi kwa kukitaja chama cha Zitto Kabwe kuwa ni ADC Wazalendo. Nilichomaanisha ni ACT Wazalendo. Nakiomba pia radhi chama hicho kwa kosa hilo.
Mengine yote niliyozungumza kuhusu chama hicho kipya kwamba kama hakitatetereka kimwelekeo miaka si mingi kitakuwa chama mbadala wa Chadema katika siasa za Tanzania, yanabaki kama yalivyo.
Hayo pembeni, naomba leo nirejee makala niliyopata kuandika huko nyuma kuhusu utafiti uliowahi kufanywa ulioonyesha ya kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi duniani ambazo watu wake wana bongo zenye uwezo mdogo wa kufikiri (IQ).
Nakumbuka makala ile iliibua mjadala mkubwa mitandaoni; huku baadhi wakinitumia sms za matusi na kejeli kana kwamba mimi ndiye niliyefanya utafiti huo. Nilichokieleza wakati huo, na ninachotaka kukirudia leo ni kwamba, kwa namna Watanzania tunavyoenenda, yawezekana Wazungu waliofanya tafiti hizo hawakuwa mbali sana na ukweli!
Hebu tafakari yafuatayo: Miezi miwili na ushee iliyopita Edward Lowassa aliulizwa na wahariri wa magazeti iwapo ataihama CCM kama haitamchagua kugombea urais mwaka huu. Jibu lake lilikuwa kwamba hatahama CCM kamwe kwa sababu ilimlea, na kwamba huyo ambaye hamtaki ndani ya CCM ndiye akihame chama hicho!
Hata hivyo, kabla hata mwezi haujakatika Lowassa akakihama chama hicho na kujiunga na chama cha Upinzani cha Chadema, na kikamteua kugombea urais, na sasa maelfu ya vijana wanamshabikia! Kimsingi, Lowassa aliongopa katika jibu lake lile na taswira aliyojijengea ni ya mtu asiyeaminika katika anayosema na ambaye ni kigeugeu.
Ingekuwa ni Wazungu au ingekuwa sisi ni watu wenye kufikiri sawasawa, tusingemshabikia Lowassa kwa maelfu katika mbio zake za urais kwa sababu ni mtu mwongo, kigeugeu na asiyeaminika – mtu asiyeweza kusimamia maneno yake mwenyewe.
Lakini kwa uwezo wetu mdogo wa kufikiri, baadhi yetu Watanzania 'tunamzawadia' mtu huyo kwa kumuunga mkono kwenye kampeni yake ya kuusaka urais kwa udi na uvumba!
Uongo na ukigeugeu kama huo pengine ungevumilika kama nafasi yenyewe anayowania si urais. Lakini urais ni kazi yenye heshima, utukufu, uadilifu nk. Ni kazi ambayo haimfai mtu mwongo na asiyesimamia maneno yake mwenyewe.
Lakini kwa hapa Tanzania hilo halionekani kuwa ni upungufu nyeti kwa mtu anayewania kuingia Ikulu. Vijana wetu hawajiulizi: Kama huyu alidiriki kutudanganya jana, kwa nini asiendelee kutudanganya hata leo au hata baada ya kuingia Ikulu. Tutamwini vipi katika hayo anayodai kuwa atatutendea akiingia Ikulu kama huko nyuma aliwahi kutudanganya kwa kushindwa kusimamia maneno yake mwenyewe?
Kule Uingereza kuna waziri mmoja wa zamani (simkumbuki jina) alishinikizwa na umma kujiuzulu uwaziri kwa kutokuaminika. Waziri huyo alikuwa akiusifia mno mfumo wa elimu wa shule za umma za Uingereza uliokuwa ukikosolewa na wananchi, lakini baadaye ikagundulika kwamba licha ya kuusifia sana, wanawe walikuwa wakisoma kwenye shule binafsi (private school). Ilibidi ajiuzulu.
Lakini hapa kwetu Tanzania hali ni tofauti kabisa. Mtu (Lowassa) anadanganya waziwazi na anaonyesha si mtu wa kusimamia maneno yake mwenyewe, lakini maelfu ya Watanzania wanamuona kuwa ndiye anayefaa kuwa rais wao! Bado wanaamini maneno yake kuwa atawaondolea umaskini! Kama huo sio uwezo mdogo wa kufikiri wa Watanzania, ni nini?
Katika hilo, Lowassa anao 'wasanii' wengine wawili wa kisiasa wanaokamilisha ile listi ninayoweza kuiita The Three Musketeers – nawamaanisha Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye.
Nianze na Mbowe. Mbowe huyu ni miongoni mwa viongozi wa Chadema ambao walizunguka nchi nzima wakimtuhumu Lowassa kuwa ni fisadi mkubwa. Mara ya mwisho Mbowe kufanya hivyo ilikuwa wakati Lowassa akitafuta saini za kuungwa mkono ili CCM imteue kugombea urais. Mbowe akasema Lowassa ni fisadi na
wananchi hawastahili kumchagua kuwa rais wao!
Leo hii, Mbowe huyo huyo anapita mikoani akiwa na Lowassa akiwahamasisha
Watanzania wamchague Lowassa kuwa rais mpya wa nchi. Tena anamkampenia bila soni wala kupepesa macho - anajitia hayakumbuki maneno yake hasi aliyoyahubiri huko nyuma dhidi ya Lowassa.
Na Watanzania, kwa uwezo wetu mdogo wa kufikiri, tunamshangilia huyo Mbowe bila hata kujali kuwa ni mtu mwongo, laghai wa kisiasa asiyeweza kusimamia maneno yake mwenyewe anayoyatamka! Na wala hatujiulizi: Kama alitudanganya jana kuhusu Lowassa, kwa nini tusiamini kuwa hata leo anatudanganya pia kuhusu huyo huyo Lowassa?
Hadithi ni hiyo hiyo kwa Frederick Sumaye. Miezi kadhaa iliyopita aliuambia umma wa Watanzania kwamba kama Lowassa (aliyemwita fisadi) atapitishwa na CCM kuwania urais, yeye Sumaye ataondoka CCM. Sasa, ni kweli aliondoka CCM lakini mbona sasa anampigia kampeni Lowassa; ilhali alimwita fisadi asiyestahili kupitishwa na CCM kugombea urais?
Na sisi wananchi katika uzuzu wetu na IQ zetu ndogo tunampigia makofi Frederick
Sumaye wakati akimnadi Lowassa; ilhali tunajua yeye Sumaye ni mtu aliyetuongopea kuhusu Lowassa. Badala ya kumkasirikia na kumzomea kwa ulaghai wake wa kisiasa, tunamshangilia kama vile ni shujaa eti tu kwa sababu kahama CCM!
Jamani, si Sumaye huyo huyo ambaye alipokuwa waziri mkuu aliwaambia wafanyabiashara wa Moshi kama wanataka mambo yao yawanyookee wahamie CCM! Leo Sumaye kama atakwenda Moshi kumkampenia Lowassa, safari hii atawaambia nini tena wafanyabiashara wale wa Moshi? Atajipa ujasiri wa kuwaambia kwamba wakitaka mambo yao yawanyookee wahamie Chadema?! Na wanapaswa wamwamini kama alishawadanganya mwanzoni?
Ndugu zangu, ninachojaribu kueleza hapa ni kwamba 'The Three Musketeers' – Lowassa, Mbowe na Sumaye ni watu waongo na wasioaminika katika wasemayo, na kwa mujibu wa Rais wa zamani wa Marekani, Dwight Eisenhower, hawastahili kuongoza hata genge la wahuni.
Eisenhower alipata kutamka hivi: The supreme quality for leadership is unquestionably integrity. Without it, no real success is possible whether it is on a section gang, a football field, in an army or in an office (sifa kuu ya uongozi ni uadilifu, unyoofu na usema kweli usio na shaka. Bila hivyo hakuna mafanikio yoyote ya maana yanayoweza kupatikana iwe ni katika genge la wahuni, viwanja vya michezo, jeshini au ofisini.)
Kwa mujibu wa Eisenhower, hata genge la wahuni linamhitaji kiongozi mkweli anayesimama katika maneno yake mwenyewe anayoyatamka! Sasa, kama hata genge la wahuni halimhitaji kiongozi mwenye udhaifu huo, sembuse Ikulu yetu? Ndo maana naamini uwezo wetu wa kufikiri una walakini.
Lakini si hivyo tu. Lowassa na Sumaye tunawashangilia pia wakisema kwamba wataleta mabadiliko Tanzania. Ni kwa sababu ya uvivu wetu wa kufikiria tunasahau ya kuwa wote wawili walikuwa na nyadhifa za juu serikalini kwa zaidi ya miaka 20 ikiwa ni pamoja na kuwa mawaziri wakuu, na hakuna mabadiliko yoyote waliyoyapigania wakiwa madarakani.
Katika miaka yote hiyo zaidi ya 20 ya utendaji kazi wao serikalini (walianza wakiwa vijana mpaka wakazeekea humo humo serikalini) hakuna mabadiliko yoyote waliyoyapigania na wakakwamishwa, lakini leo wameshazeeka na wameshaondoka serikalini baada ya kujitajirisha, na ndiyo wanaahidi kuwa wataleta mabadiliko, na sisi tunawaamini!
Kama ni uozo wa CCM na serikali yake mbona nao kwa zaidi ya miaka 20 walikuwa sehemu ya uozo huo walipokuwa viongozi waandamizi serikalini? Kwa nini leo baada ya juhudi zao za kuutaka urais kugonga mwamba ndio wanakumbuka kwamba kuna mabadiliko yanahitajika kuletwa Tanzania? Walikuwa wapi miaka yote hiyo? Kwa nini hatuuoni ulaghai ndani ya ahadi zao hizo za kuleta mabadiliko nchini!?
Kwa hakika, hili la Lowassa ndilo linalonitia shaka zaidi kuhusu viwango vya IQ zetu. Baadhi yetu tumejitahidi mno kuwaelemisha vijana wa nchi hii juu ya nakisi kubwa ya uadilifu ya Lowassa inayomfanya asistahili kuwa rais wetu, lakini vijana badala ya kuzipembua hoja hizo wao hukimbilia kwenye kutukana tu na kudai kuwa tumehongwa na CCM.
Dk. Slaa, kwa mfano, amejaribu mno kuanika hadharani kila kitu (tena kwa data na ushahidi kibao) kuhusu tuhuma za ufisadi wa Lowassa ikiwa ni pamoja na kuidanganya Tume ya Maadili ya Viongozi kuhusu mali anazomiliki, lakini vijana wetu kwa IQ zao ndogo, hawana hata muda wa kupembua na kutafuta ukweli juu ya hoja za Slaa. Badala yake wanachokimbilia wao ni matusi na kudai eti kahongwa na CCM!
Kwa miaka kadhaa sasa Lowassa ameandamwa na kashfa ya mkataba wa Richmond ambao unailazimisha Serikali kuilipa Dowans (kampuni hewa) kiasi sha Shilingi takriban bilioni 93 – fedha za walipakodi.
Utetezi wake ni kwamba alijua kuwa huo ni mkataba wa kifisadi lakini aliutia saini eti kwa kulazimishwa na mamlaka za juu (bila shaka akimaanisha Rais Kikwete). Kama hivyo ni kweli, mbona hakukataa kuusaini, na kisha kujiuzulu nafasi yake ya uwaziri mkuu?
Angeweza kumwambia Rais hivi: "Mheshimiwa Rais, huu ni mkataba wa kifisadi utakaowaumiza Watanzania, na kama unanilazimisha kuutia saini, mimi najiuzulu uwaziri mkuu, na hivyo teua waziri mkuu mwingine atakayetia saini mkataba huu wa kifisadi."
Kama Lowassa angefanya hivyo, hadithi leo ingekuwa tofauti; maana angelionekana kama shujaa aliyekubali "kufa kidogo" kutetea maslahi ya Watanzania. Lakini sivyo alivyofanya; kwani aliusaini na akaendelea na uwaziri mkuu wake. Ni hivi karibuni tu baada ya kutemwa na CCM kugombea urais ndipo alipoanza kudai eti alilazimishwa na Kikwete kuusaini! Uongo mtupu!
Ni Watanzania wenye IQ ndogo ndiyo wanaouamini utetezi wake huo, lakini wasio wavivu wa kufikiri wanajiuliza: mbona hakujiuzulu uwaziri mkuu wakati huo kama ni kweli alilazimishwa na Rais Kikwete kutia saini mkataba huo wa Richmond?
Historia ya chama alichojiunga nacho cha Chadema inaonyesha kuwa mwasisi wake, Edwin Mtei alijiuzulu uwaziri wa fedha wakati Mwalimu Nyerere alipomshurutisha ayakatae mapendekezo ya Benki ya Dunia ya kurekebisha uchumi wa Tanzania.
Mbona Lowassa hakufuata nyayo za Mtei kwa kujiuzulu uwaziri mkuu siku alipolazimishwa na Kikwete kusaini mkataba wa Richmond? Hivi kweli vijana wetu hawauoni ulaghai uliomo kwenye utetezi huo wa Lowassa kuhusu kashfa hiyo ya ufisadi ya Richmond?
Kuna hili suala jingine analowadanganya maelfu ya vijana wanaomshabikia kwamba eti akiwa rais ataendesha 'mchakamchaka' wa maendeleo nchini. Hivi hao vijana hawaoni (hata kwenye TV) kuwa Lowassa ana matatizo ya kiafya kiasi kwamba hawezi kuhutubia mkutano wa kampeni kwa muda mrefu, na hata kushika tu kipaza sauti kwake ni tatizo?
Hivi mtu mwenye umri mkubwa na mwenye matatizo ya afya ya kiasi hicho anawezaje kuahidi 'mchakamchaka' wa maendeleo? Mbona huo 'mchakamchaka' hatukuuona katika miaka zaidi ya 20 ya utumishi wake serikalini hasa alipokuwa kijana na mwenye afya nzuri? Mbona hata kule Monduli alikokuwa mbunge kwa miaka 20 hatujaona 'mchakamchaka' wa maendeleo alioufanya? Hivi hata hilo vijana wetu hawalioni?
Sumaye naye ni hivyo hivyo. Anasimama majukwaani na kuzungumza lugha ya
Chadema na ya Ukawa ya 'kuwakomboa' vijana kiuchumi. Hivi hawa vijana wetu hawajui kwamba Sumaye anamiliki hekta 40,000 za ardhi kule Mvomero alizozitwaa akiwa waziri mkuu na mpaka leo hajaziendeleza; ilhali vijana wa Mvomera hawana mashamba?
Kama kweli dhamira yake ni ya kweli, mbona haanzi kwa kutangaza kwamba anazitoa hizo hekta 40,000 za ardhi anazozimiliki ili zigawanywe kwa vijana wasio na ajira nchini na wanaotafuta maeneo ya kulima? Angeanza na hilo, tungemuamini; maana angekuwa amekubali "kufa kidogo" kwa ajili ya vijana wa Tanzania! Kinyume cha hicho, anachofanya ni usanii mtupu, na ni wavivu tu wa kufikiri ndiyo wanaoweza kumwamini.
Hivi taifa hili la kesho (tunaambiwa vijana ni taifa la kesho) litakuwa taifa la namna gani kama lina vijana wenye IQ ndogo kiasi hicho cha kutouona ulaghai wa watu kama hao? Yaani hatuna vijana ambao hawana uwezo wa kuchanganya akili za kuambiwa na akili zao wenyewe na kuung'amua ulaghai uliomo katika ugombea urais wa Lowassa?
Kwa ufupi ndugu zangu, japo si jambo jema kulisema lakini ni lazima lisemwe. Jambo hilo ni kwamba sisi Watanzania ni wavivu wa kufikiri, na tunapenda kufuata mambo kwa pupa na kwa mkumbo bila kufikiri, na mwisho wake mara nyingi hauwi mwema kwetu.
Kinachosikitisha na kukatisha tamaa ni kwamba hata wenzetu wengine wanapojaribu kuchokonoa bongo zetu na kutushawishi tufikirie kidogo kabla ya kuchukua maamuzi, tunawapuuza na kuwakejeli lakini mwishowe hatima inakuwa ni wao "kulizwa".
Labda msomaji nikukumbushe mambo mawili au matatu hivi kuthibitisha hicho ninachokisema. La kwanza ni lile suala la moto wa Upatu (pyramid scheme) uliowaka Tanzania mwaka 1992. Mtakumbuka kuwa baadhi ya Watanzania wachache waliona mapema ulaghai ndani ya mpango huo na walijaribu kuwaelemisha wananchi kuwa watapoteza pesa zao.
Nini kilitokea? Kilichotokea ni kwamba wananchi walikataa kupima hoja zilizotolewa, na badala yake wakamiminika kwa maelfu kuwekeza pesa za akiba zao za maisha katika Upatu ule. Na mwisho wa yote mpango huo uliporomoka kama ilivyobashiriwa, na maelfu ya Watanzania wakapoteza fedha zao hizo!
Katika hali ya kawaida ya wananchi wenye IQ nzuri, usingelitaraji ulaghai kama huo ujitokeze tena baadaye na kushabikiwa tena na maelfu ya watu. Lakini ndivyo ilivyotokea tena hapa Tanzania kwani mwaka 2012 'upatu mpya' kwa jina la DECI uliibuka, na Watanzania kwa maelfu wakawekeza tena fedha zao licha ya kuonywa tena na wachambuzi walioona ulaghai wa mpango huo sawa na ule wa upatu wa mwanzo.
Nini kilitokea? Maelfu ya Watanzania 'wakalizwa' tena kwa kuibiwa pesa zao chini ya upatu huo mpya kwa jina la DECI. Yaani Watanzania wale wale 'waliolizwa' kwa kupoteza fedha zao kwenye Upatu 'wakalizwa' tena fedha zao kwenye DECI. Ni kwa nini tusihoji kwanza mambo, na badala yake tukimbilie kwa maelfu kwa kufuata mkumbo tu? Kama sababu si IQ zetu kuwa ndogo, ni nini?
Mfano wa tatu ni suala lile la Kikombe cha Babu wa Loliondo mwaka 2011. Binafsi nilijitahidi sana, kupitia safu hii, kuwatahadharisha Watanzania juu ya ulaghai uliokuwemo katika 'tiba' ya kikombe hicho cha Babu wa Loliondo aliyedai kaoteshwa na Mungu.
Juhudi zangu hizo zilipokewa na matusi na kejeli kama ninayoyapokea hivi sasa ninapojaribu kuwatahadharisha Watanzania juu ya urais wa Edward Lowassa. Maelfu kwa maelfu ya Watanzania, wakiwemo viongozi, wakaenda Loliondo kufuata kikombe cha Babu.
Nini kilitokea baadaye? Kilichotokea baadaye ni kwamba maelfu ya wagonjwa wa sukari na ukimwi walipoteza maisha yao kwa kuacha sindano za insulin na vidonge vya ARVs baada ya kunywa kikombe cha Babu. Baadaye, ikadhihirika kwamba kumbe Kikombe cha Babu kilikuwa ulaghai mtupu! Wale walionikejeli na kunitukana mpaka leo wanaona haya nikikutana nao!
Kwa ufupi, kama Watanzania wasingekuwa wavivu wa kufikiri wangelizichambua hoja zilizotolewa na Watanzania wenzao dhidi ya pyramid schemes za Upatu na DECI na pia tiba ya kikombe cha Babu wa Loliondo. Na kama wangefanya hivyo, wangeliona ulaghai uliomo ndani yake na "wasingelizwa" kwa maelfu kama "walivyolizwa".
Sasa, nakiona kile kilichotokea kwenye Upatu, DECI na Kikombe cha Babu wa Loliondo – yaani kufuata mambo kwa mkumbo bila kutafakari kikitokea pia katika suala hili la mbio za urais za Edward Lowassa. Maelfu wanamfuata bila kujihoji na kujitambua.
Yaani, pamoja na juhudi zote za kina Slaa na kina sisi (ambao wala si wana CCM) kujaribu kuwatahadharisha Watanzania kuhusu hatari ya urais wa Lowassa, bado maelfu ya vijana wanamfuata kwa maelfu ki- mkumbo bila kwanza kufikiri, kutafiti au kuusaka ukweli wa hoja zinazotolewa dhidi yake.
Kuanzia Upatu, DECI, kikombe cha Babu wa Loliondo, na sasa Lowassa, Watanzania tunadhihirisha kwamba sisi ni watu wa kufanya mambo kwa kufuata mkumbo, na hatima ya watu wanaofuata mkumbo bila kwanza kutafakari ni "kulizwa" . Je, hiyo inathibitisha kwamba IQ zetu Watanzania ni ndogo kama tafiti za Wazungu zinavyodai?
Rais mstaafu Benjamin Mkapa aliwahi kutamka maneno yaliyowaudhi Watanzania wengi ambayo leo nikiyatafakari naona yalikuwa na ukweli wa kiasi fulani ndani yake. Alisema sisi Watanzania ni wavivu wa kufikiri. Rais Kikwete alikuja baadaye kuiboresha kauli hiyo ya Mkapa kwa kutupa changamoto hii: "Akili za kuambiwa changanya na zako za kuzaliwa ndipo ufanye maamuzi."
Mimi nimechanganya akili za kuambiwa na akili zangu mwenyewe, na ndiyo maana nilikataa na nitaendelea kukataa kuifuata sauti ya mlio wa mpiga filimbi wa Hamelin (Lowassa), kwa sababu sina hakika na anakotupeleka Watanzania.
Kwa akili za kuambiwa na nikichanganya na za kwangu za kuzaliwa, nauona wazi ulaghai na uongo unaoenezwa na hawa Three Musketeers – Mbowe, Sumaye na Lowassa. Ndugu zangu, tusiifanyie Ikulu yetu upatu – ni mahali patakatifu! Tafakari.
Chanzo Raia Mwema
0 Comments