Ukweli ni Mmoja tu na Haubadiliki: CCM ya Magufuli ni CCM ya Mabadiliko!
Na Dkt. Hamisi Kigwangalla
Leo nimeamka nikifikiria kuandika tena. Mzuka wa kuandika nimeupata kutokana na hoja zinazoukumba wakati tulionao, wakati wa uchaguzi – ambapo makada wa vyama mbalimbali wanahaha kutafuta kura, kila mmoja anatoa ahadi za 'mabadiliko' ya hali ilivyo.
Wengine wakidhani wao ndiyo haswa 'mabadiliko' tunayoyahitaji, wengine wakijiona wao ndiyo bora kuliko wengine, basi alimradi tu siku zinasonga mbele na siasa za mabadiliko zinaendelea. Wengine wakihubiri mabadiliko huku wakiamini wao ni masiha aliyekuja kuikomboa nchi yetu. Wengine wakijinasibu kwa umahiri na uzoefu wa kuibadilisha nchi kutoka hatua moja mpaka nyingine.
Wanaozungumzia 'ukombozi' wa Tanzania ya leo majuzi hapa walikutana na tafsiri sahihi ya ukombozi kutoka kwa Mzee Benjamin Mkapa, ambaye aliwaeleza kuwa ukombozi wa Tanganyika na Zanzibar ulifanywa na vyama viwili vya 'ukombozi', yaani TANU na ASP, ambao baadaye walizaa chama kipya kinachoitwa CCM, ambacho nacho si tu kimeendelea na ukombozi wa wananchi kiuchumi na kijamii bali pia kimeshiriki kuongoza na kuwezesha ukombozi wa watu weusi kutoka kwenye mikono kandamizi ya wakoloni na mabeberu kwenye nchi za Afrika.
Chama Cha Mapinduzi, CCM ni chama maarufu kwa ukombozi duniani, ni miongoni mwa vyama vichache vyenye heshima kubwa ya namna hiyo duniani.
Wazazi wa CCM, yaani TANU na ASP, ni vyama vya 'mabadiliko', kwa maana vilitutoa kwenye ukoloni na kutuleta kwenye uhuru na ujenzi wa Taifa letu kupitia kujitawala wenyewe. CCM imefanya kazi ya kuleta mabadiliko, hatua kwa hatua, kwenye Nyanja mbalimbali za maisha ya mtanzania, siku hata siku, na kazi yake inaonekana.
Kuna mapungufu yanayoweza kusemwa, ndiyo, lakini ukweli ni kwamba huwezi kudharau kazi kubwa na nzuri ya ujenzi wa Taifa letu iliyofanywa na serikali ya CCM – huwezi kusema eti hakuna kilichofanyika, kama wanavyosema marafiki wa CCM wanaotaka kuiondoa madarakani.
Labda nifafanue nini haswa maana ya mabadiliko; Mabadiliko, ni kuondoka kwenye moja kwenda kwenye hali nyingine katika nyakati mbili tofauti, ni sawa na kusema Mabadiliko ni kufanya kitu kitoke kwenye uasili wake, muundo wake ama hali yake na kwenda kwenye hali mpya na tofauti na ile ya awali ambayo kingekuwa kama kingeachwa kama kilivyo.
Mabadiliko ni kitu kinachotokea kila sekunde iendayo kwa Mungu, hakuna kitu ama mtu asiyebadilika.
Mabadiliko ni hali inayovutia na kuleta mihemko. Viongozi wanamabadiliko ni wale walioyaona mabadiliko yanayohitajika kwenye jamii ama taasisi, wakaweka maono ya mbali kuhusu mabadiliko hayo, wakaijenga jamii kuamini kwenye maono hayo na kisha wakahamasisha jamii iamini mabadiliko hayo na kuiongoza kuyafuata.
Serikali ya CCM imekuwa ikipata viongozi wa aina hii mara kwa mara na wamekuwa wakifanya kazi kubwa ya kuijenga nchi yetu. Ninawapongeza. Pamoja na mafanikio makubwa yaliyopatikana, bado, kwa mfumo uliopo wa kidemokrasia, watu wana haki ya kuona kazi iliyofanyika ingeweza kufanyika vizuri zaidi! Pia wana haki ya kutaka kuwapa kazi ya kuleta mabadiliko watu wengine.
Kuna nadharia kuu mbili za kuleta mabadiliko kwenye mfumo: kwanza, ni kuleta mabadiliko ya mfumo kutokea ndani ya mfumo – kwamba unapambana na kisha unaingia ndani ya mfumo kisha unaubadilisha mfumo kutokea ndani, na ya pili, ni kwamba unapambana kuleta mabadiliko kutokea nje ya mfumo.
Na sisi viongozi wa kisiasa waumini wa mabadiliko hatuna ugomvi wowote ule binafsi sema, kwa wale waumini wa kweli wa mabadiliko, tunatofautiana kwenye mtazamo wa nadharia ipi tufuate kuleta mabadiliko chanya kwa watu wetu. Mimi kwa mfano ni mwanamabadiliko ninayeamini kuwa mabadiliko ya kweli yatatokea ndani ya mfumo, na kamwe siyo nje. Wengine wanaamini kwamba ni ngumu kuleta mabadiliko kutokea ndani, wakati mwingine wakifananisha na dhana ya kujaribu 'kukata tawi la mti uliokalia'. Mimi huwa siafikiani na muktadha huu, maana sidhani kama mfumo ni mbovu kiasi cha kufikiria kuukata.
Mimi ninaamini kuwa mfumo umekuwa mzito sana kukubali mabadiliko haraka, na hii ni kwa sababu, siyo bure tu. Mfumo wa uongozi wan chi yetu umekomaa na una misingi na kanuni zake, ambazo si mbaya sana na hivyo haupaswi kuharibiwa kwa kubadilishwa wote na kwa ghafla, mimi ninaamini tunahitaji kuurekebisha ili uwe bora zaidi na uendane na wakati (perfectioning) tu na siyo kuuondoa kabisa. Maana baada ya uhuru kazi iliyofuata ni ujenzi wa Taifa la Tanganyika kwa miaka miwili tu, na baada ya Muungano, kujenga Taifa la Tanzania kwa miaka takriban 50 sasa – hatuwezi kujiita eti ni taifa lililokomaa sasa, la hasha. Bado tunajenga utaifa wetu kwanza.
Tulipofikia, hata kama tuna tamaa ya kupaa kwa kuleta mabadiliko ya fasta fasta, bado tunalazimika kukubali kazi iliyofanywa na kujipima kama kweli tuko tayari kukubali kuharibu mfumo kwa sababu tu tuna mapungufu madogo madogo hapa na pale, hapana.
Mfano, mfumo wa kupata viongozi wanaotokana na CCM umewakataa baadhi ya wagombea kwa sababu za ukosefu wa maadili, watu hawa wamekubalika kwenye upinzani, ilimradi tu ikiaminika kuwa uwepo wao kule utakuja na nguvu za ziada kidogo kusaidia kazi ya kushika dola.
Kama hii ndiyo aina ya upinzani tulio nao nchini, kwa vyovyote vile tuna kila sababu ya kutia shaka juu ya imani yao kwenye misingi ya kizalendo na hatimaye ni lazima tutie shaka juu ya uwezo wao wa kuendeleza kazi nzuri inayoendelea kufanywa na CCM na serikali yake.
Wengine watadhani najaribu kukiuka misingi ya Katiba yetu, kusema kuwa upinzani usiaminiwe kupewa mamlaka ya kuongoza nchi, hapana. Najaribu kutoa maoni yangu kuwa, watanzania wawe macho sana kuchagua watu wa kuongoza nchi, maana kama watu walioshiriki kukosoa na kutupa mawe kwa baadhi ya viongozi wa CCM, kana kwamba wana uchungu sana na nchi, leo wameamua kuwakumbatia watu wale wale kwa malengo ya kuwarahisishia kazi ya kuwapeleka ikulu, maana yake hawana wanachoamini na hawana misingi wanayosimamia, na nchi haiwezi kupewa kwa watu wasioamini kwenye chochote.
Tujiulize, mfano, kwenye sifa za kiongozi wa kimabadiliko niliyemfafanua hapo juu, wao wana ipi? Je, wamebaini watanzania wanataka mabadiliko gani? Watanzania wana ajenda gani? Na je wao wana maono gani ya mbali juu ya ajenda ya watanzania? Na je wamefanikiwa kiasi gani kuwaaminisha watanzania juu ya ajenda hiyo? Na je watanzania wamewaelewa kiasi cha kuwafuata ili kufanya nao kazi kutekeleza ajenda hiyo ya watanzania?
Uchambuzi wangu wa kina umebaini yafuatayo: kwamba, watanzania hawako tayari kubadilisha mfumo wa utawala wa CCM, kwanza hawaelewi ni kwa nini wafanye hivyo? Wapinzani wameshindwa kubaini ajenda ya watanzania na kuiuza ipasavyo kwa sababu hawana maono waliyoyaweka wazi kwenye macho ya watanzania – siku zote ajenda kuu ya wapinzani ilikuwa ni ufisadi, sasa wamepoteza uhalali wa kuzungumzia usafi, uadilifu maana wana wagombea wengi na wafuasi walioingia karibuni wenye mashaka makuu kwenye maeneo hayo. Mabadiliko ya ukweli yataletwa na CCM mpya inayokuja na Ndg. Magufuli.
Watanzania wengi wanaamini kwenye kuleta maendeleo ya kiuchumi na kijamii kutokana na uwepo wa mfumo imara wa kisiasa unaolelewa na kuongozwa na CCM. Wengi wanachohitaji ni amani, utulivu na mshikamano wa kitaifa ili waweze kufanya shughuli zao za uzalishaji kwa tija na ufanisi. Na mwisho, watanzania walio wengi wanaamini katika CCM yenye kuendesha vita endelevu dhidi ya ubaguzi wa kidini, kikabila, kikanda, kijinsia na ubaguzi wa rangi ya ngozi.
Mabadiliko – Ndiyo, lakini si ya chama bali ya namna tunavyofanya mambo, na ukweli ni ukweli tu, na ni mmoja, na siku zote haubadiliki wala haufuati mkumbo. Ukweli una sifa ya kubaki kuwa ukweli tu, hata kila kitu kibadilike. Ukweli ni kwamba, mpaka sasa hakuna chama cha siasa chochote kile kinachoweza kubeba matumaini na matarajio ya watanzania moyoni kabisa, bila hila wala inda ndani yake, zaidi ya CCM. Huo ndiyo ukweli. Na hautobadilika. Mabadiliko sahihi yatatoka ndani ya CCM, na CCM hiyo imefika sasa. Inaitwa CCM ya Magufuli. CCM ya Magufuli ni CCM ya Mabadiliko.
Mwandishi ni Mbunge wa Jimbo la Nzega anayemaliza muda wake. Ni msomi wa digrii za udaktari, afya ya jamii na uongozi na usimamizi wa biashara. Pia ni mwandishi wa vitabu na mchambuzi wa mambo ya afya, siasa, uchumi na maendeleo. Anapatikana kwa email: hkigwangalla@gmail.com
Hamisi A. Kigwangalla, MD, MPH, MBA
P.O.Box 22499,
Dar es salaam.
Tanzania.
Phone No: +255 754 636963
+255 782 636963
website: www.peercorpstrust.org or www.hamisikigwangalla.com
Email: hamisi.kigwangalla@peercorpstrust.org or info@hamisikigwangalla.com
Skype ID: hkigwangalla
Blog: blog.hamisikigwangalla.com
Unapokea Email hizi kwa sababu umejiunga na Jukwaa la 'Mabadiliko'.
Kuchangia mada tuma kwenye Email hii: mabadilikotanzania@googlegroups.com
For more options, visit this group at:
http://groups.google.com/group/mabadilikotanzania?hl=en?hl=en
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Mabadiliko Forum" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to mabadilikotanzania+unsubscribe@googlegroups.com.
To post to this group, send email to mabadilikotanzania@googlegroups.com.
Visit this group at http://groups.google.com/group/mabadilikotanzania.
To view this discussion on the web visit https://groups.google.com/d/msgid/mabadilikotanzania/CAGnhviB_gLhMOzyjmwjg5GTGN0wxX3tVusLYOnam8HDtytJu7Q%40mail.gmail.com.
For more options, visit https://groups.google.com/d/optout.
0 Comments