[Mabadiliko] 2015: NI KURA YA MAAMUZI MAGUMU

Thursday, September 10, 2015
UCHAGUZI 2015: NI KURA YA MAAMUZI KUHUSU UMASKINI WA WANANCHI
Na Ananilea Nkya
Tanzania ni moja ya nchi chache barani Afrika ambazo zimejaliwa utajiri mkubwa wa mali asili yakiwepo madini, ardhi yenye rutuba iliyosheeni milima mabonde na wanyama lakini mamilioni ya wananchi ni masikini wa kutisha ingawa nchi ilipata uhuru zaidi ya miaka 50 iliyopita.

Ili nchi iweze kuondokana na umasikini hata kama inazo rasilimali nyingi inapaswa kuwa na rasilimali nyingine muhimu—rasilimali uongozi –uongozi unaohakikisha kuwa mali za nchi zinanufaisha wananchi wote na siyo kikundi kidogo cha viongozi.

Uongozi wa nchi kwa kawaida hupatikana kupitia vyama vya siasa. Hivyo ni muhimu wanaotafuta fursa ya uongozi katika uchaguzi wa mwaka huu 2015, kutambua kuwa mamilioni ya Watanzania hivi sasa ni maskini ili hali kikundi kidogo cha viongozi ni matajiri sana.

Kibaya zaidi mamilioni ya Watanzania wanaotaabika kwa umaskini hivi sasa wametambua kuwa umaskini wao unatokana na uongozi unaotoa fursa kwa viongozi kuwa matajiri wa kupindukia na mamilioni ya wananchi kubaki maskini.

Mamimioni hayo ya wananchi wanateseka kwa umaskini mwaka huu wanataka mabadiliko ya uongozi wa nchi yao.

Wanataka mabadiliko hayo baada ya kutambua kuwa mfumo wa utawala (Katiba) uliotengenezwa na serikali ya CCM ndio unawezesha watawala wachache kuwa matajiri wa kutupa kwa kulipana fedha nyingi za umma na kujigawia rasilimali za nchi kujitajirisha wao wenyewe.

Kwa mfano wananchi wanajua kuwa watawala walijiuzia kwa bei chee nyumba za umma zilizojengwa kwa mabilioni ya fedha za kodi ya Watanzania wanaoteseka kwa umaskini.
Kadhalika, wananchi wanafahamu kuwa viongozi wa serikali walijigawina fedha za umma zilizoibiwa kwenye akaunti ya Tegeta escrow mwaka jana 2014.

Vilevile wananchi wanajua kuwa watawala mfano wabunge wanalipwa mishahara mikubwa na kiinua mgongo kikubwa katika muda wa miaka mitano tu huku watumishi wengine wa umma mfano walimu, wauguzi na madaktari wakiwa wanalipwa mishahara midogo sana.

Kwa sasa, mtu ambaye haijamuingia akilini kwamba mamilioni ya wananchi wamechoka na umaskini ambao chanzo chake ni uongozi mbovu katika nchi yao—uongozi ambao unatajirisha wachache na hivyo wanataka mabadiliko ya uongozi wa nchi yao, mtu huyo atakuwa anajidanganya.

Jambo jema ni kuwa hata baadhi ya wagombea Urais kwa mfano mgombea wa CCM, Dr John Magufuli na mgombea wa CHADEMA, Edward Lowassa kwa niaba ya vyama vinavyounda UKAWA wamekuwa wakizungumza wazi kwenye mikutano yao ya kampeni kwamba wananchi wanataka mabadiliko ya uongozi.

Tena wagombea hawa wanatambua wazi kuwa mabadiliko watayaleta hao Watanzania wenyewe wanaoteseka kwa umaskini kwa kutumia sanduku huru la kura hapo tarehe 25 Oktoba mwaka huu 2015.
Kwa maneno mengine mamilioni ya wapiga kura maskini wanajua kuwa uchaguzi wa mwaka huu 2015 kura yao ni kura ya maamuzi juu ya maisha yao. Ni kura muhimu ya KUAMUA KUENDELEA KUWA MASKINI AU KUUKATAA UMASKINI.

Ni kura ya kuamua iwapo wanataka watawala wachache wanaotengenezwa na serikali ya CCM waendelee kuwa matajiri wa kutisha na mamilioni ya Watanzania waendelee kuumizwa na umaskini ili hali nchi yetu ikiwa ni tajiri mkubwa wa rasilimali za asili za kuwawezesha Watanzania wote kuwa matajiri na kuishi maisha ya furaha na yenye hadhi.

Wananchi wenyewe wanajua kuwa mabadiliko wanayoyataka yanawezekana ingawa kumekuwa na njama za kujaribu kupunguza nguvu ya umma inayodai mabadiliko kutumia baadhi ya viongozi wa ngazi za juu kwenye vyama vya upinzani vinavyounda UKAWA (CUF, CHADEMA, NCCR Mageuzi na NLD)--vyama vinavyoongoza wananchi katika kutafuta mabadiliko.

Wananchi wameshuhudia baadhi ya viongozi wa upinzani wakiamua ghafla kuondoka kwanye uongozi na kuungana na watawala ambao mfumo wa uongozi umewafanya kuwa matajiri wa kutisha huku wananchi wengi wakiwa ni maskini wa kutupa.

Lakini pamoja na viongozi hao kuachia ngazi, mamilioni ya wananchi hawajabadilika, hawajayumba, msimamo wao uko pale pale na wanasonga mbele hadi waweze kufanya mabadiliko wanayoyataka.

Ni kwa nini wananchi wanataka mabadiliko ya uongozi wa nchi yao?
Wanataka nao wawe matajiri katika kipindi cha miaka mitano kama ambavyo wananchi wenyewe wameshuhudia wanaochaguliwa kuwa viongozi wakitajirika ghafla baada ya kuchaguliwa kuwa viongozi!

Wananchi wamechoka kuwa mafukara katika nchi yao yenye utajiri mwingi wa asili lakini utajiri huo unatajirisha makundi mawili tu-- watawala wachache na wawekezaji wa kigeni.

Tena baadhi ya mamilioni ya Watanzania wanaotaka mabadiliko wengi wao hawana vyama vya siasa wanavyofungamana navyo maana hata fedha za kununua kadi ya chama cha siasa hawana.
Baadhi waliobahatika kuwa wanachama wa vyama vya siasa kikiwepo chama kinachotawala nchi kwa sasa CCM, lakini wengi wa wanachama hao ni mafukara wa kutupa pia wanaohangaika kwa umaskini kama wananchi wengine.

Kimsingi, mamilioni ya watu maskini (nguvu kubwa ya umma) ambayo mfumo wa uongozi wa serikali ya CCM umezalisha, mabadiliko wanayoyataka ya uongozi hayaepukiki maana hakuna anayeweza kuizuia nguvu ya umma inapoamua kuleta mabadiliko.

Isitoshe, mamilioni ya wananchi hawa maskini, ni kama bomu ambalo serikali ya CCM imelitengeneza kwa kujua au kwa kutokujua kwa miaka kadhaa sasa na hivi sasa linasubiri kulipuka lenyewe kwa amani kwenye sanduku huru la kura tarehe 25 Oktoba 2015.

Jambo la kuzingatia ni kwamba , atakayejaribu kuzuia kwa mkono bomu hilo lisilipuke kwa amani kwenye sanduku huru la kura---uwanja wa wazi ambao ndio pekee bomu hilo linaweza kulipuka bila kuleta madhara ya kuvuruga amani ya nchi, mtu huyo historia ya taifa hili itamhukumu. Mungu ibariki Tanzania.

NOTE: Naridhia anayetaka kuichapisha au kusambaza makala hii isomwe na Watanzania wengi afanye hivyo.

Ananilea Nkya
 E-mail:ananilea_nkya@yahoo.com

--
Unapokea Email hizi kwa sababu umejiunga na Jukwaa la 'Mabadiliko'.
Kuchangia mada tuma kwenye Email hii: mabadilikotanzania@googlegroups.com


For more options, visit this group at:
http://groups.google.com/group/mabadilikotanzania?hl=en?hl=en
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Mabadiliko Forum" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to mabadilikotanzania+unsubscribe@googlegroups.com.
To post to this group, send email to mabadilikotanzania@googlegroups.com.
Visit this group at http://groups.google.com/group/mabadilikotanzania.
To view this discussion on the web visit https://groups.google.com/d/msgid/mabadilikotanzania/1441877007.16472.YahooMailBasic%40web121001.mail.ne1.yahoo.com.
For more options, visit https://groups.google.com/d/optout.

Share this :

Related Posts

0 Comments