Mayage S. Mayage
Je, katika mazingira hayo ya sasa ya kisiasa ndani ya Chadema, chama hicho kinaweza kuwahitaji sana kweli wanasiasa aina ya James Lembeli na Esther Bulaya?
Kwamba katika jimbo zima la Kahama mjini au jimbo la Ushetu, Chadema haina mgombea ubunge wa maana kuliko Lembeli?
Kwamba katika jimbo zima la Bunda, Chadema haina mwanachama wake wa maana, anayeweza kukileteaushindi chama hicho kuliko Esther Bulaya? Jibu ni kwamba Chadema inao wanachama wake wengi tu wanaowazidi wanasiasa hao, kimvuto na kimaadili, wanaoweza kukubalika kwa wanachama wenzao na wananchi wengine kwa ujumla wao katika majimbo hayo, na wanaoweza kukiletea ushindi mzuri kuliko Lembeli na Esther.
Ndugu zangu, zama zile za kusubiri watu wengine wafyeke mapori, wachomwe na miba, watoke jasho jingi, halafu wao waende kuvuna tu na kufaidi jasho la wenzao, halipo tena Chadema. Ndani ya chama chochote cha siasa makini, mtu atathaminiwa kwa jasho lake jingi alilolitoa kwa ajili ya ujenzi wa chama husika
. Ndani ya Chadema ya sasa, hakuna yeyote anayeweza kujiona ni lulu ya kisiasa, akaondoka CCM na kwenda kukabidhiwa tu ubunge ndani ya chama hicho. Ikitokea viongozi wakuu wa chama hicho wakahendekeza hilo, watakuwa wanakosea sana, watakuwa hawawatendei haki wanachama wao waliokitolea jasho jingi chama chao!
Kuwapokea watu wanaojiona wao ni lulu ya kisiasa wakati si lolote, na kisha kuwakabidhi majimbo ya uchaguzi ambayo wala hawajui kiasi cha jasho lilitumika kulifikisha jimbo hilo katika hali ya mwamko wa kisiasa uliopo leo, itakuwa ni kuwavunja moyo, itakuwa ni kuwavunja nguvu wale wote waliovumilia jua na mvua kwa matarajio ya kulia kivulini baadaye.
Lembeli alikuwa kada wa CCM, ameshiriki kwa njia moja au nyingine kudhibiti nguvu na ukuaji wa Chadema katika jimbo na wilaya nzima ya Kahama, halafu huyo ndiye anataka apewe Jimbo la Kahama kwa tiketi ya chama hicho alichotumia nguvu zake kukiuwa.
Lembeli akaribishwe kwa mikono miwili ndani ya Chadema. Apewe miaka mitano ya kuongeza nguvu za ujenzi wa Chadema ndani ya jimbo na wilaya hiyo, baada ya miaka mitano ijayo chama chake mpya hicho kimpime kama kweli anastahili kupata ubunge kulingana na mchango wake.
Ni katika kumpokea na kumpima katika kipindi hicho cha miaka mitano, uongozi wa Chadema unaweza ukamtathimini kama kweli mwanachama wao huyo mpya ameingia kutokana na mapenzi yake juu ya itikadi na sera za chama hicho au ameingia ili kutafuta fursa tu, na baada ya kupata atageuka kuwa Shibuda mwingine?
Ndiyo! Kina Shibuda waliingia Chadema mwaka 2010 kwa ajili ya kusaka fursa ya ubunge tu. Kwa kauli na kwa matendo yake, Shibuda, ndani ya miaka yake mitano ya ubunge wa Jimbo la Maswa Magharibi, amedhihirisha kwamba hakuwahi kuwa na mapenzi na Chadema, hakuwahi kuwa na imani na viongozi wakuu wa chama hicho.
Katika funzo hilo la Shibuda kwa viongozi wakuu wa Chadema, kuna sababu gani kwa viongozi wakuu hao wa chama hicho kikuu cha upinzani nchini, waache mbachao za vijana wao waliojitolea kwa hali na mali kuijenga Chadema yao katika wilaya nzima ya Kahama na badala yake wakumbatie msaala upitao wa Lembeli yule yule aliyekuwa anakisulubu?
Lembeli huyu ambaye ameikimbia CCM yake baada ya viongozi wake wa chama katika ngazi hiyo ya wilaya kukataa kuwa chini yake na kutii amri zake, kwa tabia yake hiyo ya kujiona yeye ni mwanasiasa bora, atashindwaje kukosana na Mbowe na Dk Slaa baada ya kuupata ubunge kupitia chama ambacho hajawahi kukitolea jasho lolote?
Esther Bulaya, ambaye mashabiki wake ndani ya Chadema katika jimbo zima la Bunda ni wale tu alioungana nao kupitia mitandao ya whatsap na facebook, atawezaje kusimama mbele ya wazee, kina baba na kina mama wa jimbo hilo na kuongea lugha yao tofauti na lugha yake ya ndani ya WhatsApp na Facebook?
Kuna wasomi wazuri wangapi wafuasi wa Chadema ambao wameshiriki kwa nguvu zao na rasilimali zao kiasi cha kukifanya chama hicho kionekane vile kinavyoonekana leo ndani ya jimbo lile. Vijana wenye staha zao, wenye lugha zinazofanana na wazee wa jimbo lile, kina baba na kina mama, wanaovaa mavazi yanayozingatia mila na desturi za jamii ya wana-Bunda, wanaoweza kukaa chini kwenye mkeka na kula pamoja na wazee hao kamongo wao, bila kupata shida ya kushikilia nguo zao kwanza ili waweze kuketi kwenye mkeka?
Vijana wa Bunda wanamhitaji mwakilishi wao kijana, lakini naamini kijana huyo hawezi kuwa Esther Bulaya, kama ambavyo vijana wa Tarime walihitaji kuwakilishwa na mbunge kijana, lakini wakasema Mwita Waita Mwikabe, hawafai na hadi leo haijulikani alikopotelea kisiasa!
Ndugu zangu, nasema hapa kutoka moyoni mwangu, Chadema ya sasa haimhitaji sana Lembeli wala Esther Bulaya ili kutwaa majimbo ya Kahama na Bunda. Kila mwana-Kahama na mwana-Bunda, anafahamu udhaifu wa watu hawa, kitabia na kimaadili. Nahitimisha! –
Raia Mwema
Toleo la 416
29 Jul 2015
0 Comments