[wanabidii] Lowassa, nionyeshe marafiki zako na mimi nitakuambia wewe ni nani?

Friday, June 12, 2015
Lowassa, nionyeshe marafiki zako na mimi nitakuambia wewe ni nani

SIKU Edward Lowassa alipotangaza rasmi kugombea urais wa Tanzania nilibahatika kumsikiliza na nilishuhudia umati mkubwa wa watu waliofurika kumsikiliza. Ni kweli yalikuwa ni mafuriko ya watu.

Sijui kama walikwenda kwa hiari yao au walilipwa ili waende kwenye mkutano huo. Hilo sijui wala si ajenda yangu kwenye makala hii. Jambo ambalo ninataka wasomaji wa makala hii walizingatie ni aina ya watu waliokuwepo kwenye mafuriko hayo, kwani ndege wenye manyoa yanayofanana ndiyo wanaoruka pamoja.

Tumeona utawala wa Rais Jakaya Kikwete. Rais aliyeingia kwa hamasa kubwa akibeba matumaini na matamanio ya mamilioni ya Watanzania . Utawala wa Kikwete ulikuja na kila ahadi za kurudisha utukufu wa Taifa. Lakini Kikwete atakapoondoka mwezi wa kumi mwaka huu, Je atakuwa amefanikiwa kurudisha heshima ya taifa letu? Na wakati wa mchakato wa kugombea urais, Watanzania wengi walimuunga mkono Kikwete hadi baadhi ya viongozi wa dini walifikia kusema alikuwa chaguo la Mungu. Walisema sauti ya wengi ni sauti ya Mungu!

Leo ukisema kwamba Kikwete alikuwa chaguo la Mungu, sijui kama Watanzania wengi watakubaliana na wewe. Sijui. Rais Kikwete alitengeneza mtandao uliomsaidia kuingia Ikulu.Lowassa ametengeneza mtandao unaomsaidia aingie Ikulu.

Isipokuwa katika maelezo yake Lowassa, amejitahidi kujitofautisha na Kikwete na hasa aliposema suala la urafiki wao lisihusishwe katika azma yake ya kuomba nafasi ya kuwa rais. Anawataka Watanzania wampime kama yeye binafsi na wasilihusishe suala la urafiki wao.

Sijui kwa nini kwa sasa Lowassa anajitenga na Kikwete. Lakini Watanzania wanakumbuka Lowassa aliwahi kusema urafiki wao si wa kukutana barabarani.

Kwa kuwa Lowassa anaomba nafasi ya nyeti ya urais ni muhimu Watanzania wajiridhishe bila shaka yoyote Lowassa ni nani. Na je anaweza kukabiliana na changamoto zinazolikabili Taifa letu hasa ufisadi, rushwa na kuporomoka kwa maadili.

Mwalimu Nyerere katika kitabu chake, Nyufa, cha mwaka 1995, alisema: "Sasa Tanzania inanuka rushwa… tunataka kiongozi anayejua hivyo, ambaye atasema rushwa kwangu mwiko, mwaminifu kabisa kabisa, hawezi kugusa rushwa na… watoa rushwa watamjua hivyo. Lakini hatutaki aishie hapo tu, maana haitoshi wewe mwenyewe uwe mwaminifu…Unaweza ukawa wewe mwaminifu kabisa kabisa, lakini una shinikizo la ndugu zako, jamaa zako na marafiki zako."Kwa hiyo si inatosha wewe kuwa mwaminifu tu, lakini uwe na uwezo wa kuwaambia jamaa zako kwa kauli ambayo wataiheshimu na hawatarudia tena.

Unawaambia jamaa na rafiki zako kwa dhati kabisa… Ikulu ni mahali patakatifu, mimi sikuchaguliwa na wananchi wa Tanzania kuja kupageuza pango la walanguzi na hakuna serikali yoyote duniani inayoongozwa bila miiko".

Zipo taarifa zinazoeleza kwamba fedha nyingi zimetumika katika kufanya maandalizi ya mkutano wa Arusha uliosababisha mafuriko ya watu. Aidha, ndugu Lowassa mara kadhaa amekiri kwamba marafiki zake ndio wanaomchangia kufanikisha safari yake ya matumaini.

Hivyo fedha nyingi anazochangia kwenye harambee kwenye misikiti na makanisani nyingine anatoa yeye na nyingine anachangiwa na hawa marafiki zake ambao wengi wao ni wafanya biashara matajiri na wengi wao ni wale waliotajwa kwenye kashfa za ufisadi na tuhuma mbalimbali.

Hawa marafiki zake Lowassa wamesaidia sana kumjua Lowassa ni nani, kwani wahenga walisema, "Nionyeshe marafiki zako na mimi nitakuambia wewe ni nani au wewe una tabia gani".

Hawa marafiki zake na Lowassa wanaweza kuwasababisha Watanzania wamtilie shaka Lowassa kama anaweza kuwa safi na kustahili kupewa dhamana ya kuongoza nchi. Naomba niwakumbushe kauli ya Mwalimu Nyerere kuhusu mmoja wa wagombea urais kwenye NEC Dodoma mwaka 1995, "Hapa hatuchagui mtu maarufu, tunachagua mtu safi na huyu si safi". "Kama unapenda sura yake basi nenda kanywe nae chai. Wengine mnasema aaah ni tuhuma tu.

Hapa mnasema ni tuhuma tuhuma tu! Lakini mtakumbuka mke wa Kaisari alipotuhumiwa kwa ugoni, Kaisari akaagiza uchunguzi ufanyike". "Uchunguzi ukafanyika na ikabainika kwamba si kweli. Lakini Kaisari bado akamwacha, akasema mke wa Kaisari hapaswi hata kutuhumiwa. Na sisi hapa mgombea wetu hapaswi hata kutuhumiwa wakati wapo wengine wasafi ambao hawana tuhuma."Kama mtamteua huyu mimi sitapiga kampeni. Siko tayari kumsafisha mtu matope halafu nimwombee kura.

Hapana kabisa . Huyu najua si msafi na nchi nzima inajua si msafi. Hafai kuwa mgombea wetu".

Aidha, mtakumbuka pia kuwa mwaka 1995, kundi la Vijana lilimtaka Lowassa ateuliwe kugombea urais wa Tanzania. Hata hivyo, ilitolewa kauli kuwa Lowassa alikuwa na tuhuma za rushwa, kujilimbikizia mali na kupungukiwa na maadili, kinyume na katiba ya CCM na kanuni za chama hicho.

Kamati Kuu ilipopeleka mapendekezo ya kutompendekeza kugombea urais, Lowassa alitetewa kwa makelele, kihuni, bila kufuata taratibu za kikao cha NEC Dodoma. Kundi moja lilikuwa limejiandaa kumpitisha kwa hoja ya nguvu na si kwa nguvu ya hoja.

Waliyatetea maelezo ya Kamati Kuu, lakini waliyakataa yale ya nyongeza aliyoyatoa Mwenyekiti Ali Hassan Mwinyi (Rais wa wakati huo) ambaye alielezea tuhuma hizo zilizokuwa zinamkabili Lowassa. Hivyo, naomba kusisitiza kwamba Lowassa hakuwa chaguo la CCM katika uchaguzi wa mwaka 1995. Katika kikao hicho cha Kamati Kuu, Mwalimu Nyerere aliamua kusaidia kikao kwa kutoa maelezo ya nyongeza.

Aliwauliza wajumbe wa NEC maswali, kwamba wao ni wahuni au ni viongozi wa CCM? Ikiwa wao ni viongozi wa CCM, je, hivyo ndivyo wanavyopaswa kumtafuta mgombea wa urais, kwa makelele?

Kama Watanzania wangewaona walivyokuwa wanafanya katika kikao hicho, je, wangeamini kuwa wao ni viongozi kweli? (Wajumbe walibaki kimya). Kisha Mwalimu aliendelea kusisitiza maelezo aliyoyatoa Mwenyekiti Ali Hassan Mwinyi akisema: "Mwinyi amemstahi sana Lowassa".

Hakuwaambia wajumbe wa NEC baadhi ya tuhuma mbaya kabisa kuhusu Lowassa. Ikiwa NEC inachoombwa ni kuchagua kati ya wenye tuhuma za rushwa kuchaguliwa kwa nafasi ya urais, na wale wasioitaka, basi huu ni wakati muafaka kwao kuipeleka hoja hiyo mbele ya Watanzania waiamue kwa kuwa ndani ya NEC hakuna mwenye uwezo wa kumfukuza mwenzie, wote ni wajumbe sawa kwa mujibu wa katiba ya CCM".

Hatimaye kikao cha NEC kiliondoa jina la Lowassa, kikawateua Benjamin William Mkapa, Cleopa David Msuya na Jakaya Mrisho Kikwete kuwa wagombea. Majina yaoyaliwasilishwa kwenye Mkutano Mkuu ambao ndio uliopaswa kumchagua miongoni mwao kuwa mgombea

Mwandishi Fred Mpendazoe

Toleo la 409: Jun 10 2015

--
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com

Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma

Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/d/optout.

Share this :

Previous
Next Post »
0 Comments