[wanabidii] Lowassa anadanganywa na wabunge wanaonyemelea mamilioni aliyonayo

Tuesday, February 10, 2015

Lowassa anadanganywa na wabunge wanaonyemelea mamilioni aliyonayo

Na Mwandishi Maalum

MAGAZETI kadhaa yatolewayo kila siku nchini, Jumatatu Februari 9, 2015, yaliongozwa na habari kuu kuhusu Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa kwamba 'anang'ara katika mbio za urais'.

Katika habari hiyo, magazeti hayo yote yalinukuu kauli za wabunge saba wa CCM wanazodaiwa kuwa walizitoa katika hafla iliyotajwa kuwa "ya aina yake" ya chakula cha jioni, Jumamosi iliyopita.

Lakini katika hali isiyokuwa ya kawaida, hafla hiyo kamwe haikutaja ilikofanyika zaidi ya kuelezwa tu kuwa "nyumbani kwa kigogo mmoja wa CCM", Kilimani mjini Dodoma.

Kwa nini kigogo huyo alifichwa utadhani hafla hiyo ilikuwa haramu au kwamba iliambatana na vitendo vya kihalifu?

Wabunge waliotajwa na kunukuliwa wakizungumza ni Deogratius Ntukamazina (Ngara), Diana Chilolo (Viti Maalum – Singida), Stephen Ngonyani au 'Profesa Maji Marefu' (Korogwe Vijijini) na Mary Chatanda ambaye pia wa Viti Maalum (Tanga) na Katibu wa CCM wa Mkoa wa Singida.

Wengine ni Kapteni John Komba (Mbinga Magharibi), Mussa Azzan Zungu (Ilala) na Yahya Kassim Issa ambaye ni mbunge wa Chwaka, Zanzibar.

Wote walinukuliwa wakimwelezea Lowassa ambaye pia ni Waziri Mkuu wa zamani kwamba "ni kiongozi bora, kiongozi makini, chaguo la Watanzania" na kadhalika.

Ntukamazina kwa mfano alisema: "Kule kwangu Ngara wananiuliza yule waziri mkuu aliyeleta hizi shule za kata yuko wapi? Mimi nawajibu atarudi na kila mtu mitaani anataja jina lako, kwa hiyo sauti ya wengi ni sauti ya Mungu".

Wasiwasi kuhusu habari hiyo
Kila gazeti, licha ya habari hiyo kuandikiwa ukumbini na isiyokuwa ya uchunguzi, yote hayakutaja jina la mwandishi kwa kusema ni "Mwandishi Wetu, Dodoma", halafu zote zinafanana kwa kila kitu katika mambo yafuatayo:
(i) Kutotaja jina la kigogo wa CCM aliyeandaa hafla hiyo kuwa ni nani;

(ii) Idadi ya wabunge waliohudhuria hafla hiyo imetajwa na kila gazeti kuwa 150 utadhani kila mwandishi aliwahesabu au walihesabiwa mlangoni, kisha hesabu yao ikatangazwa hadharani;

(iii) Wabunge waliotajwa kwenye magazeti hayo kuwa waliongea ni walewale; na

(iv) Wabunge hao pia wametajwa kwa mtiririko uleule, nukuu zilezile, namna ileile huku kila kitu kikiwa kinafanana kama barua iliyopigwa photocopy na kusambazwa huko kote;

Katika hali hiyo, yapo mambo kadhaa ya kutilia wasiwasi kwa wasomaji makini ambayo ni pamoja na haya yafuatayo:
(i) Kuna kila mwelekeo wa kuwa hafla hiyo iliandaliwa kwa agizo au kwa gharama za Lowassa mwenyewe;

(ii) Kuna kila mwelekeo wa kuwa hafla hiyo iliandaliwa maalum kwa ajili ya kampeni za urais za Lowassa, lakini ukakosekana umakini wa kutosha ili kufanikisha siri iliyolenga kuwadanganya Watanzania;

(iii) Wabunge waliozungumza inaelekea kwamba waliandaliwa maalum, halafu inawezekana kuwa maneno waliyozungumza walipewa au walielekezwa na Lowassa mwenyewe ama na washauri wake; na

(iv) Habari hiyo imeandikwa na mwandishi mmoja, kisha ikasambazwa katika magazeti hayo yote kwa gharama za mwanasiasa na mbunge huyo ikiwa ni sehemu ya kampeni zake za urais.

Ili kuthibitisha vinginevyo, magazeti hayo inabidi yajibu maswali makubwa yafuatayo kwa wasomaji wake ambao ni pamoja na mimi kwamba ilikuwaje habari hiyo ifanane kwa zaidi ya asilimia 75 kuhusu:

(i) Mpangilio wa wabunge walivyozungumza katika hafla hiyo?

(ii) Ilikuwaje idadi ya wabunge waliozungumza na kunukuliwa na magazeti hayo yote iwe ileile?

(iii) Ilikuwaje mtiririko wa habari hiyo ufanane kiasi hicho kwa magazeti yote na kuonekana kuwa imeandikwa na mwandishi mmoja kama kweli ni tofauti?

(iv) Kama habari hiyo iliandikwa na waandishi tofauti, wapi walikokutana, kisha wakakubaliana kuwa nukuu zao zote ziwe ni zilezile?

(v) Wapi waandishi hao walikokutana na kukubaliana kuwa vilevile mtiririko wa nukuu zote hizo ufanane kama mayai?

Mfano ninaomaanisha ni kama pale Mbunge wa Ngara, Deogratius Ntukamazina aliponukuliwa na magazeti hayo yote akisema:

"…Oktoba tutakuwa na uchaguzi mkuu wa kumchagua kiongozi atakayesukuma mbele nchi yetu.

"Sote tunafahamu chama chetu bado hakijatangaza utaratibu, lakini sisi wabunge marafiki zako tunakuomba muda ukifika uchukue fomu kwa sababu unatosha".

Nukuu hiyo ya neno kwa neno ipo katika kila gazeti, halafu imeandikwa kwa staili ileile na kwa aya zinazofanana utadhani ilipigwa 'photocopy' na kusambazwa huko kote.

Mbali na hapo, habari hiyo pia inafanana kwa kila kitu katika magazeti hayo yote ambapo, pale palipoandikwa bila ya kunukuu neno kwa neno inakuwa hivyo kwa kila gazeti, na pia kila paliponukuliwa (quoted) napo panakuwa vilevile utadhani pamefanyiwa 'scanning'.

Aidha, magazeti hayo yote yamemwandika Chilolo kwa aya moja yenye maneno 22 tu kama ifuatavyo:

"Kwa upande wake, Mbunge wa Viti Maalum, Diana Chilolo (CCM) aliunga mkono kauli ya Ntukamazina kwa kusema Lowassa ni chaguo la wengi".

Wasomaji wote makini walioisoma habari hiyo ndani ya magazeti hayo au baadhi yake hakuna mashaka kwamba waligundua kuwa ilitengenezwa maalum kwa ajili ya kumbeba Lowassa katika harakati zake za urais.

Pamoja na ukweli kuwa kila mwanasiasa anayetafuta madaraka ya uongozi wa umma huwa na njia zake mwenyewe za kutafuta ushindi, lakini mbinu hiyo ya Lowassa haiwezi kuwadanganya walengwa ambao hasa ni viongozi waandamizi wa CCM.

Wabunge aliowatumia kutaka kufanikisha mkakati wake huo wa kuitisha CCM ili iogope kuwa isipomteua kugombea urais itaondoshwa madarakani na wapinzani, kwamba asipoteuliwa yeye ili kusimama katika kinyang'anyiro hicho basi chama hicho kitashindwa kuna wengine wamekubali kutumika kiasi hicho kwa sababu inaelezwa kwamba ana pesa nyingi.

Ukimwondoa mtu kama Ntukamazina ambaye ameshasema kuwa hagombei tena ubunge mwaka huu, Chatanda anajipanga kutaka kugombea ubunge wa jimbo la Korogwe Mjini huku Komba au 'Maji Marefu' nao wakikabiliwa na hali ngumu majimboni kwao.

Ili waweze kupata ushindi kwanza kwenye kura za maoni za ndani ya CCM, wabunge hao inabidi kila mmoja awe na kiwango kikubwa kabisa cha pesa za kampeni, fedha ambazo hakuna hata mmoja aliyenazo.

Wote wanategemea kiinua mgongo ambacho kila mmoja atalipwa na serikali baada ya muda wao wa sasa kumalizika kiasi cha miezi mine ijayo, lakini wanafahamu kwamba hazitoshi kuwapa ushindi wanaoutafuta.

Kwa mfano, Komba amekuwa akitishiwa hadi kufilisiwa na benki anakodaiwa mamia ya mamilioni ya fedha alizokopa pamoja na riba, deni linalotishia hadi kukamatwa kwa mali zake kwa sababu ameshindwa kulipa.

Wote walijitolea mhanga kumsifia hadharani mbele yake mwenyewe siyo kwa sababu eti wanamuunga mkono kwelikweli, bali walifanya hivyo kwa sababu wanayataka mamilioni ya pesa zake.

Wanataka kumdanganya kwa sababu wanataka fedha hizo ili nao pia wakahangaikie ubunge kwa muhula mwingine kwenye majimbo yao. Walikuwa hawamsifu eti kwa sababu anatakiwa kiasi hicho kuwa Rais wa Serikali ya Awamu ya Tano.

Wote wananyemelea mamilioni ya fedha anazodaiwa kufadhiliwa au kwa yeye mwenyewe kujikusanyia kwa namna moja ama nyingine.NI MTAZAMO WANGU

--
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/d/optout.

Share this :

Related Posts

0 Comments