> MSHUMAA ULOZIMIKA
> ( Dr. Muhammed Seif Khatib)
>
> Mengi husemwa kuhusu mshumaa.Waimbaji wa Taarab wameutetea kuwa
> unaonewa na haupewi heshima inayostahiki ingawa unawaka na kufurahisaha
> umati.Mshumuaa unalinganishwa na chumvi inayopewa pole kuwa nayo haina
> thamani hata ikiwa ndani ya gunia zima.Chakula husifiwa kuwa kitamu lakini chumvi katu
> haitajwi wala kudhukuriwa.Lakini ikiwa kidogo itaongezwa ikwa nyingi watu
> wanakerekwa. Mshumaa hulinganishwa siyo na chumvi tu bali pia na sabuni.
> Sabuni hung'arisha nguo,hutoa povu lakini hatimaye huyayuka na kupoteza
> maisha yake kwaajili ya umaridadi wa watu wengine.Kadhia hii ya mshumaa,chumvi na sabuni tuwaachiye washairi na waimbaji wa Taarab.Mshumaa ni aina chanzo cha kutoa meangaza panapo kiza. Wengine
> hupata mwangaza kwa kutumia taa za umeme.Hawa ni wale wenye uwezo.Wapo wachochele hutegemea vibatari,kandili au karabai.Mshumaa ndio itegemewao nao
> kutoa mwangaza.Tamaduni tofauti za makabila na dini hitumia mshumaa kwa dhamira
> tofauti.Kwa kiasi kikubwa mshumaa hutoa ujumbe unaofanana.Wapo wanaowasha
> katika misiba.Wapo wanaowasha kuashiria mshikiamano kwa jambo ambalo wanalipigania.Wapo wanaowasha kuashiria mapenzi na huba nzito.Wapo wanaowasha
> kutaka mwanga,nuru na matumaini.Mshumaa huo ukizimika huwakosesha jamii mambo
> yote hayo.Alhamis tarehe 19.02.15 kama saa tano hivi asubuhi, mshumaa uliokuwa unawaka na kutoa nuru ukazimika ghafla.Ni kifo cha ghafla cha Salmin Awadhi,kiongozi
> na mwanasiasa wa Zanzibar kutoka chama cha Mapinduzi.Salmini alikuwa sawa na
> mshumaa uliozimika ghafla kabla matarijio ya wakati wake.Kama mshumaa hutoa mwanga
> na kulifurusha kiza, Salmini aliwatimua mbio wapinzani wa chama chake. Hawakuwaacha
> kutamba.Aliwadhibiti kwa nguvu ya hoja na kuwaambia kinagaubaga yale wanayostahiki
> kuambiwa.Kwao ulikuwa mwiba mkali. Hakuchelea kuwaambia ukweli ingawa hawakupenda
> kupashwa.Wanasiasa wenzake wa chama chake katika Baraza la Wawakilishi walipokuwa
> wanamungunya maneno katika mambo mazito yeye alisimama kifua mbele kuyasema
> yale yanayopaswa kusemwa bila kigugumizi.Wakati wengine katika chama chake huanglia
> sura ya kiongozi na matashi yake, yeye hakuwa kiongozi wa msimu.Mbichi huita mbichi na mbovu huita mbovu.Uzalendo wake na utaifa wake ulijitokeza waziwazi wakati wa mchakato wa Bunge la Katiba.Siyo tu alikitetea chama chake na sera zake bali alikuwa
> muhamasishaji mkubwa wa vipengele vya Katiba inayopendekezwa.Wapo waliokuwa naye,wapo waliokesha naye katika vikao vya dhahiri na siri na wapo waliokorofishana
> naye kwa kuonesha unaafiki au usaliti ndani ya chama chake.Mambo matatu makubwa
> alikuwa hakuabali kusalimu amri nayo.Utukufu,umuhimu na uhalali wa Mapinduzi ya Zanzibar kwake ni damudamu.Uhalali,utetezi na umuhimu wa Muungano wa Tanganyika na
> Zanzibar na kwake ni jambo la kufa kupona! Na la tatu haki na masilahi ya Zanzibar
> huzitetea pasi shaka. Ni kiongozi aliyekuwa mstari wa mbele wa kutetea uadilifu na uwazi
> katika serekali.Sifa kubwa iliyomjengea heshima katika majukwaa ya siasa ni tabia yake
> ya kutoyumba kwa jambo analoliamini.Husimama kifua mbele kwa kutetea kwa nguvu
> zote jambo aliloliamini.Salmin, kwa tabia na hulka hii ya kutotetereka kwa jambo analiliamin
> limezua kambi za marafiki na maadui.Marafiki wamo ndani ya chama chake na katika kambi ya upinzani.Maadui wake ndani ya chama chake na ndani ya upinzani.Tofauti hizo
> zatokana na misimmo wa kiitikadi anaouamini.Wanasiasa wapo wengi lakini mwenye
> tabia na msimama kama Salmini Awadhi.Kama mshumaa hutumika kama kielelezo cha
> mshikamano,Salmini alikuwa ruwaza njema.Muda wote alikuwa tayari kushikamana
> na wenzake kwa masilihi ya wapiga kura wake,chama chake na taif zima.Tukio la kifo
> chake kutokea katika ofisi ya chama chake na katika kikao ni ushahidi wa kutosha wa
> kuonesha itayari wake wa kufanya kazi pamoja.Mshumaa ni ishara ya mapenzi na
> upendo.Kifo hiki kimemshitua kila mtu.Kwa nini? Alikuwa mtu wa watu.Heshima
> anaowapa wakubwa zake,jinsi anavyonyenyekea wapigakura wake,hayo yatosha
> kuziteka hisia za umma.Umati uliomshindikiza katika safari ya mwisho isiyo na marejeo
> ni mkubwa.Wakubwa walikuwepo.Wadogo walihudhuria.Rika zote zilikuwepo.Jinsia zote
> zilishiriki.Vyama vyote vya siasa viliwakilishwa.Wakati maadui zake kisiasa wanapumua,
> wale marafiki zake wapaswa kumuenzi.Kumuenzi huko kuwe katika kusimamia yale
> mambo aliyokuwa akiyaamini na kuyatetea.Mbali na kutunukiwa na mema na thawabu
> itokaayo na amali yake,yale yote aliyokuwa akiyatetea yakifanikishwa vyema yatampa
> faraja adhimu huko katika malazi yake ya kudumu.Salmin Awadhi ni mshumaa ulion'gara
> na kutuzimikia ghafla.Buriani!
>
>
>
>
> Sent from my iPad
--
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/d/optout.
0 Comments