[Mabadiliko] Ivory Coast Vs Ghana Na Falsafa Ya Kandanda...

Sunday, February 08, 2015


Ndugu zangu,

Wakati tukisubiri ' Fainali ya Njozi' kati ya Ivory Coast na Ghana, nimeona niwaletee simulizi elimishi za kandanda.

Mchezo wa kandanda ni sawa na sanaa, utamaduni. Ni siasa. Kwa wengine soka 
ni imani kama ilivyo imani nyingine za dini. Soka ni zaidi ya soka. 
Imejengeka kifalsafa.

Mathalan, katika Argentina kandanda ni sawa na dini, imani. Diego 
Maradona ni Mungu. Kuna wafuasi wa dhehebu la Maradona ndani na nje ya 
Argentina. Diego Armando Maradona ametokea kupendwa sana, na kuchukiwa sana pia.

Ni wanasoka wachache sana katika ulimwengu huu wa kandanda waliotokea 
kuibua hisia za wapenzi wa mchezo huo kwa namna ya pekee kama ilivyo kwa 
Maradona.

Uwezo wa Maradona katika uchokozi wa kisoka na umahiri wake katika 
kulisakata kandanda ulionekana bayana mwaka ule wa 1986. Ni katika michuano ya 
Kombe la Dunia, na hususan katika pambano la Argentina dhidi ya Uingereza. 
Kwanza Maradona alifunga goli la mkono, baadae kidogo Maradona alifunga goli 
la kiufundi na kibingwa pale alipoambaa kwa kasi na mpira akitokea nusu ya 
uwanja. Aliwapiga chenga za maudhi karibu wachezaji wote wa Uingereza
waliomkabili. Kisha aliukwamisha mpira kimiani. Maradona alidhihirisha 
umahiri wake katika sanaa ya kandanda. Itakumbukwa , Argentina ilishinda Kombe 
la Dunia mwaka ule.

Miaka minne baadae, juhudi za Maradona binafsi ziliiwezesha nchi yake 
kushika nafasi ya tatu katika michuano ya Kombe la Dunia. Katika fainali 
zile mechi kati ya Brazil na Argentina ndiyo iliyokuwa na kivutio cha pekee.
Brazil waliwazidi Argentina katika idara zote uwanjani, hivyo basi, Argentina na 
Maradona hawakupumua kwa muda mrefu wa mchezo. Lakini, mara, na kama radi, alizinduka Diego Maradona. Akiwa amenabwa vikali na walinzi wa Brazil, Maradona 
alifanikiwa kutoa pasi muhimu kwa Claudio Caniggia aliyefunga goli pekee
katika mchezo huo.

Argentina waliingia fainali na kushindwa na Ujerumani. Fainali za Kombe 
la Dunia za 1994 zilimshuhudia Maradona akiwa katika hatua za kuporomoka 
kisoka. Alijitahidi kidogo katika mechi za awali, kisha likalipuka bomu. 
Maradona alibainika kutumia vidonge vya kuongeza nguvu aina ya efedrin. 
Argentina nayo ikapotoea katika hatua za awali za fainali hizo.

Naam, Soka kama dini ina wafuasi wengi. Mpira ule wa mviringo, 
wenye kudunda ni kama Mungu wa soka. Bila mpira uwanjani hakuna soka. Kama 
ulivyo mpira wenyewe, mviringo, wenye sura nyingi na wenye kudunda, basi,
hata pambano lenyewe la soka laweza kuwa na sura nyingi. Naam. Mpira 
unadunda, katika soka lolote laweza kutokea.
Soka, kandanda, kabumbu, kipute au ndinga. Yote hayo na mengineyo ni 
majina yenye kuzungumzia aina moja ya mchezo; mpira wa miguu. Kuna aina 
nyingi za michezo ya mipira; kuna mpira wa wavu, mikono, meza, pete na 
mingineyo.

Michezo yote hiyo niliyoitaja hapo juu inatofautina sana na mchezo 
wa mpira wa miguu. Ni kwanini basi michezo hiyo na mingine yenye kuhusisha 
mpira isiwe na wapenzi wengi kulinganisha na mpira wa miguu? Jibu lake 
linapatikana kwa kutafakari falsafa nzima ya kandanda.

Kandanda huchezwa kwa kutumia miguu. Hii ndio inatufanya wengi 
tuvutiwe na mchezo huu. Kupitia kandanda tunaona kuwa binadamu anaweza 
kufanya mambo mengi ya ajabu kwa kutumia mguu wake. Ni mambo yenye kutoa 
burudani kwa anayetazama. Ndio maana hatuchoki kushabikia mchezo huu.

Kama lilivyo jina la mchezo wenyewe, yaani mpira wa miguu, basi, 
mchezaji haruhusiwi kutumia mikono. Ni golikipa tu anayerusiwa kutumia 
mikono katika kuudaka mpira uliopigwa kwa mguu. Golikipa amepewa eneo lake 
dogo la kujidai kwa kutumia mikono yake. Nje ya eneo hilo golikipa naye 
haruhusiwi kutumia mikono, bali miguu.

Mpira unatakiwa wakati wote huwe ndani ya uwanja. Mpira unaotoka 
nje unaweza kurushwa kwa mikono kuingizwa uwanjani, aliye uwanjani 
haruhusiwi kuupokea kwa mikono isipokuwa golikipa.

Katika mpira wa miguu mchezaji anaruhusiwa kutumia sehemu 
nyingine zote za mwili, kichwa, kifua, tumbo, mgongo, kisigino na hata 
kidevu, lakini , kamwe si mkono. Dhambi kubwa katika soka ni kwa mchezaji 
kuucheza mchezo huo kwa kutumia mkono, na kibaya zaidi akifanya hivyo kwa 
kudhamiria, kwa makusudi. Dhambi hiyo haisameheki katika soka, adhabu yake 
ni kutolewa nje kwa kadi nyekundu. Mkono ni shetani wa soka.

Waingereza ambao kihistoria ndio waliovumbua mchezo wa soka mwaka 
1908, kamwe hawatakoma kumlaani Diego Maradona wa Argentina kwa kufunga goli la mkono nililolielezea hapo juu. Kwa Waingereza, Maradona alifunga goli 
kwa kumtumia shetani wa soka. Maradona mwenyewe anadai ni mkono wa Mungu!

Mpira wa miguu umechangia katika kuleta furaha kwa mamilioni ya 
watu hapa ulimwenguni, pale timu ama taifa linaposhinda mashindano muhimu. 
Lakini mchezo huu umekuwa pia ni chanzo cha huzuni kwa mamilioni ya watu 
katika ulimwengu huu, pale timu au taifa linaposhindwa katika mashindano 
muhimu.

Mpira wa miguu unaingia katika historia ya Dunia kwa kuwa chanzo 
cha vita baina ya mataifa. Katika mika ya sabini, kule Marekani ya Kusini, 
nchi za El Salvador na Honduras zilingia vitani kutokana na matokeo ya 
mpira wa miguu baina ya timu za nchi hizo mbili! Mpira ni siasa pia, kuna 
serikali au viongozi waliobaki ama kuondoka madarakani kutokana na matokeo 
ya mechi za mpira wa miguu.

Siku moja nitawasimulia kisa kile cha mataifa yaliyoingia vitani kwa matokeo ya uwanjani.

Nawatakia utazamaji mwema wa mechi ya usiku huu; Ivory Coast Vs Ghana.
Utabiri wangu: Ivory Coast 3- Ghana 1

Maggid,
Iringa.


--
Unapokea Email hizi kwa sababu umejiunga na Jukwaa la 'Mabadiliko'.
Kuchangia mada tuma kwenye Email hii: mabadilikotanzania@googlegroups.com
 
 
For more options, visit this group at:
http://groups.google.com/group/mabadilikotanzania?hl=en?hl=en
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Mabadiliko Forum" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to mabadilikotanzania+unsubscribe@googlegroups.com.
To post to this group, send email to mabadilikotanzania@googlegroups.com.
Visit this group at http://groups.google.com/group/mabadilikotanzania.
To view this discussion on the web visit https://groups.google.com/d/msgid/mabadilikotanzania/CAMD-ye47Rnq-Pb%2BnoRXoYUUeyoyQ0M9TcxEMwQm83Wh%2BQpMTbQ%40mail.gmail.com.
For more options, visit https://groups.google.com/d/optout.

Share this :

Previous
Next Post »
0 Comments