[wanabidii] Salaam Za Krismasi: Krismasi imekuja ghafla, na matokeo ya darasa la saba pia!

Thursday, December 25, 2014

Na Maggid Mjengwa,
KWA mujibu wa matokeo yaliyotangazwa kwenye vyombo vya habari hivi karibuni, wanafunzi 12, 432 wamekosa nafasi ya kwenda Kidato cha Kwanza 2015. Tunazungumzia watoto wetu elfu kumi na mbili. Ni hawa ambao wengi wataishia kuuza karanga mitaani na wengine kuwa vibaka. Tujiulize, kwanini, kama taifa, tunashindwa kuwa na mipango madhubuti kwenye elimu kiasi cha kuwafanya watoto hawa walio chini ya miaka 18 wapotee mitaani?

Nimepata kuandika, kuwa ni  mzazi anayeonyesha kutokujali yule anayetoa kisingizio cha kutowaandalia siku kuu njema ya krismas watoto wake kwa kuwatamkia; " Wanangu Krismasi hii imekuja ghafla, ndio sababu nimeshindwa kuwanunulia nguo na viatu vya siku kuu!"
       Hakika,  hicho ni kisingizio cha kijinga. Kila anayefikiri anajua kuwa kwenye kalenda ya mwaka Krismasi inaangukia tarehe 25 ya mwezi Desemba. Kamwe Krismasi haiwezi kuja ghafla!
        Kisingizio hiki kinafanana sana na taarifa za watoto wetu kufaulu lakini tumeshindwa kuwaandalia nafasi kuingia Kidato cha Kwanza. Na kwamba ifikapo Januari mwakani maelfu kwa maelfu ya watoto wetu waliofaulu darasa la saba na kupata nafasi ya kuendelea na kidato cha kwanza.
       Ndipo hapa siku zote tunazungumzia, kwamba tunafanya masihala na elimu yetu.  Hivi wahusika hawakufahamu idadi hii ya wanafunzi kuwa wangefaulu mitihani? Hivi hawakufahamu idadi ya wahitimu?
        Nilipata kuzungumzia udhaifu wetu wa kushindwa kutunza kumbukumbu na takwimu. Nilimtolea mfano mfanyabiashara na mkulima maarufu kule Iringa aliyepata kunialika  kutembelea shamba lake la mifugo.  Bwana yule, Salim Abri Asas   ana ng'ombe wa maziwa zaidi ya 600. Aliweza kuwapanga ng'ombe wake katika makundi kutokana na jinsi walivyozaliwa. Ng'ombe wale walikuwa na namba maalumu na kila ndama alipewa jina lake. Kwani Salim yule, kamwe hawezi kutamka" Ndama hawa wamezaliwa ghafla mno, sina pa kuwaweka!" Au; " Lita hizi za maziwa zimeongezeka ghafla, sina pa kuzihifadhi!"
        Ufugaji wa Bwana Salim Asas ni wa kisayansi zaidi, ameajiri wataalam wa mifugo, ametunza  takwimu ya idadi ya ng'ombe na ndama wake. Amewapa majina, anawajua ng'ombe wake kwa majina, akiwaita, wanageuka. Anafahamu idadi ya lita za maziwa yanayozalishwa kwa siku na kwa mwaka.  Na sisi kama nchi tumeajili watalamu wa elimu. Hivi hawa maofisa wa elimu waliotapakaa nchi nzima hadi katika kata wanafanya kazi gani?
         Siku zote, inasemwa kitaalam, kuwa bila takwimu hakuna mipango ya maana ya maendeleo. Utakachofanya itakuwa ni  kubahatisha tu. Niliwahi kuitolea mfano nchi ya Sweden, kwamba mipango mingi ya maendeleo katika nchi ya Sweden na nyingine  nyingi zilizoendelea inategemea takwimu.
          Tuchukue mfano katika sekta ya elimu . Halmashauri  ya mji katika Sweden sio tu inategemea takwimu katika kupanga bajeti ya mwaka, bali upangaji wa mipango yake ya maendeleo kwa miaka mitano au ishirini mbele hutegemea takwimu zilizopo. Halmashauri ya mji katika Sweden inajua idadi ya watoto wanaozaliwa kila siku na kwa mwaka. Inajua idadi ya watu wanaokufa kwa siku na kwa mwaka. Watendaji wanachambua takwimu na kuangalia mwelekeo wa kijamii.
          Kwa idadi tu ya watoto wanaozaliwa kwa mwaka wanaweza kujua idadi ya watoto watakaohitaji huduma ya chekechea miaka 3 hadi 5 ijayo. Watafahamu idadi ya watoto watakaoanza darasa la kwanza miaka sita ijayo. Watafahamu idadi itakayohitajika ya walimu wa chekechea, shule za msingi na hata sekondari kwa miaka 5 hadi 20 ijayo. Watafahamu wastani wa idadi ya nafasi za chuo kikuu zikazohitajika kwa wanafunzi watakaopenda  kuendelea na elimu hiyo katka miaka 20 hadi 30 ijayo.
         
               Kwenye ili la takwimu,  tuchukue mfano, Mkoa wa Mbeya  mwaka 2015 utawahimiza  wazazi wawaandikishe watoto wao darasa la kwanza. Katika hilo kila mhusika atapaswa kuelewa, kuwa kama idadi ya watoto watakaoanza darasa la kwanza mwaka 2015 kwa moa wa Mbeya ni laki moja. Basi, akili ya kawaida kabisa bila hata kuwa na utalaam wa takwimu inatwambia, kuwa  miaka 7 ijayo, yaani mwaka 2022, idadi ya watoto watakaomaliza darasa la saba mkoani Mbeya haitapungua 80,000 kati ya wale 100,000. Kati ya hao 80,000 watakaomaliza darasa la saba tuseme basi 50,000 watafaulu kuendelea na kidato cha kwanza. Hiyo itakuwa ni nusu ya wale laki moja walioanza darasa la kwanza mwaka 2015.
            Tujiulize, je, kama mkoa umewahimiza wazazi wawandikishe watoto wao 2015, je mkoa umeandaa pia nafasi 50,000 za kidato cha kwanza kwa mwaka 2022? Umeandaa vyumba vya madarasa na walimu wa kutosha? Mara nyingi huwa hatuna majibu ya maswali hayo. Badala yake hatua za zimamoto huchukuliwa kama vile tumeshtukizwa na hali hiyo. Naam, Krismasi haiji ghafla, jipange nayo. Heri ya Krismasi! ( Makala haya yamechapwa kwenye Raia Mwema juma hili)
0754 678 252, mjengwablog.com

--
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/d/optout.

Share this :

Previous
Next Post »
0 Comments