Ndugu zangu,
Siku ya Uhuru ni siku ya kutafakari. Siku ya Uhuru inahusu muda ama wakati. Kwamba tumefikisha miaka 53 ina maana ya wakati uliopita tangu tupate uhuru.
Na kwa mwanadamu, utajuaje kuwa cha hakika ulichonacho, iwe kwa masikini au tajiri, ni muda? Maana, mwanadamu waweza kukosa vyote, lakini, muda utabaki nao. Utaupoteza tu mara ile utakapokata roho.
Ona pale mtoto anapozaliwa, kwamba ghafla kiumbe kitakuwa kimezaliwa. Kiumbe che muda wote mbele yake, na pengine, ni kiumbe kitakachohitaji pia muda wako, kama mzazi. Lakini, wakati huo huo, kiumbe kinapozaliwa, kuna mwanadamu mwingine anakata roho. Na hakuna tena atakayeweza kugawana muda na aliyekufa.
Lakini, nchi inazaliwa, haifi. Tumezaliwa, tutakufa na kuicha nchi yetu tuliyozaliwa. Kuipenda nchi uliyozaliwa si jambo la kuchagua. Nchi ni Mama, mwanadamu huwezi kumchagua mama mwingine mbali ya aliyekuzaa.
Na kila siku ya mwanadamu imejazwa na matukio, watu na maeneo. Nimeangalia televisheni leo. Nimeshangaa kuwaona vijana wale wakifanya vurugu pale Dumila. Tena siku ya Uhuru wetu. Vijana wale wamezuia magari na kufanya uharibifu wa mali. Sababu ni ugomvi wa wakulima na wafugaji. Sikuwaona wakulima wala wafugaji katika vijana wale, bali, wengi ni vijana wasio na kazi na wametumia fursa ile kufanya vurugu. Kuna lazima ya kutafakari namna ya kuepuka maafa zaidi huko twendako.
Tumekuwa tukidhani tunaishi katika wakati uliopo, au tukitamani kufanya hivyo. Lakini, wakati uliopo unaweza ukatufunga mikono tusijue cha kufanya.
Maana, kuna media zinazochochea chuki ya wananchi kwa Serikali yao. Zinaripoti lakini hazifafanui wananchi wakaelewa na wakachangia fikra zao katika kukosoa kwenye kujenga, au kupongeza kwenye kustahili kupongeza. Tunaacha haya yakiendelea bila kukemea. Na utafika muda tutauma vidole, labda ni kesho tu. Muda utakuwa umeshapita. Mungu apishilie mbali.
Kwa mwanadamu, kupata picha ya kitakachotokea baadae ni jambo muhimu kwa maisha yake ya sasa. Na ndivyo hivyo hivyo, kwa ya zamani yaliyo kwenye miliki ya kumbukumbu. Jana, Sasa na Baadae ndio MSINGI wa kuendelea kwa mwanadamu. Kuendelea kwa Nchi.
Ni Neno La Leo.
Mungu Ibariki Tanzania.
Happy Independence Day!
Maggid Mjengwa,
Iringa.
Unapokea Email hizi kwa sababu umejiunga na Jukwaa la 'Mabadiliko'.
Kuchangia mada tuma kwenye Email hii: mabadilikotanzania@googlegroups.com
For more options, visit this group at:
http://groups.google.com/group/mabadilikotanzania?hl=en?hl=en
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Mabadiliko Forum" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to mabadilikotanzania+unsubscribe@googlegroups.com.
To post to this group, send email to mabadilikotanzania@googlegroups.com.
Visit this group at http://groups.google.com/group/mabadilikotanzania.
To view this discussion on the web visit https://groups.google.com/d/msgid/mabadilikotanzania/CAMD-ye5ypymRgAKEcG-cowdBTg2Qgmwfcq22hqmVE8cN7mOptQ%40mail.gmail.com.
For more options, visit https://groups.google.com/d/optout.
0 Comments