Na Chambi Chachage
Tunahitaji Viongozi Wenye U Tatu
Tunahitaji Viongozi Wenye U Tatu
Chambi Chachage
Ili kuudhibiti ufisadi tunahitaji viongozi wenye 'u' tatu. Utatu huu ni: utu, uadilifu na utaalamu. Cha tatu ni kirahisi kukipata hata ukubwani. Hivyo vingine ndivyo vigumu.
Kama zilivyo kuta za piramidi au ilivyo pembetatu yenye mistari mitatu, ndivyo zilivyo hizi u tatu katika mantiki hii. Zinasimama pamoja. Ukiondoa moja unaziangusha zingine.
Aliyekuwa diwani katika sehemu mmojawapo ya nchi yetu ni kielelezo. Kwa kipimo cha haraka haraka alikuwa na utu. Ubinaadamu wake ulishuhudiwa na wanakijiji mbalimbali niliokutana nao. Hata uadilifu wake haukuonekana kutiliwa shaka. Tatizo lilikuwa ni utaalaamu. Pamoja na jitihada zake za kupigania haki ya watu wake, alipata taabu alipokuwa akijaribu kusoma na kuchambua makabrasha mazito ya bajeti, yaliyoandikwa kwa lugha ngumu za kitakwimu na kihasibu. Lakini hakukata tamaa, alijitahidi hivyo hivyo kuyasoma na kuyatafsiri hasa katika sehemu alizohisi zimechakachuliwa ili kuwachanganya madiwani hasa wale ambao hawana utaalamu na elimu ya kutosha.
Baadaye alipata fursa ya kuwa Mbunge. Sijamsikia akichangia sana kwenye mijadala mikali, kama huu wa akaunti ya Escrow ya Tegeta, ambao unahusisha ripoti na taarifa zenye dhana ngumu sana ambazo zilimpelekea hata Waziri mmoja kujikanganya Bungeni na 'kupotezea' baada ya kuambiwa alichokuwa anakisema sicho kinachojadiliwa. Na pia tuliona Wabunge wengi tu wakichangia bila kuelewa masuala yaliyoibuliwa kitaalamu.
Hapa ni vyema nieleze wazi kuwa mimi sio muumini wa kuwanyima fursa za uongozi wananchi (wa kawaida) eti kwa kuwa tu hawana stashahada na shahada za elimu ya juu. Naamini kuwa viongozi hutokea/huibuka katika jamii na hutokana na watu. Na kama nilivyosema, katika hizo u tatu hiyo inayohusiana na utaalamu inaweza kupatikana hata kwa wale ambao hawakuipata utotoni na ujanani. "Elimu haina mwisho," wahenga wetu walinena. Na kama HakiElimu inavyotukumbusha, "Elimu Ni Uwezo Siyo Cheti".
Lakini kwa sasa ni muhimu sana kuwa na u hii ya utaalamu hata kama mtu tayari ana hizo u zingine. Bila u hiyo kiongozi atawezaje kupambana na ujanja na uchakachuaji wa wale wenye u hizi: unyama, ufisadi na utaalamu? Hakika utu na uadilifu tu havitoshi.
Jenerali Ulimwengu amejaribu kutueleza jinsi "kitoto kilichozaliwa katika familia ya mafisadi kinavyolelewa kifisadi, kinavyosomeshwa kifisadi, kinavyofanywa 'kifaulu' kifisadi, kinavyoajiriwa kifisadi, kinavyoozeshwa kifisadi na kinavyokuwa kitu kingine cha ufisadi katika mwendelezo wa utamaduni wa ufisadi kilimozaliwa." Kwa masikitiko anatuambia kuwa hadhani "kwamba tunaweza kuwa na matumaini ya kupata lo lote la maana kutoka kitoto hicho kwa maana ya kuiendeleza nchi na kuwaendeleza watu wake" maana watu "wa aina ya kitoto hicho hawawezi kuijenga wala kuiongoza nchi, kwa sababu wao hawajajengwa wala kuongozwa katika misingi ya kujenga lo lote la maana isipokuwa kuendeleza utamaduni uliowazaa na kuwalea."
Kwa maana nyingine, ukoo/uzao huo wa ufisadi hauna u zote tunazohitaji. Ila inapokuja kwa mwanadamu, mwana wa nyoka siyo lazima awe nyoka. Hii ni kwa kuwa mwanadamu ana utashi na hivyo anaweza kuutumia kuamua kuwa kile ambacho mwandishi wa kitabu cha Seven Habits of Highly Effective People - Tabia Saba za Watu Wanaofanikisha Sana Mambo - anakiita mtoto/mtu wa mpito/mabadiliko, yaani ambaye haendelezi kile kibaya alichokirithi kutoka kwa wazazi/walezi wake au/na jamii yake.
Pamoja na hayo inabidi tukubali kuwa kwa kiasi kikubwa u za uadilifu na utu hujengwa na kukuzwa wakati wa malezi yetu ya utotoni na ujanani. Japo inawezekana, ni vigumu sana mtu kupata tunu hizi adhimu ukubwani. Mathalan hutokea mtu asiye na utu akajikuta akiwa katika safari ya Dameski kama yule Sauli mtesi aliyeandikwa msahafuni na kuuona mwanga mkuu kisha kubadilika na kuwa Paulo mjoli au kuiona njia iliyo njema baada ya kuupanda mti kama Zakayo mchakachuaji na hivyo kuachana na dhuluma.
Samaki, kama wahenga wetu walivyotuasa, mkunje angali mbichi. Pa kujenga u hizi adimu ni utotoni na ujanani. Watu wakipita hapo, kuzijenga ukubwani ni majaliwa – ama kama waumini wa ile imani ipitayo uelewa wote wanavyosema, ni muujiza utokao juu. Msahafu mmojawapo wenyewe unasisitiza kuwa ukimuelekeza mtoto katika njia impasayo hataiacha hata ukubwani. Kwa maana nyingine, utu na uadilifu ni vitu vijikitavyo ndani ya moyo.
Vipi kuhusu suala la taasisi za uwajibikaji? Ni kweli ili kudhibiti ufisadi tunahitaji kujikita kitaasisi. Lakini taasisi sio majengo na maelekezo au mbinu na miundo ya kiuwajibikaji tu. Ni watu pia. Taasisi huundwa na watu na hata uwe na Kamera za Video za Kiuchunguzi (CCTV), Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (PCCB), Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) na kadhalika bado taasisi hizi huundwa na watu ambao hukabiliana na watu. Ni heri yetu pale watu katika taasisi hizo wanapokuwa na zile u zetu na ole wetu wasipokuwa nazo.
Siku moja niliwahi kwenda kwenye taasisi mojawapo ambayo inasifiwa sana kwa mabadiliko makubwa ya kitaasisi. Polisi walikuwepo mule. Kamera nazo zilikuwepo. Lakini bado mtu niliyemweleza shida yangu aliongea kwa ujasiri kabisa kuhusu njia mbili za kupata ninachohitaji – njia ndefu iliyohusisha kwenda mbali kwenye ofisi nyingine na njia fupi ambayo ingepitia kwake. Na hata nilipochagua njia ndefu na kwenda kwenye hiyo ofisi nyingine bado nilikutana na mlinzi mlangoni aliyeniambia kile kile – kuna njia ndefu na ya mkato. Hapo ina maana utafanya uamuzi kama mtu, yaani, kwa kuzingatia kama una u ya uadilifu au una u ya ufisadi ama kuamua kubadilisha u yako kutokana na mazingira.
Pia u ya utaalamu inaanza kujengwa kwa kiasi kikubwa utotoni na kuimarishwa ujanani. Na tukubali tu kuwa kwa kiasi kikubwa inatokana na elimu ya kufundishwa darasani na vyuoni. Na pale tunapokuwa tumeikosa muda huo basi inabidi tuipate ukubwani kupitia elimu ya watu wazima ambayo tumeidororesha sana baada ya muasisi wake mkuu nchini, Mwalimu Nyerere, kung'atuka na kututoka. Hali kadhalika tunaweza kuipata kazini, kupitia ziara za mafunzo ama hata kwa kujisomea na kujielimisha wenyewe tu.
Wakati anajaribu kulijibu swali la Je, tunaweza kuzitambua sifa za uongozi? Jenerali Ulimwengu anauelezea mchakato huu hivi: "Katika marika ya jando na unyago watoto wenye mwelekeo wa uongozi walitambuliwa kirahisi zaidi na walijitokeza kuwaongoza wenzao katika mitihani mingi waliyokabiliwa nayo. Katika unyago kwa kisasa, ambayo ni elimu ya shule, kiongozi wa aina hiyo hujitokeza na kuwa ama kiranja au kiongozi wa migomo pale wanafunzi wanapohisi kwamba hawatendewi haki. Ni hususan shuleni (pamoja na vyuoni) wanapochomoka viongozi wa baadaye. Katika shule za kimapokeo (za kizamani) walimu waliwateua watoto wakubwa wa mwili na wakali wa tabia kuwa viranja na monita. Katika shule za kisasa wanafunzi wenyewe huchagua viranja wao na kuwaheshimu badala ya kuwaogopa kama ilivyo kwa shule za kizamani. Inapotokea kwamba wanafunzi wanahisi kwamba wanaonewa kwa njia yoyote ile, viongozi wa wanafunzi hujitokeza na kuongoza ama majadiliano baina ya wanafunzi na utawala wa shule, ama mgomo wa wanafunzi pale majadiliano yanapokuwa hayana tija. Viongozi wa migomo shuleni mara nyingi hukua na kuingia katika harakati za kisiasa ama za vyama vya wafanyakazi; aghalabu huwa ni watu wa kudai na kutetea maslahi ya wenzao."
Ulimwengu anaendelea kutujuza hivi: "Kama vile ambavyo viongozi wa wanafunzi wakati wa migomo na misuguano baina ya wanafunzi na walimu hujikuta mara kwa mara wanapewa adhabu, pia viongozi wa kisiasa nao hujikuta wakikamatwa, wakipigwa au hata kuuawa. Kama ilivyo mtaani na shuleni wakati wa utoto, pia katika umri mkubwa (ofisini, kiwandani, majeshini, katika biashara) kiongozi ni mtu anayesema wazi kile anachokiamini na kukitetea bila kutafuna maneno. Kiongozi ni mtu wa kujitolea nafsi yake, wala si mtu wa kutumia nafasi ya uongozi kupata faida binafsi juu ya wengine. Anaposafiri nchini na kuona hali duni ya maisha ya watu wake, kiongozi anasononeka na anazidi kukuna kichwa akitafuta namna ya kuwaokoa watu wake watokane na umasikini huo. Akikuta eneo ambako wananchi wake wana neema anafurahi kuwaona walivyonawiri, mashamba yao yalivyostawi, mifugo yao ilivyonona; hatafuti njia za kuwanyang'anya kwa ujanja mashamba yao au mifugo yao. Ukwasi wa raia ndiyo furaha ya kiongozi, si ukwasi wake binafsi." Naam, huo ndio utu na uadilifu katika uongozi.
Ndugu Msomaji labda unajiuliza, tunawezaje kuzipima hizo u tatu kiyakinifu/kisayansi na hivyo kuchagua/kuteua viongozi walionazo? Jibu ni rahisi: Kuweka mfumo wa wananchi, kwa kupitia wawakilishi wao au mabaraza ya uwakilishi – kama vile Mkutano Mkuu wa Kijiji na Bunge la Nchi – kupitisha kila aliyeteuliwa na mamlaka ya uteuzi. Hili linapaswa kusimikwa katika Katiba. Huku ndiko kujenga taasisi/utaasisi unaozingatia watu/wananchi. Wanakijiji wanawajua wenye u za utu na uadilifu kijijini kwao. Wapiga kura wanawajua wenye hizo u majimboni mwao. U ya utaalamu inapimika kwa wasifu wa kitaalamu na kwa shuhuda za jinsi mtu anavyoutumia utaalamu wake kwa ajili yetu.
Tuliwahi kuambiwa na Mwalimu kuwa maadui wakuu watatu wa maendeleo yetu ni: ujinga, umaskini na maradhi. Baadaye akatuambia kuna wa nne: rushwa. Pia akatueleza kuwa ili tuendelee tunahitaji vitu vinne: watu, ardhi, siasa safi na uongozi bora.
Ni kweli kabisa. Lakini ili hao watu tuwe na siasa safi na uongozi bora katika ardhi yetu tunahitaji viongozi wenye u hizi tatu: utu, uadilifu na utaalamu. Tukiongeza u ya nne basi iwe hii: ujasiri.
+260 962 161607
Unapokea Email hizi kwa sababu umejiunga na Jukwaa la 'Mabadiliko'.
Kuchangia mada tuma kwenye Email hii: mabadilikotanzania@googlegroups.com
For more options, visit this group at:
http://groups.google.com/group/mabadilikotanzania?hl=en?hl=en
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Mabadiliko Forum" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to mabadilikotanzania+unsubscribe@googlegroups.com.
To post to this group, send email to mabadilikotanzania@googlegroups.com.
Visit this group at http://groups.google.com/group/mabadilikotanzania.
To view this discussion on the web visit https://groups.google.com/d/msgid/mabadilikotanzania/CA%2BTTPHpcB5dZ8wMHavChBT9bY94wZp5yvBUdqiBsmYjeffcBnQ%40mail.gmail.com.
For more options, visit https://groups.google.com/d/optout.
0 Comments