MATIBABU YA WAKUBWA YAKIISHA, TUULIZIE AFYA ZA HOHEHAHE! - 1
Na. Julius Mtatiro -(Gazeti la Mwananchi, Jumapili - 16 Nov 2014)
Wiki moja iliyopita Serikali yetu kupitia ikulu iliujulisha umma kuwa mhe. Rais anakwenda nje ya nchi kukagua afya yake. Baada ya siku chache Ikulu ikatoa taarifa na picha za mhe. Rais wet akiwa katika maandalizi na baada ya kufanyiwa oparesheni huko nchini Marekani na ugonjwa unaomsumbua ukitajwa kama tezi dume au kwa kimombo "prostate gland" na mwisho tulijulishwa amendolewa wodini na kurejeshwa hotelini ambako anaendelea na matibabu. Darubini yetu inapenda kutoa pole kwa mhe. Rais, mkewe mama Salma Kikwete na wanafamilia wote katika kipindi hiki ambacho mhe. Rais anaendelea na matibabu. Watanzania pia wanaguswa na hali yake ya sasa, tunampa pole na kwa hakika tunamuombea akamilishe matibabu na kurejea nyumbani salama kukamilisha majukumu yake kabla ya kukabidhi kijiti kwa mtanzania mwingine ifikapo mwakani.
Kutibiwa kwa mhe. Rais nje ya nchi na ama marais wengine wengi siyo jambo la ajabu na geni, tumekwishajionea mara nyingi viongozi wa ngazi za chini na hata raia mbalimbali wakipata bahati ya kutibiwa nje ya nchi aidha kwa fedha zao binafsi ama kwa kulipiwa na mashirika mbalimbali na hata serikali za nchi zao. Lakini, kutibiwa kwa mhe. Rais wetu mpendwa mara hii kumezua gumzo huku na kule na wiki hii wabunge woji bungeni wakioanisha na hali duni ya huduma za afya nchini. Kuna walikuja juu na kusema masuala ya ugonjwa ni ya kuombea tu na si kulaumu, lakini kuna ambao walisisitiza kuwa pamoja na kumuombea mgonjwa afya njema tuna wajibu wa kuhoji na kutafakari kama tuko mahali salama. Mimi niko kwenye hili kundi la pili "namuombea mhe. Rais lakini nahoji pia dhana nzima ya wakubwa kutibiwa nje ya nchi huku masikini hohehahe wakiwa hawana hata panadol kwenye zahanati".
Msema kweli mpenzi wa mungu, sekta ya afya nchini Tanzania iko taabani, imekufa na inasikitisha, kuchefusha, hukuzunisha na kuumiza kichwa. Ukitaka kujua hakuna matibabu nchi hii nenda mahospitalini ujionee vituko, hali ni mbaya sana. Hospitali zetu hazina vifaa vya kawaida na muhimu, hazina madawa, hazina majengo ya maana, hazina mazingira rafiki, hazina vitanda vya kutosha hata robo ya wagonjwa, hazina samani kwa ajili ya madaktari na wauguzi, hazina wauguzi na madaktari wa kutosha na zilizo nyingi hata "gloves" hakuna! Hiyo ndiyo hali halisi kwa miji mikubwa na Vijijini. Tofauti iliyopo ni kuwa, vijijini wagonjwa hufa kwa kukosa matibabu madogo hata kama wana pesa na mijini hali ikiwa kwamba mgonjwa kama ana fedha anaweza kuishi siku mbili tatu walau akavuta pumzi, lakini kote vijijini na mijini changamoto ni kubwa.
Wakati fedha nyingi za serikali kwa mabilioni zinatapanywa na kuliwa na wajanja, mamlaka za ukusanyaji kodi zimelala, maliasili za nchi zinavunwa na kuliwa na wachache na kila aina ya uzembe na kutowajibika, fedha za kuendesha hospitali zetu hazipo na juhudi zinazochukuliwa kuimarisha sekta ya afya nchini bado zinatambaa kama mtoto mchanga. Mpango wa kutibu magonjwa makubwa hapa nchini unaonekana kusuasua, mtu akiguswa ubongo tu matibabu ni nje na ikiwa madaktari wetu watajaribu hapa wakikutana na hali tete tu wanampa huduma za awali na kumpa rufaa kwenda nje, wengi wa wanaopewa rufaa huishia kufariki dunia kwa sababu serikali haina uwezo wa kutibu kila mwananchi aliyepewa rufaa kwenda nje ya nchi. Ninao marafiki zangu kadhaa ambao wamewahi kupata rufaa hizo lakini serikali ilishindwa kabisa kuwasaidia kupata matibabu nje ya nchi na ikabidi marafiki na ndugu tubanane.
Matibabu salama na ya uhakika yaliyoko nje ya nchi yamebakia kuwa rahisi kwa viongozi wa serikali, watu walio karibu yao, wabunge na mwananchi yeyote wa kawaida ambaye ataunganishwa vizuri na wajanja. Kama hauko kwenye makundi hayo hauwezi kupata matibabu nje ya nchi na ukweli ni halisi kwamba hakuna serikali duniani ambayo inaweza kugharamia matibabu ya raia wake wote watakaotaka kwenda kutibiwa nje ya nchi, ingawa kwa nchi za wenzetu vigezo vya kwenda kutibiwa nje kwa magonjwa yasiyowezekana ndani ya nchi zao viko wazi na hakuna rushwa kwa hiyo kila ambaye kesi yake ni "complicated" anaweza kupata fursa hiyo. Kutokana na hali halisi iliyopo, serikali yetu haina ujanja zaidi ya kuimarisha miundombinu yote ya sekta ya afya. Ni aibu baada ya miaka hamsini ya uhuru kila magonjwa yanayotibika kitaalamu yanawashinda madaktari wetu bingwa na tunakimbilia nje, mengine madaktari wetu wanaweza kuyatibu lakini hatuna vifaa vya kuwasaidia, mengine hayana madaktari wazalendo kwa sababu tulishindwa kuwalipa wakakimbilia nchi za kigeni na mengine hatuwezi kuyatibu kwa sababu hatujawekeza katika taaluma za vijana wazalendo wanaoweza kuja kuwa madaktari wa kawaida na madaktari bingwa.
Shirika la Afya Duniani (WHO) linaeleza kuwa kila nchi inapaswa kuwa na daktari mmoja kwa wananchi 600. Afrika Kusini (South Africa) ambao tuliwasaidia kupata uhuru wamefikia uwiano wa daktari mmoja kwa watu 1,200. Kwa mfano, Dar es salaam, ambayo ina raia milioni 4.5, inatakiwa kuwa na madaktari 3,750; na kwa nchi yote ya Tanzania (raia milioni 45) tutatakiwa kuwa na madaktari 37,500. Jambo baya zaidi ni kuwa idadi ya madaktari nchi nzima ya Tanzania hawafiki 2000 (Takwimu za mwaka 2012), ambayo ni sawa na daktari mmoja kuhudumia raia 22,550 kiasi ambacho ni mara 11 ya kiwango cha kimataifa cha matibabu salama na ya uhakika kwa wananchi. Wakati hapa Tanzania hali ni mbaya kiasi hicho, hapo nchini Kenya wamefikia kiwango cha daktari mmoja kutibu wagonjwa 7500 na hivi sasa mikakati yao ni walau kila mkenya atibiwe na daktari bingwa ili kuwa na matibabu ya uhakika, hapa nyumbani ni raia wachache mno wanaopata fursa za kutibiwa na madaktari bingwa.
Unapoona wakubwa wa nchi zetu wanakwenda kupewa matibabu nje ya nchi sababu iko wazi sana, kwamba hapa ndani ya nchi hakuna madaktari wanaoweza kutibu magonjwa hayo, (matibabu hakuna), hayaridhishi, yakifanyikia hapa yanaweza kuhatarisha afya zao, hakuna madaktari wa kutibu magonjwa hayo, hakuna vifaa vya kutibia magonjwa hayo japo madaktari wapo na hata sababu ya kwamba yote hayo yapo lakini matibabu ya ndani ya nchi hayaaminiki kulingana na hadhi ya mgonjwa. Hii sababu ya mwisho ni ya ajabu sana(najua haimuhusu mhe. Rais). Lakini ukweli unabakia kuwa nchi yetu imedumaa mno kimatibabu na hatujachukua hatua thabiti za kupambana na hali hiyo na mwisho wa siku kila tukiugua ugonjwa unaoonekana unatutisha lazima huduma zetu tutazipata ulaya, Marekani, India, Afrika ya Kusini na kwingineko.
Hali hii inazidi kukomaa na imefikia mahali pabaya. Na siyo kwamba fedha hazipo, zipo tele. Kusomesha daktari mmoja kunagharimu pesa za kitanzania zisizopungua shilingi milioni 60. Hii ina maana kuwa, ili Tanzania iongeze madaktari 3333 ambao ukijumlisha na waliopo tutafikisha idadi ya madaktari 5333 ambao watafanya uwiano wa daktari mmoja kutibu wagonjwa 8438, tutahitaji jumla ya shilingi bilioni 200 tu ili kusomesha madaktari hao 3333. Bilioni 200 zilizochotwa na wajanja wachache, na wezi wachache, na familia zisizozidi tano katika akaunti ya ESCROW zingalitosha kutusomeshea madaktari wapya 3333 na wakaokoa maisha ya mamilioni ya watanzania. Mnasema hatuwezi kuboresha sekta ya afya ili kila mmoja wetu atibiwe hapa ndani ya nchi? Hebu tusaidiane kuzuia wizi mbalimbali wa fedha za umma ambao umekuwa ukitokea. Familia tano au sita za wajanja zimekwamisha kupata madaktari elfu tatu walio bora, watanzania wanakufa kwa kukosa kumuona daktari, ina maana familia tano au sita zilizochota mabilioni ya ESCROW zina thamani kubwa kuliko mamilioni ya wananchi masikini walioko kila pembe ya Tanzania wakilima na kuuza mazao na kulipa kodi, familia chache za wezi na waliochukua mgao huo zina thamani kuliko maelfu ya wafanyakazi ambao wanakatwa kodi kubwa katika mishahara yao na familia hizo zina hadhi kuliko walimu wetu ambao wanalazimishwa kuchangia shilingi elfu kumi kujenga maabara.
Wiki ijayo tutamalizia sehemu ya pili ya makala haya.
(Julius Mtatiro amewahi kuwa kiongozi wa juu wa Wanafunzi wa Vyuo Vikuu Tanzania "DARUSO & TAHLISO, 2006 – 2008", pia amekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi CUF Tanzania Bara (2011 – 2014). Ana shahada ya Elimu ya Sanaa (B.A) na Shahada ya Uzamili ya Utawala na Uongozi (M.A). Hivi sasa ni mwanafunzi wa mwaka wa mwisho katika fani ya sheria (L LB) - 0787536759.).
0 Comments