[wanabidii] TUSHIRIKIANE ILI KUPATA KATIBA HALALI

Thursday, October 09, 2014
Bunge Maalum la Katiba chini ya Mwenyekiti wake Samwel Sita limehitimisha kazi yake ya kuandaa katiba itakayopelekwa kwa wananchi kwaajili ya kupigiwa kura. Zoezi hilo lili lilihitimishwa kwa kupigiwa kura na wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba kwa namna ambayo haijawahi kushuhudiwa hapa nchini wala Taifa jingine lolote hapa Duniani. Baada ya kuwa na mashaka makubwa ya kutopatikana kwa theluthi mbili kutoka upande wa Zanzibar, Mwenyekiti alibuni njia mpya ya upatikanaji akidi ya theluthi mbili kutoka pande zote mbili za Mwungano. Hatimaye wajumbe walitangaziwa kuwa akidi amepatikana, jambo ambalo liliwafanya wajumbe wa Bunge la katiba waliokuwepo ukumbuni kuonesha furaha yao ambayo huenda ilikuwa ni vigumu sana kuielezea kwa maneno. Walio wengi waliionesha kwa kucheza na kushangilia.

Lakini kwenye huu mchakato uliotengeneza hii katiba inayopendekezwa, kuna mambo ya msingi ya kujiuliza:
  1. Uhalali wa Katiba unatokana na nini?
  2. Je, katiba inayopendekezwa ni halali?
  3. Wajumbe wa Bunge la Katiba na viongozi wao, wanaelewa utofauti wa katiba na ushindani wakati wa uchaguzi?
  4. Ni nani mwenye haki ya kufurahia kupatikana kwa katiba nzuri inayopendekezwa, ni waandaaji au wananchi?
  5. Tunajua kwa nini mataifa mbalimbali huweka hitaji la theluthi mbili katika kupitisha katiba lakini huweka asilimia hamsini au ushindi wa uwingi tu wa kura bila ya kujali ni asilimia ngapi kwenye uchaguzi?

UHALALI WA KATIBA HUTOKANA NA NINI?

Nilimsikia mara kadhaa Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba akisema kuwa atawashangaa Watanzania kama hawataikubali katiba hiyo kutokana na mambo mazuri yaliyomo ndani yake. Na jana pia nilikatishwa tamaa zaidi na Mheshimiwa Rais ambaye alitumia muda mwingi sana kuelezea mambo mazuri yaliyopo ndani ya katiba inayopendekezwa.

Kuna kitu cha msingi sana katika demokrasia mnapofanya uamuzi. Katika mfumo wa kidemokrasi unaheshimu mamlaka ya umma, hakuna kitu muhimu kama kitu kilichoamuliwa kuwa  'halali'. Na uhalali hautokani na ubora au uzuri bali hutokana na uhalali wa mchakato wa ushirikishwaji. Kama lengo letu lingekuwa kupata tu katiba iliyo nzuri bila ya kuzingatia 'uhalali' sidhani kama kungekuwa na haja ya kuunda Tume ya Kukusanya maoni wala kusingekuwa na haja ya kuwa na Bunge Maalum la Katiba au hata upigiaji kura katiba inayopendekezwa. Tungepata katiba iliyo nzuri zaidi kama tungewatafuta wanasheria wazuri kabisa ndani na nje ya nchi, wakajifungia mahali, wakachambua katiba mbalimbali Duniani, wakafanya utafiti wao binafsi, na baadaye wakatuletea Watanzania na kutueleza kuwa hii ndiyo katiba mpya. Na huenda katiba hiyo ingekuwa bora kuliko katiba ya nchi yoyote ile Duniani lakini nina uhakika isingekuwa katiba halali.

Nina hakika watanzania walichokuwa wanataka siyo katiba nzuri tu bali muhimu zaidi walitaka iwe 'halali'. Na ikumbukwe pia uhalali wa kitu hautokani na sheria pekee yake. Kuna nchi ziliwahi kutawaliwa na viongozi madikteta na wauaji lakini katika nchi hizo hata walipokuwa wanawaua watu wao ovyo walikuwa wakitumia sheria. Hata makaburu kule Afrika Kusini wakati wa utawala wa kibaguzi walikuwa wakiwakamata Waafrika na kuwafungulia mashtaka ya kukiuka sheria za kibaguzi. Kwa hiyo walikuwa wakitumia sheria. Hata Yesu alihukumiwa kuuawa kwa kutumia sheria. Hapa tunachotakiwa kujiuliza, mtu anaposema kuwa mchakato wa upatikanaji wa katiba inayopendekezwa ni halali kwa sababu umefuata sheria, Je, sheria yenyewe halali? Tutambue kuwa uhalali ni zaidi ya sheria maana hata sheria yenyewe inaweza kuwa sheria halali au sheria ya kibaguzi au sheria gandamizi. Sisi sheria yetu ya mabadiliko ya katiba ilikuwa halali? Kwangu mimi sheria ile haikuwa halali maana haikulenga kuufanya mchakato wa upatikanaji wa katiba usihodhiwe na makundi fulani, na hasa Bunge la Jamhuri ya Mwungano, na wanasiasa na vyama vya siasa.

KATIBA INAYOPENDEKEZWA NI HALALI?

Katiba inayopendekezwa na Bunge Maalum la katiba inaweza kuwa ni nzuri lakini siyo halali. Wanaoipigie debe ikiwa ni pamoja na Mheshimiwa Rais, wameelezea vizuri sana uzuri wa katiba hiyo lakini hawajaelezea ni kwa namna gani katiba hiyo ni halali. Katiba inayopendekezwa siyo halali kwa sababu mchakato wake, kuanzia sheria iliyotumika kuitengeneza haikuwa halali.

Katiba ya wananchi ni lazima itengenezwe na wananchi wenyewe na wala kusiwe na kundi la kuhodhi mchakato wake. Katika mchakato wa utengenezaji wa katiba ilistahili kuondoa dalili zozote zile za kuonesha kundi fulani ndilo lenye mamlaka ya kuandika katiba kwaajili ya watu wengine. Tangu awali ilitakiwa kuyatambua makundi ambayo yatabanwa zaidi na katiba mpya. Kundi mojawapo kubwa ilikuwa ni wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Mwungano. Katiba mpya tulitaka idhibiti ununuaji wa madaraka na uwakilishi kwa njia ya rushwa wakati wa uchaguzi. Malalamiko mengi ya rushwa yamekuwa wakati wa uchaguzi yakihusisha wagombea wa nafasi za ubunge na mawakala wao. Kundi la wabunge ambamo ndani yake kuna wengi wanajitambua kuwa nafasi zao wamekuwa wakizipata kwa njia ya rushwa hawawezi kuwa ni watu sahihi wa kutunga katiba itakayodhibiti rushwa wakati wa uchaguzi.

Wananchi wengi wamekuwa wakilalamikia upeo na uwezo mdogo wa baadhi ya wabunge kutokana na elimu zao kuwa ndogo kupindukia. Itawezekana vipi wabunge ambao ni darasa la pili, la nne au la saba wapitishe katiba inayotamka kuwa hitaji la chini la elimu ya mtu anayetaka kuwa mbunge ni kidato cha nne? Hivyo wabunge wa Bunge la Mwungano walistahili kuwakilishwa kwenye Bunge Maalum la katiba kama taasisi nyingine lakini siyo kila mbunge kuwa mjumbe na hivyo kuwa na maamuzi ya mwisho juu ya Katiba inayopendekezwa. Kama Bunge la Jamhuri ya Mwungano wa Tanzania wangewakilishwa na wajumbe wachache kama taasisi nyingine, kungekuwa na uwakilishi mpana zaidi wa wananchi kuliko kulifanya Bunge la Jamhuri ya Mwungano kuhodhi mchakato wa katiba.

Jambo la pili la kujiuliza ni kuwa kulikuwa na ulazima gani Rais kuteua wajumbe waliopendekezwa badala ya taasisi na makundi mbalimbali kuwateua moja kwa moja?

DHAMIRA CHAFU HAIZAI KITU HALALI

Uhalali wa kitu kwanza hutokana na dhamira safi na wala hautokani na uzuri wa kitu. Ningependa kuwalizeni - Mathalani nyumbani kwako ulikuwa na upungufu wa visu na ulikuwa unahitaji sana kisu kizuri chanye makali lakini bahati mbaya huna uwezo wa kukipata. Siku moja jambazi mmoja akaenda kutafuta kisu chenye makali sana huku akiwa na dhamira kuwa akija nyumbani kwako akutoe uhai, na baada ya hapo atoweke na mali zako. Lakini usiku aliokuja akiwa anafikiria kuwa wewe upo pekee yako, akakukuta upo na majirani waliokuja kukufariji kutokana na msiba wa ndugu yako uliotokea kijijini kwenu. Jambazi alipoingia akawakuta watu wengi ambao hataweza kukabiliana nao, hivyo naye akajifanya ni mmoja wa waombolezaji. Baadaye yule jambazi akagundua wapishi hawana visu vizuri vya kukatia nyama, naye akatoa kisu chake ambacho alikichukua kwaajili ya kuja kufanyia ujambazi. Wote mkafurahi maana tatizo la kisu limekwisha. Kisu cha jambazi kinaonekana ni kizuri, kimetatua tatizo lakini kisu hiki ni haramu kutoka na dhamira mbaya ya aliyekuwa amekileta. JAMBO BAYA LIKIFANYIKA KWA NIA NJEMA MUNGU HULITAKATIFUZA LAKINI JAMBO JEMA LIKIFANYIKA KWA NIA MBAYA MUNGU HULINAJISISHA.

Wale waliofuatilia vizuri hotuba ya Mheshimiwa Rais Kikwete watakuwa walimsikia Rais akisema kuwa alipotaka kuanzisha mchakato wa uandaji wa katiba mpya, CCM haikutaka lakini akachukua maamuzi yake. Nadhani kwaajili ya kumheshimu Rais, CCM waliamua kumkubalia lakini miyoyo yao haikuridhia. Kuna mengi yaliyotokea, na kwa kiasi kikubwa ndiyo yaliyochelewesha upatikanaji wa katiba mpya, ukijiuliza huelewi kwa nini mchakato umeenda kwa namna ulivyoenda. Jambo lililodhahiri ni kuwa CCM japo walishindwa kumkatalia Mheshimiwa Rais lakini waliamua kuchukua njia nyingine kuhakikisha katiba mpya haipatikani, na hilo lingewezekana kwa kuhodhi mchakato wa upatikanaji wa Katiba. Mahali pekee ambapo waliona wanaweza kuhodhi bila shida ni kuhakikisha Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Mwungano ndiyo wanaokuwa na maamuzi makubwa kuhusu katiba mpya, wakitambua kuwa ndani ya Bunge la Jamhuri ya Mwungano, wabunge wa CCM ni zaidi ya 75%. Wabunge hawa wa CCM nia yao kubwa haikuonekana kutengeneza katiba mpya bali ilikuwa kuzuia kupatikana kwa katiba mpya. Dhamira hiyo inaonekana wazi kwenye Katiba mpya inayopendekezwa.

Mambo ambayo wananchi wengi waliyaona ni muhimu kwenye katiba mpya ni pamoja na:
  • Kupunguza madaraka ya Rais katika uteuzi. Kwenye hili wananchi wengi wanaona kuwa uteuzi wa Rais kwa nafasi fulani, japo ni nafasi muhimu sana kwa maisha yao ya kila siku lakini wanaoteuliwa wanapewa kama zawadi maana baadhi yao hawaonekani kuwa na uwezo wa kuzimudu kazi zao. Lakini pia kudhibiti uteuzi wa Rais kungesaidia wateule hawa kufanya kazi kwa kujiamini zaidi kuliko pengine kufanya kazi kwa lengo la kumfurahisha aliyewateua. Pia kuna ukweli kuwa ikitokea bahati mbaya mkampata Rais dikteta ni vigumu sana kuweza kumdhibiti Rais ikiwa wasimamizi wa ofisi zote kubwa za umma ni wateule wake
  • Wananchi walitaka kuona katiba ambayo ina miongozi mikali kwenye mambo ya kudhibiti rushwa maana wananchi wengi wanaamini hili ni tatizo kubwa kwa nchi yetu kwa sasa, na linahitaji kudhibitiwa kwa nguvu zote
  • Wananchi walitaka kuona nchi inakuwa na dira. Dira hiyo ielezwe na tunu zetu kama Taifa. Sababu kubwa ya kuwekwa tunu hizo ni kwa vile watu wengi wanaamini kuwa pamoja na katiba yetu inazungumzia usawa wa binadamu lakini kiuhalisia inaonekana kuna Watanzania wengine na hasa viongozi na matajiri, wao ni binadamu zaidi kuliko wengine. Kutambua tunu za Taifa kungesaidia kuundwa kwa sheria kali kwa watakaokiuka au kutenda kinyume na yale ambayo Taifa limeyaweka kama mambo makuu ambayo Taifa linaamini.
Wajumbe waliobakia Bungeni wameyaondoa mambo hayo ambayo yalichangiwa na wananchi walio wengi na badala yake kumekuwa na majigambo sana kuwa katiba inayopendekezwa imetambua haki za makundi mbalimbali kama vile wafugaji, wakulima, walemavu, wasanii, n.k. Kwangu mimi haya yanayotajwa ni sawa na mtu ambaye ana paka wake ambaye ana njaa, na paka huyu wakati Bwana wake anakula naye anataka apande juu ya meza ili apate kushiba. Bwana wake anachukua mfupa anaurusha nje, paka anaufuata mfupi nje, na kisha Bwana wake anafunga mlango. Paka alirushiwa mfupa nje alidhani kilio chake cha njaa kimesikika kwa Bwana wake kumbe Bwana wake alikuwa na nia ya kumwondoa ndani ya nyumba asimsumbue tena. Paka atalamba mfupi na kisha kuendelea na njaa yake.

Ukiwa na katiba inayotambua na kuzingatia haki na usawa wa watu wote na mahitaji yao yanayoendana na hali zao, tayari mlemavu naye atakuwemo, mkulima yumo, mfanyabiashara yumo, mvuvi, mfugaji, na wengine wote. Tunatajiwa haki za makundi lakini hatuambiwi ni wapi ndani ya katiba kiu yetu ya kuona wanaoteuliwa wanapata nafasi hizo kwa uwezo wao na siyo sababu nyingine. Maana hawa wateule katika baadhi ya maeneo wamekuwa ni kikwazo kwa maendeleo ya wananchi au kutokana na maadili yao au uwezo wao mdogo. Ndani ya katiba hatuambiwi ni wapi tumedhibiti kikatiba kuhakikisha watu hawapati madaraka kwa kutumia pesa au vyeo vya wazazi na ndugu zao. Ndani ya katiba hatuambiwi ni wapi tumedhibiti uwezekano wa mikataba mibovu, n.k.

MTU SAFI UKIGUNDUA MWENZIO AMEFANYA KOSA AU HILA KWA MAKUSUDI NA WEWE UKAUNGANA NAYE, WEWE NI MHALIFU ZAIDI. MTU MWADILIFU ANATAKIWA KUSIMAMA KIDETE NA KUSEMA KUWA ULICHOFANYA SIYO SAHIHI. TUNAPOFANYA HIVYO KWA DHAMIRA SAFI NA SIYO KWA MASLAHI YAKO AU KIKUNDI FIULANI, KAULI HIYO ITAKUWA NI TAKATIFU.

Napenda kuwaambia watanzania wenzangu kuwa ni aheri katiba isipatikane kuliko kukubali watu wengine kutumia sheria zisizo halali kuhalalisha katiba isiyo halali.

WABUNGE WA CCM WANAELEWA UTOFAUTI WA KUPATA KATIBA YA WOTE NA USHINDANI WA UCHAGUZI?

Ukifuatilia toka mwanzo wakati wa utengenezaji wa sheria ya kusimamia mchakato wa kupata katiba mpya, ni dhahiri kuwa mchakato uligeuzwa kuwa ni ushindani kati ya CCM na CHADEMA, na baadaye kati ya CCM na UKAWA. Hili lilikuwa ni kosa kubwa sana. Ni ukweli huo ndiyo uliowafanya wabunge wa CCM kushangilia sana baada ya kuelezwa kuwa kura zilizopigwa kwa fax, email na sms zimefanya akidi ya theluthi mbili kufikiwa. Furaha ile ilikuwa ni kushangilia kuwa CCM imewashinda UKAWA kama vile kulikuwa na kiti kinachogombaniwa kati ya CCM na UKAWA.

Ni fikra hizo ndizo zilizomfanya Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba hata kubuni upigaji kura ambao haujawahi kutokea nchi yoyote katika sayari hii. Yote hiyo ilifanyika ili CCM ipate ushindi dhidi ya UKAWA. Wajumbe hawa na Mwenyekiti wao hawakujua kuwa ilistahili Watanzania wote tufurahie kuwa tumepata katiba mpya ambayo ina 'ownership' ya watanzania wote kama mchakato wake ungekuwa umelenga kuwashirikisha wananchi wote na siyo wanasiasa kuhodhi mchakato mzima. Leo tuna katiba inayopendekezwa na CCM ambayo ownership yake ipo kwa CCM. Hawa ndiyo watakaohitajika kuwashawishi wananchi waikubali na huku UKAWA na sisi wengine tunaoamini kuwa haitakuwa katiba halali tukiwashawishi wananchi waikatae kwa kuwa katiba iliyotengenezwa imehusisha kundi dogo ambalo lina msimamo unaofana kisera. KWENYE JAMBO HILI NI LAZIMA WATANZANIA TUSIMAME NA TUTAMKE KUWA TUNATAKA KATIBA YETU AMBAYO SISI WENYEWE TUTAIPIGIE DEBE, TUTAIFANYIA KAMPENI KWA WATANZANIA WENZETU. HATUTAKI UUNDWAJI WA KATIBA MPYA UBADILIKE NA KUWA NI MASHINDANO KATI YA CCM NA UKAWA.

KWA NINI MATAIFA MBALIMBALI HUWEKA HITAJI LA THELUTHI MBILI KWENYE KATIBA?

Katiba husimamia masuala yote kwa ujumla ya kila mwananchi na ndiyo msingi wa sheria zote za nchi. Msingi huu ni lazima uwe imara, mzuri lakini muhimu zaidi uwe halali. Katika nchi ambazo watu hutanguliza dhamira njema, viongozi wanaosimamia upatikanaji wa katiba huwa hawataki washinde bali huwa wanataka kujiridhisha kuwa angalao watu walio wengi kabisa kama si wote, wanaafiki katiba walioitengeneza ili wailinde, waitetee na wajivunie. Na ili hayo yafanyike ni lazima kuwe na 'ownership'. Hii katiba inayopendekezwa ikipitishwa ni lazima kutakuwa na kundi kubwa (significant number) ambalo haliwezi kujivunia na huenda wasiilinde katiba ambayo imetengenezwa na wajumbe wa CCM na kisha kupelekwa kwa wananchi. Katiba hailindwi na Polisi, Usalama wa Taifa, mahakama au Jeshi bali hulindwa na wananchi wenyewe. Katiba mbovu na isyopendwa itazaa sheria mbovu na zisizopendwa. WATANZANIA TUSIKUBALI KUWA SEHEMU YA KUWEZESHA UTENGENEZAJI WA SHERIA MBOVU KWA KUPITISHA MSINGI AMBAO HATUAMINI KUWA MCHAKATO WAKO UMEBEBA UHALALI WA DHAMIRA SAFI.

NINI CHA KUFANYA

KWA MTU MWADILIFU KABISA KABISA, KUUNGA MKONO KITU UNACHOJUA WAZI SIYO SAHIHI NI UHAINI DHIDI YA NAFSI YAKO MWENYEWE. Kama wananchi tunaamini kwa dhati ya mioyo yetu kwa kadiri ya utashi wetu, kuwa katiba hii haikukidhi vigezo vya uhalali wa kimaadili na uhalisia (siyo kisheria), tutakuwa tumelisaidia sana Taifa letu la leo na vizazi vyetu vingi vijavyo kwa KUIKATAA. Na tufanyapo hivyo, isiwe kwa nia ya kushindana, isiwe kwa nia ya kuishinda CCM au kumshinda Mwenyekiti wa Bunge au kwa nia ya kukomoana, bali tufanye hivyo kwa dhamira safi kwaajili ya faida ya watu wetu wote. Kuna watu ni wanaCCM, wengine CUF, CHADEMA, n.k. lakini ninyi nyote mtambue kuwa katiba yetu ya nchi ni moja tu. Tunataka katiba ambayo itatoa uhakika wa kila mtu kuishi katika Taifa letu kwa kujivunia Uraia wake na wala siyo fedha, cheo, kabila, dini, ukoo au familia yake. Tunataka katiba ambayo itamfanya kila mmoja akimwona Mtanzania mwenzake aone ni mtu wa karibu kwake kuliko mtu wa Taifa jingine lolote. Tunataka katiba itakayoyaweka mamlaka ya umma juu ya kitu chochote.

Kuna siku nilikuwa nasafiri, nilikuwa na haraka sana. Nilipokuwa naondoka nilihisi gari yangu haikuwa vizuri sana, kwanza nilifikiria niahirishe safari yangu kwa siku moja ili niifanyie matengenezo. Lakini kwa kufikiria umuhimu wa safari ile niliamua kusafiri bila hata ya kujua kwa undani tatizo la gari langu, nia ilikuwa moja tu kuwa nisichelewe kwenye program niliyoipanga. Siku ya pili ya safari yangu, gari iliharibika kabisa, chombo kilichoharibika sikukipata duka lolote, nilikokuwa nawahi sikufika. Siku ya tatu nilitarajia nifike Mbeya nipande ndege. Nilikopanga kwenda sikufika, mbeya nilichelewa ndege iliyotakiwa kunichukua kwenda Dar ili nikapande ndege nyingine, Tiketi zote za ndege zilipotea.

Nimeelezea kisa hiki kwa sababu wapo watakaosema kuwa gharama ambayo Taifa limeingia kwenye uandaaji wa katiba inayopendekezwa ni kubwa mno na hivyo kitendo chochote cha kuufuta au kuurekebisha mchakato mzima ni upotevu wa fedha na muda. Ukweli ni kwamba, kwa Taifa letu kuwa na katiba ambayo haina uhalali wa kimaadili ni gharama ambayo haiwezi kupimika. Tusipoliona hili sasa, tunaweza kulipia maradufu huko mbeleni. KWA KUUJUA UKWELI HUO NAPENDEKEZA YAFUATAYO:

  • Wananchi WAIKATAE katiba inayopendekezwa lakini iwe ni kwa dhamira safi na siyo ushindani au kukomoana Baada ya katiba inayopendekezwa kukataliwa, mchakato urudi nyuma
  • Sheria ya mabadiliko ya katiba iangaliwe upya ili kuhakikisha sheria hiyo inalenga kuhakikisha hakuna mtu au kundi linalohodhi mchakato wa upatikanaji wa katiba
  • Mchakato wa katiba uanze na uteuzi wa wajumbe wa Bunge la Katiba kwa kuhakikisha hakuna kundi au taasisi ambayo inakuwa na wawakilishi zaidi ya 10% ya wajumbe wa Bunge la Katiba (Bunge la Jamhuri  lichukuliwe kama taasisi ambayo itawakilishwa na wajumbe wachache)
  • Wajumbe wa Bunge la Katiba wachaguliwe na makundi yao moja kwa moja na idadi yao iongezwe
  • Kwenye Bunge la Katiba wawepo pia wataalam huru wa mambo ya katiba ambao kazi yao itakuwa ni kushauri na kuandika katiba kwa muundo unaokubalika
  • Muundo wa Mwungano upigiwe kura
Bart Mkinga



Share this :

Previous
Next Post »
0 Comments