BISMILLAHI RAHMANI RAHIM
TAMKO LA TAASISI YA MASHEIKH NA WANAZUONI WA KIISLAMU TANZANIA KUFUATIA KADHIA YA MAHAKAMA YA KADHI KATIKA BUNGE MAALUM LA KATIBA
Sekretarieti ya Taasisi ya Masheikh na Wanazuoni wa Kiislamu Tanzania, imekutana leo Jumapili tarehe 14/09/2014 katika kikao maalumu cha dharura kwa ajili ya kujadili jambo moja tu, ambalo ni kadhia ya sisi Waislamu kudai kuanzishwa kwa Mahakama ya Kadhi nchini na mvutano uliojitokeza katika Bunge Maalum la Katiba, kati ya wanaotaka Mahakama ya Kadhi itamkwe waziwazi katika Katiba na wale wasiotaka iingizwe kwenye Katiba ya nchi.
Baada ya kutafakari kwa kina hoja za pande zote mbili, Sekretarieti imejiridhisha kwamba wanaodai Mahakama ya Kadhi iingizwe katika Katiba ya nchi pamoja na Mahakama hizo kuendeshwa na Makadhi Waislamu katika kesi za Waislamu zinazohusu ndoa, talaka, mirathi, waqfu, wasia na malezi ya watoto, wako sahihi kuwasilisha madai hayo.
Waliojenga hoja hiyo wamesukumwa kudai hivyo kutokana na sababu kuu tatu zifuatazo:-
· Kwanza, Mahakimu wa mahakama za kawaida, wanakosea sana katika kuzitoleoa hukumu kesi za ndoa, talaka, mirathi n.k za Waislamu kutokana na kutozijua vizuri sheria husika za Kiislamu ambazo ni pana sana katika kadhia hizo, na ambazo zinahitaji mafunzo maalum zaidi ya mafunzo ya sheria za kawaida za kisekula, ili kumuwezesha hakimu wa kawaida kuamua kwa haki kesi hizo.
· Pili, Kitabu kinachotumika kutolea hukumu hizo ambacho ni Qur-an kinamuhitajia Hakimu kukijua vema kukikubali, kukiamini na kukiheshimu. Jambo ambalo linaweza kupatikana tu kwa Kadhi Muslamu.
· Tatu, jaribio la Waislamu kuwa na Makadhi wao wenyewe bila ya nguvu za serikali limeshindikana baada ya hukumu zao kukosa thamani na nguvu za kisheria mbele ya Mahakama za kawaida hapa nchini.
Kwa kuzingatia hayo, Taasisi ya Masheikh na Wanazuoni wa Kiislamu Tanzania inatoa Tamko lifuatalo:-
· Kwa kuwa hivi sasa tumo katika Mchakato wa Kurekebisha Katiba ya nchi, si kosa kwa Waislamu kudai Mahakama ya Kadhi iingizwe kwenye Katiba kwani huu haswa ndio wakati muafaka wa kuwasilisha madai hayo.
· Wale wanaopinga Mahakama ya Kadhi kuingizwa katika Katiba wajenge hoja zenye mifano iliyo wazi, huku wakizitazama nchi ambazo zimeingiza mahakama hizo katika Katiba zao, kama vile Kenya, Uganda na hata ndugu zetu wa Zanzibar kama mifano hai ya jinsi mahakama hizo zisivyovunja mshikamano na umoja wa wanadini mbili mbali wanaoishi pamoja.
· Wenye hoja ya hofu ya matumizi ya pesa za serikali, zinazotolewa na walipa kodi wa dini zote kuendeshea Mahakama ya Kadhi kwa ajili ya kesi za Waislamu tu, tunawaomba wazingatie yafuatayo:-
o Hivi sasa serikali inawalipa fedha zisizo na tija, Mahakimu wanaotoa hukumu kimakosa katika kesi hizo za Waislamu kutokana na udhaifu wa uelewa wao wa kitabu cha Qur-an na kuwaacha Waislamu katika hali ya kutoridhika na mwenendo mzima wa uendeshwaji wa kesi hizo.
o Kama yalivyopitishwa maamuzi ya kuanzishwa kwa mahakama maalum za Ardhi, Kazi na Biashara ambazo zimesadia sana katika kupunguza msongamano wa kesi katika mahakama za kawaida kutokana na maudhui kufanana, uwepo wa Mahakama ya Kadhi utapunguza sana msongamano mkubwa wa kesi katika mahakama za kawaida kwa kuzihamishia kesi za aina hiyo katika mahakama maalum ya Kadhi na hivyo kuharakisha utoaji wa haki kwa ujumla.
Uharakishwaji wa kuamua kesi, kutokana na hatua hiyo, utaongeza ufanisi wa uendeshwaji wa mahakama kwa ujumla na mwishowe utapunguza gharama zitokanazo na mlundikano wa kesi.
o Kuna hoja inayotolewa kuwa, kwa kuwa serikali haina dini, mahakama za kusikiliza kesi za kidini zisiingizwe katika Katiba ya nchi kwani jambo hilo litaingiza udini katika serikali. Ukiiangalia kwa undani utaona kuwa hoja hii haina msingi kwani ikumbukwe kuwa serikali hiyo hiyo ndio imetoa uhuru wa wananchi wake kuabudu kwa misingi ya dini zao.
Na serikali hiyo hiyo ndio huwajengea mazingira wanadini, ya kufanya ibada zao hizo kwa uhuru na haki kama moja ya wajibu wa serikali.
Ndio maana serikali hutenga maeneo maalum ya kujenga nyumba za ibada, siku maalum za kusherehekea sikukuu za kidini, kutia moyo mchango wa viongozi wa dini katika kujenga maadili mema katika jamii ili wapatikane raia wema, n.k.
Haya yote yanafanywa na serikali kwa kuheshimu na kutambua umuhimu wa wanadini kuridhika na uendeshwaji wa dini zao chini ya himaya yake.
o Kama mahakama ya Kadhi itaingizwa katika Katiba ya nchi na Makadhi wakapata fursa ya kuhukumu kwa usahihi kesi zao, matarajio ya Waislamu ni kufurahia na kuridhika na ufumbuzi huo na hivyo kuzidi kujengeka kwa amani na utulivu katika nchi.
· Taasisi ya Masheikh na Wanazuoni wa Kiislamu Tanzania, inawanasihi Waheshimiwa Wabunge wa Bunge Maalum la Katiba pamoja na Watanzania wote kwa ujumla kudumisha umoja wao na wasiigeuze kadhia ya Mahakama ya Kadhi kuwa ndio "kisu" cha kuukata umoja na Utanzania wao waliodumu nao kwa muda mrefu na kuishi pamoja kwa amani bila kujali tofauti za dini zao.
· Tunaomba mjadala huu uendelee lakini uongozwe na busara na hekima na kamwe asijaribu mtu yeyote kuondoa anachokiona yeye kuwa ni "Udini" kwa kutumia "Udini".
· Pamoja na Waislamu kuwa na dai hilo muhimu la Mahakama ya Kadhi na Wasiokuwa Waislamu nao kujipanga ili kuhakikisha mahakama hiyo haipatikani, Taasisi ya Masheikh na Wanazuoni wa Kiislamu Tanzania inawahimiza Waislamu wote nchini kuwa na subira pamoja na kujenga imani ya dhati kwa serikali yao kuwa itawatendea haki, huku wakijipa matumaini kwamba hakuna safari isiyokuwa na mwisho.
Tamko hili limetolewa na:
Sekretarieti
Taasisi ya Masheikh na Wanazuoni wa Kiislamu Tanzania
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/d/optout.
0 Comments