c/o Islamic Club, P.O Box 11392. Tel.: 185258/0511 613422, Dar es Salaam.
26/08/1999.
Mhe. Benjamin William Mkapa
Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania
Ikulu, Dar es Salaam
YAH: MASHAURIANO KUHUSU MADAI YA WAISLAMU.
Kwa heshima na unyenyekevu mkubwa tunaomba uhusike na kichwa cha maneno; na urejee mazungumzo yetu ya awali pamoja nawe yaliyofanyika nyumbani kwako, hapo Ikulu, jioni ya jumatano, tarehe 7 july 1999.
Awali ya yote halmashauri inatoa shukurani za dhati kwako kwa kitualika kukutana nawe siku hiyo na kutukirimu. Mkutano huo ulitupa matumaini makubwa juu ya uwezekano wa kipatikana na ufumbuzi wa kudumu wa madai ya waislamu ambayo tuliyawasilisha rasmi kwako mwazoni mwa mwaka huu, wakati wa baraza la Eid el Fitri. Madai hayo kwa ufupi yanahusu:
- Ubaguzi uliojitokeza dhidi ya waislamu katika baadhi ya vyombo vya dola ambao unafanywa na naadhi ya watendenaji walio katika serikali. Mfano wa hili umejitokeza katika:
- Kuwepo kwa idadi ndogo ya waislamu katika vyuo na maofisi ya serikali ukilinganisha na iwiano halisi ulivyo katika jamii yetu ya watanzania; na
- Kuwepo kwa idadi kubwa ya waislamu "wazururaji" na "wahalifu"katika magereza;
- Suala la Mwembechai kupatiwa utatuzi;
- Suala la Mahkama za Makadhi na
- Suala la nchi yetu kujiunga na "organization of Islamic conference" (OIC) na kiboresha uhusiano wake na nchi za Kiislamu.
- Serikali inatambua kuwepo "imbalances" dhidi ya waislamu katika jamii yetu ya Watanzania;
- Sio lengo wala njama za serikali au hata sera za Chama cha Mapinduzi (CCM) kuwa na hizo "imbalances"
- "Imbalances" hizo zipo tu kwa sababu ya kihistoria na ubinafsi ya baadhi ya watu katika CCM na Serikali; na
- Serikali bado inajukumu na wajibu wa kuondoa hizo "imbalances" kama inavofanya na maeneo mengine.
- Maelekezo uliyokwisha kuyatoa juu ya kutatuliwa kwa matatizo ya Waislamu yanayohusu "hijabu" na kuwepo kwa mabaa (bars), nyumba za wageni (gest houses), ufugaji ovyo na uchuuzi wa nguruwe na mabucha yake.
- Ofisi yako ina "update human resources bank" yake, ikiwa ni pamoja na kutafuta waislamu wenye taaluma za kushika nyadhifa mbali mbali; na
- Katika masuala ya utoaji wa vyeo, serikali imeanza suala la kuzingatia uwiano baina ya waumini wa dini tafauti.
- Utatuzi kamili wa matatuzi ya Waislamu utachukuwa muda;
- Masuala ya OIC na Mahkama za Makadhi bado yanahitaji utafiti, matayarisho na kuelimishana; kwa vile baadhi ya watu bado wanadhana au khofu kuwa kukubali masuala haya ni sawa na kukubali kuifanya Tanzania kuwa nchi ya Kiislamu; na
- Kuwapa Waislamu nafasi zote wanazostahiki kunataka busara na hekima kubwa kwa vile inabidi kwanza baadhi ya nafasi hizo wanyimwe au wanyanganywe watu wengine.
- Badala ya Waislamu kudai kwenye majukwaa, ni vyema madai hayo kuletwa kwako moja kwa moja kwa vile uko tayari kuyapokea na kuyashughulikia.
- Siyo muhimu sana kwa Waislamu hivi sasa kujua nani amesababisha hizo "imbalances", bali muhimu zaidi ni serikali kutambua kwamba "imbalances" hizo zipo na inapaswa kuziondoa.
- Suala la ku "update human resource bank" ya serikali ni suala muhimu sana kwani inawezekana Waislamu kukosa baadhi ya nafasi kwa sababu ya Serikali kutojua kama kati yao wamo wenye taaluma za kushika nafasi hizo.
- Waislamu hawataraji miujiza ya kutatuliwa matatizo yao yote kwa usiku mmoja; bali wanahitaji kuona kuwa hatuwa thabiti zinachukuliwa za kutatua matatiza hayo ikiwa ni pamoja na:
- Kuundwa kwa tume huru za kuchunguza suala la Mwembechai;
- Kuanzishwa kwa mpango, hata kama ni wa muda mrefu, na ratiba ya kuondoa hizo "imbalances" na
- Kukemewa na kukomeshwa kwa propaganda potofu dhidi yao.
- Imbalances zipo kwa vile hakuna "mechanism" ya kuzuia kuwepo kwake; na zipo kwa sababu takwimu zote takriban zinaonesha hivyo.
- Ilikuwa ni kinyume na Katiba kuondoa Mahkama za Makadhi kwa vile Katiba ya Tanzania inadhamini uhuru wa kuabudu na Waislamu kuwa na Mahakama hizo ni sehemu ya ibada.
- Haifanyi haya yote kwa sababu ya choyo, uroho au maslahi ya ubinafsi ya Waislamu peke yao; ila inafanya hayo kwa maslahi ya Taifa zima na kwa nia safi ya uzalendo na kutaka kuimarisha demokrasi na uadilifu.
na baada ya kuona muda mrefu umepita tangu Halmashauri yetu kukupatia Madai ya Waislamu, tulikuwa tumejiandaa kulieleza Baraza la Maulid siku ya tarehe 10 julai 1999 katika Ukumbi wa Diamond Jubilee, kuwa Serikali inachelewa kushughulikia Madai hayo. Lakini, kutokana na mazungumzo hayo ya tarehe 7 julai 1999, Halmashauri kwa furaha ilibidi ibadilishe risala yake na kutoa tamko rasmi kwamba madai hayo sasa yameanza kushughulikiwa na Serikali ipasavyo.
Mhe Rais, pamoja na mkutano wetu huo nawe hapo Ikulu, kumetokea mambo mengine kadhaa ambayo tunapaswa kuyazingatia kwa vile yana uhusiano mkubwa na masuala yetu.
- Mosi, kumekuwa na tamko la CCT la kutaka Serikali iache mara moja fikra ya Tanzania kujiunga na OIC kwa hoja kwamba OIC ni jumuiya ya Kiislamu na nchi hii ina Waislamu na Wakiristo
- Tamko hilo ambalo tunatarajia kuwa limetolewa kwa nia nzuri linathibitisha kauli yako kwamba baadhi ya wananchi wana dhana kuwa Tanzania ikijiunga na OIC itakuwa nchi ya Kiislamu. Ndio maana Halmashauri inakubadiliana nawe kuhusu kuelimishana ili kuondoa dhana hii. Ni muhimu wenzetu wajue kuwa nchi zisizo za Kiislamu ambazo zimejiunga na OIC kama vile Uganda na Mozambique, zinaendelea kuwa si za Kiislamu. Tangu kujiunga na OIC bado hatujasikia hizo nchi kutakiwa au kushauriwa kuwa za Kiislamu. Badala yake nchi hizo zinashiriki kikamilifu kakika shughuli za OIC kwa sababu ya maslahi yake. Aidha, kwa maoni yetu, nchi kuwa yenye Waislamu na Wakiristo ndio sababu nzuri zaidi ya nchi hiyo kujiunga, na sio kutojiunga na jumuiya hizo za kimataifa ama za Kiislamu au za Kikristo. Hivi sasa kwa mfano nchi yetu tayari ni mwanachama wa jumuiya ya madola (ya Commonwealth) ambayo kiongozi wake lazima awe Mkristo na mkuu wa Kanisa la Kianglikana; na hii haifanyi Tanzania, Kenya, Uganda, Nigeria n.k kuwa nchi za Kianglikana.
- Bali hata ingalikuwa Tanzania haijajiunga na jumuiya kama hizo, isingekuwa vibaya kuanza kwa kujiunga na OIC. Kwani Watanzania tunajiamini na tunajulikana kwa utamaduni wetu mkubwa na mzuri wa kuvumiliana katika masuala ya itikadi. Mfano nzuri ni kwamba katika Tanzania Waislamu na Wakristo wanapumzika Jumamosi na Jumapili, na sio Ijumaa na wanasherehekea mwaka mpya wa Kikristo, na sio wa Kiislamu. Aidha Vatican inayo mwakilishi wake hapo nchini ambae amepewa hadhi na anatambuliwa na kuheshimika kama Balozi. Ikiwa haya na mengi mengine ya aina hii yanafanyika hapa Tanzania kwa usalama na amani, ni dhahiri kwamba hakutakuwa na tatizo nchi yetu ikiboresha uhusiano wake na nchi za Kiislamu au ikijiunga na OIC.
- Zaidi ni kwamba tunataka Tanzania iboreshe uhusiano wake na nchi za Kiislamu kama invyoboresha uhusiano wake na nchi za Kikristo, na ijiunge na jumuiya za kimataifa za kidini sio tu kwa maslahi ya kiroho, bali pia kwa maendeleo ya kidunia. Ikijiunga na OIC, nchi yetu itastahiki misaada na mikopo kama ile ya Islamic Development Bank (IDB) ambayo ni nafuu zaidi kuliko mingi tuipatayo kutoka jumuiya au nchi nyingine. Aidha, kwa kufanya hivyo nchi yetu itakuwa imejipatia jukwaa jengine ambalo ni muhimu kwa harakati zake za kidiplomasia.
- Pili, kulitokea upinzani mkubwa katika Bunge, wakiwemo baadhi ya Mawaziri, dhidi ya Waziri wa Elimu na Utamaduni, Mhe. Juma Kapuya, kwa sababu ya kutangaza baadhi ya yale mambo ambayo wewe umeagiza yatekelezwe. Katika maelezo yake Mhe. Kapuya alizungumzia:
- Haki ya wanafunzi wa itikadi mbali mbali ya kuabudu nyakati za sala, na kuvaa mavazi yanyokubalika katika maadili yao.
- Wajibu wa wanafunzi wa kuendesha miradi yao ya uchumi kwa kuzingatia tafauti za udini zilizopo bila ya kuleta bughudha kwa kundi au dhehebu lolote.
- Jukumu la Wizara la kuhakikisha kwamba suala la udini halijitokezi wakati wa kujaza fomu za maandalizi ya kujiunga na Kidato cha 1, cha V pamoja na kujiunga na mafunzo ya ualimu.
Tunashukuru kuwa kwa upeo wako mpana, ulibainisha hivi karibuni kwamba:
- Wapo wanasiasa au viongozi wengine wa jamii wanaozungumza wazi wazi lugha ya udini, ukabila na majimbo. Tusiwapuuze na wala tusiwaonee haya.
- Tatu, kumetokea teuzi mbali mbali za viongozi wa Chama, Serikali na Mashirika ya Umma. Wahusika wa teuzi hizo hawakuonekana kuzingatia suala la uwiano baina ya waumini wa itikadi tofauti; jambo ambalo linaonesha sio tu kupuuza Madai ya Waislamu, bali pia kutokujali maelekezo yako. Katika chaguzi ndogo zilizofanyika Temeke na Ubungo hivi karibuni, kwa mfano, CCM iliteuwa wagombea wote wawili kutoka dini moja. Aidha katika bodi la ya Wakurugenzi wa shirika la PPF walioteuliwa hivi karibuni wote ni kutoka dini moja; na wale watatu ambao walikuwemo kabla wa dini nyingine wametolewa kwa mpigo. Mifano ya aina hii ni mingi na hapa hatuwezi wala hatuhitaji kuitaja yote. Ila ni muhimu kutanabahi kwamba Waislamu wanaangalia kwa makini sana teuzi zote zinazofanywa hivi sasa katika CCM, Serikali na Mashirika ya Umma.
- Nne, kumekuwa na Mkutano Mkuu wa Bakwata ambao umefanyika Dodoma mnamo siku ya Alhamisi, tarehe 29/07/1999. Ukihutubia katika ufunguzi wa mkutano huo kama mgeni rasmi ulisema kuwa:
- Uko tayari, na kwa kweli, umeshaanza kuyashughulikia matatizo ya kitaifa yanayohusu Waislamu.
- Kwanza, kuna suala la "machanism" ambayo itatumika kusawazisha hizi "imbalances". Ukizungumzia suala hili ulisema:
- Serikali haitasuta kumchukulia hatua kali mtu yeyote atakae bainika akimbagua mwengine katika masuala ya elimu, ajira, upandishaji vyeo na utoaji wa leseni au hati mbali mbali kwa misingi ya jinsia, dini, kabila au eneo anakotoka mtu.
- Serikali haiwezi kuweka kanuni ya kudumu ya kugawa vyeo kwa misingi hiyo ya udini, ukabila na jnsia.
- Kwa faida ya taifa ni vizuri tugawe vyeo kwa vigezo vya ujuzi, uwezo na upimaji makini wa matokeo ya kazi.
- Haitakuwa rahisi kuwachukulia hatuwa wabaguzi bila ya kuwa na vituo vya kutosha vyenye taratibu madhubuti na uwezo wa kupokea na kufuatililia madai ya wanaobugudhiwa.
- Itakuwa vigumu kukomesha ubaguzi na kuhukumu wabaguzi kama hakutakuwa na sheria maalumu, hata kama ni ya muda ya kufanya hivyo.
- Katika kuomba au kutoa nafasi za elimu au ajira, utaratibu wa kutumia nambari badala ya majina ni vyema utumike; kwani usipo saidia kuinua wanyonge, utasaidia kuondoa zana ya upendeleo.
- "Affirmative action" au "positive discrimation" tayari inatumika hapa nchini na inasaidia kuinua wanyonge wa jinsia; kwa hiyo ni bora pia ijaribiwe katika kuinua wanyonge wa dini, kabila na maeneo, n.k.
Kwa maneno mengine, sisi tunaona kuwa si vyema uwezo na ujuzi kuwa ndio vigenzo pekee vya kuzingatiwa katika kugawa vyeo. Kuna haja pia ya kuwa na "mechanism" ya kuzuia watu wa dini, kabila au jinsia moja kuchukua vyeo vyote au (vingi mno) mpaka wenzao wa dini, kabila au jinsia nyengine wakakosa kabisa (au wakapata vichache sana) hali nao wanafaa. Kwa hiyo, badala ya kuchagua baina ya vigezo vya kabila, jinsia na dini kwa upande mmoja, na vigezo vya ujuzi, uwezo au uzalishaji kwa upande mwengine, ni muhimu vigezo vyote hivi vitumike kw wakati mmoja.
- Kisha, kuna suala la matokeo ya utafiti ambao sote tumefanya. Hotuba yako imetupa hisia kwamba sasa Serikali imemaliza kufanya utafiti wake juu ya Madai ya Waislamu; na ndio maana iko tayari kuyashughulikia. Ila pia hotuba hiyo imetupa wasiwasi kuwa labda "conclusion" ya utafiti huo ni tofauti ba ile ya utafiti wa Halmashauri. Wasiwasi huu umekuja baada ya kusikia kauli yako kwamba:
- Hakuna mchujo wowote katika kuandikisha watoto shule, kwenda sekondari, au vyuo vikuu, au katika ajira, unaofanywa kwa msingi wa kuwabagua watu wa dini fulani. Hiyo nawahakikishia kabisa.
- Na kama yupo mwenye ushahidi kwamba mwanafunzi fulani amezuiliwa kuendelea na elimu kwa sababu tu ya dini yake, jinsia yake au kabila lake basi wanaohusika wajulishwe.
- Ukosefu wa ushahidi wa kwepo kwa mchujo, si uthibitisho wa kutokuwepo kwa mchujo huo; kwani ushahidi unaweza kukosekana hata kama mchujo ukiwepo madhali unafanywa kwa siri au uangalifu wa kutosha.
- Ushahidi wa kesi za mchujo si rahisi kupatikana kwa kuwataka wanaobaguliwa waripoti kesi zao kwa wahusika au hata kwa Rais mwenyewe. Kwani mara nyingi hao wahusika huwa hawajulikani au wenyewe ndio wabaguzi. Aidha si rahisi kwa mwananchi wa kawaida kuwa na uwezo na ujasiri wa kufika Ikulu.
- Athari ya mchujo ipo, inaonekana, nayo ni hizi "imbalances" ambazo tunakubaliana kwamba zipo.
- Itakuwa ni kitu cha ajabu sama mchujo kutokuwepo; kwani kwa kawaida, binadaamu haachi kuchuja (kujipendelea yeye mwenyewe na kupendelea walio wake) kama hakuna cha kumzuia.
- Takwimu zetu zinaonyesha kwamba watoaji wa nafasi za masomo au ajira wengi, kama si wote, ni waumini wa dini moja; na wanaopewa nafasi hizo wengi, kama si wote, pia ni waumini wa dini hiyo; ila wakosaji sasa, kama si wote, wengi wao ndio waumini wa dini vyingine.
- Halafu kuna suala la kujenga badala ya kubomoa madaraja ya kijamii. Ni vyema umelitaja suala hili katika hotuba yako; na umesema kuwa:
- Mojawapo ya visingizio vinavyotumiwa na wanaotaka kuvunja madaraja ya umoja na utaifa wetu ni kwamba watu wa eneo fulani wameachwa nyuma, au watu wa dini fulanai hawapewi nafsi fulani katika uongozi wa nchi na jamii.
- Kuwa na utaratibu wa nambari badala ya majina katika kuomba na kutoa nafasi za elimu;
- Kutumia mpango wa "positive discrimination" au "affirmative action" katika kutoa nyadhifa na ajira;
- Tanzania kuboresha uhusiano wake na nchi muhimu za Kiislamu kwa kufungua balozi zake katika nchi hizo na kujiunga na OIC;
- Mahkama za Makadhi kurudishwa;
- Serikali kukemea propaganda potofu na kukomesha ubaguzi dhidi ya Waislamu kwa:
- Kuanzisha tume ua kuchunguza kesi muhimu za aina hiyo, hususan Kesi ya Mwembechai;
- Kuanzisha vituo maalum na vya kutosha vya kupokea na kufuatilia kesi za ubaguzi.
- Kutatua matatizo ya Waislamu yanayohusu "hijabu", sala wakti wa ibada na kuwepo kwa mabaa (bars), nyumba za wageni (guest houses), ufugaji ovyo na uchuuzi wa nguruwe na mabucha yake.
- Kuzingatia suala la uwiano baina ya watu wa itikadi tofauti katika uteuzi wa viongozi mbalimbali.
- Kutozungumza lugha ya udini, ukabila na majimbo.
Ahsante.
Al-Miskry, Saleh
Secretary.
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/d/optout.
0 Comments