[wanabidii] Usuluhushi Bunge la Katiba kama mazingaombwe

Wednesday, August 27, 2014

Usuluhushi Bunge la Katiba kama mazingaombwe

Mchakato wa Katiba Mpya umeendelea kuzua vioja mjini hapa kufuatia mkutano wa kusuluhisha wajumbe wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) na Tanzania Kwanza ili kunusuru Bunge Maalum la Katiba lililogawanyika vipande vipande kushindwa kujitokeza katika ukumbi uliokuwa umepangwa.

Mkutano huo ambao ulipangwa kufanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Dodoma, haukufanyika kutokana na kutojitokeza hata mjumbe mmoja kutoka katika wajumbe wa Ukawa unaounda na vyama vya Chadema, CUF na NCCR-Mageuzi na Tanzania Kwanza inayoundwa na wajumbe kutoka CCM na baadhi kutoka kundi la 201.

Katika hali iliyoonekana kama sinema, mratibu mmoja wa mkutano huo alijikuta akitiwa mbaroni na polisi baada ya kudaiwa kutapeli Sh. 400,000 zilizotolewa kama malipo ya awali ya ukumbi huo.

Katibu wa Ukawa, Tundu Lissu, alisema amekuwa akipigiwa simu na waandaaji wa mkutano huo wakimueleza mpango wao huo, lakini hakuwahi hata kufikiria kufika mjini hapa kwa kuwa ana uhakika hawana uwezo wa kutatua mgogoro ulioshinda jitihada nyingi.

"Nisingekuja Dodoma kwa mambo ambayo binafsi nayashangaa, kweli jitihada zote zilizoshindwa kumaliza shida hii, kituo cha yatima kingeweza, sasa nasikia wameishia kutapeliwa, kweli wajinga ndiyo waliwao," alisema Lissu.

Naye mmoja wa viongozi wakuu wa Bunge Maalum la Katiba, alithibitisha kuwahi kukutana na watu hao, lakini alisema hawakuwa na maelezo yenye uzito wa kufanikisha usuluhishi na hivyo hakuwahi kufikiria kuhudhuria mkutano huo.

"Kwanza Ukawa walishakataa kukutana na mimi, ningefika ili iweje?" Alihoji kiongozi huyo na kuongeza: "Labda kama yalilenga kukutanisha CCM na Ukawa kwa sababu sisi tunaendelea kuandika Katiba mpya, kwa vyovyote vile nisingekuja."

NIPASHE ilimshuhudia Mratibu wa mkutano huo, Omari Kombe, akiwa na John Thomson, anayetuhumiwa kutapeli wakiingia katika Hoteli ya Dodoma wakiongozana na watu watatu ambao baadaye ilifahamika kuwa ni askari polisi.

Meneja wa hoteli ya Dodoma, Augustino Malingumu, aliwaeleza askari waliofika katika hoteli hiyo kuwa Thomson alifika juzi akiwa na wenzake wakala na kunywa na kwamba walipopelekewa bili akataka aisaini ili malipo yafanyike jana wakati wa mkutano huo wa upatanishi.

Malingumu alisema jana Tomson alifika na kumueleza kuwa mkutano umeahirishwa na kwa kuwa waliishiwa fedha za kulipia hoteli walikofikia, aliomba deni lake la juzi lilipwe kwa sehemu ya fedha zilizolipwa hotelini hapo kama malipo ya awali ya ukumbi na kiasi kinachosalia arejeshewe.

Malingumu alisema baadaye alifuatwa na Kombe akitaka kujua taratibu za ukumbi, ndipo alipomueleza kuwa Thomson alifika na kuchukua fedha zote zilizokuwa zimelipwa awali.

Kwa upande wake, Kombe alisema kwa mara ya kwanza alikutana na Thomson maeneo ya Bunge, alipokwenda kuzungumza na mmoja wa viongozi wakuu wa Bunge Maalum, na kwamba baada ya kumueleza sababu za uwapo wake akamuahidi kushirikiana naye akisema naye yupo Dodoma kwa masuala hayo ya kutafuta usuluhishi kati ya Ukawa na Tanzania Kwanza.

Alisema kuwa pamoja na kujitambulisha kwake kuwa ni Ofisa Usalama wa Taifa, pia alisema ni mjumbe wa maveterani wa CCM katika Jumuiya ya Vijana wa CCM (UVCCM) na kwamba ujio wake wa Dodoma ni kuwakilisha maveterani wa Jumuiya hiyo.

Thomson akizungumza mbele ya vyombo vya habari jana, alikiri kuchukua fedha hizo ingawa alisema stakabadhi ya malipo hayo alikuwa nayo Kombe na kuwa yeye alichangia Sh. 300,000 kati ya Sh. 400,000 walizokuwa wamelipa awali.

Hata hivyo, madai hayo yalikanushwa na Kombe.Thomson alipoulizwa zilipo fedha hizo, alishika simu na kumpigia Mwenyekiti wa Wazazi CCM Taifa, Abdallah Bulembo, kwamba anataka achukue fedha kutoka kwake alizomuahidi, mmoja wa askari alimwelekeza aliopokuwa amekaa Bulembo.

Thomson alimfuata Bulembo na baada ya kuzungumza naye kwa kifupi alirejea eneo la mahojiano na kueleza kuwa Bulembo alimuuliza sababu za kumfuata kuomba fedha mbele ya vyombo vya habari.

Baada ya kufuatwa mara mbili na Thomson, Bulembo alifika eneo la mahojiano na kuhoji kilichojiri na kuelezwa na mmoja wa askari kuwa Thomson alikuwa anatuhumiwa kwa utapeli, ndipo ikabainika kuwa hata Bulembo alikuwa akiwindwa kutapeliwa na Thomson tangu juzi.

Bulembo alieleza kuwa yupo kamati yake ya Bunge Maalum namba sita inayofanya vikao katika hoteli hiyo na kuwa juzi alifuatwa na mtuhumiwa huyo akimuomba msaada wa Sh. 400,000 na kuwa yeye ni mwakilishi wa kituo cha watoto yatima.

Bulembo alisema alimuahidi aende jana ampatie kiasi atakachokuwa nacho.Baada ya maelezo ya Bulembo, polisi waliondoka na Thomson kwenda Kituo Kikuu cha Polisi kwa ajili ya mlalamikaji kuandika maelezo na mtuhumiwa huyo kumfungulia jalada.

Kombe akizungumzia hatma ya mkutano huo, alisema Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, aliwasiliana naye juzi na kusema kuwa walishindwa kuwapeleka viongozi wastaafu kwa ajili ya mkutano huo kutokana na muda kuwa mfupi.

Hata hivyo, Kinana alipotafutwa kwa simu jana, hakupokea.Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Dodoma, David Misime, hakupatikana kuzungumzia suala hilo.

Ipp Media


--
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/d/optout.

Share this :

Related Posts

0 Comments